018-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sunnah Za Swalaah
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
018-Sunnah Za Swalaah
Sunnah za Swalaah ni maneno au matendo ambayo yamesuniwa kuyafanya ndani ya Swalaah. Mwenye kuyafanya hupata thawabu, na Swalaah haibatiliki kwa kuyaacha hata kwa kusudi, na kwa kuyaacha pia hakuna sujudi ya kusahau.
Ijulikane kwamba katika mlango huu kuna mambo ambayo Maulamaa wote kwa pamoja wamekubaliana nayo, na kuna mambo mengine ambayo Maulamaa wamekhitalifiana. Kwa hiyo, imekuwa ni vizuri zaidi niyathibitishe yale tu ambayo dalili zake ni sahihi bila ya kujisokomeza kwenye yale waliyokhitalifiana kwa ajili ya kuchelea urefushaji mada, kwani makusudio hasa ni kuujua mwongozo wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah yake ili tuweze kumfuata. Na baada ya kuujua mwongozo huu, hakuna madhara kumkhalifu mwenye kwenda kinyume vyovyote awavyo.
Sunnah hizi zimegawanyika katika Sunnah za kimaneno na Sunnah za kivitendo.
Sunnah Za Kimaneno
1- Kusoma baada ya Al-Faatihah
Imesuniwa kusoma Suwrah katika rakaa mbili za mwanzo baada ya Al-Faatihah kwa makubaliano ya Ijma’a ya Maulamaa. Aidha, imesuniwa vile vile, kusoma Suwrah wakati mwingine katika rakaa za tatu na nne.
Imepokelewa toka kwa Abuu Qataadah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika rakaa mbili za mwanzo za Adhuhuri na Alasiri Al-Faatihah pamoja na Suwrah na wakati mwingine anatusikilizisha Aayah, na katika rakaa mbili za mwisho husoma Al-Faatihah tu”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (421), na mfanowe, na katika Al-Bukhaariy (759)].
Ama kusoma Suwrah katika rakaa ya tatu na ya nne, hii ni kwa Hadiyth ya Abuu Sa’iyd Al-Khudriy akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Adhuhuri kwenye rakaa mbili za mwanzo kiasi cha aya 30 katika kila rakaa, na katika mbili za mwisho kiasi cha aya 15”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (452)].
Kutokana na Hadiyth hii, tunapata faida nyingine kuwa imesuniwa Suwrah zinazosomwa katika rakaa mbili za mwanzo ziwe ndefu zaidi kuliko katika rakaa mbili za mwisho.
Mambo mengine yaliyosuniwa hapa ni pamoja na:
- Kuisoma Qur-aan kwa tartiyl na kuitadaburi kwa mujibu wa Ijma’a ya Maulamaa. Ni makruhu kuisoma haraka haraka kutokana na Neno Lake Ta’alaa:
((أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا))
((Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali)). [Al-Muzzammil (73:4)]
- Kumwomba Allaah Mtukufu na kujilinda Kwake zinaposomwa Aayah za rehma au adhabu.
Imepokelewa toka kwa Hudhayfah akisema: “Niliswali pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku mmoja akaanza na Al-Baqarah. Alikuwa akisoma kwa tartiyl na utuvu. Akiipita Aayah yenye tasbiyh husabbih, akiipita yenye du’aa huomba, akiipita ya kujilinda hujilinda, kisha hurukuu”. Imesimuliwa na Muslim.
- Aseme ndani ya Swalaah “Subhaanal Laah” anaposoma Neno Lake Ta’alaa:
((سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ))
((Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Ametukuka kabisa kuliko vyote)). [Al-A’alaa (87:1)]
Na anaposoma:
((أَلَيْسَ ذَٰلِكَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يُحْيِيَ الْمَوْتَىٰ))
((Je hivyo sivyo (Allaah Anayeumba) kuwa ni Muweza wa kuhuisha wafu?)) [Al-Qiyaamah (75:40)]
..aseme “Subhaanaka fabalaa”. Dalili thabiti ya mawili haya ipo.
- Anaposoma:
((أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ))
(( Je, kwani Allaah Si Mwadilifu zaidi wa wanaohukumu kuliko mahakimu wote?)) [At-Tiyn (95:8)]
..hairuhusiwi kusema: “Balaa, wa ana ‘alaa dhaalika minash shaahidiyn”, au kusema: “Aaman-naa bil Laahi” mtu anaposoma:
((فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَهُ يُؤْمِنُونَ))
(( Basi kauli gani baada ya hii (Qur-aan) wataiamini?)) [Al-Mursalaat (77:50)]
Au kusema: “Ista-‘antu bil Laahi” imamu anaposoma:
((إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ))
((Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada)). [Al-Faatihahh (1:5)]
Haya yote hayana Hadiyth yoyote inayoyathibitisha.
