12-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Kujilinda Dhidi Ya Njaa Na Khiyana

 

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

12-Kuomba Kujilinda Dhidi Ya Njaa Na Khiyana

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akijilinda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  akisema:

 

 ((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْجُوعِ؛ فَإِنَّهُ بِئْسَ الضَّجِيعُ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ الْخِيَانَةِ؛ فَإِنَّهَا بِئْسَتِ الْبِطَانَةُ))

((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na njaa, kwani njaa ni mwenza mbaya sana ninayelala naye. Na najilinda Kwako na khiyana, kwani khiyana ni mwandani mwovu kabisa)). [Imekharijiwa na Abuu Daawuwd 1547, An-Nasaaiy 5483, na Ibn Maajah 3354]

 

 

Faida Na Sharh:

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amejilinda na njaa. Njaa ni ngumu kuikabili, huleta maumivu ya kipekee mwilini, humdhoofisha mtu, huchafua akili, huibua fikra mbaya na mawazo potovu, huteteresha ‘ibaadah, hulegeza uimara wa mtu katika kumcha Allaah ('Azza wa Jalla) , huchemsha hamaki na ghadhabu, husababisha tabia mbaya na hata wakati mwingine humwondolea mtu haiba yake na hishma yake akajikuta anafanya mambo ya ovyo asiyoyatarajia.

 

 

Aidha, inaweza kumsukuma akaiba, akasema uongo, akajidhalilisha na hata wakati mwingine kujiuza kimwili kwa akina mama. Pia inamfanya asiwajali wengine na kuangalia tumbo lake tu. Tunaona misaada ya vyakula inapogawanywa kwa wahanga wa janga fulani mathalan ambao wamepoteza kila wanachokimiliki, watu wananyosukumana na kukanyagana bila kujali kati ya mtoto na mtu mzima, mzee na kijana, mwanamke au mwanamume, mlemavu au mzima;  kila mtu anajiwania yeye apate kwanza kabla ya mwingine. Hayo yote ni madhara ya njaa aliyojilinda nayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Mtu akibanwa na njaa, usingizi pia humruka. Usingizi huja pale tumbo linapokuwa na kitu. Kama halina kitu, basi usingizi nao hupaa.  Na madhara ya mtu kutopata usingizi ni makubwa kwa mwili wake.

 

 

Kadhalika, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    amejilinda na khiyana. Khiyana ni kuvunja ahadi kwa siri. Inaweza kuwa khiyana kati ya mtu na mtu, au kati ya mtu na Rabb wake (Azza wa Jalla). Inakusanya makalifisho yote ya ki-Shariy’ah Aliyoyaamuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Anayetuambia:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ

Enyi walioamini! Msimfanyie khiyana Allaah na Rasuli na wala msikhini amana zenu na hali nyinyi mnajua. [Al-Anfaal (8:27)]

 

 

Mtu akiwa na sifa hii, anakuwa kana kwamba ndani ya mwili wake anaishi na mwandani mbaya kabisa. Kuishi na mwandani kama huyu ni khatari kubwa kabisa. Ni lazima Muislamu aachane na tabia kama hii. Ni sawa na mtu kuishi na ugonjwa hatari kabisa kama saratani. Asipoutibu haraka, basi utamuua na kummaliza.

 

 

Ni lazima Muislamu achunge makalifisho yote ya ki-Shariy’ah aliyokalifishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na ayatekeleze kama inavyotakikana. Pia achunge amana, ahadi na yote yanayohusiana na wenzake wana Aadam, kwani hayo yote ataulizwa Siku ya Qiyaamah.

 

 

 

Share