017-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Waajibati Za Swalaah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
017-Waajibati Za Swalaah
Waajibati ni yale ambayo ni lazima kuyafanya au kuyasema katika Swalaah. Mambo haya yanapomoka kwa kusahau lakini huungwa kwa sijdah ya kusahau, na mwenye kuacha kwa kusudi, Swalaah yake itabatilika ikiwa anajua kwamba aliloliacha ni wajibu.
Tafsiri hii ni kwa Mahanafi na Mahanbali isipokuwa Mahanafi hawaoni kwamba mwenye kuwacha la wajibu kwa makusudi Swalaah yake inabatilika, bali atapata madhambi na anakuwa fasiki anayestahiki adhabu!!
Ama Maalik na Ash-Shaafi’iy, wao hawana isipokuwa nguzo na Sunnah kimjumuisho.
Wajibati katika Swalaah ni:
1- Du’aa ya ufunguzi wa Swalaah
Kwa mujibu wa kauli yenye nguvu, du’aa hii ni wajibu sawasawa ikiwa Swalaah ni ya faradhi au ni ya Sunnah. Ni lazima Swalaah ianzwe kwa du’aa hii baada ya takbiyr na kabla ya kusoma Al-Faatihahh kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya Rifa’a bin Raafi’i kwa aliyeswali kwa kukosea:
((Hakika haitimu Swalaah ya yeyote katika watu mpaka atawadhe..kisha apige takbiyr, amhimidi Allaah Mtukufu na amsifu, asome kilicho chepesi katika Qur-aan. Na anapofanya hivi, basi Swalaah yake imetimia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (859), An-Nasaaiy (2/20), At-Tirmidhiy (302) na Ibn Maajah (460)].
Neno lake ((Amhimidi Allaah Mtukufu na amsifu)) linaonyesha kwamba ni du’aa ya ufunguzi. Asw-Swan-’aaniy amesema: “Huchukuliwa kutokana na kauli hii kwamba ni wajibu kufanya himdi yoyote na sifa yoyote baada ya takbiyr ya kuhirimia Swalaah”. [Subulus Salaam (1/312)]
Ninasema: “Hakuna kinachozuia kusema kuwa ni wajibu, kwa kuwa Hadiyth ni Swahiyh, na hakuna makhitilafiano yoyote yaliyotokea kwa Ijma’a. Kusema kuwa ni wajibu ni kwa riwaya toka kwa Ahmad iliyokubaliwa na Ibn Battwah. [Al-Furu’u (1/413) na Al-Inswaaf (2/120)]
Na Ibn Rushdi katika Bidaayatul Mujtahid (1/172) ametoa kauli inayosema kwamba du’aa ya ufunguzi ni wajibu katika Swalaah akinukuu toka kwa Ash-Shaafi’iy na Abuu Haniyfah!! Nami sikupata linalotilia nguvu maneno haya kutoka kwa wawili hawa isipokuwa yaliyoandikwa kwenye Ad-Durru Al-Mukhtaar (1/476) yanayozingatia kwamba (kumsifu Allaah) ni katika mambo ya lazima katika Swalaah.
