066-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kutayammamu Mgonjwa Ambaye Anajihofia Madhara Kama Atatumia Maji

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

066-Kutayammamu Mgonjwa Ambaye Anajihofia Madhara Kama Atatumia Maji

 

 

Jamhuri ya Maulamaa (Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Ibn Hazm na wengineo), wanaona kuwa ikiwa mgonjwa atajihofia nafsi yake kuhiliki ikiwa atatumia maji, basi inajuzu kwake kutayamamu kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((وإن كنتم مرضى أو على سفر.....فلم تجدوا ماء فتيمموا))

((Na mkiwa wagonjwa au safarini……na hamkupata maji, basi tayamamuni)). [Al-Maaidah (5:6)].

 

Amesema Mujaahid: “Hii ni kwa mgonjwa aliyepatwa na janaba. Akijihofia nafsi yake, basi ana ruhusa ya kutayamamu kama msafiri anapokosa maji”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Raazik kwa Sanad Swahiyh]. Na kwa Neno Lake Allaah Mtukufu:

((ولا تقتلوا أنفسكم))

((Na wala msiziue nafsi zenu)).[An-Nisaai (4:29)].

 

Hii ni katika wakati ambapo ‘Atwaa na Al-Hasan wamekataza mgonjwa kutayamamu isipokuwa katika hali ya kukosekana maji tu kutokana na Aayah inavyosema. [‘Abdul Raazik amelipokea hili katika Al-Muswannaf (861) kwa Sanad Swahiyh].

 

Na jibu la hili ni kuwa Aayah ni hoja ya kutupa sisi nguvu, na taqdiyr yake ni:

((Mkiwa wagonjwa; mkashindwa au mkahofia kutumia maji, au mkawa safarini na hamkupata maji, basi tayamamuni)).  [Al-Majmu’u (2/330)].

 

Mgonjwa Akihofia Kuzidi Ugonjwa Wake Au Kukawia Kupona Kwa Kutumia Maji, Je Atatayammamu?

 

Jamhuri ya Maulamaa (Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy katika moja ya kauli zake mbili na Ibn Hazm), wanaona kwamba si lazima mgonjwa ahofie kuhiliki ndipo atayamamu, bali hata yule ambaye wudhuu unamwongezea ugonjwa au unachelewesha kupona, basi atayamamu kutokana na ujumuishi wa Aayah ya Suwrat Al-Maaidah. [Al-Mabsuwtw (1/121), Al-Majmu’u (2/331), Al-Muhalla (2/116), Al-Awsatw (2/26) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/399)].

 

Na pia kutokana na Kauli Yake Allaah Mtukufu:

((يريد الله بكم اليسر ولا يريد منكم العسر))

((Allaah Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito)). [Al-Baqarah (2:185)]

 

Ibn Hazm amesema: “Dhiki na uzito vimeondoka (na Sifa zote njema ni za Allaah) sawasawa ikiwa ugonjwa utazidi au haukuzidi. Kadhalika, ikiwa atahofia kuzidi ugonjwa, basi hilo ni uzito na dhiki vilevile”.

 

Na imepokelewa toka kwa Ahmad na Ash-Shaafiiy katika moja ya kauli zake mbili kwamba ili kuruhusika kutayamamu, ni lazima iwepo hofu ya kudhurika. Na madhehebu ya Jamhuri ndio sahihi zaidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share