022-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Qunuwt Katika Swalaah Za Faradhi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

022-Qunuwt Katika Swalaah Za Faradhi

 

Alhidaaya.com

 

 

Kwanza: Qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri

 

[Haya yamenukuliwa toka kwenye tasnifu murua kabisa ya ndugu yetu katika iymaan Magdiy bin ‘Abdul Haadiy yenye anwani isemayo: “ Isfaar As-Subhi Fiy Qunuwtis Subhi”. Imefanyiwa utangulizi na kupitiwa na Sheikh wetu Mustwafa Al-‘Adawiy (Allaah Ainyanyue hadhi yake)]

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na uhalali wa qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri na muundo wake. Wamekhitalifiana juu ya kauli nne:

 

Kauli ya kwanza:

 

Ni Sunnah endelevu iliyokokotezwa, imesuniwa kudumu nayo

 

Ni madhehebu ya Maalik na Ash-Shaafi’iy. [Al-Mudawwanah (1/100), Al-Istidhkaar (6/201), Al-Ummu (8/814), Al-Majmu’u (3/494) na Al-Adhkaar cha An-Nawawiy (69)]

 

Hoja ya kauli hii ni haya yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya Al-Barraa bin ‘Aazib aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma qunuwt Alfajiri [na Magharibi]. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (678), At-Tirmidhiy (401), Abuu Daawuud (1441) na An-Nasaaiy (2/202). ‘Amri bin Murrah amekhitalifiwa katika tamko la (Magharibi)]. 

 

2- Hadiyth ya Anas ya kuwa aliulizwa: “Je, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya qunuwt Alfajiri?” Akajibu: “Ndio”. Akaulizwa: “Je, alifanya kabla ya kurukuu?” Akajibu: “Baada ya kurukuu kwa kidogo”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraj” na Al-Bukhaariy (1001) na Muslim (677)].

 

3- Hadiyth ya Abuu Hurayrah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasema wakati anapomaliza kusoma katika Swalaah ya Alfajiri, kisha akapiga takbiyr na kunyanyua kichwa chake: ((Sami’al Laahu liman hamidah, Rabbanaa wa Lakal hamdu)). Kisha anasema na yeye amesimama:

(( اللهم أنج الوليد بن الوليد، وسلمة بن هشام وعياش بن أبي ربيعة، والمستضعفين من المؤمنين، اللهم اشدد وطأتك على مضر، واجعلها عليهم كسني يوسف، اللهم ألعن لحيان ورعلا وذكوان، وعصية عصت الله ورسوله))

((Allaahumma Anji Al-Waliyda bna Al-Waliyd, wa Salamata ibna Hishaam, wa ‘Ayyaasha ibna Abiy Rabiy’ah, wal Mustadhw’afiyna minal Muuminiyna. Allaahumma Shdud watw-ataka ‘alaa Mudhwirr Waj-’alhaa ‘alayhim kasiniyyi Yuusuf. Allaahumma Al-’an Lahyaana wa Ra’alan wa Dhakawaana, wa ‘Uswayyatan ‘aswatil Laaha wa Rasuulahu)). Kisha ikatufikia habari kwamba ameacha du’aa hiyo wakati ilipoteremka: [Msemaji ni Az Zuhriy kama alivyomwashiria Al-Haafidh katika Al-Fat-h (8/75)]

 

(( لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذِّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ ))

 [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (804) na Muslim (678) na tamko ni lake].

 

4- Na du’aa kama hiyo hiyo kama ilivyopokelewa toka kwa Ibn ‘Umar ya kuwa alimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaponyanyua kichwa chake toka kwenye rukuu ya rakaa ya mwisho ya Swalaah ya Alfajiri akisema:

((Ee Mola! Mlaani fulani na fulani na fulani)) baada ya kusema: ((Sami’al Laahu liman hamidah, Rabbanaa wa Lakal hamdu)). Na hapo Allaah Akateremsha:

(( لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذِّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ ))

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4559)].