Na asili katika du’aa hii ya ufunguzi ni kufanywa kwa sauti ya chini, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuisoma kwa sauti ya juu na hata Maulamaa wote pia. Lakini katika baadhi ya nyakati, inafaa kwa Imamu kunyanyua sauti ili awafundishe watu. [Imetajwa mfanowe katika Al-Mughniy (2/145) toka kwa Ahmad]
Ni kama alivyofanya ‘Umar bin Al-Khattwaab aliposema: ((Subhaanakal Laahumma wa bihamdika))”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (399) ikiwa ni Munqatwi-’i. Ad-daaraqutwniy (1/199) na Al-Bayhaqiy (2/34) wameifanya ni Mawswuwl na wametilia nguvu kuwa ni Mawquwf. Naye ‘Abdur Raaziq (2555-2557) na Ibn Shaybah (1/230) wameifanyia “ikhraaj” kwa njia ya kuwa Mawswuwl na Munqatwi-’i. Angalia Al-Majmu’u (3/277) na Al-Irwaa (340)]
·
Du’aa Ya Ufunguzi Haisomwi Mahala Pawili
1- Katika Swalaah ya Maiti:
Du’aa hii haisomwi katika Swalaah hii kwa kuwa ni Swalaah ya muundo wa uhafifu na ufupi. Imepokelewa toka kwa Twalha bin ‘Ubaydul Laah bin ‘Awf aliyesema: “Niliswali nyuma ya ‘Abbaas katika Swalaah ya maiti. Alisoma Suwrat Al-Faatihahh akasema: Ili wajue kwamba ni Sunnah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1335), Abuu Daawuud (3182), At-Tirmidhiy (1032), Ibn Maajah (2490), na An-Nasaaiy. Riwaya nyingine ni yake].
Na katika riwaya nyingine: “Akasoma Suwrat Al-Faatihah na Suwrah kwa sauti ili tupate kumsikia”.
Hapa kuna ishara ya kuwa du’aa ya ufunguzi haisomwi katika Swalaah ya maiti kwa kuwa hakuisoma ili awajulishe kama alivyodhihirisha kisomo cha Suwrat Al-Faatihah.
Imesemwa: “Bali inasomwa katika Swalaah hiyo kama Swalaah nyinginezo lakini kauli ya kwanza ndiyo iliyo karibu zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.”
2- Aliyetanguliwa kama atamkuta imamu hayuko katika kisimamo
Huyu hataisoma du’aa hii kwa kuwa mahala pake pashapita.
·
Muundo Wa Matamko Ya Du’aa Ya Ufunguzi
Kuna matamko mbalimbali sahihi ya du’aa hii yaliyopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kati ya matamko hayo ni:
1- Hadiyth ya Abuu Hurayrah asemaye: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoifungua Swalaah yake, hunyamaza kidogo hivi kabla ya kusoma. Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Naapa kwa baba yangu na mama yangu! Nakuona ukinyamaza kati ya takbiyr na kisomo, nini unasoma? Akasema: ((Ninasema:
اللهم باعد بيني وبين خطاياي كما باعدت بين المشرق والمغرب، اللهم نقني من خطاياي كما ينقى الثوب الأبيض من الدنس، اللهم اغسلني من خطاياي بالثلج والماء والبرد.
Al-Laahumma Baa’id bayniy wabayna khatwaayaaya kamaa Baa’adta baynal mashriqi wal maghribi. Al-Laahumma Naqqiniy min khatwaayaaya kama yunaqqa ath-thawbul abyadhu minad danasi. Al-Laahumma Ghsilniy min khatwaayaayi bith-thalji wal maai wal baradi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (744) na Muslim (598)].
2- Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) aliyesema: “Tulikuwa tunaswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na mtu mmoja katika kundi akasema: ((Allaahu Akbaru Kabiyraa, wal-Hamdulil-Laahi Kathiyraa, wa Subhaanal-Laahi bukratan wa aswiylaa”. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Nimestaajabishwa nayo, milango ya mbingu imefunguliwa kwayo)).
Ibn ‘Umar akasema: “Sikuacha tokea nilipomsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiyasema hayo.”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (601), At-Tirmidhiy (3592) na An-Nasaaiy (2/125)].
3- Hadiyth ya ‘Aaishah, Abuu Sa’iyd na wengineo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema wakati akifungua Swalaah:
(( سبحانك اللهم وبحمدك، وتبارك اسمك، وتعالى جدك، ولا إله غيرك))
((Subhaanakal Laahumma wa Bihamdika, wa Tabaaraka Smuka, Wa Ta’alaa Jadduka, wa Laailaaha ghayruka)). [Hadiyth Hasan kwa Sanad zake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (776), At-Tirmidhiy (234), An-Nasaaiy (2/132), Ibn Maajah (806) na wengineo. Angalia Al Irwaa (341)].
