37-Zawadi Kwa Wanandoa: Kuishi Nae Kwa Wema Hata Ikiwa Unamchukia
Zawadi Kwa Wanandoa
37- Kuishi Nae Kwa Wema Hata Ikiwa Unamchukia
المعاشرة بالمعروف حتّى في حال الكراهية
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
وعاشروهن بالمعروف فإن كرهتموهن فعسى أن تكرهوا شيئا ويجعل الله فيه خيرا كثيرا
“ …na kaeni nao kwa wema; na kama mkiwachukia basi (msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu Ametia kheri nyingi kwake.” (An-Nisaa: 19)
Katika hilo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:
لا يفرك مؤمن مؤمنة إن كره منها خلقا رضي منها آخر
“Habughudhiki muumini mwanamme kwa tabia ya mke wake akichukizwa na moja ( ya tabia) atapenda nyingine.” (Muslim na Ahmad)
Hata hivyo hakuna binaadamu aliyekamilika, anayeweza kusifika kwa ukamilifu wa tabia zote za kuigwa, na vile vile hakuna maisha yenye furaha yaliyokamilika. Hivyo basi ni lazima yawepo mapungufu na matatizo, ambayo yanahitajia suluhisho litakalofikiwa kwa ushirikiano wa pande zote mbili (mume na mke) ili kutatua na kuyashinda.
Katika kuamiliana na matatizo yanayojitokeza kunahitaji subira, uvumilivu na utulivu ili maisha yaweze kuendelea na mambo kuweza kurejea kama yalivyokuwa kabla.
Na katika matengamano ya maisha haya ya ndoa ni kuishi na mke kwa wema hata katika hali ya kuwa hata kama unamchukia. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) anatufundisha:
أن تطعمها إذا طعمت , وتكسوها إذا اكتسيت , ولا تضرب الوجه ولا تقبّح , ولا تهجر إلاّ في البيت
“Kumlisha unapokula, na kumvisha unapovaa, wala usimpige usoni na kumharibu na usimtusi (kwa matendo yake na maneno yake) wala usimhame kwenda nyumba nyingine (umhame kitanda tu).”
(Abu Daawuwd, Ibn Maajah na Ahmad)
Na ni juu ya mwanamme yeyote kumtizama na kumuangalia mwanamke kulingana na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) :
ارفق بالقوارير
“Wafanyieni wema vyombo vyenu (qawariira).” (Al-Bukhaariy)
Na usia huu unaohusu wema unakusudia upole na mazungumzo mazuri na kuvumilia maudhi. Hali kadhalika kumfanyia uadilifu katika hali zote.