010-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Kwanza: Adhana
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
010- Kwanza: Adhana
Fadhila Za Adhana:
1- Imepokelewa na Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Swalaah inapoadhiniwa, shaytwaan hukimbia na kupiga mashuzi ya sauti ili asiisikie adhana, na adhana inapomalizika hurudi tena. Inapoqimiwa Swalaah hukimbia, na inapomalizika huja tena akaingia kati ya mtu na nafsi yake akimwambia: “Kumbuka kadha, kumbuka kadha”, na huendelea kumsonga mtu hivyo mpaka anakuwa hajui ni rakaa ngapi kaswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (608) na Muslim (389)].
2- Abuu Sa’iyd Al-Khudriy alimwambia Ibn Abiy Swa’aswa’a: “Nakuona unapenda kondoo na nyika. Basi unapoadhini ukiwa na kondoo wako au nyikani, nyanyua sauti yako ya adhana kwani:
((Hausikii upeo wa mwisho wa sauti ya mwadhini jini, au mwanadamu au kitu chochote ila watamshuhudilia Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (609) na An-Nasaaiy (2/12)].
Abuu Sa’iyd akasema: “Nimeyasikia toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
3- Abuu Hurayrah anasema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
(( Lau kama watu wangelijua fadhila zilizopo kwenye adhana na safu ya kwanza, kisha wasipate njia ya kuzipata ila kwa kupiga kura, basi wangelipiga kura. Na lau wangelijua fadhila za kuwahi mapema (Msikitini), basi wangelishindania. Na lau wangelijua fadhila za ‘Ishaa na Alfajiri, basi wangeliziendea hata kwa kutambaa)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (615) na Muslim (437].
4- Mu’aawiyah bin Abiy Sufyaan (Radhwiya Allaahu Anhu) anasema: Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam anasema:
((Waadhini ndio watu wenye shingo ndefu zaidi Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (387), Ibn Maajah (725) na Ahmad (4/95)].
5- ‘Uqbah bin ‘Aamir anasema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((Mola wenu Anapendezwa sana na mchunga kondoo aliyeko juu kileleni mlimani; anaadhini kwa ajili ya Swalaah, kisha anaswali. Hapo Allaah ‘Azza wa Jalla Husema: Mtazameni Mja Wangu huyu! Anaadhini na kuisimamisha Swalaah, ananiogopa Mimi. Hakika Mimi Nimemghufiria Mja Wangu na Nimemwingiza peponi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1203), An Nasaaiy (2/20) na Ahmad (4/158)].
6- Abuu Hurayrah anasema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((Imamu ni mdhamini, na mwadhini ameaminiwa, Allaah Awaongoe maimamu, na Awaghufirie waadhini)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa“ikhraaj” na Abuu Daawuud (517), At-Tirmidhiy (207) na Ahmad (2/284-419). Angalia Al-Irwaa (1/231)].
7- Kuadhini kuna ubora zaidi kuliko uimamu. Ni kwa Hadiyth zilizotangulia kuhusu fadhila za adhana, na kwa kuwa imamu ni mdhamini, na mwadhini ni mwaminiwa. Kuaminiwa na watu kuna uzito zaidi kuliko udhamini, na maghfirah iko juu kuliko hidaayah. Lakini pamoja na hivyo, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya kazi ya kuadhini wala Makhalifa Waongofu, kwa vile uimamu ni jukumu lao la wajibu na ni kazi adhimu. Haikuwezekana kuzifanya kazi zote mbili kutokana na ufinyu wa wakati na kushughulishwa na mengineyo muhimu zaidi kama kuendesha mambo ya Waislamu. Uimamu ukawa na fadhila zaidi kwao kuliko adhana kutokana na umahususi wa hali yao ingawa adhana kwa watu wengine ina ubora zaidi.
Haya ndio madhehebu ya Ash Shaafi’iy na riwaya mbili sahihi zaidi toka kwa Ahmad. Masahibu zake wengi wamelikhitari hili pamoja na Maalik. Pia Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyya ameliunga mkono. [Al-Mughniy (1/402), Al-Majmu’u (3/74), Mawaahibul Jaliyl (1/422) na Al-Ikhtiyaaraat (uk 36)]
·
Mwanzo Wa Kupitishwa Adhana Kisharia
Adhana ilipitishwa kisharia mwaka wa kwanza wa Hijrah huko Madiynah kwa mujibu wa Hadiyth Swahiyh zilizokuja kuhusiana na hilo. Kati ya hizo ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema:
“Waislamu walipokuja Madiynah, walikuwa wakikusanyika na kusubiri Swalaah bila kuwepo adhana. Siku moja wakalizungumzia hilo. Baadhi wakasema: “Tupigeni kengele kama wanavyofanya Manaswara”. Wengine wakasema: “Tupulizeni tarumbeta kama ya Mayahudi”. ‘Umar akawaambia: “Kwa nini msimpeleke mtu akaadhini?” Hapo hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
((Ee Bilaal! Simama uadhini)) [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (604) na Muslim (377)].
·
Hukmu Ya Adhana
Umma wa Kiislamu, umeafikiana wote kwamba adhana imepitishwa kisharia na imekuwa ikifanywa tokea enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka hivi leo bila mvutano wowote.
Maulamaa wametofautiana kuhusiana na hukmu yake kama ni wajibu au ni Sunnah iliyokokotezwa?
La sahihi lisilo na shaka yoyote katika mfano wa ‘ibaadah hizi tukufu ni kuwa adhana ni faradhi ya kutoshelezana. Si wajibu kwa wakazi wa mji au kijiji kufanya adhana na iqaamah. Hili linatolewa dalili kwa haya yafuatayo:
1- Adhana ni moja kati ya alama tukufu na mashuhuri kabisa za utambulisho wa Uislamu na dini. Na tokea Allaah (Subhaanahu wa Taalaa) kuiweka kisharia, adhana iliendelea kupigwa nyakati zote na katika hali zote mpaka alipokufa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hatujasikia kabisa kwamba iliwahi kuachwa au kutolewa ruksa ya kuiacha.
2- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya kuwa ni nembo ya Uislamu, dalili ya mtu kushikamana nao na kuingia ndani yake. Imepokelewa na Anas akisema:
“Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotuongoza kuwashambulia watu vitani, alikuwa hatuamuru kushambulia mpaka iingie asubuhi, halafu husikilizia. Akisikia wanaadhini, basi huwaacha, na kama hakusikia, huwashambulia”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (610) na Muslim (382)].
3- Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru adhana iadhiniwe. Imepokelewa na Maalik bin Al-Huwayrath (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia yeye na wenzake:
((Wakti wa Swalaah unapoingia, aadhini mmoja wenu na mkubwa wenu awe imamu wenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (631) na Muslim (674)].
4- Imepokelewa na Anas bin Maalik akisema: “Bilaal aliamuriwa aifanye adhana shufwa, na iqaamah witri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (605) na Muslim (378).
5- Katika Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd kuhusu njozi yake ya adhana, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
((Hakika hiyo ni njozi ya kweli, In Shaa Allaah)), [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (499), At-Tirmidhiy (189), Ibn Maajah (706) na wengineo]….kisha akaamuru iadhiniwe.
6- Ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia ‘Uthmaan ibn Abil ‘Aasiy:
((Mweke mwadhini asiyechukua malipo kwa kazi hiyo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (531), An-Nasaaiy (672), At-Tirmidhiy (209) na Ibn Maajah (714)]
7- Imepokelewa na Abud Dardaai akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Hakuna katika watatu ambao adhana haiadhiniwi wala Swalaah haiqimiwi baina yao, ila shaytwaan huwatalawa)). [Isnadi yake ni laini: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (547), An-Nasaaiy (847) na Ahmad (6/446), na ziada ni yake].
Hadiyth hii inaonyesha wajibu wa adhana, kwa kuwa kuliacha lile ambalo ni aina ya kutawaliwa na shaytwaan, ni lazima kuliepuka.
Maalik na Ahmad wanasema kwamba adhana ni lazima na hususan katika Misikiti mikubwa inayoswaliwa jamaa. Hili kwa Mashaaf’iy lina walakini. ‘Atwaa, Mujaahid, Al-Awzaaiy, Daawuud na Ibn Hazm wamesema hivyo hivyo. Ibn Al-Mundhir na Sheikh wa Uislam Ibn Taymiyyah wamelikhitari hilo. [Al-Inswaaf (1/407), Mawaahibul Jaliyl (1/422), Rawdhwat At-Twaalibiyn (1/195), Al-Awsatw (3/24), Majmu’u Al-Fataawaa (22/64) na As Saylul Jarraar (1/196)]
Lakini Abuu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy, wao wanasema kwamba adhana ni Sunnah iliyokokotezwa!!
Ninasema: “Hapana shaka kwamba kauli ya kwanza kuwa ni wajibu, ndiyo yenye nguvu zaidi. Kisha Mahanafi wanaosema kwamba ni Sunnah, wameeleza kwamba Sunnah hii ni kama wajibu katika kupata madhambi, kana kwamba khilafu yao ni ya kilafudhi. [Ibn ‘Aabidiyn (1/384) na Fat-hul Qadiyr (1/240)]
Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
·
Faida
1- Adhana kwa wasafiri:
Wasafiri ni lazima waadhini wakitaka kuswali kama ilivyo kwa wakazi. Hii ni kutokana na ujumuishi wa dalili, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuendelea kulifanya hilo akiwa mjini au safarini, na kumwamrisha Maalik ibn Al-Huwayrath na wenzake kuadhini walipokuwa safarini kurudi kwa jamaa zao. Na hili ndilo la sawa kinyume na madhehebu ya Hanbali na Jamhuri.
2- Swalaah ya kulipwa iadhiniwe:
Ni lazima kuadhini kwa Swalaah zote tano za faradhi, sawasawa ikiwa zinaswaliwa katika wakati wake au zinalipwa qadhwa. Katika milango iliyopita, tuliisoma Hadiyth iliyozungumzia kuhusu kupitiwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake na usingizi, ikawapita Swalatul Fajr mpaka jua likachomoza wakati walipokuwa safarini. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru Bilaal aadhini na aqimu.
Jingine linaloonyesha hilo ni ujumuishi wa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Maalik ibn Al-Huwayrath alipomwambia:
((Wakati wa Swalaah unapoingia, aadhini mmoja wenu..))
Lakini, lau kama watu watalala (katika mji fulani ugenini), na usingizi ukawachukua mpaka wakati wa Swalaah ukatoka, huku adhana ikiwa iliadhiniwa katika mji huo, basi si lazima kuadhini, kwani adhana hiyo itatosheleza, na faradhi ya adhana itawaondokea. [Mengi zaidi ya faida yako kwenye Ash-Sharh Al-Mumti’i (2/41). Angalia yaliyozungumzwa nyuma katika mlango wa kulipa Swalaah zilizopita]
3- Hukmu ya kuadhini wanawake na kuqimu:
[Al-Mughniy (1/422), Al-Majmu’u (3/98), Al-Badaai-’i (1/135), Minahul Jaliyl (1/120), Al-Awsatw (3/53), na Jaami’u Ahkaamin Nisaa cha Sheikh wetu (1/299)]
- Si lazima kwa wanawake kuadhini wala kuqimu kwa rai ya Jamhuri ya Salaf na Khalaf kati ya Maimamu wanne na Adh-Dhwaahiriyya. Imeripotiwa Marfu’u toka kwa Asmaa: “Wanawake hawana adhana, wala iqaamah wala Ijumaa”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (1/408)]
Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haifai. Lakini pamoja na hivyo, haikuja amri yoyote kwa wanawake ya kuadhini au kuqimu.
- Haijuzu (bali haitoshelezi) adhana ya mwanamke kwa wanaume kwa mujibu wa rai ya Jamhuri kinyume na Hanafiy, kwa kuwa adhana ni tangazo na ilivyo kisharia, ni kunyanyua sauti, na mwanamke haijuzu kunyanyua sauti yake kisharia. Haikusikiwa kamwe katika masiku ya Rasuli, wala Maswahaba zake, wala waliokuja baada yao kwamba mwanamke aliadhini adhana ya kisharia ya kutangazia kuingia wakati na kuwaita watu kwenda kuswali.
- Maulamaa wametofautiana kuhusiana na adhana na iqaamah kwa wanawake ikiwa wako peke yao mbali na wanaume. Yaliyosemwa ni:
Yote mawili ni karaha, yote mawili yanafaa, yote mawili ni mustahabu, imesuniwa iqaamah bila adhana.
Linaloonekana kuwa ni la nguvu ni kuwa kama wanawake wako peke yao mbali na wanaume, kuadhini na kuqimu itakuwa ni vizuri zaidi kwao, kwa kuwa mawili hayo ni kumdhukuru Allaah Mtukufu, na hakuna lolote lililopokelewa kuzuia hilo. Ibn ‘Umar aliulizwa: “Je, wanawake waadhini?” Alighadhibika na kujibu: “Nikataze kudhukuriwa Allaah?!!” [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/223)].
Imepokelewa toka kwa Mu’utamir bin Sulaymaan toka kwa baba yake akisema: “Tulikuwa tukimuuliza Anas: “Je, ni lazima kuadhini na kuqimu kwa wanawake?” Akajibu: “Hapana, lakini kama watafanya, basi hilo ni dhikri” [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/223)].
Na hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad, na Ibn Hazm ana msimamo huu huu. [Al-Ummu (1/84), Al-Mughniy (1/422) na Al-Muhallaa (3/129)]
Ash-Shaafi’iy amesema: “Mwanamke hanyanyui sauti yake, ataadhini kwa sauti ya kujisikia mwenyewe au ya kusikiwa na wenzake, na hivyo hivyo atakapoqimu”.
4- Adhana ya mwenye kuswali peke yake ikiwa watu washaswali jamaa Msikitini:
Mtu mwenye kuswali peke yake katika mji ambao adhana ilikwisha adhiniwa, anaweza kutosheka na adhana hiyo iliyoadhiniwa. Lakini ikiwa ataadhini na kuqimu, itakuwa ni vizuri zaidi kwa ajili ya kuipata fadhila ya adhana. Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Abuu Sa’iyd na ‘Uqbah bin ‘Aamir iliyotangulia katika mlango wa fadhila za adhana.