Tumeshasema kwamba ‘Umar alikuwa akifungulia kwayo Swalaah.
4- Hadiyth ya ‘Aliyyi (Radhwiya Allaahu Anhu): “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposimama kwa ajili ya Swalaah husema:
وجهت وجهي للذي فطر السموات والأرض حنيفا وما أنا من المشركين، إن صلاتي ونسكي ومحياي ومماتي لله رب العالمين، لا شريك له وبذلك أمرت وأنا أول المسلمين، اللهم أنت الملك، لا إله إلا أنت، أنت ربي وأنا عبدك، ظلمت نفسي واعترفت بذنبي فاغفر لي ذنوبي جميعا، إنه لا يغفر الذنوب إلا أنت، واهدني لأحسن الأخلاق لا يهدي لأحسنها إلا أنت، واصرف عني سيئها لا يصرف عني سيئها إلا أنت، لبيك وسعديك، والخير كله بيديك، والشر ليس إليك، أنا بك وإليك، تباركت وتعاليت، أستغفرك وأتوب إليك
Wajjahtu wajhiy lil Ladhiy Fatwaras Samaawaati wal Ardhwa haniyfan wamaa ana minal mushrikiyna, inna Swalaahaty wa nusukiy wamhyaaya wa mamaaty lil-Laahi Rabbil ‘aalamiyna, laa shariyka lahu, wabidhaalika umirtu wa ana awwalul Muslimiyna. Allaahumma Antal Maliku, laailaaha illaa Anta, Anta Rabbiy wa ana ‘Abduka, dhwalamtu nafsiy wa’ataraftu bidhanbiy jamiy’an, innahuu laa yaghfiru dh-dhunuuba illaa Anta, wahdiniy liahsanil akhlaaq laa yahdiy liahsanihaa illaa Anta, wa swrif ‘anniy sayyiahaa laa yaswrifu ‘anniy sayyiahaa illaa Anta. Labbayka wa sa’addayka, wal khayru kulluhuu biyadika, wash-sharru laysa ilayka, ana bika wa ilayka, Tabaarakta wa Ta’aalayta, astaghfiruka wa atuwbu ilayka)).
Tamko la: “Wa ana awwalul Muslimiyna” limethibiti, na hakuna tatizo lolote kumfuata Rasuli katika kulisoma. Inakuwa ni katika mlango wa kumfuata na si katika mlango wa mtu kujieleza kuwa yeye niMuislamu wa mwanzo.
Inasemwa kuwa alikuwa akilisema tamko hili katika Swalaah za faradhi na Sunnah. [Hadiyth Swahiyh:Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (771), Abuu Daawuud (760), At-Tirmidhiy (342) na An-Nasaaiy (2/130)].
Katika ambayo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifungulia Swalaah za usiku ni yale yaliyokuja katika:
5- Hadiyth ya ‘Aaishah akisema: “Alikuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifungua Swalaah yake ya usiku kwa kusema:
(( اللهم رب جبريل وميكائيل وإسرافيل، فاطر السموات والأرض، عالم الغيب والشهادة، أنت تحكم بين عبادك فيما كانوا فيه يختلفون، اهدني لما اختلف فيه من الحق بإذنك، إنك تهدي من نشاء إلى صراط مستقيم))
Allaahumma Rabba Jibriyl wa Miikaaiyl wa Israafiyl, Faatwiras Samaawaati wal ardhwi, ‘Aaalimal ghayb wash Shahaada, Anta Tahkumu bayna ‘ibaadika fiymaa kaanuw fiyhi yakhtalifuuna, Ihdiniy limakhtulifa fiyhi minal hakki biidhnika, innaka Tahdiy man Tashaau ilaa swiraatin mustaqiym)). [Hadiyth Swahiyh:Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (770)].