2- Kufanya adhkaari zifuatazo katika rukuu:
1-
(( اللهم لك ركعت، ولك أسلمت وبك آمنت، خشع لك سمعي وبصري ومخي وعظمي وعصبي ))
(( Allaahumma laka raka’atu, wa laka aslamtu wa bika aamantu, khasha’a laka sam’iy wa baswariy wa mukh-khiy wa ‘adhwmiy wa ‘aswabiy)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (771), At-Tirmidhiy (4317), Abuu Daawuud (760) na An-Nasaaiy (2/130)].
2-
(( سبحانك اللهم ربنا وبحمدك اللهم اغفر لي ))
(( Subhaanakal Laahumma Rabbanaa wa bihamdika, Allaahumma Ghfir liy)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/247) na Muslim (484) na wengineo].
3-
(( سبوح قدوس رب الملائكة والروح ))
((Subbuwhun Qudduwsun Rabbul Malaaikati war Ruwh)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (487) na Abuu Daawuud (872)].
4-
(( سبحان ذي الجبروت والملكوت والكبرياء والعظمة ))
((Subhaana Dhil Jabaruuti wal Malakuuti wal Kibriyaa wal Adhwamah)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (873) na An-Nasaaiy (2/191) kwa Sanad Swahiyh].
3- Kufanya dhikri baada ya kusimama kutoka kwenye rukuu na baada ya kusema “Rabbanaa Lakal Hamdu”. Adhkaar hizo ni:
1-
(( اللهم ربنا لك الحمد ملء السموات وملء الأرض وملء ما بينهما وملء ما شئت من شيئ بعد، أهل الثناء والمجد، أحق ما قال العبد وكلنا لك عبد، اللهم لا مانع لما أعطيت، ولا معطي لما منعت، ولا ينفع ذا الجد منك الجد))
((Al- Laahumma Rabbanaa Lakal Hamdu mil-as Samaawaati wa mil-al Ardhi wa mil-a maa baynahumaa wa mil-a maa shiita min shay-in baadu. Ahluth-Thanaai wal Majdi, ahaqqu maa qaalal ‘Abdu wa kul- lunaa Laka ‘Abdun. Allaahumma laa maani’a limaa A’atwayta, walaa mu’utwiya limaa Mana’ata, walaa yanfa’u dhal jaddi minkal Jaddu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (477), Abuu Daawuud (747) na An-Nasaaiy (2/198)].
2-
(( ربنا ولك الحمد حمدا كثيرا طيبا مباركا فيه ))
((Rabbanaa wa Lakal hamdu hamdan kathiyran twayyiban mubaarakan fiyh)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/237), Abuu Daawuud (770), An-Nasaaiy (2/196) na At-Tirmidhiy (404)].
4- Kufanya dhikri katika sujudi. Adhkaar hizo ni:
1-
(( اللهم لك سجدت وبك آمنت، ولك أسلمت، سجد وجهي للذي خلقه وصوره، وشق سمعه وبصره، تبارك الله أحسن الخالقين))
((Al-Laahumma Laka sajadtu wa bika aamantu, wa Laka aslamtu, sajada wajhiy lil Ladhiy Khalaqahu wa Swaw-warahu, wa Shaqqa sam’ahu wa baswarahu. Tabaaraka Allaahu Ahsanul khaaliqiyna)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (771). Imeshatangulia].
2-
(( سبحانك اللهم ربنا وبحمدك اللهم اغفرلي ))
((Subhaanaka Al-Laahumma Rabbanaa wa bihamdika Allaahumma Ghfir liy )).
3-
(( سبوح قدوس رب الملائكة والروح ))
(( Subbuwhun Qudduwsun Rabbul Malaaikati war Ruwh)).
4-
(( سبحان ذي الجبروت والملكوت والكبرياء والعظمة ))
((Subhaana Dhil Jabaruuti wal Malakuuti wal Kibriyaa wal Adhwamah)). [Zote tatu zimetajwa hivi karibuni katika adhkaar za rukuu].
5- Kukithirisha kuomba du’aa katika sujudi kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Ama sujudi, basi jitahidini kuomba du’aa humo, kwani ni stahikivu kwenu kujibiwa humo du’aa)). [Imetajwa hivi karibuni]
Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema wakati anaposujudu:
(( اللهم اغفر لي ذنبي كله، دقه وجله وأوله وآخره وعلانيته وسره))
((Allaahumma Ghfir liy dhanbiy kullahu, diqqahu wa jullahu, wa aw-walahu wa aakhirahu, wa ‘alaaniyyatahu wa sirrahu)) [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (483)].
