023-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Swalaah Za Sunnah (Tatwawwu’’u)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swalaah

 

023-Swalaah Za Sunnah (Tatwawwu’’u)

 

Alhidaaya.com

 

 

Taarifu yake:

 

Asili ya neno “tatwawwu’u” ni kufanya amali ya kumtii Allaah (twa’a), kisha likawa kiistilahi kwa maana ya kufanya amali ya kumtii Allaah  isiyo ya wajibu. Swalaah za Sunnah ni zile za nyongeza juu ya Swalaah za faradhi kutokana na neno la Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipoulizwa kuhusu Uislamu na kusema:

((Ni Swalaah tano mchana na usiku)). Muulizaji akasema tena: Je, kuna jingine zaidi? Akasema: ((Hapana, ila kama utaswali za Sunnah)).  [Hadiyth Swahiyh: Takhriyj yake ishatangulia].

 

Umuhimu Wa Swalaah Za Sunnah

 

1- Swalaah ndio amali bora zaidi

 

Swalaah ndio ‘ibaadah bora zaidi ya kimwili, na ndio jambo bora zaidi ambalo mtu hujikurubisha nalo kwa Allaah Mtukufu. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( استقيموا، ولن تحصوا، واعلموا أن خير أعمالكم الصلاة))

((Lingamaneni sawa, lakini hamtoweza (kwa nguvu zenu na juhudi zenu) na jueni kwamba amali yenu bora zaidi ni Swalaah)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (277) na wengineo. Ina Sanad ambazo zote ni Swahiyh. Angalia Ta’adhiymu Qadris Swalaat (170- kwa uhakiki tulioufanya sisi)]

 

2- Hunyanyua hadhi ya mtu peponi kwa kuzikithirisha

 

Imepokelewa toka kwa Rabiy’a bin Maalik Al-Aslamiy akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Omba)). Nikasema: “Nakuomba nisuhubiane nawe Peponi. Akasema: ((Kuna jingine zaidi?)). Nikasema: “Ni hilo tu”. Akasema: ((Basi jisaidie mwenyewe kwa kukithirisha sujudi)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (489), An-Nasaaiy (2/227), Abuu Daawuud (1320) na Ahmad (4/59)].

 

Na Thawbaan alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu amali itakayomwingiza Peponi. Rasuli akamwambia:

(( عليك بكثرة السجود فإنك لا تسجد لله سجدة إلا رفعك الله بها درجة وحط عنك بها خطيئة ))

((Jilazimishe kusujudu kwa wingi, kwani hakika wewe husujudu sijda yoyote kwa ajili ya Allaah isipokuwa Allaah Hukunyanyua daraja moja na Hukupomoshea kwayo kosa moja)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (488). Angalia Ta’adhiymu Qadris Swalaahat nilichokifanyia uhakiki (300).]

 

3- Huunga mapungufu ya Swalaah za faradhi

 

Imepokelewa toka kwa ‘Ammaar bin Yaasir akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( إن الرجل لينصرف ]من صلاته[ وما كتب له إلا عشرها تسعها ثمنها سبعها سدسها خمسها ربعها ثلثها نصفها))

((Hakika mtu huondoka [toka kwenye Swalaah yake], na huwa hakuandikiwa isipokuwa moja ya kumi yake, moja ya tisa yake, moja ya nane yake, moja ya saba yake, sudusi yake, khumsi yake, robo yake, theluthi yake, nusu yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (796) na Ahmad (4/321). Angalia Qadrus Swalaahat nilichokifanyia uhakiki (156)].

 

Swalaah za Sunnah zimewekwa kwa ajili ya kuyaunga na kuyakamilisha mapungufu yanayoweza kuwa yamefanyika ndani ya Swalaah ya faradhi. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

(( Jambo la kwanza watakalofanyiwa hisabu watu Siku ya Qiyaamah katika amali zao ni Swalaah. Mola wetu Atawaambia Malaika – Naye Anajua kila kitu - : Angalieni katika Swalaah ya mja Wangu; je ameiswali kamili au ameiswali pungufu? Ikiwa kamili, ataandikiwa Swalaah kamili, na kama ameiswali pungufu Atawaambia: “Angalieni, je mja Wangu ana Swalaah za Sunnah? Ikiwa anazo Swalaah za Sunnah Atasema: Mkamilishieni Mja Wangu faradhi zake kwa Sunnah zake, kisha amali zake huchukuliwa juu ya hilo)). [Hadiyth Swahiyh katika jumla: Angalia Ta’adhiymu Qadris Swalaahat nilichokifanyia uhakiki (180)].