Ninasema: “Kuna du’aa nyingine sahihi za kufungulia Swalaah mbali ya hizi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na anayetaka aziangalie kwenye vitabu husika”. [Angalia Swifatu Swalaatin Nabiy cha Al-Albaaniy (ukurasa wa 91-95) chapa ya Al-Ma’arif]
Katika matamko yaliyotangulia, kila kundi katika Maulamaa limechagua tamko lake mahsusi. [Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (3/86), Al-Ummu (1/106) na Masaail Ahmad cha Abuu Daawuud (30)]
Ath-Thwariy, Ahmad, Is-Haaq na Abuu Haniyfah na wenzake wamechagua yaliyopokelewa toka kwa ‘Umar [na ‘Aaishah na Abuu Sa’iyd].
Ash-Shaafi’iy amechukua Hadiyth ya ‘Aliyy. Abu Thawr anasema: “Yoyote atakayoisema itamtosheleza”, na Ibn Al-Mundhir ameichagua.
Ninasema: “Imesuniwa kusoma du’aa hii au ile ambayo ni nyepesi kwa mtu katika du’aa hizi”.
Ama Maalik (Allaah Amrehemu), alikuwa haoni kwamba du’aa hii ipo, au “isti’aadhah”, au “basmalah”!! [Al-Awsatw (3/86) na Al-Mudawwanah (1/62)] Na Hadiyth hizi na zinginezo ni hoja dhidi yake. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
2- Kusema “Isti’aadhah” (A’uwdhu bil Laahi minash-shaytwaanir rajiym) kabla ya kusoma
Ni wajibu kwa kauli yenye nguvu kutokana na Kauli Yake Ta’alaa:
((فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ))
((Unapotaka kusoma Qur-aan basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa)). [An-Nahl (16:98)]
Katika Aayah hii, kuna amri ya kufanya isti’aadhah wakati mtu anapotaka kusoma Qur-aan, na uhakika wa amri hii ni wajibu kwa kuwa isti’aadhah inaondosha shari ya shaytwaan. Na lile ambalo wajibu hautimu ila kwalo, basi linakuwa wajibu.
Kati ya waliosema kuwa hili ni wajibu ni pamoja na ‘Atwaa, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy, Daawuud na Ibn Hazm, nayo ni riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Muhallaa (3/247), Al-Majmu’u (3/281), Al-Furu’u (1/413) na Al-Inswaaf (2/120)]
Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba isti’aadhah ni Sunnah, na Maalik ameizuia!! [Ibn ‘Aabidiyn (1/328), Al-Dusuwqiy (1/251), Mughnil Muhtaaj (1/156) na Kash-Shaaf Al-Qina’a (1/335)]
· Miundo Ya Matamko Ya Isti’aadhah
Mwanzoni mwa kusoma Suwrah, isti’aadhah inaweza kusomwa kwa matamko yafuatayo:
- أعوذ با لله من الشيطان الرجيم
A’uwdhubil Laahi minash-shaytwaanir rajiym.
- أعوذ بالله السميع العليم من الشيطان الرجيم
A’uwdhubil Laahi As-Samiy’il ‘Aliym minash-shaytwaanir rajiym.
- أعوذ بالله السميع العليم من الشيطان الرجيم من همزه ونفخه ونفثه
A’uwdhubil Laahi As-Samiy’il ‘Aliym minash-shaytwaanir rajiym min hamzihi wa nafkhihi wa nafthih.
Ibn Qudaamah katika Al-Mughniy (2/146) anasema: “Huu wote ni wasaa, vyovyote atakavyoisema isti’aadhah, basi ni vyema”.
· Kuisoma Kimya Kimya
Asili ya isti’aadhah ni kuisoma kimya kimya, kwani haikunukuliwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliisoma kwa sauti wala kwa Makhalifa wake waongofu kuwa wao walidumu kuisoma kwa sauti. Lakini imamu katika baadhi ya nyakati, anaweza kuisoma kwa sauti ili awafundishe watu kwa mfano uliotangulia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas.
· Je, Atairejea Kila Rakaa?