Aidha, kama jamaa imempita akaingia katika Msikiti ambao watu wake washaswali, ikiwa atatosheka na adhana yao, basi itamtosheleza. Lakini ni bora kwake kuadhini na kuqimu kama alivyofanya Anas ibn Maalik. Imepokelewa na Abuu ‘Uthmaan akisema: “ Alitujia Anas ibn Maalik katika Msikiti wa Bani Tha’alabah akauliza: “Je, mshaswali?” (ilikuwa swala ya Alfajiri). Tukamjibu ndio. Akamwambia mtu aadhini. Akaadhini na kuqimu, kisha wakaswali jamaa”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/221)].
Hivi ndivyo walivyosema Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Lakini Maalik na Al-Awzaa’iy wanasema kuwa ataqimu tu bila kuadhini. Naye Abuu Haniyfah na wenzake wanasema kuwa haadhini wala haqimu. [Al-Ummu (1/84), Al-Mughniy (1/418), Al-Mudawwanah (1/61) na Al-Awsatw (3/60-62)]
5- Adhana ya Swalaah mbili za kukusanywa:
Zikikusanywa Swalaah mbili katika wakati wa mojawapo kama kukusanya Alasiri na Adhuhuri katika wakati wa Adhuhuri ‘Arafah, au kukusanya Magharibi na ‘Ishaa Muzdalifah, itatosheleza adhana moja tu, lakini kila Swalaah itaqimiwa kwa iqaama yake kama alivyofanya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Haya ndiyo waliyoyasema Jamhuri kinyume na mashuhuri kwa Maalik anayesema kwamba kila Swalaah itaadhiniwa kivyake!! [Al-Badaai-’i (1/152), Al-Majmu’u (3/83), Mawaahibul Jaliyl (1/468), na Al-Mumti’i (2/41)]Yatafafanuliwa zaidi katika mlango wa Hajji.
6- Swalaah zinazoadhiniwa kisharia:
Maulamaa wamekubaliana kwamba adhana kisharia, ni kwa Swalaah tano tu za faradhi. Swalaah nyinginezo kama ya Maiti, Witri, ‘Iyd Mbili na kadhalika hazina adhana. Kwani lengo la adhana, ni kutangazia kuingia wakati wa Swalaah, na Swalaah tano za faradhi zimepangiwa nyakati zake maalumu. Ama Swalaah za Sunnah, hizo ziko chini ya Swalaah za faradhi, na adhana ya asili ya Swalaah ya faradhi, hujumuisha na Swalaah husika za Sunnah. Ama Swalaah ya maiti, Swalaah hii si Swalaah kiuhakika, kwani haina kisomo, wala rukuu wala sujudi.
Na kati ya yaliyokuja kuhusiana na hili, ni Hadiyth ya Jaabir bin Samrah asemaye: “Niliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Iyd, si mara moja wala mbili bila ya adhana wala iqaamah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (887), Abuu Daawuud (1148) na At-Tirmidhiy (532).
·
Vipi Hutangaziwa Swalaah Zisizo Na Adhana?
Ash-Shaafi’iy anaona kwamba kila Swalaah isiyo na adhana, hunadiwa kwa neno: " الصلاة جامعة ". Mahanbali wamekubaliana naye lakini katika Swalaah za ‘Iyd, Kupatwa Jua na Kuomba Mvua tu. Ama Mahanafi na Maalik wamekubaliana naye katika Swalaah ya Kupatwa Jua basi. [Ibn ‘Aabidiyn (1/565), Al-Majmu’u (3/77), Al-Mawaahib (1/435) na Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/211)]
Ninasema: “La sawa ni kuegemezwa na kudhibitiwa hili kwa Aayah au Hadiyth. Swalaah iliyothibitishwa kwa Aayah au Hadiyth hunadiwa kwa kusema: " الصلاة جامعة ", basi ni Sunnah kufanya, na kama hakuna, basi isifanywe. Maelezo yake kiuchambuzi yatakuja katika milango husika InshaAllaah.
·
Masharti Ya Adhana
1- Ni kuingia wakati wa Swalaah (isipokuwa Swalaah ya Alfajiri)
Sharti ya adhana ni kuingia wakati wa Swalaah ya Fardhi. Haitofaa kuadhini kabla ya wakati kuingia (isipokuwa kwa Swalaah ya Alfajiri kwa ufafanuzi utakaokuja baadaye). Wakati unapoingia, imesuniwa kuadhini mwanzo wake ili watu wajue na waanze kujiandaa kwa ajili ya Swalaah. Imepokelewa na Jaabir bin Samrah akisema:
“Bilaal alikuwa akiadhini jua linapopinduka, haachi kitu katika matamshi yake. Kisha haqimu mpaka Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amtokee. Anapotoka, huqimu anapomwona”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (606), Abuu Daawuud (537) na At-Tirmidhiy (202) na Ahmad (5/91).
Ama Alfajiri, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Is-haaq, Abuu Thawr, Abuu Yuusuf na Ibn Hazm, hawa wanasema kwamba adhana ya Alfajiri kisharia, inaweza kuadhiniwa kabla ya wakati (kabla ya kuchomoza Alfajiri ya kweli). [Al-Mudawwanah (1/60), Al-Ummu (1/83), Masaail Ahmad cha ‘Abdullaah (58), Al- Majmu’u (3/88), Al-Awsatw (3/29) na Al-Muhallaa (3/160)] Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) anayesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Bilaal huadhini usiku, basi kuleni na kunyweni mpaka Ibn Ummi Maktoum aadhini)).
Anasema: “Alikuwa ni kipofu, haadhini mpaka aambiwe: Alfajiri imeingia, Alfajiri imeingia. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (617), na ziada ni yake, na Muslim (1092)].
Adhana ya kwanza inakuwa kwa ajili ya kumwamsha aliyelala ili aanze kujitayarisha kwa Swalaah, na ili kumpunguza kasi mwenye kuswali tahajudi apate kupumzika na kupata kuswali Swalaah ya Alfajiri kwa uchangamfu, au apate kula daku kama ana niya ya kufunga. Ni kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn Mas-’oud kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
(( Isimzuie mmoja wenu adhana ya Bilaal kula daku, kwani yeye anaadhini usiku ili kumtua mwenye kuswali kati yenu, na kumwamsha aliyelala kati yenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (621) na Muslim (1093)].
Jamhuri imestahabu adhana ya pili unapoingia wakati. Wanaona kwamba inajuzu kutosheka nayo kwa kunadi “Swalaah”!! La sahihi ni lile alilolifuata Ibn Al-Mundhir na Ibn Hazm wanaosema kwamba ni lazima adhana ya pili iliyo katika wakati, kwa kuwa ndio asili. Kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wakati wa Swalaah unapoingia, aadhini mmoja wenu)), na hii ni kwa Swalaah zote; haitolewi Swalaah yoyote kando, wala halipingwi na Hadiyth: ((Bilaal huadhini usiku)), kwa kuwa adhana hii si kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri kama ilivyotangulia.
