075-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Masuala Mbalimbali Kuhusu Tayammumi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

075-Masuala Mbalimbali Kuhusu Tayammumi

 

Alhidaaya.com

 

 

·       

Je, inaswihi kuswali kwa tayamumi endapo maji yatapatikana kabla ya kuanza kuswali?

 

Ibn ‘Abdul Barri amesema: “Maulamaa wote wanakubaliana kwamba mwenye kutayamamu baada ya kukosa maji, kisha akayapata maji kabla hajaanza kuswali, basi tayamumi yake hubatilika, na hawezi kuswali kwa tayamumi hiyo, bali hurejea katika hali yake ya kabla ya kutayamamu”. [Al-Istidhkaar (3/167)]

 

·       

Mtu ametayamamu akaanza kuswali, kisha maji yakapatikana kabla hajamaliza Swalaah yake, je ataikamilisha Swalaah au ataivunja?

 

Maulamaa wamehitilafiana katika suala hili kwa kauli mbili:

 

Ya kwanza: Atalazimika kuivunja Swalaah ili ayatumie maji, kisha aanze tena Swalaah upya.

Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah na Ahmad. Hivyo hivyo kasema Ath-Thawriy na Ibn Hazm. [Al-Mabsuwtw (1/120), Al-Mughniy (1/167), Al-Istidhkaar (3/170), na Al-Muhallaa (2/126)].

 

Hoja zao ni:

 

1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( الصعيد الطيب وضوء المسلم، وإن لم يجد الماء عشر سنين، فإذا وجدت الماء فأمسه جلدك))

((Mchanga safi ni wudhuu kwa Muislamu hata kama hakupata maji miaka kumi. Ukiyapata maji, basi yagusishe ngozi yako)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Wamekhitilafiana katika kuifanya Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhy (124), Abuu Daawuud (329) na An-Nasaaiy (1/171). Tumeitaja katika mlango wa kuoga].

 

Wamesema: Hii ni kwa mwenye kuyapata maji.

 

2- Kwa vile ameweza kuyatumia maji, basi tayamumi yake hubatilika na kuwa kana kwamba yuko nje ya Swalaah.

 

3-Kwa vile tayamumi ni twahara ya dharura, hubatilika kwa kuondoka dharura. Ni kama twahara ya mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah inapokatika damu yake.

 

Ya pili: Ataikamilisha Swalaah yake mpaka mwisho

Haya ni madhehebu ya Maalik na Ash Shaafi’iy, na riwaya ya pili toka kwa Ahmad lakini inasemekana kwamba aliachana nayo. Hivyo hivyo kasema Abuu Thawr, Daawuud na Ibn Al-Mundhir. [Al-Istidhkaar (3/169), Al-Majmu’u (2/357) na Al-Awsatw (2/65)].

 

Hoja zao ni:

1-Neno Lake Allaah Subhaanahu wa Taalaa:

(( ولا تبطلوا أعمالكم))

((Wala msizibatilishe amali zenu)). [Muhammad (47:33)].

 

Wanasema: Haijuzu kuivunja Swalaah kwa ajili ya hilo.

 

2-Twahara ina wakati wake, na Swalaah ina wakati wake. Na mtu baada ya kuingia kwenye Swalaah, anakuwa wakati huo haswali kwa ufaradhi wa twahara. Kwani yeye ametayamamu kama alivyoamrishwa, na kwa kupiga takbiyr, anakuwa ashatoka nje ya wigo wa faradhi ya twahara. Na hapo inakuwa haijuzu tena kuivunja twahara hiyo ambayo muda wake ushapita, au kuvunja rakaa ambazo ameshaziswali kama alivyofaradhishiwa. Na suala hili haliwezi kufanyika ila kwa dalili kutoka kwenye Qur-aan, au Sunnah, au Ijma’a.

 

Ninasema:

“Ninaloliona lenye nguvu zaidi ni kuwa mtu ataendelea kukamilisha Swalaah yake, kwa vile hakujathibiti lolote lenye kulazimisha kuikata Swalaah baada ya kuianza. Hii ni kama mfano wa mtu anayefunga Swaum ya kafara. Ikiwa ameanza Swaum yake kisha akapata mtumwa wa kumwacha huru, basi hatoivunja Swaum yake. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi."

 

·       

Ikiwa mtu ameswali kwa kutayamamu, kisha maji yakapatikana kabla ya wakati wa Swalaah kumalizika, je ataswali tena?

 

Huyu hatorejesha tena Swalaah yake kwa mujibu wa kauli mbili sahihi za Maulamaa. Haya ni madhehebu ya Maalik, Ath-Thawriy, Al-Awzaaiy, Al-Mazniy, Atw-Twahaawiy na Ahmad katika moja ya riwaya mbili. Hivi hivi kasema Ibn Hazm. [Angalia Al-Majmu’u (2/353) na Al-Muhallaa (2/139)].

 

Lakini Abuu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy, wao wanasema kwamba ni lazima ailipe upya Swalaah yake wakati anapoyapata maji. [Al-Majmu’u (2/353)].

 

Ibn Hazm amewajibu akisema: “Ama kauli ya Abuu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy, ni wazi kwamba imedoda, kwa kuwa kumwamuru kwao mtu atayamamu na aswali, hakukosekani na; ima wao wamemwamuru kuswali Swalaah ambayo ni faradhi ya Allaah juu yake, au Swalaah ambayo Allaah Hakumfaradhishia, na hakuna la tatu hapo. Na ikiwa mwenye kuwafuata atasema: Wamemwamuru Swalaah ambayo ni faradhi juu yake, tutamwambia: Kwa nini basi aiswali tena baada ya wakati wake ikiwa alitekeleza faradhi yake? Na ikiwa atasema: Bali wamemwamuru Swalaah ambayo si faradhi juu yake, hapo atakuwa amekiri kwamba wao wamemlazimisha jambo lisilo lazima kwake, na hili ni kosa”.

 

Ninasema:

“Ndio. Si lazima kuswali tena. Lakini ni vizuri kuswali tena madhali muda upo na maji yamepatikana. Na hii ni kwa Hadiyth ya Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy aliyesema:

“Watu wawili walitoka kwenda safari. Ukawakuta wakati wa Swalaah na wao hawana maji. Wakatayamamu kwa mchanga kisha wakaswali. Halafu baadaye walipata maji kabla wakati haujatoka. Mmoja wao akatawadha na kuswali tena, lakini mwingine hakufanya. Halafu walikwenda kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakamweleza walilolifanya. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia yule ambaye hakuswali tena:

(( أصبت السنة وأجزأتك صلاتك))

((Umeipata Sunnah, na Swalaah yako imekutosheleza)).

Kisha akamwambia yule aliyetawadha na kuswali tena:

(( لك الأجر مرتين))

((Una ajri mara mbili)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (334) na An-Nasaaiy (1/213)].

 

 

Share