Maulamaa wengi wamesema kwamba inamtosheleza mtu kuisoma katika rakaa ya kwanza tu. Ash-Shaafi’iy anaona ni vizuri isomwe katika kila rakaa, na Ibn Siyriyn amesema kuwa ni lazima. [Al-Awsatw (3/89). Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (3/254) anasema kuwa ni lazima kusoma “isti’aadhah” katika kila rakaa ya kwanza]
Ninasema: ”Uzingatio wa kusema ni wajibu ni kuwa Aayah inalazimia kukariri isti’aadhah wakati wa kuikariri Aayah. Na inapotokea mtengano kati ya visomo viwili kwa rukuu, sujudi na mfano wake, hapo inabidi kusoma isti’aadhah. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.
3- Kuitikia “Aamiyn” baada ya Al-Faatihah
Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Imamu anaposema aamiyn, nanyi pia semeni aamiyn, kwani yeyote ambaye aamiyn yake inakutana na ya Malaika, hughufiriwa madhambi yake yaliyotangulia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (780) na Muslim (410) kutoka kwa Hadiyth ya Abuu Hurayrah].
Jamhuri ya Maulamaa wameichukulia amri hii kama ni amri ya Sunnah, nami sikupata njia yoyote ya kuitoa amri hii nje ya uwajibu!!
Ibn Hazm amesema: “Ni wajibu kwa maamuma. Ama mwenye kuswali peke yake, au imamu, hao kwao ni Sunnah kutokana na Hadiyth iliyotangulia. [Ibn ‘Aabidiyn (1/320), Ad-Dusuwqiy (1/248), Mughnil Muhtaaj (1/160) Kash-Shaaful Qina’a (1/339), Al-Muhallaa (3/262) na Naylul Awtwaar (2/258)]
Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapomaliza kusoma Al-Faatihah husema “Aamiyn” kwa sauti na huivuta sauti yake. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy katika Juz-ul Qiraa-at na Abuu Daawuud (932). Al-Albaaniy kasema kuwa ni Hadiyth Swahiyh katika Swifatus Swalaahat ukurasa wa 101].
Lililo sahihi ni kuwa kusema aamiyn ni lazima kwa imamu, maamuma, na mwenye kuswali peke yake katika hali yoyote, kwa sauti katika Swalaah ya kusoma kwa sauti, na kimya kimya katika Swalaah ya kusoma kimya kimya. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.
4, 5, 6- Takbiyr za kuhama (toka nguzo kwenda nguzo), kusema “Sami’al Laahu liman hamidah”, na kusema “Rabbanaa lakal hamdu”.
Ni kwa dalili zifuatazo:
1- Neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Anapopiga takbiyr na nyinyi pigeni takbiyr, na anaposema: Sami’al Laahu liman hamida”, nanyi semeni: “Al-Laahumma Rabbanaa lakal Hamdu”)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (722) na Muslim (409)].
2- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alidumu kufanya hivyo. Abuu Hurayrah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapotaka kuswali, hupiga takbiyr wakati anaposimama, kisha hupiga takbiyr wakati anaporukuu, halafu husema: ”Sami’al Laahu liman hamidah” wakati anapounyanyua mgongo wake toka kwenye rukuu, kisha husema huku amesimama: “Rabbanaa lakal Hamdu”. Kisha hupiga takbiyr wakati anapopomoka (kwenda sijdah), halafu hupiga takbiyr wakati anapokinyanyua kichwa chake, kisha hupiga takbiyr wakati anaposujudu, halafu hupiga takbiyr wakati anapokinyanyua kichwa chake, kisha hufanya hivyo hivyo katika Swalaah yake yote mpaka anapoimaliza. Na hupiga takbiyr wakati anaponyanyuka baada ya kikao cha rakaa mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (289) na Muslim (392)]
Mfano wa haya, yako katika Hadiyth ya Abuu Hamiyd As-Saa’idiy.
Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (631)].