Lakini Ath-Thawriy na Abuu Haniyfah [Al-Muhallaa (3/163), Al-Majmu’u (3/88), Al-Awsatw (3/30) na Al-Mabsuutw (1/134)]….wanaona kwamba Alfajiri haiadhiniwi mpaka baada ya kutoka Alfajiri ya kweli kupimia na Swalaah zinginezo, na kwa yaliyosimuliwa toka kwa Shaddaad mwachwa huru wa ‘Ayyaadh bin ‘Aamir kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal:
((Usiadhini mpaka uione Alfajiri)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (534). Al-Bayhaqiy ameikosoa kwamba ina mkatiko. Ibn Al-Qattaan amesema: “Shaddaad hajulikani”. Angalia Nasb Ar-Raayah (1/283)].
Hadiyth hii haifai.
Na kwa yanayosimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Bilaal aliadhini kabla ya kuchomoza Alfajiri, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru arejee anadi: “Jueni kwamba mja alilala”. [Al-Muhallaa (3/163), Al-Majmu’u (3/88), Al-Awsatw (3/30) na Al-Mabsuutw (1/134)]
Hii pia imekosolewa na Maulamaa wa Hadiyth, haifai kwa hoja.
Ama kipimo chao, hicho kiko mkabala na Hadiyth zilizotangulia katika kuithibitisha adhana kabla ya Alfajiri, nazo zinaonyesha kuwa Bilaal alidumu na hilo. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimkubalia hilo na wala hakumkataza, ikathibiti kujuzu kwake bali kuwa mustahabu. Ama Hadiyth walizozitolea hoja, zote zina kasoro na hazifai kwa hoja, mbali na kujibiwa na Hadiyth Swahiyh zilizothibiti.
2- Niya ya adhana:
Ili adhana iswihi, ni lazima pawepo niya kama zilivyo ‘ibaadah nyinginezo kwa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika amali ni kwa niya)). [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja sehemu nyingi].
Ikiwa mtu ameanza kumdhukuru Allaah kwa takbiyr, kisha baada ya takbiyr akaona aunganishe adhana, basi itabidi aanze tena mwanzo wala asijengee juu ya aliyoyasema. Haya ni madhehebu ya Maalik na Hanbali. [Mawaahibul Jaliyl (1/424) na Muntahaa Al-Iraadaat (1/129)]
3- Iwe kwa Lugha ya Kiarabu
[Ibn ‘’Aabidiyn (1/256), Kash-Shaaf Al-Qinaa (1/215) na Al-Majmu’u (3/129)]
Ni lazima matamshi ya adhana yawe kwa Lugha ya Kiarabu. Haifai kwa lugha nyingine yoyote hata kama itajulikana kwamba ni adhana. Haya ni madhehebu ya Hanafi na Hanbali. Shaafi’i wanaona hivyo hivyo isipokuwa wanasema kwamba ikiwa hakuna anayejua Kiarabu, basi itawatosheleza kwa lugha nyingine.
4- Kutokuwepo makosa yanayogeuza maana
[Ibn ‘’Aabidiyn (1/259), Muntahaa Al-Iraadaat (1/130), Al-Mawaahib (1/438) na Al-Majmu’u (3/425)]
Ni kama kuvuta “Hamzah ya (Akbar) au “Baa” yake na mengineyo yenye kugeuza maana. Pia kuvuta zaidi ya mpaka unaotakiwa. Ikiwa maana itakuwa haifahamiki, basi adhana ni batili, na kama ina makosa, inakuwa ni makruhu kwa Jamhuri kinyume na Mahanafi.
5- Matamshi yake yawe katika mpangilio
[Al-Badaai-’i (1/149), Mughniy Al-Muhtaaj (1/137), Al-Iraadaat (1/128) na Al-Mawaahib (1/425)]
Mwadhini ni lazima ayalete matamko ya adhana kwa mfumo na utaratibu uliokuja katika Sunnah (utakaokuja kuelezwa baadaye kidogo) bila kutanguliza au kuakhirisha neno juu ya jingine au sentensi juu ya nyingine. Ikiwa mwadhini atafanya hivyo, basi ni lazima aanze tena upya (kwa mujibu wa Jamhuri kinyume na Hanafiy) kwa kuwa kuacha mpangilio, hupindisha ujulisho uliokusudiwa. Haifai kupangua mtiririko huu kwa kuwa adhana ni dhikri inayotambulika hivyo. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(Mwenye kufanya tendo lolote ambalo si amri yetu, basi hurejeshewa mwenyewe)). [Hadiyth Swahiyh: Al Bukhaariy kwenye I’itiswaam ameifanya “Mu’allaq”, Muslim (1718) na wengineo ameifanya “Mawswuul”].
6- Kuandamisha kati ya matamko ya adhana
[Rejea zilizotangulia]
Ni kufuatanisha kati ya matamko bila kuyakata kwa neno au tendo. Ikiwa mwadhini atakata kidogo kwa chafya wakati wa adhana, basi ataendelea pale alipokomea kwa mujibu wa rai ya Jamhuri. Na kama mkato utakuwa mrefu kati ya matamko kwa maneno mengi, au kupotewa na fahamu na mfano wake, basi adhana itabatilika, na ni lazima aanze tena mwanzo. Haifai kuendeleza pale alipokomea, bali lazima aanze tena upya.
7- Waisikie walio mbali
[Rejea zilizotangulia]
Hii ni ima kwa kupaza sauti au kutumia kipaza sauti ili makusudio ya adhana yapatikane. Na kama anajiadhinia mwenyewe, basi si lazima anyanyue sauti isipokuwa kwa kiasi cha kujisikia yeye mwenyewe au aliye pamoja naye. Imetangulia katika Hadiyth ya Abuu Sa’iyd:
((Nyanyua sauti yako ya adhana, kwani hausikii upeo wa mwisho wa sauti ya mwadhini jini, au mwanadamu au kitu chochote ila watamshuhudilia Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa kwenye mlango wa (Fadhila za adhana)].
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ‘Abdullaah bin Zayd:
((Mfundishe Bilaal adhana, kwani yeye ana sauti kali nzuri na pumzi ndefu kuliko wewe)). [Hadiyth Hasan: Imetajwa katika (Hukmu za adhana)].
Haya ni madhehebu ya Shaafi’i na Hanbali, na kauli kwa Mahanafi. Ni Sunnah kwa Maalik, na jambo muhimu kwa Mahanafi.
·
Je, Inatosheleza Kurusha Adhana Kupitia Redio?
[Ash-Sharhul Mumt’i (2/61-62) kwa maana yake]
Kurusha adhana kwa njia ya redio au tapurikoda si sahihi, kwa kuwa adhana ni ‘ibaadah ambayo kama tulivyotangulia kusema ni bora kuliko hata uimamu. Na kama ambavyo haisihi watu kufuata Swalaah ya kurekodiwa, hali ni hivyo hivyo kwa upande wa adhana. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.
·
Je, Inafaa Kuzungumza Wakati Wa Adhana Na Iqaamah?
Maulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na hukmu ya kuzungumza mwadhini wakati anaadhini katika kauli zifuatazo:
[Al-Awsatw (3/43), Masaail Ahmad cha Abuu Daawuud (27), Al-Mudawwanah (1/59) na Al-Ummu (1/85)]
Ya kwanza: Inajuzu kuzungumza wakati wa adhana kwa hali yoyote
Hili wamelisema Al-Hasan, ‘Atwaa, Qataadah, na Ahmad (isipokuwa yeye amekataza kwenye iqaamah). Nayo imesimuliwa toka kwa Sulaymaan bin Sward ambaye ni Swahaba na ‘Urwa bin Zubayr. Hoja zao ni hizi zifuatazo:
1- Ibn ‘Abbaas alimwamuru mwadhini wake siku ya ijumaa mvua ilipokuwa kali wakati alipofikia:"حي على الصلاة" , aseme: "الصلاة في الرحال". Akaulizwa: “Nini hili?” Akasema: “Amelifanya aliye bora zaidi kuliko mimi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (616) na Muslim (699) kwa mfanowe].
2- Imepokelewa toka kwa Muusa bin ‘Abdullaah bin Zayd kwamba Sulaymaan bin Sward alikuwa akiadhini kambini, huku akimwagiza mtumishi wake kitu naye anaendelea na adhana. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa “Mu’allaq” (2/116), Ibn Abuu Shaybah kaifanya “Mawswuul” (1/212), Ibn Al-Mundhir (3/44) na Abuu Na’iym Sheikh wa Al-Bukhaariy kwa Sanad Swahiyh kama ilivyo kwenye Al-Fat-h (2/116)]
Ya pili: Ni karaha kuzungumza wakati wa adhana na iqaamah
An-Nakh’iy, Ibn Siyriyn, Al-Awzaa’iy, Maalik, Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy na Abuu Haniyfah wamesema hili.
Kauli ya tatu: Haitakikani kwa mwadhini kuzungumza wakati wa adhana isipokuwa maneno yanayohusiana na Swalaah kama kusema: "صلوا في رحالكم" . Hii ni kauli ya Is-Haaq ambayo Ibn Al-Mundhir kaikubali.
Kauli ya nne: Kama atazungumza katikati ya iqaamah, basi atairudia.
Hii ni kauli ya Az-Zuhriy.
·
Sifa Za Mwenye Kuadhini
Imesuniwa mwadhini awe na sifa zifuatazo:
1- Afanye kwa ajili ya Allaah tu
Asichukue malipo yoyote kwa kuadhini na kuqimu, kwa kuwa haijuzu kudai malipo kwa kazi ya twa’a. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia ‘Uthmaan bin Abiyl ‘Aasw:
((Mweke mwadhini asiyechukua malipo kwa adhana yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika “Hukmu za adhana”].
Kama hakupatikana wa kujitolea, basi Imamu atampangia mshahara atakayeadhini toka Baytul Maal, kwa kuwa Waislamu wanamhitajia.
2- Awe mwadilifu na mwaminifu
Hii ni kwa vile “mwadhini ni mwaminiwa”[Hadiyth Swahiyh: Imetajwa katika “Fadhila za adhana”], yaani ni mtu anayeaminika kwa kuchunga nyakati za Swalaah. Ni lazima pia ayachunge macho yake yasiangalie aibu na nyuchi za watu. Adhana ya mtu fasiki inasihi pamoja na umakuruhu kama wanavyosema Jamhuri. Sheikh wa Uislamu anaona kwamba adhana ya fasiki anayejulikana haijuzu kwa kuwa anakwenda kinyume na amri ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kwa Mahanbali, hili lina khilafu. [Ibn ‘Aabidiyn (1/263), Al-Mawaahib (1/436), Mughniy Al-Muhtaaj (1/138), Al-Mughniy (1/413) na Al-Ikhtiyaaraat (37)]
3- Awe na sauti nzuri
[Ibn ‘Aabidiyn (1/259), Al-Mawaahib (1/437), Mughniy Al-Muhtaaj (1/138), Al-Mughniy (1/413) na Muntahaa Al-Iraadaat (1/125)]
Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwambia ‘Abdullah bin Zayd:
((Nenda na Bilaal umfundishe uliyoyaona, kwani yeye ana sauti kali nzuri na pumzi ndefu kuliko wewe)).[Hadiyth Hasan: Imetajwa mara kadhaa, na itakuja tena kwenye “Sifa ya adhana”].
Na ili kulifanikisha hili, ni vizuri kutumia vyombo vya kisasa vya sauti ili kuichekecha sauti na kuifikisha. Na hii ni pamoja na ukaraha wa kuvuta sana na kughani kwa madoido.
4- Ajue wakati
Ili aweze kuadhini mwanzoni mwa wakati na kuepusha matatizo, inajuzu kuadhini kwa asiyeweza kujua wakati yeye mwenyewe kama kipofu ikiwa atakuwa na mtu wa kumweleza wakati. Ibn Ummi Maktoum aliyekuwa kipofu, alikuwa haadhini mpaka aambiwe: “Alfajiri imeingia, Alfajiri imeingia”. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni.]
·
Sifa Ya Adhana
Matamko ya adhana yamekuja kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa miundo mitatu:
Wa kwanza:
Ni sentensi 15; Takbiyr mara nne, na matamshi yaliyobakia mara mbili isipokuwa tamko la mwisho la Tawhiyd ambalo ni mara moja tu. Namna hii imethibiti katika Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd (Radhwiya Allaahu Anhu) aliposema:
“Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam alipoamuru kengele ipigwe ili watu wakusanyike kuswali, alinizungukia mtu nikiwa usingizini akiwa amebeba kengele mkononi. Nikamuuliza: Ee ‘Abdullah: Unauza kengele? Akasema: Nawe utaifanyia nini? Nikamwambia: Tutawaitia watu Swalaah. Akaniambia: Kwa nini nisikuonyeshe kilicho bora zaidi kuliko kengele? Nikamwambia sawa. Akasema: Utasema:
" الله أكبر الله أكبر الله أكبر الله أكبر، أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله أشهد أن محمدا رسول الله، حي على الصلاة حي على الصلاة، حي على الفلاح حي على الفلاح، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله"
Halafu akarudi nyuma mbali kidogo akaniambia: Kisha utasema utakapoqimu Swalaah:
" الله أكبر الله أكبر، أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله، حي على الصلاة، حي على الفلاح، قد قامت الصلاة قد قامت الصلاة، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله"
Kulipopambauka, nilimwendea Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikamweleza niliyoyaona usingizini. Akaniambia: Hakika hiyo ni njozi ya kweli In ShaaAllaah. Basi nenda na Bilaal umfundishe uliyoyaona ili ayatolee adhana, kwani yeye ana sauti kali nzuri na pumzi ndefu kuliko wewe. Nikaenda pamoja na Bilaal, nikaanza kumfundisha na yeye anaadhini. ‘Umar ibn Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu Anhu) akalisikia hilo akiwa nyumbani kwake, akatoka mbio akikokota nguo yake akisema: Naapa kwa Yule Ambaye Amekutuma wewe kwa haki ee Rasuli wa Allaah! Hakika mimi nimeoteshwa kama hayo hayo aliyooteshwa. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: " Falil-Laah Al-Hamdu". [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (499), At-Tirmidhiy (189) na Ibn Maajah. Angalia Al-Irwaa (2/264)].
