065-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Ikiwa Kuna Maiti, Mwenye Janaba, Mwenye Hedhi na Mwenye Najsi Mwilini, Na Maji Yaliyopo Hayatoshi Ila Kwa Mmoja Wao Tu, Nani Atapewa Kipaumbele?
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Twahara
065-Ikiwa Kuna Maiti, Mwenye Janaba, Mwenye Hedhi na Mwenye Najsi Mwilini, Na Maji Yaliyopo Hayatoshi Ila Kwa Mmoja Wao Tu, Nani Atapewa Kipaumbele?
1- Ikiwa maji ni milki ya mmoja wao, basi atakuwa yeye ndiye mwenye haki nayo zaidi. Hili ndilo lililopitishwa na Jamhuri. [Al-Majmu’u (2/316) na Al-Mughniy (1/170)].
2- Ikiwa hayamilikiwi na yeyote kati yao, basi hukmu ni kama ifuatavyo:
(a) Maiti ana haki zaidi kuliko hao wenye hadathi kama walivyosema Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Majmu’u (2/318) na Al-Mughniy (1/170)].Hii ni kwa sababu mbili:
Sababu ya kwanza ni kuwa huu ndio mwisho wa maiti. Kwa ajili hiyo, amehusishwa na twahara timilifu zaidi kati ya mbili. Walio hai kwa hali yoyote, watayapata maji baadaye.
Sababu ya pili ni kuwa makusudio ya kumwosha maiti ni kumsafisha, na hili haliwezekaniki kwa mchanga, wakati ambapo makusudio ya kujitwaharisha kwa walio hai ni kupata idhini ya kuswali, na hili linapatikana kwa kutayamamu.
(b) Mwenye najsi ndiye mwenye haki zaidi ya maji kuliko wenye hadathi. Wameyasema haya Mashaafi’iy na Mahanbali. [Al-Mughniy (1/171) na Al-Majmu’u (2/319)]
An-Nawawiy amesema: “Kwa sababu hakuna badali ya twahara yake”.
(c) Mwenye hedhi ana haki zaidi kuliko mwenye janaba. Hii ni kutokana na uzito wa hadathi yake, na kwa kuwa yeye anaitekeleza haki ya Allaah Mtukufu na haki ya mumewe ya kuruhusika kumwingilia.
Katika suala hili kuna mvutano. Kwa Mahanbali na Mashaafi’iy kuna njia mbili. Na kwa Mashaafi’iy kuna njia ya tatu, nayo ni kuwa wako sawasawa na watapiga kura. [Al-Mughniy (1/171) na Al-Majmu’u (2/319)]
(d) Akikusanyika mwenye janaba na mwenye hadathi, maji yaliyopo yatatizamwa. Ikiwa yatatosha kuogea janaba, basi mwenye janaba atakuwa na haki zaidi. Na kama hayatoshi, basi mwenye hadathi. [Yaliyotangulia].
(e) Akikusanyika maiti na mwenye najsi mwilini, hapa kuna mvutano. [Al-Mughniy (1/170) na Al-Majmu’u (2/318)]
Atakayekubaliana na sababu tuliyoitaja ya kumtanguliza maiti kabla ya mwenye hadathi, basi maji ni haki ya maiti.
Na atakayekinaika kuwa mwenye najsi mwilini hana badali nyingine ya kutwaharika, basi atakuwa ndiye mwenye haki zaidi.