5- Kuomba du’aa kati ya sijdah mbili. Du’aa hizo ni kama:
1-
((اللهم اغفر لي وارحمني واجبرني واهدني وارزقني))
((Allaahumma Ghfir liy Warhamniy Wajburniy Wahdiniy Warzuqniy)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (850) na At-Tirmidhiy (284). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].
2-
(( رب اغفرلي ..رب اغفر لي ))
(( Rabbi Ghfir liy..Rabbi Ghfir liy )). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (874) na An-Nasaaiy (3/226). Angalia Al-Irwaa (335)].
6- Kumswalia Rasuli baada ya tashah-hudi ya kwanza na ya mwisho
Imepokewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Tulikuwa tukimtayarishia Rasuli wa Allaah mswaki wake na maji yake ya kutawadhia. Halafu Allaah Humwamsha katika wakati Alioutaka usiku. Hupiga mswaki na kutawadha, kisha huswali rakaa tisa; hakai kati ya rakaa hizo isipokuwa katika rakaa ya nane. Na hapo humwomba Mola wake na humswalia Rasuli Wake, kisha hunyanyuka na wala hatoi tasliym. Kisha huswali rakaa ya tisa, akakaa, halafu humhimidi Mola wake, humswalia Nabii Wake, kisha hutoa tasliym”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (746)].
Tamko bora zaidi la kumswalia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni:
(( اللهم صل على محمد وعلى آل محمد كما صليت على آل إبراهيم إنك حميد مجيد، اللهم بارك على محمد وعلى آل محمد كما باركت على إبراهيم إنك حميد مجيد))
((Allaahumma Swalli ‘alaa Muhammadin wa’alaa aali Muhammadin kama Swallayta ‘alaa aali Ibraahiyma innaka Hamiydun Majiydun. Allaahumma Baariyk ‘alaa Muhammadin wa’alaa aali Muhammadin kamaa Baarakta ‘alaa Ibraahiyma innaka Hamiydun Majiydun)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6357), Muslim (406) na wengineo].
7- Du’aa baada ya tashah-hudi ya kwanza na ya pili
Du’aa baada ya tashah-hudi ya kwanza imekuja kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mnapokaa katika kila rakaa mbili semeni: At-Tahiyyaatu lil-Laahi, was- Swalawaatu wat-Twayyibaatu, As- Salaamu ‘alayka ayyuhan-Nabiyyu warahmatul-Laahi wabarakaatuhu, as- Salaamu ‘alaynaa wa’alaa ‘ibaadil-Laahis-Swaalihiyna. Ash-hadu an laailaaha illal-Laahu wa ash-hadu anna Muhammadan ‘Abduhu wa Rasuwluhu. Kisha achague mmoja wenu du’aa inayompendeza, halafu amwombe Mola wake ‘Azza wa Jalla)). [“Takhriyj” yake ishatangulia].
Ama baada ya tashah-hudi ya pili ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Anapomaliza mmoja wenu tashah-hudi ya mwisho, basi ajilinde kwa Allaah na mambo manne: Adhabu ya Jahannam na adhabu ya kaburi, fitna ya uhai, fitna ya mauti, na shari ya Masihi Dajjaal)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3/192), Muslim (588) na wengineo].
Na katika riwaya: ((na madhambi na madeni)).
Kuna du’aa nyinginezo Swahiyh kati ya tashah-hudi na tasliym. Kati ya du’aa hizo ni:
1-
(( اللهم إني ظلمت نفسي ظلما كثيرا، ولا يغفر الذنوب إلا أنت، فاغفر لي مغفرة من عندك، وارحمني إنك أنت الغفور الرحيم)).
(( Allaahumma inniy dhwalamtu nafsiy dhulman kathiyran, walaa yaghfiru dh-dhunuwba illaa Anta, Faghfir liy maghfiratan min ‘in-dika, warhamniy Innaka Anta Al-Ghafuwru Ar Rahiymu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6357), Muslim (406)].
2-
(( اللهم اغفر لي ما قدمت وما أخرت، وما أسررت وما أعلنت، وما أسرفت، وما أنت أعلم به مني، أنت المقدم، وأنت المؤخر لا إله إلا أنت ))
((Allaahumma Ghfir liy maa qaddamtu wamaa akh-khartu, wamaa asrartu wamaa a’alantu, wamaa asraftu, wamaa Anta A’alamu bihii minniy, Anta Al-Muqaddimu, wa Anta Al-Muakh-khiru laa ilaaha illaa Anta)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (771), Abuu Daawuud (760), At-Tirmidhiy (3417) na An-Nasaaiy (2/130)].