 

Vigawanyo Vya Swalaah Za Sunnah

 

1-     Sunnah “Mutwlaq”

 

Hizi ni zile zisizo na sababu, zisizo na hesabu au idadi maalumu ya rakaa zake. Mwenye kuswali anaweza kunuwia idadi ya rakaa au kutonuwia, bali atanuwia tu Swalaah. Na ikiwa ataingia kuswali Sunnah bila kunuwia idadi maalumu, basi anaweza kutoa tasliym katika rakaa ya kwanza, au akaongeza akatoa katika rakaa ya pili, au ya tatu, au ya kumi au zaidi. Na kama ataswali rakaa ambazo hajui idadi yake kisha akatoa tasliym, basi itakuwa sahihi. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (3/541)]

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kuwa aliswali rakaa nyingi sana. Baada ya kutoa tasliym, Al-Ahnaf bin Qays alimuuliza: “Je, umemalizia kwa shufwa au Witr?” Akajibu: “Kama sijui, basi Allaah Anajua. Hakika mimi nimemsikia Kipenzi changu Abal Qaasim akisema:

(( ما من عبد يسجد لله سجدة إلا رفعه الله بها درجة وحط عنه بها خطيئة ))

((Hakuna mja yeyote anayemsujudia Allaah sijdah moja, isipokuwa Allaah Humnyanyulia kwayo daraja, na Humpomoshea kwayo kosa moja)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/164), ‘Abdul Razzaaq (3561, 4847), Al-Bazzaar (9/345) na Al-Bayhaqiy (2/489)]

 

 

Wakati Gani Atafanya Tashah-hudi?

 

Kama ataswali Sunnah ya rakaa moja, ni lazima afanye tashah-hudi mwisho wake, na kama ataswali zaidi ya rakaa moja, basi atatosheka na tashah-hudi moja tu mwishoni mwa Swalaah yake. Tashah-hudi hii ni nguzo ambayo ni lazima aifanye. Pia anaweza kufanya tashah-hudi baada ya kila rakaa mbili kama ilivyo katika Swalaah za faradhi za rakaa nne. Na kama idadi ya rakaa ni Witr, basi ni lazima afanye tashah-hudi katika rakaa ya mwisho vile vile ikiwa Swalaah yake ni ya rakaa nne. Na ikiwa ni ya rakaa sita, au kumi au zaidi ya hizo, sawasawa ikiwa ni shufwa au Witr, basi hapo kuna njia nne:  [Al-Majmu’u (3/542-543)]

 

1- Inajuzu kufanya tashah-hudi katika kila rakaa mbili hata kama tashah-hudi zitakithirika, lakini tashah-hudi katika rakaa ya mwisho ni lazima. Pia anaweza kutosheka na tashah-hudi moja tu ya mwisho, au akafanya tashah-hudi baada ya kila rakaa nne, au tatu, au sita na kadhalika. Lakini pamoja na hivi, haijuzu kufanya tashah-hudi katika kila rakaa moja, kwani hiyo itakuwa ni kuzua picha ambayo haijawahi kufanyika katika Swalaah.

 

2- Haijuzu zaidi ya tashah-hudi mbili katika Swalaah moja, au kuwepo kati ya tashah-hudi mbili zaidi ya rakaa mbili ikiwa idadi ya rakaa ni shufwa, na ikiwa ni Witr, haijuzu kati yao zaidi ya rakaa moja. An-Nawawiy kasema: “Hii ina nguvu, na ndio mwelekeo wa Sunnah”.  Dalili ya njia hii itakuja kuelezewa katika mlango wa “Qiyaamul Layl”.

 

3- Asikae ila katika rakaa ya mwisho. An-Nawawiy kasema: “Ni makosa”. Nami nasema: “Bali imethibiti Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya hilo. Tutakuja kufafanua hilo katika mlango wa Swalaah ya Witr”.

 

4- Inajuzu kufanya tashah-hudi katika kila rakaa mbili na katika kila rakaa moja. An-Nawawiy kasema: “Hili ni dhwa’iyf, au batili”.

 

 

 

 

Ni Bora Kuswali Rakaa Mbili Mbili

 

Hakuna makhitilafiano yoyote kwamba lililo bora ni kutoa tasliym baada ya kila rakaa mbili katika Sunnah za usiku na mchana. Imeripotiwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( صلاة الليل ] والنهار[ مثنى مثنى))

((Swalaah ya usiku [na mchana] ni rakaa mbili mbili)).  [Ni Hadiyth Shaadh kwa nyongeza hii: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1295), At-Tirmidhiy (594), An-Nasaaiy (3/227) na Ibn Maajah (1322). Angalia Fataawaa Ibn Taymiyah (21/289). Imekosolewa na Ahmad, An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy, Ad-daaraqutwniy, Ibn ‘Abdul Barri na Ibn Hajar]

 

Hadiyth hii si Swahiyh. Iliyo Swahiyh ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( صلاة الليل مثنى مثنى، فإذا خشيت الصبح فأوتر بواحدة))

((Swalaah ya usiku ni rakaa mbili mbili. Ukichelea Alfajiri, basi swali Witr kwa rakaa moja)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (990) na Muslim (749) toka Hadiyth ya Ibn ‘Umar]

 

Haya niliyoyaeleza ya kujuzu kukusanya rakaa nyingi za Swalaah za Sunnah “mutwlaq” kwa tasliym moja, na kwamba lililo bora katika Sunnah za usiku na mchana ni kutoa tasliym baada ya kila rakaa mbili, yote haya ni matamshi ya akina Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Daawuud na Ibn Al-Mundhir. Pia yameripotiwa toka kwa Al-Hasan, na Sa’iyd bin Jubayr.

