011-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Pili: Iqaamah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
011-Pili: Iqaamah
· Taarifu Yake:
Tumeshasema nyuma kwamba iqaamah maana yake ni kujulisha watu wasimame kuswali kwa matamshi yaliyopokelewa na kwa sifa mahsusi.
· Sifa Za Iqaamah
Sifa za iqaamah kama ilivyothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni namna mbili:
Ya kwanza: Ni sentensi 11
(( الله أكبر الله أكبر، أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله، حي على الصلاة، حي على الفلاح، قد قامت الصلاة، قد قامت الصلاة، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله ))
Aina hii ndiyo iliyokuja katika Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Zayd tuliyoielezea katika adhana. Hadiyth hii inaongezewa uzito na yaliyothibiti toka kwa Anas aliyesema:
“Bilaal aliamuriwa afanye shufwa katika adhana, na witri katika iqaamah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (605) na Muslim (378)].
Na kwa vile Bilaal alikuwa akiadhini kwa namna alivyofundishwa na ‘Abdullah bin Zayd, Jamhuri ya Maulamaa wa salaf na khalaf wamekwenda juu ya msingi huo huo.
Ya pili: Ni sentensi 17
(( الله أكبر (X4)، أشهد أن لا إله إلا الله(X2) ، أشهد أن محمدا رسول الله (X2) ، حي على الصلاة (X2) ، حي على الفلاح (X2) ، قد قامت الصلاة (X2) ، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله ))
Namna hii imethibiti katika Hadiyth ya Abuu Mahdhuurah iliyoelezewa kwenye adhana.
Mwenye kuamua kujiwajibishia Hadiyth ya Ibn Zayd katika adhana, ni lazima katika iqaamah atumie namna ya kwanza, na mwenye kujiwajibishia Hadiyth ya Abuu Hudhayfah, ni lazima atumie namna ya pili. Ama mwenye kuchagua yoyote, basi atafanya hivyo hivyo kwenye iqaamah, nalo ndilo bora zaidi, na Allaaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
· Je, Ni Lazima Aqimu Aliyeadhini?
Ni bora aliyeadhini aqimu, kwa kuwa Bilaal (Radhwiya Allaahu Anhu), alikuwa ndiye mwenye kuadhini na kuqimu kama itakavyokuja. Msimamo huu ndio walionao Maulamaa wengi. Lakini kama ataadhini mtu, akaqimu mwingine, basi itajuzu.
Ama Hadiyth Marfu’u ya Zayd Asw-Swadaaiy: “Anaqimu Akhu Asw-Swadaaiy, kwani mwenye kuadhini, ndiye mwenye kuqimu”. [Hadiyth hii si Swahiyh, ni Dhwa’iyf Angalia Adh-Dhwa’iyfah (35) na Al-Irwaa (237)]
Pia Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd kwamba yeye aliqimu baada ya Bilaal kuadhini ni Dhwa’iyf. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (499) na Ahmad (4/43)]
· Je, Mtu Atamjibisha Mwenye Kuqimu?
Kisharia, mwenye kusikia iqaamah, anatakikana aseme kama anavyosema mwenye kuqimu kutokana na ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mkisikia wito, basi semeni kama anavyosema mwadhini)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni].
Iqaamah ni wito na adhana pia. Ni kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((Kati ya kila adhana mbili ni Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Itakuja kwenye mlango wa Swalaah za Sunnah].
Yaani adhana na iqaamah.
Imesemwa: Hakuna kujibisha ila katika adhana.
Ninasema: “La kwanza ndilo lenye nguvu zaidi, na suala lina wasaa”.
· Mwenye Kuqimu Akisema: “Qad Qaamatis Swalaah, Qad Qaamatis Swalaah”, Nini Mtu Atajibu?
Sunnah, ajibu kama alivyosikia “Qad Qaamatis Swalaah, Qad Qaamatis Swalaah” kutokana na ujumuishi wa Hadiyth iliyotangulia. Ama yanayosimuliwa kwamba mtu aseme: Aqaamahal Laahu wa Adaamahaa”, hayo hayapo. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (528). Angalia Al-Irwaa (241)]
· Ni Upi Wakti Wa Kuqimu Swalaah?
1- Kiasili, inatakiwa asiqimu mpaka amwone imamu. Imepokelewa toka kwa Jaabir bin Samrah (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “Bilaal alikuwa anaadhini jua linapopinduka, haqimu Swalaah mpaka Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) atoke. Anapotoka huqimu Swalaah anapomwona”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (606). Ishatajwa].
2- Wakati mwingine inafaa kuqimu kabla imamu hajatoka kama atamwona kwa mbali, au akajua kwamba karibu atatoka. Ni kama ilivyo katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah inayosema: “Swalaah ilikuwa ikiqimiwa kwa Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam, na watu huanza kujipanga safu kabla Rasuli Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam hajasimama mahala pake”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (605)].
· Ni Wakti Gani Watu Husimama Kwa Swalaah?
1- Kama imamu hayuko nao Msikitini, ni Sunnah kwao wasisimame mpaka wamwone, sawasawa ikiwa mwadhini ameqimu au hajaqimu. Na hii ni kauli ya Jamhuri kutokana na Hadiyth ya Abuu Qataadah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Ikiqimiwa Swalaah, msisimame mpaka mnione)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (637) na Muslim (604)].
2- Kama imamu yuko nao Msikitini, Ash-Shaafi’iy na wengineo wengi, wanaona kwamba watu wasisimame mpaka iqaamah imalizike. Maalik anasema wasimame anapoanza kuqimu. Ahmad anasema wasimame wakati mwenye kuqimu anaposema: “Qad qaamatis Swalaah”. Na Abuu Haniyfah anasema wasimame anaposema: “Hayya alas Swalaah”. [Sharhu Muslim cha An-Nawawy (3/840)]
Ninasema: “Ninaloliona mimi ni kuwa watu wasimame wanapomwona imamu ashasimama, kwa kuwa kusimama imamu mahala pake ni sawa na kutoka kwa wenye kuswali. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msisimame mpaka mnione)). Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”
· Tanbihi
Baadhi ya Mashekhe wetu wa enzi ya leo, wanasema kwamba si sharia kuqimu Swalaah kwa kutumia kipaza sauti ili walioko nje ya Msikiti waisikie!! Kauli hii imenasibishwa kwa Al-‘Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahul Laah).
Ninasema: “Huenda kiegemeo cha kauli hii ni kuwa makusudio ya iqaamah ni kujulisha kuingia kwenye Swalaah na kuihirimia, na si kujulisha kuingia wakati wa Swalaah ili kujitayarisha nayo na kuiitia kama ilivyo kwenye adhana. Pamoja na hivyo, hakuna kinachozuia kuwasikilizisha iqaamah waliopo nje ya Msikiti. Imethibiti kwamba Ibn ‘Umar alisikia iqaamah akiwa Baqiy’i, akaharakia kuwahi Msikitini”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi’iy kama ilivyo kwenye Musnadi wake (183)].