8- Tasliym ya pili
Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitoa tasliym mbili. Imepokelewa na ‘Aamir bin Sa’ad toka kwa baba yake akisema: “Nilikuwa nikimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akitoa tasliym kuliani kwake na kushotoni kwake mpaka ninaona weupe wa shavu lake”. [Imepokewa na Muslim (1/582)].
Tasliym ya kwanza ni nguzo lakini ya pili ni Sunnah. Imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitosheka na ya kwanza basi. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitoa tasliym moja mkabala wa uso wake akimili kidogo upande wa kulia)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (295) kwa Sanad Swahiyh].
9- Kuleta nyiradi na kuomba du’aa baada ya Swalaah
Ama nyiradi, kuna Hadiyth kadhaa Swahiyh zilizothibitisha hilo. Kati ya hizo ni:
1- ((Mwenye kufanya tasbiyh baada ya kila Swalaah mara 33, akamhimidi Allaah mara 33, na akapiga takbiyr mara 33, basi hizo ni mara 99, na akasema katika kutimiza 100: Laa ilaaha illa Allaahu Wahdahuu laa shariyka Lahuu, Lahul Mulku, Walahul Hamdu, wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr, basi husamehewa makosa yake hata kama yako mithili ya povu la bahari)). [Imepokewa na Muslim (597)].
2-
(( لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد وهو على كل شيئ قدير، لا حول ولا قوة إلا بالله، لا إله إلا الله، ولا نعبد إلا إياه، له النعمة والفضل، وله الثناء الحسن، لا إله إلا الله مخلصين له الدين ولو كره الكافرون))
((Laailaaha illa Allaahu Wahdahuu laa shariyka Lahuu, Lahul Mulku Walahul Hamdu Wahuwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyrun. Laa hawla walaa quwwata illaa bil Laahi, laa ilaah illa Allaahu, walaa na’abudu illaa Iyyaahu, Lahun ni’imata wal fadhwli, walahuth-thanaaul hasan. Laa ilaaha illa Allaahu mukhliswiyna Lahud Diyna walaw karihal kaafiruwna)). [Imepokewa na Muslim (594)].
3-
(( لا إله إلا الله، وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد، وهو على كل شيء قدير، اللهم لا مانع لما أعطيت ولا معطي اما منعت، ولا ينفع ذا الجد منك الجد))
((Laailaaha illa Allaahu Wahdahuu laa shariyka Lahuu, Lahul Mulku Walahul Hamdu Wahuwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyrun. Allaahumma laa maani’a limaa A’atwayta, walaa mu’utwiya lima Mana’ata, walaa yanfa’u dhal jaddi mikal jaddu)). [Imepokewa na Al-Bukhaariy (844) na Muslim (471)].
4- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapomaliza Swalaah yake husema: “Astaghfiru” mara tatu, kisha husema:
(( اللهم أنت السلام ومنك السلام، تباركت يا ذا الجلال والإكرام ))
((Allaahumma Anta As-Salaam waminka as-salaam, Tabaarakta yaa Dhal Jalaal wal Ikraam)). [Imepokewa na Muslim (591)].
5- Imepokelewa toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniamuru nisome “Mu’awwadhaati” baada ya kila Swalaah”. [Imepokewa na Abuu Daawuud (1523), At-Tirmidhiy (2903) na An Nasaaiy kwa Sanad Swahiyh].
6- ((Mwenye kusoma aayatil Kursiy baada ya kila Swalaah ya faradhi, hayatazuia kati yake na kuingia peponi isipokuwa mauti)). [Imepokewa na Ibn As-Sunniy kwa Sanad Swahiyh]
Ama du’aa za kuomba baada ya Swalaah, du’aa hizo zimethibiti kwa njia sahihi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa matamko mbalimbali. Kati yake ni:
1-
((اللهم أعني على ذكرك وشكرك وحسن عبادتك))
((Allaahumma A’inniy ‘alaa dhikrika wa shukrika wa husni ‘ibaadatika)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1508) na An-Nasaaiy (3/53) kwa Sanad Swahiyh].