 

Wamesema: “Mwelekeo wa Maalik na Ash-Shaafi’iy kutoa dalili hizi ni kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya qunuwt baada ya kusimama toka kwenye rukuu katika Swalaah ya Alfajiri, na hii inaonyesha kwamba alikuwa akiomba kila siku. Ama kuacha kuomba du’aa baada ya kuteremka Aayah, basi hilo haliharibu kitu kwa mambo mawili: Moja ya mawili hayo ni kuwa kauli hii ni taarifa toka kauli ya Az-Zuhriy kama ilivyo katika riwaya ya Abuu Hurayrah, nayo imekatika, haifai. [Fat-hul Baariy (8/75) na Ma’arifatus Sunan wal Aathaar cha Al-Bayhaqiy (2/74)]

 

Na kama tutajaalia kwamba ni sahihi, basi makusudio yanayoweza kukubalika ni kuwa aliacha kulaani tu na si kuomba du’aa kabisa”. [Angalia: Al-Ummu (8/815), Ibn Khuzaymah (1/316), Ma’alimus Sunan (1/250), Al-Majmu’u (3/505) na Twarhut Tathriyb (2/289). Angalia Isfaarus Swubh ukurasa 52]

 

5- Ni yale yaliyoripotiwa toka kwa Anas kwamba amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuacha kuomba qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri mpaka alipofariki”.  Kauli hii ni munkari na haifai. [Hadiyth Munkar: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/162), Ad-daaraqutwniy (2/39), Al-Bayhaqiy (2/201) na Ibnul Jawziy katika Al’Ilal Al-Mutanaahiyah (1/441)].

 

Kauli ya pili:

 

Qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri na nyinginezo imenasikhiwa na ni bid-’a

 

Ni madhehebu ya Abuu Haniyfah. [Al-Mabsuwtw (1/165) na Fat-hul Qadiyr (1/431)] Dalili za kauli hii ni haya yafuatayo:

 

1- Ni Hadiyth ya Abuu Maalik Al-Ashja’iy aliyemuuliza baba yake: “Wewe umeswali nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan, na ‘Aliyy bin Abiy Twaalib hapa Kufa kiasi cha miaka hamsini, je walikuwa wakifanya qunuwt?” Akasema: “Ndio, ee mwanangu”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (402), Ibn Maajah (1241), na Ahmad (3/472). Al-‘Uqayliy ameitia doa katika Adh-Dhu’afaa (2/119)].

 

Hoja hii inapingwa kwa kusema kwamba hakuna lolote linaloonyesha kuwa baba wa Abuu Maalik –Twaariq bin Ashyam (Allaah Amridhie) – alisuhubiana na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aidha, upo uwezekano mkubwa kuwa hakuwa akijua kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya qunuwt. Isitoshe, hata Maswahaba wakubwa waliokuwa wakiandamana sana na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa hawajui mambo kadhaa aliyokuwa akiyafanya. [Angalia mifano ya hili katika MaFaatihahu Lilfiqhi Fid Diyn cha Sheikh wetu (Allaah Amhifadhi) ukurasa wa 82]

 

Ninasema: “Kisha qunuwt imethibiti toka kwa Makhalifa wanne vile vile!!”

 

2- Ni yale yaliyoripotiwa toka kwa Ummi Salamah aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri”. [Isnadi yake mbovu: Imefanyiwa “ikhraj” na Ad- Daaraqutwniy (2/38)].

 

3- Ni yale yaliyoripotiwa toka kwa Ibn Mas-’oud aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya qunuwt isipokuwa mwezi mmoja tu, hakufanya kabla yake wala baada yake”. [Isnadi yake mbovu: Imefanyiwa “ikhraj” na Atw-Twahaawiy katika Sharhul Ma’aniy (1/245) na Al-Bayhaqiy (2/213)].

 

4- Na mfano wake toka kwa Ibn ‘Umar aliyesema: “Ni bid-’a, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya qunuwt ila mwezi mmoja tu, kisha akaiacha”. [Isnadi yake ni dhwa’iyf: Imefanyiwa”ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (2/213)].

 

Riwaya hizi tatu ni dhwa’iyf, hazifai kutolewa dalili lakini imethibiti toka kwa Ibn ‘Umar kwamba alisema: “Sikushuhudia yeyote akiifanya!!” [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (4954)].

 

Imepokelewa kwamba Ibn Mas-’oud alikuwa hafanyi qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (4949)].

 

5- Kuacha qunuwt katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar na Abu Hurayrah iliyotangulia katika dalili za kundi la kwanza, inaonyesha naskh, na hilo limeshajibiwa katika njia mbili.

 

6- Wamesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya qunuwt katika Swalaah za Magharibi na Alfajiri, kisha ikaondoshwa qunuwt ya Magharibi, na pia ya Alfajiri!!

Linajibiwa hili kwamba naskhi haiingii kwa hili wala lile.

