033-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Wudhuu Unapasa Kwa Ajili Ya Swalaah Tu Na Si Vinginevyo
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
033-Wudhuu Unapasa Kwa Ajili Ya Swalaah Tu Na Si Vinginevyo
Wudhuu unapasa kwa yule anayetaka kuswali – kama hana wudhuu – sawasawa ikiwa Swalaah ni ya Faradhi, Sunnah au Maiti. Hii ni kwa Neno Lake Subhaana:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُواا))
(( Enyi mlioamini! Mnaposimama kuswali, basi osheni…..)). [Al Maaidah (5:6)]
Na kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((لايقبل الله صلاة بغير طهور))
((Allaah Haikubali Swalaah bila ya wudhuu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (224) na wengineo].
Haipasi kutawadha kwa jambo jinginelo lisilokuwa Swalaah, na wala haikatazwi kwa asiyekuwa na wudhuu kufanya jambo jingine lolote isipokuwa Swalaah. Lakini wudhuu umesuniwa katika mambo yafuatayo:
Kutufu Al-Ka’abah
“Hatujagundua au kuipata dalili yoyote sahihi na ya wazi yenye kuwajibisha kutawadha kwa wenye kutufu. Maelfu kwa maelfu ya Maswahaba ambao idadi yao hakuna aijuaye ila Allaah, walikuwa wakitufu katika enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na sisi hatujapata habari yoyote inayoeleza kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamrisha yeyote kati yao kutawadha kwa ajili ya kutufu pamoja na kuwepo uwezekano wa kutenguka wudhuu kwa wengi kati yao wakati wa kutufu, na kuingia wengi wao katika ‘ibaadah hiyo bila ya wudhuu na hususan katika siku hizo ambapo msongamano ulikuwa mkubwa kama katika twawaf za “Quduwm” na “Ifaadhwah”.
Na kwa vile hakuna dalili yoyote iliyopokewa juu ya kupasa kutawadha kwa ajili ya twawaf, na wala hakuna Ijma’a ya Maulamaa juu ya kupasa hilo pamoja na kuhitajika, basi inabainika kwamba si lazima”. [Jaami'u Ahkaamin Nisaai cha Shaykh wetu Allaah Amhifadhi (2/515)].
Maulamaa wameitolea dalili Hadiyth Marfu’u ya Ibn 'Abbaas juu ya ulazima wa kutufu isemayo:
((الطواف بالبيت صلاة إلا أن الله أباح فيه الكلام))
"Kutufu Nyumba ni Swalaah, isipokuwa Allaah Ameruhusu kuzungumza ndani yake". [Hadiyth Mawquwf: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Al-Haakim na wengineo.
Na haifai kuwa ni Hadiyth Marfu’u, bali lililo sawa ni kuwa ni Hadiyth Mawquwf kama alivyobainisha Shaykh wetu Allaah Amnyanyulie cheo chake katika kitabu cha Jaami'u Ahkaamin Nisaai (2/515-521) kinyume na Mwanachuoni Mkubwa Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) aliyesema kuwa ni Swahiyh katika kitabu cha Al-Irwaa'i (1/156)].
Wamesema: "Ikiwa twawaf ni Swalaah, basi inapasa kutawadha kama ilivyo katika Swalaah". Lakini kauli yao hii inakataliwa kwa mambo mawili:
Kwanza: Si sahihi kwamba Hadiyth hii ni Marfu’u. Lililo sawa ni kuwa ni Hadiyth Mawquuf kutokana na maneno ya Ibn 'Abbaas. Aidha, hili limetiliwa nguvu na At-Tirmidhiy, Al-Bayhaqiy, Ibn Taymiyah, Ibn Hajar na wengineo.
Pili: Na kama tukijaalia kuwa ni Hadiyth Swahiyh, basi haimaanishi kuwa twawaf ni kama Swalaah katika kila kitu mpaka ishurutishiwe masharti yanayohusiana na Swalaah. [Tazama katika Majmu'u Al-Fataawaa (26/198) na Jaami'u Ahkaamin Nisaai (2/522). Ndani yake kuna tofauti 11 kati ya Swalaah na twawaf].
Si hivyo tu, bali Swalaah ya kisharia ambayo sharti yake ni utwahara na mfano wake, ni ile inayofunguliwa kwa takbiyr na kumalizwa kwa tasliym.
