13-Du'aa Za Ruqyah: Kujilinda Dhidi Ya Kupotea Au Kupoteza, Au Kuteleza Au Kutelezesha, Au Kudhulumu

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

13-Kujilinda Dhidi Ya Kupotea Au Kupoteza, Au Kuteleza Au Kutelezesha, Au Kudhulumu

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini Ummu Salamah Hind Al-Makhzuwmiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akisema: Hakutoka kamwe Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  nyumbani kwangu ila hunyanyua macho yake mbinguni na kusema:

 

((اللَّهُمَّ اني أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَضِلَّ أَوْ أُضَلَّ أَوْ أَزِلَّ أَوْ أُزَلَّ أَوْ أَظْلِمَ أَوْ أُظْلَمَ أَوْ أَجْهَلَ أَوْ يُجْهَلَ عَلَيَّ ))

((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kupotea au kupoteza, au kuteleza kufanya kosa au kutelezeshwa, au kudhulumu au kudhulumiwa, au kufanya kitendo cha kisafihi au mimi kufanyiwa usafihi)). [Imesimuliwa na Ahlus-Sunan wanne na wengineo]

 

 

Faida Na Sharh:

 

 

Hii ni du’aa adhimu ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haiachi kila anapotoka nyumbani. Kunyanyua kwake macho mbinguni kunaashiria 'Uluwa wa Allaah (Jalla wa ‘Alaa) juu ya Viumbe Vyake vyote, na kuwa Yeye Anaviona viumbe hivyo katika hali zao zote, na kuwa hakuna chochote kinachofichikana Kwake. Na hili linatukumbusha sisi kuwa mtu anapotoka nyumbani, basi amche Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  popote pale awapo katika mihangaiko yake ya kutafuta rizki, na ajue kwamba Allaah (‘Azza wa Jalla) Anaziona nyenendo zake zote. Huko anakokwenda ni lazima atatangamana na watu wa aina zote na tabaka zote; wema na wabaya, atasuguana nao, na ataamiliana nao.

 

 

Katika mtangamano huu, panatokea mengi mabaya ya haramu ambayo yeye anaweza kuyafanya au kufanyiwa ambayo inabidi ajihadhari nayo.

 

 

Na hayo ndio haya aliyotukusanyia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katika du’aa hii adhimu. Yote haya ni katika madhambi makubwa angamizi.

 

 

Ameomba akingwe asitumbukie kwenye dhwalaalah (upotofu) ambayo ni kinyume na hidaayah, au mtu mwingine kumtumbukiza. Na hili ndilo daima tunaloliomba katika Swalaah zetu zote tunaposoma Suwrah Al-Faatihah kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atuongoe Njia iliyonyooka isiyo ya waliopotea kutokana na hatari ya dhwalalah (upotofu).

 

 

Akaomba akingwe asiteleze au kumtelezesha mwingine. Kuteleza huku ni kufanya dhambi bila ya kujua au kuhisi. Hii inawezekana kutokana na kitendo au kauli, na haya yanafanyika sana katika maisha yetu ya kila siku. Kuna mengi ambayo tunayaona ni madogo na hayana neno, lakini dhambi zake ni kubwa kwa Allaah ('Azza wa Jalla).

 

 

Akaomba alindwe asije kumdhulumu mtu sawasawa katika mali yake, hishma yake, utu wake na kadhalika, au yeye kufanyiwa dhulma, kwani dhulma ya aina yoyote inamuumiza sana mdhulumiwa ingawa haki yake atakwenda kuipata Siku ya Qiyaamah. Lakini pamoja na hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa anajilinda, kwani mdhulumiwa wakati mwingine anaweza kujisahau na kupetuka mipaka zaidi ya alivyodhulumiwa, na hapo yeye kuwa mkosa.

 

 

Mwisho akaomba kinga asifanye kitendo cha kijahili au kisafihi kama kukebehi watu, kuwadhihaki, kuwakejeli au kuwadharau na kadhalika, au yeye kufanyiwa hayo.

 

 

Kuongezea na haya, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    alikuwa pia akisema anapotoka nyumbani:

 

  بِسْمِ اللَّهِ تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ لا حَوْلَ وَلا قُوَّةَ إِلا بِاللَّهِ  

((BismiLLaah. Nimetawakkal kwa Allaah, hakuna uwezo wala nguvu ila kutoka kwa Allaah)). [Imepokelewa na Anas bin Maalik. Imesimuliwa na At-Tirmidhiy katika Sunan yake 3348. Abuu ‘Iysaa kasema ni Hadiyh Hasan Swahiyh]

 

 

Na mwenye kusema hivi basi huambiwa: "Umetoshelezwa na umekingwa", na shaytwaan hukaa mbali naye.

 

 

Haya ndiyo maelekezo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ambayo inabidi tuyazingatie ili tupate kinga ya duniani na kesho Aakhirah.

 

 

 

Share