Abuu Haniyfah na Ahmad kwa ilivyo mashuhuri kwake wanautumia muundo huu.
Wa pili:
Ni sentensi 19 kama uliotangulia pamoja na kuongeza “Tarji’i” katika shahada mbili. “Tarji’i” maana yake ni mwadhini kupunguza sauti yake kwenye shahada mbili kiasi cha kusikia waliopo karibu naye, kisha ainyanyue tena kwa shahada zingine mbili.
Muundo huu umethibiti katika Hadiyth ya Abuu Mahdhuurah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimfundisha adhana:
(( الله أكبر الله أكبر الله أكبر الله أكبر، أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله أشهد أن محمدا رسول الله ))
Kisha akasema:”Rudia tena kwa sauti ya chini”. Halafu akasema: “Sema:
((أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله أشهد أن محمدا رسول الله، حي على الصلاة حي على الصلاة، حي على الفلاح حي على الفلاح، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله)) الحديث
Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (500-503), At-Tirmidhiy (192), An-Nasaaiy (2/3) na Ibn Maajah (709).
Na katika riwaya nyingine toka kwake kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimfundisha adhana maneno 19 na iqaamah maneno 17.
Muundo huu anautumia Ash Shaafi’iy. [Al-Ummu (1/85)]
Wa tatu:
Sentensi 17 kama uliotangulia lakini kwa kufanya takbiyr mara mbili mwanzoni, si mara nne. Na hii ni riwaya nyingine ya Hadiyth ya Abuu Mahdhuurah iliyotangulia kwamba Rasuli wa Allaah alimfundisha adhana hii:
((الله أكبر الله أكبر، أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله أشهد أن محمدا رسول الله))
Kisha hurejea akisema:
((أشهد أن لا إله إلا الله أشهد أن لا إله إلا الله، أشهد أن محمدا رسول الله أشهد أن محمدا رسول الله، حي على الصلاة حي على الصلاة، حي على الفلاح حي على الفلاح، الله أكبر الله أكبر، لا إله إلا الله ))
[Imekosolewa kwa tamko hili. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (379) na wengineo]
Riwaya hii imekosolewa, haifai. La sahihi ni kufanya takbiyr mara nne kama ilivyotangulia.
Muundo huu anautumia Maalik na masahibu wawili wa Abuu Haniyfah. [Al-Mudawwanah (1/57) na Al-Badaai-’i (1/147)]
Baadhi ya Maulamaa wametilia nguvu kufanya takbiyr mara nne (muundo wa pili) katika Hadiyth ya Abuu Mahdhuurah wakisema kwamba hiyo ni ziada inayokubalika kwa kuwa haiendi kinyume, matoleo yake ni sahihi na inawafikiana na riwaya ya: “Alimfundisha adhana maneno 19”.
Kisha wakaitilia nguvu kuliko namna ya kwanza (isiyo na takbiyr nne) wakisema kwamba Hadiyth ya Abuu Mahdhuurah ni ya mwaka wa nane wa Hijrah baada ya Hunayn, na Hadiyth ya Ibn Zayd ilikuwa ni mwanzo wa suala la adhana, na kwamba watu wa Makkah na Madiynah wanafanya takbiyr nne. [Al-Muhallaa (3/203-206), Al-Awsatw (3/16), Naylul Awtwaar (2/45) na Zaaadul Ma’ad (2/389)]
Wengine wanasema kwamba miundo yote hii inafaa na mtu anaweza kuchagua muundo wowote. Waliosema hili ni Ahmad (ingawa yeye kapendelea zaidi muundo wa kwanza), Is-Haaq na Ibn Taymiyah. [Masaail Ahmad cha Abuu Daawuud (27), Al-Mughniy (1/404), Majmu’u Al-Fataawaa (22/336-337) na Al-Mumti’i (2/51)]
Msimamo huu unaweza kuwa bora zaidi kuliko kuchagua muundo fulani na kuufanya kuwa ndio sahihi zaidi, kwa kuwa qaida inasema: “‘ibaadah zilizokuja katika njia tofauti, ni bora kuzifanya katika njia hizo”. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
·
“Tathwiyb” Katika Adhana Ya Alfajiri
“Tathwiyb”, ni mwadhini kusema: "الصلاة خير من النوم" mara mbili baada ya “Hay-‘alatayn” katika adhana ya Alfajiri.
”Hay-‘alatayn” ni: حي على الصلاة، حي على الفلاح .
Kufanya hivi ni Sunnah kwa Jamhuri. [Mawaahibul Jaliyl (1/431), Al-Majmuu (3/92), Al-Mughniy (1/407) na Subulus Salaam (1/250)]
Na hii ni kwa Hadiyth ya Abuu Mahdhuurah iliyotangulia ambapo alisema: “Ikiwa ni Swalaah ya Alfajiri utasema:
((الصلاة خير من النوم، الصلاة خير من النوم، الله أكبر ألله أكبر، لا إله إلا الله))
Na katika tamko jingine: “Mwanzoni mwa Alfajiri”. [Hasan kwa Sanad zake: lmefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (501), An-Nasaaiy (2/7-8), na Ahmad (3/408). Al-Albaaniy kaipitisha kuwa Swahiyh kwa yenyewe katika “takhriyj” ya Al-Mishkaat (645). Inapata hadhi ya kuwa Hasan kwa Sanad tofauti. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi]
“Tathwiyb” katika adhana ya Alfajiri imekuja katika Hadiyth ya Bilaal, Sa’ad Al-Qardh, Abuu Hurayrah, Ibn ‘Umar, Nu’aym An-Nahaam, ‘Aaishah, na Abuu Mahdhuurah. Sanad zake zina walakin, na bora zaidi zake ni tatu za mwisho ambazo zote zinathibitisha uhalali wa “tathwiyb” katika adhana ya Alfajiri.
“Tathwiyb” ni kwenye adhana ya kwanza tu na si ya pili
Hadiyth tulizoziashiria hivi punde, kuna zilizotaja “tathwiyb” bila kuainisha kama inafanywa kwenye adhana ya kwanza au ya pili, na kuna nyingine zinazoeleza kwamba ni katika adhana ya kwanza. Hakuna hata Hadiyth moja iliyoeleza kwamba inafanywa kwenye adhana ya pili. Hii inaonyesha kwamba “tathwiyb” kisharia inakuwa katika adhana ya kwanza kwa ajili ya kumwamsha aliyelala kama ilivyotangulia. Ama adhana ya pili, hii ni kwa ajili ya kutangazia kuingia wakati na kuwaita watu kwenda kuswali.
