074-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Namna Sahihi Ya Kutayammamu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

074-Namna Sahihi Ya Kutayammamu

 

Alhidaaya.com

 

 

Namna sahihi ya kutayamamu iliyokuja kwa njia sahihi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni:

 

Atapiga mtu pigo moja kwenye mchanga kwa mikono miwili, kisha ataipuliza, halafu atajipukusa kwayo uso wake na vitanga vyake viwili.

 

Haya ni madhehebu ya Mahanbali na Ibn Hazm. Na ndivyo walivyosema baadhi ya Masalafu, na Ibn Taymiyyah amelikhitari.  [Al-Mughniy (1/159), Al-Muhallaa (1/146) na Al-Fataawaa (21/422)].

 

Dalili ya hili ni:

 

1-Hadiyth iliyoelezewa na ‘Ammaar bin Yaasir akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ilikuwa inakutosha kufanya hivi”. Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapiga ardhi kwa vitanga vyake, akavipuliza, kisha akapukusa kwavyo uso wake na viganja vyake[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (338) na Muslim (798).

 

2-Hadiyth ya Abuu Hurayrah aliposema: “Ilipoteremka Aayah ya tayamumi, sikujua namna ya kutayamamu. Nikamwendea Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini sikumkuta. Nikaondoka kumtafuta nikamwona nikamwelekea. Aliponiona alilijua lililonileta, akaenda haja ndogo, kisha akapiga mikono yake chini, akapukusa kwayo uso wake na viganja vyake”. [Isnadi yake ni laini. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/159). Hadiyth iliyotangulia inaitilia nguvu].

 

Na kwa upande mwingine, kundi jingine la Maulamaa linaona kwamba tayamumi ni mapigo mawili: Pigo moja la uso, na pigo jingine la mikono miwili mpaka kwenye viwiko viwili. Haya ni madhehebu ya Hanafiy, Maalik na Ash Shaafi’iy. Ath-Thawriy na Al-Layth wamesema hivi, nalo limepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar. Wengine ni Ash-Sha’abiy, Al-Hasan Al-Baswriy na wengineo. [Al-Mabsuwtw (1/106), Al-Istidhkaar (3/162) na Al-Majmu’u (2/242)].

 

Hoja zao ni:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((Tayamumi ni mapigo mawili: Pigo la uso, na pigo la mikono miwili hadi kwenye viwiko viwili)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/179) na Al-Bayhaqiy (1/207)].

 

2- Hadiyth ya Ibn ‘Umar kuhusiana na kisa cha mtu aliyepita kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa ameshughulika, akamsalimia. Ibn ‘Umar anasema: “Alipiga mikono yake miwili ukutani, akapangusa kwayo uso wake, kisha akapiga pigo jingine, akapukusa mikono yake miwili, kisha akaijibu salamu ya mtu yule”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1/88) na Al-Bayhaqiy (1/207). Imaam Ahmad ameikataa].

 

3- Yaliyoelezewa na Abuu Juhaym aliposema: “Akasimama mbele ya ukuta, akaukwangua kwa fimbo aliyokuwa nayo, kisha akaweka mikono yake ukutani, halafu akapukusa uso wake na mikono yake, kisha akanijibu salamu”[Hadiyth Munkari: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash Shaafi’iy katika musnadi yake (130) na Al-Bayhaqiy (1/205). Imekhalifiana na riwaya ya Swahiyh Mbili iliyotangulia].

 

4-Hadiyth ya ‘Ammaar isemayo kwamba alieleza kuwa walijipangusa kwa mchanga kwa ajili ya kuswali Salatul Fajr wakiwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wakaupiga mchanga kwa viganja vyao mara nyingine tena, wakajipangusa kwa mikono yao yote hadi kwenye mabega na makwapa kwa matumbo ya viganja vyao. [Hadiyth Mudhtwarib: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1/84), Ibn Maajah (571), An Nasaaiy (1/168) na Al-Bayhaqiy (1/208)].

 

Ninasema: “Lenye nguvu ni kuwa tayamumi ni pigo moja tu kwa uso na mikono miwili hadi kwenye viwiko viwili kama tulivyotangulia kusema. Na hii ni kwa mambo mawili:

 

1-Dalili zote za wenye kukhalifiana na hilo ni dhwa’iyf. Hawana hata Hadiyth moja Marfu’u.

 

2-Hukmu ya tayamumi inafungamana na mikono miwili basi, dhiraa haiingii. Ni kama kuukata mkono wa mwizi. Hili linaashiriwa na kuhoji Ibn ‘Abbaas kuhusiana na kuainisha sehemu ya kukatwa mkono iliyoelezewa kwenye Aayah kwa mwizi kwa Neno Lake Allaah kuhusiana na tayamumi:

(( فامسحوا بوجوهكم وأيديكم منه))

((Basi pakeni nyuso zenu na mikono yenu kwa mchanga huo)). [Al-Maaidah (5:6)].

 

Na ukataji kwa mujibu wa Sunnah, ni viganja viwili.

 

Yanayotengua Tayammumi

 

Hadathi yoyote inayotengua wudhuu, hutengua tayamumi. Hili halina mvutano wowote kati ya Maulamaa. [Al-Muhallaa cha Ibn Hazm (2/122)].

 

 

Share