Na kwa ajili hiyo, Shaykh wa Uislamu amesema: " Imenidhihirikia kwamba kujitwaharisha na hadathi, - bila shaka yoyote - hakushurutishwi katika twawaf na wala si wajibu. Lakini twahara ndogo (wudhuu) imesuniwa katika twawaf, kwani dalili za kisharia zinaonyesha kuwa si wajibu, na hakuna katika sharia lenye kuthibitisha wajibu wa kutawadha katika twawaf." [Majmu'u Al-Fataawaa (26/298)].
Abu Muhammad Ibn Hazm amekubaliana na hili. [Al-Muhalla (7/179)].
Kugusa Mswahafu:
Maalik, Ash-Shaafiiy, Ahmad na Jamhuri ya Maulamaa, wanaona kwamba haijuzu kwa mwenye hadathi kugusa Mswahafu. [Al-Majmu'u (1/17), Al-Istidhkaar (8/10), Al-Mughniy (1/147) na Al-Awsatw (2/102)].
Kigezo cha ushahidi wao ni mambo mawili:
1- Neno Lake Allaah Mtukufu:
((لَا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ))
(( Hapana akigusaye ila waliotakaswa)). [Al-Waaqi'ah (56: 79)].
2- Hadiyth ya Amri bin Hazm kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaandikia watu wa Yemen barua. Kati ya yaliyoandikwa ni:
((لا يمس القرآن إلا طاهر))
((Asiiguse Qur-aan isipokuwa aliye twahara)). [Hadiyth Dhwaíyf: Ina Sanad Dhwa’iyf na baadhi yake ni karatasi tu zisizo na Sanad yoyote. Maulamaa wametofautiana katika kuipandisha ifikie ngazi ya Hadiyth Hasan. Lakini Al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika kitabu cha Al-Irwaa (1/158). Lililo wazi zaidi ni kuwa Hadiyth hii haipandi. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi].
Ninasema: "Waliyoyatolea ushahidi yanajibiwa kwa yafuatayo:
1- Haiwezekani kuitolea dalili Aayah hiyo Tukufu isipokuwa kama kiwakilishi kilichopo katika (يمسه) kitarejeshwa kwa Qur-aan. Na kauli dhahiri iliyoshikiliwa na wafasiri wengi ni kuwa kiwakilishi hicho kinarejea kwa Kitabu kilichohifadhiwa huko mbinguni; nacho ni "Al-Lawh Al-Mahfuwdh". Na waliotwaharika ni Malaika. Na hili linaonyeshwa kutokana na muundo wa Aayah Tukufu:
إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ ﴿٧٧﴾
Hakika hii bila shaka ni Qur-aan tukufu.
فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ ﴿٧٨﴾
Katika Kitabu kilichohifadhiwa.
لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ ﴿٧٩﴾
Haigusi isipokuwa waliotakaswa kabisa. [Al-Waaqi'ah (56: 77-79)].
Na hili linatiliwa nguvu na Neno Lake Subhaanah:
فِي صُحُفٍ مُّكَرَّمَةٍ ﴿١٣﴾
Katika Sahifa zenye kuadhimishwa.
مَّرْفُوعَةٍ مُّطَهَّرَةٍ ﴿١٤﴾
Zimetukuzwa na zimetakaswa.
بِأَيْدِي سَفَرَةٍ ﴿١٥﴾
Katika mikono ya Malaika waandishi.
كِرَامٍ بَرَرَةٍ ﴿١٦﴾
Watukufu, watiifu. ['Abasa (80 : 13-16)].
2- Ama Hadiyth, basi ni Dhwa’iyf na haifai kutolewa dalili, kwa vile imetokana na nyaraka zisizosikika mbali na kuwepo mvutano mkali kuhusu wapokezi wake.
Ama kama tukijaalia kuwa Hadiyth hii ni Swahiyh na kwamba kiwakilishi kinarejea kwa Qur-aan, basi tunasema:
"Kilichotwahara" ni katika visawe vya kilafudhi. Inaweza kuwa kwa maana ya Muumini, au kwa maana ya mtu aliyejitwaharisha na hadathi kubwa, au kwa maana ya mtu aliyejitwaharisha na hadathi ndogo, au kwa maana ya mtu ambaye hana najsi katika mwili wake. Hivyo suala inabidi lirejeshwe katika taaluma ya fani ya "Uswuul" isemayo:
"Mwenye kujuzisha kukichukulia kisawe cha kilafudhi kwa maana zake zote, basi maana hizo atazichukulia hapa. Lakini kwa vile haijuzu kutumia jina la najsi kwa Muumini asiye na wudhuu au mwenye janaba sawasawa ikiwa ni kweli anayo najsi hiyo, au kimajazi, au kilugha kwa kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((المؤمن لا ينجس))
((Muumini hawi najsi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (279) na Muslim (371)]…….mbali na kuthibiti kuwa Muumini daima ni twahara, basi haiwezekani Aayah au Hadiyth kuitumia maana hiyo. Hivyo basi, inalazimu kulichukulia tamshi kwa asiye mushriki kama Alivyosema Allaah Mtukufu:
((إنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَس))
((Hakika washirikina ni najsi)). [At-Tawbah (9 : 28)].