Inajulikana kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na waadhini wawili. Wa kwanza ni Bilaal ambaye alikuwa akiadhini na “tathwiyb”, na wa pili ni Ibn Ummu Maktoum. Adhana ya Bilaal ilikuwa ya kwanza, na haikuwahi kuelezewa kwamba Ibn Ummu Maktoum alikuwa akifanya “tathwiyb” kwenye adhana yake. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. [Angalia Tasnifu: ((تحفة الحبيب ...بحكم الأذانين للفجر والتثويب)) ya Sheikh wetu Majdiy bin ‘Arfaan Allaah Amtukuze]
·
Faida
Baadhi ya Mahanafiy na Mashaafi wamejuzisha kufanya “tathwiyb” katika adhana ya ‘Ishaa. Wanasema kwamba sababu ni kuwa huo ni wakati wa mdororo na kusinzia sinzia kama Alfajiri!! Na baadhi ya Mashaafi wamejuzisha “tathwiyb” nyakati zote!! Hii ni bid-’a yenye kukhalifu Sunnah. ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) aliipinga. Alipoingia Msikitini kuswali, alimsikia mtu anafanya “tathwiyb” kwenye adhana ya Adhuhuri, akatoka nje. Akaulizwa: “Wapi?” Akasema: “Bid-’a imenitoa”. [Al-Albaaniy anasema ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (538), na Al-Bayhaqiy (1/424). Angalia Al-Irwaa (236)]
·
Yaliyosuniwa Kwa Mwadhini
1- Awe na twahara
Ni kutokana na ujumuishi wa dalili juu ya kusuniwa kumdhukuru Allaah mtu akiwa twahara. Na haya yametangulia katika mlango wa wudhuu. Imepokelewa Hadiyth:
((Haadhini isipokuwa mwenye wudhuu)), lakini si Swahiyh.
Ikiwa ataadhini bila wudhuu, adhana itaswihi kwa mujibu wa Mafuqahaa wote. Vile vile, hata akiwa na janaba, adhana itaswihi kwa vile hakuna dalili yoyote ya kuzuia hili, na mwenye janaba si najsi. Ahmad na Is-Haaq wamezuia kuadhini na janaba. [Al-Awsatw (3/28)]
2- Aadhini kwa kusimama
Wanachuoni hawakukhitalifiana, bali wote wamekubaliana kwamba ni Sunnah mwadhini aadhini kwa kusimama isipokuwa tu kama mgonjwa. Kama ni mgonjwa, basi ataadhini kwa kukaa.
Maalik, Al-Awzaa’iy na Abuu Haniyfah na wenzake, wamesema kuwa ni makruhu kusimama kwa kuketi katika hali yoyote. [Al-Awsatw (3/46)]
Imetangulia katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
((Simama ee Bilaal unadie Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: “Takhriyj” yake ishatangulia].
Na katika Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd:
“Niliona usingizini kama vile mtu amesimama, akaadhini mbili mbili, akaqimu mbili mbili”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/203) na Ahmad (5/232)].
3- Aelekee Qiblah
Maulamaa wote wanakubaliana kwamba ni Sunnah mwadhini aelekee Qiblah anapoadhini. [Al-Awsatw (3/28)]
Zimesimuliwa Hadiyth tofauti kuhusiana na hili zikiwa na mengi tofauti. Katika baadhi ya riwaya, kuna Hadiyth ya Ibn Zayd kwamba Malaika aliyemwona akiadhini, alikuwa ameelekea Qiblah. [Angalia Irwaaul Ghaliyl (1/250)]
4- Aingize vidole vyake kwenye masikio mawili
Ni kwa Hadiyth ya Abuu Juhayfah aliyesema: “Nilimwona Bilaal akiadhini na kuduru, anafuatisha kinywa chake hapa na hapa, na vidole vyake viwili ndani ya masikio yake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (1/203) na Ahmad (5/232)].
5- Azikusanye kwa pamoja kila takbiyr mbili
Ni kwa Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Anaposema mwadhini: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, akasema mmoja wenu: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, kisha akasema: Ash-hadu an laa ilaaha illal Laah, akasema: Ash-hadu an laa ilaaha illal Laah,……)). [Hadiyth Swahiyh: Itakuja kamili karibuni].
Hadiyth hii inaashiria wazi kwamba mwadhini hukusanya kati ya kila takbiyr mbili, na mwenye kumsikia humjibisha hivyo hivyo. [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (3/79)]
Si kama wanavyofanya baadhi ya waadhini ambao hutenga kila takbiyr moja kwa pumzi nne!!
6- Ageuze kichwa chake kulia wakati anaposema:"حي على الصلاة" , na kushoto wakati anaposema:"حي على الفلاح"
Ni kwa Hadiyth ya Abuu Juhayfah aliyemwona Bilaal akiadhini. Anasema: “Nikawa nafuatilia kinywa chake hapa na hapa kwa adhana”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (634) na Muslim (503)].
Hivyo ni Sunnah ageuze kichwa tu na kiwiliwili kibaki kimeelekea Qiblah. Hivi ndivyo walivyosema Jamhuri kinyume na Maalik aliyelikataa!! Ahmad na Is-Haaq wamelihusisha hilo kwa mwenye kuadhini kwenye mnara tu ili watu wamsikie, na si vinginevyo. [Al-Awsatw (3/26,27)]
7- Afanye “tathwiyb” katika adhana ya kwanza ya Alfajiri
Hili tushalizungumza.
·
Yaliyosuniwa Kwa Mwenye Kusikia Adhana
1- Kuitikia kwa sauti ya chini kila sentensi ya mwadhini
Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mkisikia adhana, semeni mfano wa anayoyasema mwadhini)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (611) na Muslim (383)].
Anaposema mwadhini: " حي على الصلاة "، " حي على الفلاح ", aseme:
" لا حول ولا قوة إلا بالله " Ni kwa Hadiyth ya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Anaposema mwadhini: Allaahu Akbaru Allaahu Akbar, akasema mmoja wenu: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, kisha akasema: Ash-hadu an laailaaha illa Laah, akasema: Ash-hadu an laailaaha illa Laah, kisha akasema: Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulul Laah, akasema: Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulul Laah, kisha akasema: Hayya alas Swalaah, akasema: Laa hawla walaa quwwata illaa bil Laah, kisha akasema: Hayya alal falaah, akasema: Laa hawla walaa quwwata illaa bil Laah, kisha akasema: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, akasema: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, kisha akasema: Laailaaha illa Laah, kutoka moyoni mwake, ataingia peponi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (385) na Abuu Daawuud (523)].
Jamhuri wamezihusisha “hay-ala” mbili na Hadiyth hii kutokana na ujumuishi wa Hadiyth ya Abuu Sa’iyd iliyotangulia. Na kwa vile “hay-ala” mbili ni kitenzi agizi (njoo kwenye Swalaah, njoo kwenye mafanikio), kumjibu mwadhini itakuwa ni upuuzi.
·
Mwadhini Anaposema: " الصلاة خير من النوم ", Atajibiwa Nini?
