36-Zawadi Kwa Wanandoa: Tabia Njema

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

36-Tabia Njema

 

حسن الخلق

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

 

وعاشروهن بالمعروف

 

“ … na kaeni nao kwa wema…” (An-Nisaa: 19)

katika Aayah nyingine ya sura hiyo hiyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaendelea kututanabaisha

 

وأخذن منكم ميثاقا غليظا

 

“…Nao wanawake wamepokea kwenu ahadi thabiti (kuwa mtakaa nao kwa uzuri).” (An-Nisaa: 21)

Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  akielezea fadhila za tabia njema anasema:

 

أكمل المؤمنين إيمانا أحسنهم خلقا, وخياركم خياركم لنسائهم خلقا

 

“Muumini aliyekamilika kwa imani ni yule mwenye tabia njema, na mbora wenu ni yule aliye mbora kwa wake zake kwa tabia.”

(Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy)

 

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  amesema tena:

 

خيركم خيركم لأهله , وأنا خيركم لأهلي

 

“Mbora wenu ni yule aliye mbora kwa mke wake, na mimi ni mbora kwa watu wangu wa nyumbani (ahli).”

(Ibn Maajah na Ad-Daarimy)

 

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:

 

إنّ المرأة خلقت من ضلع وإنّ أعوج شيئ في الضّلع أعلاه , فإن ذهبت تقيمه كسرته , وإن تركته لم يزل أعوج , فاستوصوا بالنساء

 

Mwanamke Ameumbwa kwa ubavu, na sehemu iliyopinda ya ubavu ni juu yake, ukijaribu kuunyoosha utauvunja, na lau utauacha utaendelea kupinda, nakuusieni (kuwafanyia wema) wake zenu.” (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Si hayo tu aliyohimiza Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  kuhusu wanawake. Bali kwa umuhimu na unyeti wa suala hili tunaona kuwa katika usia wake wa mwisho anatuuusia:

 

الله الله في النساء فإنّهن عوان في أيديكم , أخذتموهنّ بأمانة الله , واستحللتم فروجهنّ بكلمة الله

 

“Allaah, Allaah, kwa wanawake, hao ni wasaidizi wenu walio kwenye mikono yenu, mmewachukuwa kama ni amana kutoka kwa Allah, na imekuwa halali tupu zao kwenu kwa neno lake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) (Iijaab na Qubuwl).” (Muslim, Abu Daawuwd, Ibn Maajah na Ahmad)

 

Na katika jumla ya tabia nzuri katika maisha ya ndoa ni kuacha kumfanyia mke maudhi ya aina yoyote ile. Vile vile kumfanyia na kumtendea mazuri, na kucheza nae na kuongea nae kwa upole. Hali kadhalika kujali zaidi uadilifu katika mambo yake na kufuata siasa za kati kwa kati katika muamala wako nae na haswa katika yale yenye maslahi kwake na yale yenye kuhifadhi akhlaq zake kulingana na haja, sehemu au tukio.

 

Share