 

Kauli ya tatu:

 

Qunuwt haisomwi ila wakati wa misukosuko tu

 

Ni kauli ya Ahmad na baadhi ya Mahanafi waliofuatia. [Al-Mughniy (2/587) na Fat-hul Qadiyr cha Ibnul Hammaam (1/434)]

 

Dalili yao ni Hadiyth ya Anas Allaah Amridhie anayesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hafanyi qunuwt isipokuwa pale anapowaombea watu mema au anapowaombea watu mabaya”. [Isnadi yake Laini: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abu Khuzaymah (620). Inaonekana kwamba ni muhtasari toka katika Hadiyth ya Anas iliyotangulia katika kuelezea qunuwt yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa ‘aalihi wa sallam) na kuwaombea du’aa mbaya makabila. Hadiyth hii imefunga mpaka wa kuwa qunuwt haifanyiki ila katika kuwaombea tu watu du’aa mbaya. Ninakhofia mzigo katika hili akaubeba Muhammad bin Muhammad bin Marzouq, kwani Ibn ‘Uday amezikanusha Hadiyth zake mbili ambazo yeye peke yake kazipokea toka kwa ‘Abdullah bin Answaar, na yeye hapa, anasimulia toka kwake!!]

 

Kauli ya nne:

 

Inajuzu kuifanya au kuiacha

 

Ni kauli ya Ath-Thawriy, Ibn Jariyj Atw-Twabariy, Ibn Hazm na Ibnul Qayyim. [Tahdhiybul Aathaar (1/337), Al-Muhallaa (4/143) na Zaadul Ma’ad (1/274)]

 

Wamesema: “Imethibiti kutokana na mjumuiko wa riwaya kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiifanya qunuwt wakati, na kuiacha wakati mwingine kwa ajili ya kuufundisha umma wake kwamba wana khiyari ya ima kuifanya au kuiacha.

 

Ibn Al-Qayyim anasema: “Maulamaa wa Hadiyth wako kati na kati; kati ya hawa na hawa [yaani: wale walioizuia kabisa] na kati ya wale wanaosema kwamba ni Sunnah wakati wa misukosuko na mengineyo. Maulamaa hawa hawana tatizo na makundi yote mawili, kwani wanaifanya qunuwt pale alipoifanya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wanaiacha pale alipoiacha. Wao humfuata katika kutenda kwake na kuacha kwake wakisema: “Kufanya kwake ni Sunnah na kuacha kwake ni Sunnah”. Pamoja na hivi, hawamkatalii mwenye kuifanya daima, wala hawachukulii kuifanya kama ni makruhu, wala hawachukulii kama ni bid-’a, na wala hawamzingatii mfanyaji wake kama anakwenda kinyume na Sunnah. Aidha, hawamkatalii mwenye kukataa kufanywa wakati wa kuzuka misukosuko, wala hawaoni kwamba kuiacha ni bid-’a wala mwenye kuiacha kama anakwenda kinyume na Sunnah, bali mwenye kuifanya katenda wema, na mwenye kuiacha katenda wema pia”.

 

Lenye nguvu

 

Hakuna shaka yoyote kwamba kufanya qunuwt daima katika Swalaah ya Alfajiri, haikuwa katika mwenendo wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Pia hakuna shaka yoyote kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliifanya. Hivyo basi, suala linabakia ndani ya mzunguko wa kati ya kuwa kwake ni Sunnah wakati wa kutokea misukosuko tu, au kuwa ifanywe baadhi ya nyakati na iachwe wakati mwingine ingawa ninaloliona mimi kupitia Hadiyth zilizothibiti katika suala hili ni kuwa lililo karibu zaidi ni kuwa qunuwt haifanywi ila wakati wa misukosuko tu. Na hii si kwa Hadiyth iliyotolewa dalili na Maulamaa wa kauli ya tatu, bali ni kwa Hadiyth zinazohusiana na du’aa alizoziomba Rasuli katika qunuwt ya Alfajiri. Du’aa zote hizi ni za ima kuwaapizia watu mabaya au kuwaombea mema. Kadhalika, kuna yale yaliyothibiti toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab yasemayo:

((..وانصرهم على عدوك وعدوهم، اللهم العن كفرة أهل الكتاب... اللهم خالف بين كلمتهم، وزلزل أقدامهم، وأنزل بهم بأسك الذي لا ترده عن القوم المجرمين..))

((..wan Swurhum ‘alaa ‘aduwwika wa aduwwihim. Allaahumal ‘An kafarata Ahlil Kitaab..Allaahumma Khaalif bayna kalimatihim, wa Zalzil aqdaamahum, wa Anzil bihim baasakal ladhiy laa Tarudduhuu ‘anil qawmil mujirimiyna)). [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Razzaaq (4969)].

