034-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Mambo Ambayo Mtu Akiyafanya Imesuniwa Awe Na Wudhuu
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
34-Mambo Ambayo Mtu Akiyafanya Imesuniwa Awe Na Wudhuu
1- Wakati wa kumdhukuru Allaah Mtukufu
Hapa unaingia uradi wowote, kusoma Qur-aan, kutufu Al Ka’abah na mengineyo.
Wudhuu umesuniwa kwa hayo kutokana na Hadiyth ya Al-Muhaajir bin Qunfudh kwamba yeye alimsalimia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anatawadha, naye hakumjibu mpaka alipomaliza. Kisha akamwambia:
((إنه لم يمنعني أن أرد عليك إلا أني كرهت أن أذكر الله إلا على طهارة))
((Hakika hakuna kilichonizuilia kukujibu isipokuwa tu niliona uzito kumdhukuru Allaah mpaka niwe katika twahara)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (17), An-Nasaaiy (1/16), Ibn Maajah (350), Ad-daaramiy (2/287) na Ahmad (5/80). Ni Hadiyth Swahiyh kama ilivyo katika As-Silsilat As-Swahiyhah (834)].
Lakini, Hadiyth hii haiambatani na Hadiyth ya 'Aaishah iliyosajiliwa na Muslim (4/68) isemayo:
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimtaja Allaah katika nyakati zake zote.
2- Wakati wa kulala
Imepokelewa toka kwa Al-Barraa bin 'Aazib Allaah Amridhie, amesema: " Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((إذا أتيت مضجعك فتوضأ وضوئك للصلاة، ثم اضطجع على شقك الأيمن، ثم قل: اللهم أسلمت نفسي إليك...))
((Unapotaka kulala, basi tawadha wudhuu wako wa Swalaah, kisha lala kwa ubavu wako wa kulia, halafu sema: Ee Allaah! Nimeisalimisha nafsi yangu Kwako)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (247), Muslim (2710) na wengineo].
3- Kwa mwenye janaba kama akitaka kula, au kunywa, au kulala, au kumwingilia tena mkewe
Imepokelewa toka kwa 'Aaishah Allaah Amridhie, amesema: "Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapokuwa na janaba na akataka kula au kulala, alikuwa akitawadha wudhuu wa Swalaah". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (288), Muslim (305) na tamko ni lake, Abuu Daawuud (222), At-Tirmidhiy (118), An-Nasaaiy (1/138) na wengineo].
Na imepokelewa na Abuu Sa'iyd Allaah Amridhie toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((إذا أتى أحدكم أهله ثم أراد أن يعود فليتوضأ))
((Anapomwingilia mmoja wenu mkewe kisha akataka kurejea tena, basi atawadhe)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (3/217), Abu Daawuud (217), At-Tirmidhiy (141) na An-Nasaaiy (1/42)].
4- Kabla ya kuoga
Imepokelewa na 'Aaishah Allaah Amridhie, amesema: "Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akioga janaba, huanza kwa kuosha mikono yake, kisha humimina maji katika mkono wake wa kushoto kwa kutumia mkono wa kulia na kuosha utupu wake, kisha hutawadha wudhuu wake wa Swalaah".[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (248), Muslim (316) na wengineo].
5- Baada ya kula kilichopikwa kwa moto
Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((توضأوا مما مست النار))
((Tawadheni kwa (kula) kilichopikwa kwa moto)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (351), Abuu Daawuud (192), At-Tirmidhiy (79), An-Nasaaiy (1/105) na Ibn Maajah (485)].
Amri hapa ni ya kupendezeshea kutokana na Hadiyth ya 'Amri bin Umayyah Adh-Dhamriy aliyesema: "Nilimwona Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akilikata bega la kondoo, akala sehemu, kisha akaitwa kwenda kuswali, akasimama, akakitupa kisu, akaswali na wala hakutawadha". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1/50), Muslim (4/45 An-Nawawiy) na Ibn Maajah (490)].
6- Kujadidisha wudhuu kwa kila Swalaah
Ni kwa Hadiyth ya Buraydah Allaah Amridhie, amesema: "Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitawadha wakati wa kila Swalaah. Na ilipokuwa siku ya Al Fat-h, alitawadha, akapukusa juu ya khufu zake, akaswali Swalaah nyingi kwa wudhuu mmoja.." Hadiyth. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (277), Abuu Daawuud (171), At-Tirmidhiy (61), An-Nasaaiy (1/89) na Ibn Maajah (510)].
7- Kila pale wudhuu unapotenguka
Ni kutokana na Hadiyth ya Bilal iliyotajwa nyumba ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisikia mchakato wa viatu vyake mbele yake peponi. Akamwambia:
((بم سبقتني إليها))
((Ni kwa jambo gani umenitangulia kuelekea huko))?
Akasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Kamwe sikuadhini ila niliswali rakaa mbili, na wala kamwe sikupata hadathi ila nilitawadha".
Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((لهذا))
((Ni kwa hili)). [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy alipotaja wudhuu wakati wa hadathi (3689), Abuu Daawuud (3055), Ahmad (21962) na tamko ni lake. Asili yake ni katika Swahiyh Mbili bila ya sehemu ya ushahidi].
8- Kwa kutapika
Ni kwa Hadiyth ya Mu'daan bin ‘Abi Twalha toka kwa Abu Ad-Dardaai kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua, kisha akatawadha. Kisha alikutana na Thawbaan katika Msikiti wa Damascus akalitaja hilo kwake na Thawbaan akamwambia: "Amesema kweli, na mimi ndiye niliyemmiminia maji yake ya kutawadhia". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (87) na Abuu Daawuud (2381) kwa Sanad Swahiyh].