2-
((اللهم إني أعوذ بك من الجبن، وأعوذ بك أن أرد إلى أرذل العمر، وأعوذ بك من فتنة الدنيا، وأعوذ بك من عذاب القبر))
(( Allaahumma inniy auwdhu bika minal jubni, wa auwdhu bika an uradda ilaa ardhalil ‘umuri, wa auwdhu bika min fitnatid dunyaa, wa auwdhu bika min ‘adhaabil qabri)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2822), At-Tirmidhiy (3562) na An-Nasaaiy (8/266)].
3-
(( رب قني عذابك يوم تبعث عبادك ))
((Rabbi Qiniy ‘adhaabaka yawma Tab’athu ibaadaka)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (709)].
4-
(( اللهم اغفر لي ما قدمت وما أخرت وما أسررت وما أعلنت وما أسرفت وما أنت أعلم به مني، أنت المقدم وأنت المؤخر، لا إله إلا أنت ))
(( Allaahumma Ghfir liy maa qaddamtu wamaa akh-khartu, wamaa asrartu, wamaa a’alantu, wamaa asraftu, wamaa Anta A’alamu bihii minniy, Antal Muqaddimu wa Antal Muakh-khiru, laailaah illaa Anta)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (771). Ishatajwa].
5-
((اللهم إني أسألك علما نافعا، ورزقا طيبا، وعملا متقبلا))
(( Al Laahumma inniy as-aluka ‘ilman naafi’an, wa rizqan twayyiban, wa ‘amalan mutaqqabalan )). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (771). Ishatajwa].
6-
(( اللهم إني أعوذ بك من الكفر والفقر وعذاب القبر))
((Allaahumma inniy a’uwdhubika minal kufri wal faqri wa ‘adhaabil qabri)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (8262) na Ibn As-Sunniy (111) kwa Sanad Hasan].
· Faida
Du’aa baada ya Swalaah inajibiwa Insha Allaah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Ni du’aa gani inajibiwa zaidi? Akajibu: ((Ni ile ya usiku wa manane, na baada ya Swalaah za faradhi)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (3499) na Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].
· Sunnah Za Kivitendo
1- Kuweka kizuizi katika Swalaah
Imesuniwa kuweka mbele kizuizi kitakachozuia mtu kupita mbele yake na kuzuia macho yake yasitembee huku na kule kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
(( إذا صلى أحدكم فليصل إلى سترة، وليدن منها، لا يقطع الشيطان عليه صلاته))
((Anaposwali mmoja wenu, basi aswali kikiweko kizuizi mbele yake na akikurubie ili shaytwaan asimkatizie Swalaah yake)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (681), An-Nasaaiy (2/62), na Al-Haakim (1/251). Tamko ni lake, nayo ni Swahiyh].
Kizuizi hiki kinaweza kuwa ni ukuta, nguzo, fimbo iliyokitwa na kadhalika. Uchache wa hilo ni kipande kidogo cha mbao anachokiegemea msafiri kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Anapoweka mmoja wenu mbele yake mfano wa kiegemeo cha msafiri, basi aswali na wala asishughulishwe na anayepita nyuma yake)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (499), At-Tirmidhiy (334) na Abuu Daawuud (671)].
Mtu akiweka kizuizi wakati anaswali, basi asimruhusu yeyote kupita mbele yake kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Anaposwali mmoja wenu, basi asimruhusu kabisa mtu kupita mbele yake na amzuie kwa nguvu zake zote. Na kama atakataa basi apigane naye, kwani huyo ni shaytwaan)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (487) na Muslim (505) na wengineo].
Na hii ingawa baadhi ya Maulamaa wamelipinga hili kwa dalili sahihi lakini haziko wazi, au kwa dalili wazi lakini si sahihi. Wanasema kwamba hakuna kitu chochote chenye kuweza kuikata Swalaah, kwani makusudio ya kuikata katika Hadiyth, ni kuikata khushuu na si kubatilika Swalaah kwa mtu kupita tu mbele yake. [Zaadul Ma’ad (1/306) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/424)]
· Faida mbalimbali
[Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/414)]
1- Kupita msichana mdogo ambaye hakubaleghe mbele ya mwenye kuswali, hakuikati Swalaah kwa kuwa haitwi mwanamke. Qataadah anasema: “Mwanamke haikati Swalaah ya mwanamke”. Na aliulizwa: “Je, msichana ambaye hajabaleghe anaikata Swalaah?” Akajibu: “Hapana”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Razzaaq katika Al-Muswannaf (2/28) kwa Sanad Swahiyh iliyoegemezwa kwa Qataadah].
2- Mwanamke akipita kulia au kushotoni mwa mwanamume anayeswali, basi haikati Swalaah yake.