Na kwa Hadiyth iliyokataza kusafiri na Qur-aan kwenda nayo katika nchi ya adui.
Na mwenye kusema kuwa kisawe tamshi kimekusanya maana zote, kwa hivyo hakiwezi kutumiwa mpaka ibainishwe, atajibiwa kuwa hakuna hoja katika Aayah wala Hadiyth na hata kama jina la "aliyetwaharika" litakuwa na maana ya mtu asiye na hadathi ndogo au kubwa. [Limezungumziwa katika Nayl Al- Awtwaar (1/260)].
Kwa hivyo, imejulikana kuwa hakuna dalili yoyote inayoashiria kuwa ni lazima kutawadha kwa ajili ya kugusa Msahafu. Na haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Daawuud na Ibn Hazm. Na ndivyo hivyo hivyo alivyosema Ibn 'Abbaas na kikundi cha watangu wema. Pia Ibn Al-Mundhir yupo katika mkondo huo huo. [Al-Badaai-'i (1/33), Haashiyat Ibn 'Aaabidiyn (1/173), Al-Muhalla (1/81) na Al-Awsatw (2/103)].
Faida
Hakuna ubaya kusoma Qur-aan kwa mwenye hadathi ndogo au hadathi kubwa bila kugusa Msahafu kwa mujibu wa kauli za Maulamaa zenye nguvu. Suala la kusoma Qur-aan ni jepesi zaidi hapa kuliko suala la kugusa Msahafu kwa mambo yafuatayo:
1- Hakuna Hadiyth yoyote Marfu’u ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayokataza kusoma. Kila Hadiyth iliyopokelewa ni dhwa’iyf na haina hoja yoyote. Ni kama Hadiyth Marfu’u ya ‘Abdullah bin 'Amr:
((لا يقرأ الجنب ولا الحائض شيئا من القرآن))
((Mwenye janaba au hedhi asisome chochote katika Qur-aan)).
Na Hadiyth ya Ibn Rawaaha:
((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza yeyote kati yetu kusoma Qur-aan akiwa na janaba)).
Na Hadiyth ya ‘Abdullahi bin Maalik:
((إذا توضأت وأنا جنب أكلت وشربت، ولا أصلي ولا أقرأ حتى أغتسل))
"Ninapotawadha nami nina janaba, ninakula na kunywa, lakini siswali wala sisomi mpaka nioge".
Hadiyth zote hizi si Swahiyh. [Zitazame katika Al-Irwaa (192, 485) cha Mwanachuoni Mkubwa Al-Albaaniy na maelezo ya Shaykh Mash-huwr katika Al-Khilaafiyyaat cha Al-Bayhaqiy (2/11). Basi ni vizuri yapitiwe].
2- Imethibiti kutoka kwa 'Aaishah kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimdhukuru Allaah Mtukufu katika nyakati zake zote. [Hadiyth Swahiyh Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (373), na imetolewa maelezo na Al-Bukhaariy kabla ya Hadiyth ya (608)].
3- Ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamuru wanawake wenye hedhi kutoka siku ya ‘Iyd waketi nyuma ya watu na wafuatilize takbiri zao na du’aa zao. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (971) na Muslim (890)].
Kwa hiyo, hii inaonyesha kuwa mwenye hedhi hupiga takbiyr na humdhukuru Allaah Mtukufu.
4- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia 'Aaishah wakati alipokuwa na hedhi:
((إفعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت))
((Fanya yote ayafanyayo mwenye kuhiji isipokuwa tu usizunguke Ka’abah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1650)].
Inajulikana kwamba mwenye kuhiji humdhukuru Allaah na husoma Qur-aan.
Na kwa vielelezo hivi, inafahamika kuwa mwenye hadathi hazuiliwi kusoma Qur-aan. Shaykh wa Uislamu anasema: "Haya ndiyo madhehebu ya Abu Haniyfah na ndio madhehebu mashuhuri ya Ash-Shaafi'iy na Ahmad". [Majmuu Al-Fataawaa (21/459) na Al-Awsatw (2/97)].