11-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Fadhla Na Rahmah Za Allaah
Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake
11-Kuomba Fadhila Na Rahmah Za Allaah
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Allaah akisema:
((اللَّهُمَّ إنِّي أَسْأَلُك مِنْ فَضْلِكَ وَرَحْمَتِكَ، فَإِنَّهُ لاَ يَمْلِكُهَا إِلاَّ أَنْتَ ))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Fadhila Zako na Rahmah Zako, kwani hazimiliki yeyote isipokuwa Wewe tu)). [Imekharijiwa na Atw-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr" 10/178 na Ibn Shaybah 7/94. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As-Silsilat Asw-Swahiyhah 4/57]
Faida Na Sharh:
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameomba katika du’aa hii fadhila kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyoamuru katika Kauli Yake:
"وَاسْأَلُوا اللَّهَ مِنْ فَضْلِه"
Na mwombeni Allaah Fadhla Zake. [An Nisaa (4:32)]
Yaani mwombeni Awaongezeeni Ihsaan Zake zaidi na Neema Zake katika mambo ya kidunia na ki Aakhirah, kwani hayo yote yako Mkononi Mwake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قُلْ إِنَّ الْفَضْلَ بِيَدِ اللَّـهِ يُؤْتِيهِ مَن يَشَاء
Sema: Hakika fadhla zi Mkononi mwa Allaah, Humpa Amtakaye. [Aal-‘Imraan (3:73)]
Na kwa kuwa iko Mkononi Mwake, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huitumia na Huisarifu Atakavyo Mwenyewe kwa Hikma Yake. Humpa Amtakaye kwa Hikma na Uwezo Wake uliokamilika, na Humnyima Amtakae kwa Hikma Yake na Uwezo Wake Uliokamilika.
Pia ameomba Rahmah, kwa kuwa Rahmah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) imekienea kila kitu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amemwomba Allaah ('Azza wa Jalla) Amfunike nayo ili aweze kufaulu hapa duniani na huko Aakhirah.