3- Mwanamke akisimama pembeni mwa mwanamume Swalaah yake haibatiliki. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali usiku nami niko pembeni mwake nikiwa na hedhi na nimejifunika nguo, sehemu ya nguo iko pembezoni mwake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (499)].
4- Ikiwa panaswaliwa jamaa, basi hakuna ubaya kupita kati ya safu, kwa kuwa kizuizi cha imamu ndio kizuizi cha maamuma. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Nilikuja nikiwa nimepanda punda jike, na wakati huo nilikuwa nimekwisha baleghe. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaswalisha watu Mina. Nikapita mbele ya safu, nikateremka, kisha nikamwacha punda akajilie. Niliingia katika safu na hakuna yeyote aliyelipinga hilo”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (493), Muslim (504) na wengineo].
2- Kunyanyua mikono miwili wakati wa takbiyr ya kuhirimia, kurukuu, na kunyanyuka toka rukuuu. Pia wakati wa kunyanyuka toka tashah-hudi ya kwanza na katika kila kinyanyuko na kiinamo.
Imepokelewa na Naafi’i kwamba Ibn ‘Umar alikuwa anapoingia katika Swalaah hupiga takbiyr akanyanyua mikono yake miwili, anaporukuu hunyanyua mikono yake miwili, na anaposema “Sami’a Allaahu liman hamidah” na anaposimama toka rakaa mbili, hunyanyua mikono yake miwili”. Hilo limerufaishwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (739), Abuu Daawuud (727) na Hadiyth mwenza iko kwa Muslim (390)].
Ninasema: “Hizi ndizo sehemu nne ambazo ukokotezo wa kunyanyua mikono miwili uko lakini wakati mwingine imesuniwa kunyanyua mikono miwili katika kila kinyanyuko na kiinamo kutokana na Hadiyth ya Maalik bin Al-Huwayrath kwamba alimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinyanyua mikono yake katika Swalaah yake anaporukuu, anaponyanyua kichwa chake toka kwenye rukuu, anaposujudu na anaponyanyua kichwa chake toka kwenye sujudi mpaka mikono inakuwa usambamba wa ndwele za masikio yake.”[Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (2/206) na Ahmad (493). Ni Hadiyth Swahiyh].
· Mahala Pa Kunyanyua Mikono Na Namna Yake
Imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alikuwa wakati mwingine ananyanyua mikono yake pamoja na takbiyr, wakati mwingine baada yake, na wakati mwingine kabla yake. Imesuniwa ainyanyue mikono miwili vidole vikiwa vimenyooshwa, na aiweke mikono yake mkabala wa mabega yake kama ilivyo katika Hadiyth ya Abuu Qataadah [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy na wengineo]., au aiweke mkabala wa masikio yake mawili kama ilivyo katika Hadiyth ya Waail bin Hajar iliyotangulia.
3- Kuweka mkono wa kulia juu ya wa kushoto juu ya kifua
Imepokelewa toka kwa Shal bin Sa’ad akisema: “Watu walikuwa wakiamuriwa kwamba mwanamume aweke mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto katika Swalaah yake. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (740) na Maalik katika Al-Muwattwai (376)].
Imepokelewa toka kwa Waail bin Hajar akisema: “Niliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akaweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wake wa kushoto juu ya kifua chake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (479). Al-Albaaniy kasema ni Hadiyh Swahiyh katika Al-Irwaa (352)].
4- Kuangalia mahali pa kusujudia
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingia Al-Ka’abah macho yake hayakuacha kuangalia mahala anaposujudia mpaka alipotoka humo”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Haakim (1/479) na Al-Albaaniy kasema kuwa ni Hadiyth Swahiyh].
5- Kunyooka mgongo sawasawa katika rukuu bila kukinyanyua kichwa au kukiinamisha, kuyakamata magoti mawili kwa viganja na kuvitawanya vidole vyake, na kuviweka mbali viungabega na mbavu.
Ni kwa Hadiyth ya Abuu Humayda katika sifa ya Swalaah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: “Anaporukuu, huyakamata vizuri magoti yake, kisha huupindisha mgongo wake ukanyooka sawasawa bila kibyongo”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (828) na Abuu Daawuud (717)].
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaporukuu, hakinyanyui kichwa chake (kikawa juu kuliko mgongo) wala hakiteremshi, lakini inakuwa kati na kati”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498) na Abuu Daawuud (768)].
Na katika Hadiyth ya Abuu Humayd: “Kisha alirukuu, akaweka mikono yake juu ya magoti yake kana kwamba ameyakamata, na akaipindisha mikono yake ikawa mbali na mbavu zake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (720) na At-Tirmidhiy (259), nayo ni Swahiyh].