3- Amri ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea katika Hadiyth ya Rifa’a bin Raafi’i:
((Hakika haitimu Swalaah ya yeyote katika watu mpaka atawadhe, na atawadhe kama inavyotakikana, kisha aseme: Allaahu Akbar na amhimidi Allaah ‘Azza wa Jalla na amsifu, kisha asome akitakacho katika Qur-aan, halafu aseme: Allaahu Akbar, kisha arukuu mpaka viungo vyake vitulie, halafu aseme: “Sami’al Laahu liman Hamidah” mpaka alingamane wima sawasawa, kisha aseme: “Allaahu Akbar”, kisha asujudu mpaka viungo vyake vitulie, halafu aseme: “Allaahu Akbar”, na anyanyue kichwa chake mpaka alingamane hali amekaa, kisha aseme: “Allaahu Akbar”, kisha asujudu mpaka viungo vyake vitulie. Halafu anyanyue kichwa chake apige takbiyr. Anapofanya hivi, basi Swalaah yake imetimu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (859), An-Nasaaiy (2/2), At-Tirmidhiy (302) na Ibn Maajah (460)].
4- Ni ujulisho wa kuhama toka nguzo hadi nyingine, na kipengee kwenda kingine. [Ash-Sharhul Mumti’i (3/432)]
Na mambo haya matatu ni wajibu katika Swalaah kwa mtu anayeswali peke yake, imamu na maamuma kwa kauli sahihi. Ni madhehebu ya Hanbali, na ni Sunnah kwa upande wa Jamhuri. [Ibn ‘Aabidiyn (1/334), Ad-Dusuwqiy (1/243), Mughnil Muhtaaj (1/165) na Kash-Shaaful Qinaa (1/348)]
· Faida
Imepokewa kwa njia sahihi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) matamko manne katika tahmiyd baada ya kusema “Sami’al Laahu liman Hamida”, nayo ni:
1- ((ربنا لك الحمد))
Rabbanaa walakal Hamdu
[Al-Bukhaariy (689) na Muslim (392)]
2- ((اللهم ربنا ولك الحمد))
Allaahumma Rabbanaa walakal Hamdu
[Al-Bukhaariy (795), At-Tirmidhiy (3432), An-Nasaaiy (1060) na Abuu Daawuud (770)]
3- ((ربنا لك الحمد))
Rabbanaa lakal Hamdu
[Al-Bukhaariy (722) na Muslim (409)]
4- ((اللهم ربنا لك الحمد))
Allaahumma Rabbanaa lakal Hamdu
[Al-Bukhaariy (792) na Muslim (404)]
7- Tasbiyh katika rukuu na sujudi
Ni kusema “Subhaana Rabbiyal ‘Adhwiym” katika rukuu, na “Subhaana Rabbiyal A’alaa” katika sijdah. Ahmad bin Hanbal, Is-Haaq, Daawuud na Ibn Hazm wanasema kwamba ni lazima katika Swalaah. [Al-Inswaaf (2/115) na Al-Muhallaa (3/260)]
Dalili zao ni:
1- Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir aliyesema: “Wakati iliposhuka Aayah:
(( فسبح باسم ربك العظيم ))
..Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituambia: ((Ifanyeni katika rukuu zenu)), na iliposhuka Aayah:
(( سبح اسم ربك الأعلى))
..alituambia: ((Ifanyeni katika sujudi zenu)). [Isnadi yake ni Laini: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (869), Ibn Maajah (887) na Ahmad (16773)]
Maulamaa wamesema kwamba amri hii ni ya wajibu kwa vile Amri za Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimekusanyika, na pia kutokana na kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ninasema: “Hadiyth ni laini katika Sanad yake isipokuwa inaafikiana na haya yafuatayo yanayoitilia nguvu:
2- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Jueni na tambueni! Hakika mimi nimekatazwa kusoma Qur-aani katika rukuu na sijdah. Ama katika rukuu, basi mtukuzeni humo Mola ‘Azza wa Jalla. Ama sujudi, basi jitahidini kuomba du’aa humo, kwani ni stahikivu kwenu kujibiwa humo du’aa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (479) na Abuu Daawuud (876)].