Mwenye kumsikia atamjibu kwa kusema: " الصلاة خير من النوم ", juu ya ujumuishi wa Hadiyth ya Abuu Sa’iyd iliyotangulia. Ama baadhi yao kujibu kwa kusema: " صدقت وبررت ", hakuna Hadiyth yoyote Swahiyh iliyothibitisha hilo, hivyo haijuzu kuitaabudia. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
·
Faida
Inatosha kumjibu mwadhini kwenye shahada mbili kwa kusema: "وأنا" au " وأنا أشهد " na mfano wa hilo kwa Hadiyth ya Sahl bin Hunayf kwamba alimsikia Mu’aawiyah bin Abiy Sufyaan (Radhwiya Allaahu Anhu) akiwa ameketi juu ya mimbari. Mwadhini aliadhini, akasema: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Mu’aawiyah akasema: Allaahu Akbar Allaahu Akbar, akasema: Ash-hadu an laailaaha illa Laah, Mu’aawiyah akasema: Na mimi, akasema: Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulul Laah, Mu’aawiyah akasema: Na mimi. Adhana ilipomalizika akasema: “Enyi watu! Hakika mimi nimemsikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya mimbari hii (wakati alipoadhini mwadhini) akiyasema mliyoyasikia nikiyasema”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (914), An-Nasaaiy (2/24) na Ahmad (4/95)].
2- Kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwombea “Al Wasiylah” baada ya kumalizika adhana
Imepokelewa na ‘Abdullaah bin ‘Amri kwamba alimsikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Mkimsikia mwadhini, basi semeni mfano wa anayoyasema, kisha niswalieni, kwani mwenye kuniswalia mara moja, Allaah Humswalia mara kumi. Kisha niombeeni kwa Allaah Wasylah, kwani Wasylah ni daraja peponi, haitakikani isipokuwa kwa mja kati ya Waja wa Allaah, nami nataraji niwe mimi. Basi mwenye kuniombea Wasylah, atastahiki kupata shufaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (384), Abuu Daawuud (523), At-Tirmidhiy (3694) na An-Nasaaiy (4/95)].
Jaabir anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kusema wakati anaposikia adhana: Ewe Mola wa wito huu uliotimu, na Swalaah ya kudumu! Mpe Muhammad Wasylah na daraja ya juu zaidi, na Mfufue Umpe maqaam ya kuhimidiwa Uliyomwahidi, basi atastahiki kuipata shufaa yangu Siku ya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (614), Abuu Daawuud (529), At-Tirmidhiy (211) na An-Nasaaiy (2/27)].
3- Kushuhudia tawhiyd, risala, na kumridhia Allaah, Rasuli Wake na Dini Yake
Imepokelewa na Sa’ad bin Abiy Waqqaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kusema wakati anapomsikia mwadhini: Na mimi ninashuhudia kwamba hapana mola mwingine isipokuwa Allaah, Mmoja Asiye na mshirika, na nashuhudia kwamba Muhammad ni Mja Wake na Rasuli Wake, nimemridhia Allaah Mola, na Uislamu Dini, na Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi wasallam Rasuli, Hughufiriwa madhambi yake yaliyotangulia)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (386), Abuu Daawuud (525), At-Tirmidhiy (210) na An-Nasaaiy (2/26)].
4- Kuomba du’aa kati ya adhana na iqaamah
Kwa kuwa du’aa wakati huu hujibiwa. Anas anasema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Du’aa hairejeshwi kati ya adhana na iqaamah {basi ombeni})). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (521), At-Tirmidhiy (212), Ibn Khuzaymah (425) na Ahmad (3/155)].
Imepokelewa na ‘Abdullah bin ‘Amri kwamba mtu mmoja alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Waadhini wanatuzidi sana sisi”. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
((Sema kama wanavyosema, ukimaliza, omba utajibiwa)). [Haina ubaya: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (524), Ahmad (2/172) na Ibn Hibaan (1695)].
·
Kutoka Msikitini Baada Ya Adhana
Imepokelewa toka kwa Abu Ash-Sha’asha’a akisema: ”Tulikuwa tumeketi Msikitini pamoja na Abuu Hurayrah, na mwadhini akaadhini. Na hapo hapo, akasimama mtu mmoja akatoka Msikitini. Abuu Hurayrah akawa anamtizama mpaka akatoka nje, kisha akasema: “Ama huyu, hakika amemwasi Abal Qaasim Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (655), Abuu Daawuud (536), An-Nasaaiy (2/29) na At-Tirmidhiy (131)].
An-Nawawiy kasema: “Kutoka Msikitini baada ya adhana ni karaha mpaka aswali Swalaah ya faradhi ila kwa udhuru”. [Sharhu Muslim (5/157). Angalia Sunan At-Tirmidhiy (1/398) – Shaakir]
Ninasema: “Asitoke mtu ila kwa dharura kama kutawadha, au kuoga na kadhalika. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka baada ya kuqimiwa Swalaah na safu kunyoroshwa, akaoga kisha akarudi tena. Maelezo zaidi yatakuja katika mlango wa “Iqaamah”.
Al Haafidh katika Al Fat-h (2/143) anasema: “Mwenye hadathi, mwenye kutokwa na damu, aliyebanwa na haja na mfano wao, ni kundi moja na mwenye janaba. Pia, yule ambaye ni imamu katika Msikiti mwingine na mfano wake”.
·
Baadhi Ya Makosa Na Bid-’a Zinazohusiana Na Adhana
Adhana ni ‘ibaadah, na asili yake ni kuifanya kwa mujibu wa yaliyomo ndani ya wigo wa Sunnah basi. Yasiingizwe humo isipokuwa Aliyoyapanga Allaah na Rasuli Wake. Katika jamii zetu, kuna mambo mengi yenye kwenda kinyume pamoja na makosa mengi katika suala zima la adhana. Mfano wa hayo kwa ufupi ni:
(a)
Baadhi ya makosa ya waadhini
1- Kuvuta sana na kughani kwa madoido.
2- Kuongeza tamko la “Sayyidinaa” kwenye tamko la shahaadah.
3-Kuleta tasbihi, tawashihi na mfano wake kabla ya adhana.
4- Kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sauti kubwa baada ya adhana.
5- Kutowajibika na Sunnah za adhana tulizozitaja nyuma.
6- Kuacha adhana ya kwanza Alfajiri, na kuacha kufanya “tathwiyb” humo.
(b)
Baadhi ya makosa ya wenye kuisikia adhana
1- Kutowajibika na Sunnah tulizozitaja nyuma.
2- Kusema: (( الله أعظم والعزة لله )) wakati wa kusikia takbiyr.
3- Kuapa kwa haki ya adhana.
4- Kuzidisha: (( والدرجة العالية الرفيعة )) na (( إنك لا تخلف الميعاد )) katika du’aa ya baada ya adhana.
5- Kusema: (( لا إله إلا الله )) mwadhini anaposema takbiyr ya mwisho. Kwa kufanya hivi, wanakuwa wamemtangulia mwadhini.
(c)
Baadhi ya makosa wakati wa kuqimiwa Swalaah
1-Kutomjibu mwenye kuqimu
2- Kusema: (( أقامها الله وأدامها )) wakati mwenye kuqimu anaposema: (( قد قامت الصلاة ))
3- Kusema baada ya iqaamah: (( اللهم أحسن وقوفنا بين يديك ))