Imepokelewa na Waail bin Hajar akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anavitandaza vidole vyake anaporukuu”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (594) na Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh].
6- Kutanguliza mikono miwili kabla ya magoti wakati wa kwenda kusujudu
Ni kwa Hadiyth ya Abuu Hurayrah aliposema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( إذا سجد أحدكم فلا يبرك كما يبرك البعير، وليضع يديه قبل ركبتيه))
(( Anaposujudu mmoja wenu asipige magoti kama anavyopiga magoti ngamia bali atangulize mikono yake kabla ya magoti yake)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud, An-Nasaaiy na Ahmad kwa Sanad Swahiyh].
7- Kuambatisha paji la uso, pua na mikono miwili ardhini, kuiweka mikono miwili kando isigusane na mbavu, kuweka viganja viwili mkabala wa mabega mawili au masikio mawili, kunyanyua vifundo vya mikono miwili, kuikita miguu miwili barabara na kuvilingamanisha vifundo vyake, na kuvielekeza Qiblah vidole vya viganja na miguu.
Katika Hadiyth ya Abuu Humayda ameeleza: “Anaposujudu, huweka mikono yake miwili bila kutandaza vidole wala kuvibana, na huvielekeza Qiblah viungo vya mikono yake na miguu yake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy na Abuu Daawuud].
Na imepokelewa toka kwa ‘Abdullaah bin Buhaynah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaposwali, hutanua kati ya mikono yake mpaka ukaonekana weupe wa kwapa zake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (807), Muslim (495) na wengineo].
Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((Unaposujudu, viweke viganja vyako na unyanyue vifundo vya mikono yako)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (494)].
Na katika Hadiyth ya Abuu Humayda anasema: “Alikuwa anaposujudu, huambatisha pua yake na kipaji chake ardhini, huiweka mikono yake mbali na mbavu zake, na huweka viganja vyake mkabala wa mabega yake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah na At-Tirmidhiy].
Na katika Hadiyth ya ‘Aaishah anasema: “Nikamkuta amesujudu akiwa amevilingamanisha vifundo vya miguu yake na kuvielekeza vidole vyake Qiblah”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Khuzaymah (654) na Al-Bayhaqiy (2/116). Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh].
· Faida
Baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba mwanamke hutofautiana na mwanamume katika vipengee vya kurukuu na kusujudu. Wanasema kwamba mwanamke hukusanya viungo vyake kwa pamoja badala ya kuviweka mbalimbali na huyashikanisha mapaja yake na sehemu nyinginezo, kwani hilo ndio sitara zaidi kwake. [Angalia Sunan Al-Bayhaqiy (2/222), Al-Mughniy (1/562) na Subulus Salaam (1/308). Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (4/124) ameijibu hoja hii bila kupambanua kati ya mwanamke na mwanamume katika vipengee vya Swalaah]
Hakuna dalili yoyote yenye Sanad Swahiyh iliyokuja toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayoelezea utofauti wowote wa vitendo vya mwanamume na mwanamke katika Swalaah. Aidha, hakuna chochote swahiyh thabiti kilichopatikana toka kwa Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) chenye kuthibitisha hilo.
Hivyo basi, mwenye kushikamana na uasili, akavifanya sawa vipengee vyote vya Swalaah kati ya mwanamke na mwanamume kutokana na ujumuishi wa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)), basi rai yake huyo ndiyo iliyo sawa zaidi na yenye nguvu zaidi na hasahasa ikiwa mwanamke anaswali peke yake. Ama yule anayeona kinyume na hivyo na kwamba mwanamke anaamuriwa ajisitiri kiasi inavyowezekana, basi huyo ana mwelekeo wake. Mwelekeo huu wanao idadi kubwa ya Watangu wema. Allaahu Ndiye Mjuzi Zaidi. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa cha Sheikh wetu (1/378) kwa mabadilisho madogo]
8- Kuulaza mguu wa kushoto na kuusimika wa kulia katika kikao cha kati ya sijdah mbili
Imepokelewa na ‘Aaishah akisema: “Alikuwa akiulaza mguu wake wa kushoto na kuusimika mguu wake wa kulia”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (498) na Abuu Daawuud (768)].
Inajuzu wakati mwingine aisimike miguu yake miwili na avikalie visigino vyake kati ya sijdah mbili. Kikao hiki huitwa “Al-Iq’aau”. Hii ni kwa Hadiyth ya Twaawus aliyesema: “Tulimuuliza Ibn ‘Abbaas kuhusiana na kuisimika miguu na kuvikalia visigino viwili, akasema kuwa hiyo ni Sunnah. Tukamwambia: “Tunaona kuwa hilo ni ukavu kwa mwanamume”. Ibn ‘Abbaas akasema: “Bali hiyo ni Sunnah ya Nabii wako (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.