3- Hadiyth ya Hudhayfah aliyesema: “Niliswali na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na katika rukuu alikuwa anasema: “Subhaana Rabbiyal ‘Adhwiym”, na katika sujudi: “Subhaana Rabbiyal A’alaa”. [Hadiyth Hasan Lighayrih: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (262), Abuu Daawuud (871), An-Nasaaiy (3/226) na Ibn Maajah (888)].
Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba tasbiyh katika rukuu na sujudi ni Sunnah na si wajibu kwa kigezo kwamba Rasuli hakumwamuru kufanya hivyo aliyeswali kwa kukosea. [Ibn ‘Aabidiyn (1/474), Mawaahibul Jaliyl (1/525), Al-Ummu (1/101), na Al-Majmu’u (3/410)]
Hili litapata uimara kwa yule anayeoina Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir kama ni Dhwa’iyf na pia haoni Hadiyth nyingine yenye kuisapoti Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas. Ama yule ambaye anaona kwamba Hadiyth ya ‘Uqbah iko sawasawa, basi itamlazimu kusema kuwa hilo ni wajibu.
8, 9- Tashah-hud ya kati na kikao chake
Ni kwa amri yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyeswali kwa kukosea katika Hadiyth ya Rifa’a – kwa kusema:
(( Unapokaa katikati ya Swalaah, basi tulizana ulitandike paja lako la kushoto, kisha fanya tashah-hudi)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (860) na Al-Bayhaqiy (2/133). Angalia Al-Irwaa (337)].
Na kwa dalili nyinginezo zilizotangulia zinazoonyesha kwamba tashah-hudi ya mwisho ni nguzo, tashah-hudi hii ya kati kati hatusemi kwamba ni nguzo kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoisahau, hakurudi tena kuifanya, bali aliiunga kwa sujudi ya kusahau. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1230) na Muslim (570) kutokana na Hadiyth ya ‘Abdullah bin Buhaynah]. Na lau kama ingelikuwa ni nguzo, basi isingeliungwa. [Ash-Sharh Al-Mumti’i (3/441)]
Ahmad, Is-Haaq, Al-Layth, Abuu Thawr, Daawuud na Ibn Hazm wanasema kuwa tashah-hudi ya katikati ni wajibu. Lakini Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba ni Sunnah. [Al-Muhallaa (3/268) na Al-Majmu’u (3/430)]
Kwa kuwa lau kama ingelikuwa ni wajibu, basi isingelipomoka kwa kuisahau kama nguzo za Swalaah!!
Inajibiwa kwamba hili linakuwa ni dalili lau kama sujudi ya kusahau inahusishwa kwa kuacha lisilo la wajibu, na hilo haliruhusiwi. [As-Saylul Jarraar (1/229)]
Bali sujudi ya kusahau haifanywi ila kwa kuacha la wajibu kwa kuwa asili ni kuzuia ziada katika Swalaah, na sujudi ya kusahau kabla ya tasliym ni ziada katika Swalaah, na kuzuia huku hakukiukwi ila kwa kufanya la wajibu. Na itakapokuwa sujudi ya kusahau ni wajibu kwa kuacha kwake, hilo litaonyesha kwamba ni wajibu, na kama si hivyo, basi kuwepo kwake na kutokuwepo kungelikuwa ni sawa)). [As-Sharhul Mumti’i (3/443-444)]
· Kusoma Tashah-hudi Kimya Kimya
Maulamaa wote kwa sauti moja wanasema kwamba tashah-hudi mbili husomwa kimya kimya na ni karaha kusoma kwa sauti. Ni kwa vile haikunukuliwa toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alisoma kwa sauti, na watu tokea enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka hivi leo wamerithiana kusoma kimya kimya, na kurithiana ni kama tawaaturi. [Al-Mabsuutw (1/32). Angalia Al-Awsatw (3/207) na Al-Majmuu (3/444)]