 

Nami nasisitiza hapa kwamba ikiwa mtu atachukua msimamo huu, basi haijuzu kwake kumzingatia anayekwenda kinyume nao kama ni mtu wa bid-’a au mtu asiyefaa kuwa imamu. Anayefanya hivi atakuwa haijui Dini ya Allaah (Subhaanah) ambayo sisi tunajitakasa nayo kuelekea Kwake. Imamu Ahmad alipoulizwa kuhusu watu wanaosoma qunuwt mjini Basrah kama inafaa kuwafuata au la alijibu: “Waislamu walikuwa wakimfuata anayesoma qunuwt, na wanamfuata asiyesoma qunuwt pia”. [Ibn Al-Qayyim kainukuu kutoka kwake katika kitabu cha As-Swalaahat wa Hukmu Taarikihaa uk. 120]

 

·       

Qunuwt Alfajiri inakuwa ni baada ya kurukuu

 

Lililothibiti katika Hadiyth zilizotangulia za Anas, Ibn ‘Umar na Abu Hurayrah ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma qunuwt baada ya kuitadili toka kwenye rukuu. Haya ndiyo waliyoyasema akina Ash-Shaafi’iy, Ahmad, na Is-Haaq, nayo ni riwaya toka kwa Maalik.

 

Maalik kwa ilivyo tangaa kwake ni kuwa mahala pa qunuwt ni kabla ya kurukuu. Na hili limethibiti kwa baadhi ya Maswahaba kama vile ‘Umar, ‘Aliyyi na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhum). Suala uwanja wake ni mpana, lakini la kwanza la kuisoma baada ya kuitadili, ni bora zaidi kama tunavyoona.

 

Pili: Qunuwt katika Swalaah tano

 

Qunuwt inaruhusiwa katika Swalaah zote tano za faradhi endapo kama patazuka kwa Waislamu janga au misukosuko. Ni kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alifanya qunuwt mwezi mzima mfululizo katika Swalaah za Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, ‘ishaa na Alfajiri baada ya kusema: “Sami’al Laahu liman hamidah” katika rakaa ya mwisho akiwaombea walio hai katika ukoo wa Baniy Sulaym dhidi ya Ra’al, Dhakawaan na ‘Uswayyah, na walio nyuma yake wakiitikia “aamiyn”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/301), Ibn Al-Jaarowd (197), Ibn Khuzaymah (618), Al-Haakim (1/225) na Al-Bayhaqiy (2/200). Ina Hadiyth mwenza toka kwa Abuu Hurayrah].

 

·       

Faida Kadhaa Kuhusiana Na Qunuwt

 

1- Imamu hunyanyua sauti wakati wa kuomba du’aa kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo. Na kwa kufanya hivyo, Anas, Abuu Hurayrah na Ibn ‘Abbaas waliweza kuinukuu du’aa yake katika qunuwt.

 

2- Watu wanaomfuata imamu huitikia “aamiyn”. Ni kutokana na yaliyomo ndani ya Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia yasemayo: “Na huitikia aamiyn walioko nyuma yake”. Ibn Qudaamah amesema: “Hatujasikia makhitilafiano yoyote hapa”.

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Uthmaan akisema: “Niliswali nyuma ya ‘Umar bin Al-Khattwaab, akasoma aayah 200 za Al-Baqarah, akasoma qunuwt baada ya rukuu, akanyanyua mikono yake mpaka nikaona weupe wa kwapa zake, na akanyanyua sauti yake kwa du’aa mpaka wakasikia walio nyuma ya ukuta. [Angalia Isfaarus Swubh ukurasa wa 66-69 na rejea zinazofuatia]

 

3- Je, mikono hunyanyuliwa katika qunuwt?  [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy katika Ma’arifatus Sunan (2/83)]

 

Jamhuri ya Maulamaa akiwemo Abuu Haniyfah, Ahmad na Is-Haaq wote wananyanyua mikono katika qunuwt. Ibn Al-Mundhir ameliripoti hili toka kwa ‘Umar - nayo ni sahihi toka kwake kama ilivyotangulia – pamoja na Ibn Mas-’oud na wengineo. Mwelekeo huu unaungwa mkono na Hadiyth ya Anas isemayo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – katika Swalaah ya Alfajiri – alinyanyua mikono yake akawaombea…Hadiyth”. [Al-Awsatw (5/212), Al-Mughniy (2/584) na Al-Majmu’u (3/499)]

 

Maalik amesema: “Mikono hainyanyuliwi, na la kwanza ni sahihi zaidi. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

Masuala mengineyo yanayohusiana na qunuwt yatakuja kuelezewa kwenye mlango wa Witr InshaAllaah.

 

 

Share