Imepokelewa na Abu Zubeyr akisema kwamba alimwona ‘Abdullah bin ‘Umar wakati ananyanyua kichwa chake toka katika sijdah ya kwanza, akikaa juu ya ncha za vidole vyake, kisha akasema: “Hii ni katika Sunnah”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (536), Abuu Daawuud (830) na At-Tirmidhiy (282)].
9- Kukirefusha kikao kati ya sijdah mbili
Hii ilikuwa ni maongozi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokelewa toka kwa Anas akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa kati ya sijdah mbili mpaka tunadhania pengine amepitikiwa”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (473)].
Sunnah hii watu wengi wameiacha baada ya kumalizika enzi ya Maswahaba. Na kwa ajili hiyo, Thaabit amesema: “Anas alikuwa akifanya jambo ambalo siwaoni mkilifanya; anakaa kati ya sijdah mbili mpaka tunasema: Pengine amesahau au amepitikiwa”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (536)].
10- Kikao baada ya sijdah kabla ya kusimama kwenda rakaa ya pili au ya nne
Imesuniwa baada ya kumaliza sijdah ya pili katika rakaa za kwanza na tatu, kukaa kikao chepesi kabla ya kusimama kwenda rakaa ya pili na ya nne. Ni kwa Hadiyth ya Maalik bin Al-Huwayrith kwamba alimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali, anapokuwa katika rakaa ya Witr ya Swalaah yake, hanyanyuki mpaka alingamane akiwa amekaa”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (823) Muslim (829)].
11- Kuegemeza mikono chini wakati wa kunyanyuka kwenda rakaa nyingine
Ni kwa neno la Maalik bin Al-Huwayrith: “Je, nikuzungumzieni kuhusu sifa ya Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Ni kuwa anaponyanyua kichwa chake toka sijdah ya pili, hukaa akaegemeza mikono yake chini, kisha husimama”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (824)].
12- Kukaa kikao cha “iftiraash” katika tashah-hud ya kwanza, na kikao cha “tawar-ruk” katika tashah-hud ya mwisho.
“Iftiraash” ni kuusimamisha mguu wa kulia na kuulaza wa kushoto na kuukalia. Ama “tawar-ruki” ni kuunyanyua mguu wa kulia na kuutanguliza wa kushoto na kulilaza tako lake chini.
Katika Hadiyth ya Abuu Humayda: “Anapokaa katika rakaa mbili, hukalia mguu wake wa kushoto na kuunyoosha wa kulia, na anapokaa katika rakaa ya mwisho, huutanguliza mguu wake wa kushoto akausimamisha mwingine, kisha hukalia juu ya tako lake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1/201), Abuu Daawuud (194) na At-Tirmidhiy (2/105)].
· Faida
Ikiwa Swalaah ni ya rakaa mbili tu kwa maana kuwa ina tashah-hudi moja tu, basi imesuniwa kukaa kikao cha iftiraash. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah katika sifa ya Swalaah ya Rasuli isemayo: “Alikuwa akisema katika kila rakaa mbili “at-tahiyyaat”, na alikuwa akiulaza mguu wake wa kushoto na kuunyanyua mguu wake wa kulia..”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1/357)].
13- Kuashiria kwa kidole cha shahada katika tashah-hudi toka mwanzoni hadi mwishoni mwa du’aa na kutuliza jicho kwenye kidole
Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar isemayo: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapokaa katika Swalaah, huweka mikono yake miwili juu ya magoti yake, hukinyanyua kidole chake cha kulia kinachofuatia dole gumba [na huyakita macho yake juu yake], na huuweka mkono wake wa kushoto juu ya goti lake la kushoto akivitandaza vidole vyake”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (580)]
· Faida
Haijuzu kuashiria kwa kidole kingine kisicho cha shahada cha mkono wa kulia. Imepokelewa toka kwa Sa’ad bin Abiy Waqqaas akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinipitia nami nanyoosha vidole vyangu viwili. Akaniambia: “Kimoja, kimoja basi”, akaashiria kidole cha shahada”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2/80) na An-Nasaaiy (3/83)].
Na kama kidole cha shahada cha mkono wa kulia kimekatwa, basi kwa kauli yenye nguvu ni kuwa uashirio hupomoka, na hairuhusiki kuashiria kwa kidole kingine. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.