 

Abu Haniyfah amesema: “Tasliym ni baada ya rakaa mbili au nne katika Swalaah ya mchana, na isizidi zaidi ya hapo, na Swalaah ya usiku ni rakaa mbili, au nne, au sita, au nane kwa tasliym moja, wala zisizidi rakaa nane”.

 

2-     Sunnah “Muqayyad”

 

Hizi ni zile ambazo Hadiyth zimethibitisha uwepo wake. Sunnah hizi ni za aina mbili:

 

(a)  Sunnah “Rawaatib”

 

Hizi ni zile zinazofungamana na Swalaah tano za faradhi. Kati ya Sunnah hizi, kuna zile zinazoswaliwa kabla ya Swalaah za faradhi, nazo hujulikana kama “As-Sunnat Al-Qabliyyah”, na kuna zingine zinazoswaliwa baada ya Swalaah za faradhi, nazo huitwa “As-Sunnat Al-Ba’adiyyah”. Kuna maana murua kabisa na mwafaka ya kuwepo Sunnah hizi za kabla na baada ya Swalaah za faradhi. Ama za kabla, ni kuwa nafsi kutokana na kushughulishwa na mihangaiko ya kidunia, inakuwa iko mbali na khushui na uwepo wake ambao ndio roho ya ‘ibaadah. Swalaah hizi zinaposwaliwa kabla ya faradhi, basi nafsi ya mtu inapata utulivu ndani ya Swalaah anayoiswali. Ama zile za baada, ni kuwa kama tulivyosema kwamba Swalaah za Sunnah hujazilia mapungufu yaliyotokea kwenye Swalaah za faradhi, basi faradhi inaposwaliwa, imekuwa ni mwafaka kuswaliwa Sunnah baada yake ili ijazilie pengo lolote lililotokea.

 

·        Rawaatib: Kuna zilizokokotezwa, na zisizokokotezwa

 

Sunnah hizi zinazofungamana na faradhi, kuna kati yake ambazo zimekokotezwa, nazo ni zile ambazo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akidumu nazo bila kuziacha, nazo ziko kumi.

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhumaa) akisema: “Nimehifadhi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) rakaa kumi: Rakaa mbili kabla ya Adhuhuri na rakaa mbili baada yake, rakaa mbili baada ya Magharibi, rakaa mbili baada ya ‘ishaa, na rakaa mbili kabla ya Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1180) na Muslim (729)].

 

Haya kayasema Ash-Shaafi’iy na Hanbali. [Al-Majmu’u (3/501) na Kash-Shaaf Al-Qina’a (1/422)]

 

Kwa Mahanafi [Ibn ‘Aabidiyn (1/441)], “Rawaatib” zilizokokotezwa ni kumi na mbili: Ni hizo kumi zilizotangulia lakini kabla ya Adhuhuri ni rakaa nne kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haachi rakaa nne kabla ya Adhuhuri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1182)].

 

Imepokelewa toka kwa Ummu Habiybah (Allaah Amridhie) akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Mwenye kuswali rakaa kumi na mbili mchana na usiku, atajengewa kwa rakaa hizo nyumba peponi)). Ummu Habiybah anasema: “Sikuziacha kamwe tokea nilipomsikia Rasuli wa Allaah akisema hivyo”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (728), At-Tirmidhiy (415), na ziada ni yake, Abuu Daawuud (1250), na Ibn Maajah (1141). Ina mwenza wake kutoka Hadiyth ya ‘Aaishah iliyoko kwa At-Tirmidhiy (414), An-Nasaaiy (3/260) na Ibn Maajah (1140)].

 

At-Tirmidhiy kaongeza: “Nne kabla ya Adhuhuri na mbili baada yake, rakaa mbili baada ya Magharibi, rakaa mbili baada ya ishaa, na rakaa mbili kabla ya Alfajiri”.

 

Ama Maalik, wao hawana idadi maalumu ya rakaa za rawaatib. Inatosha kwao kuipata Sunnah kwa kuswali rakaa mbili wakati wote.

 

Ama rawaatib ambazo hazikukokotezwa, hizi ni zile ambazo zimesuniwa kuziswali kiujumla bila kutiliwa mkazo.

 

Sunnah Ya Alfajiri

 

·        Kusisitizwa Kwake

 

Rakaa mbili kabla ya Alfajiri, ni katika Sunnah za rawaatib iliyohimiziwa sana. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Allaah Amridhie) akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa ameshikamana zaidi na chochote katika Swalaah za Sunnah kama alivyokuwa ameshikamana na rakaa mbili za Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1094) na Muslim (1191)].

 

Na katika tamko jingine: “Hakuwa akiziacha kamwe”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1159)].

 

Na katika Hadiyth nyingine iliyosimuliwa na bibi huyu huyu, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Rakaa mbili za Alfajiri, ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani yake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (725) na At-Tirmidhiy (416)].

 

Ibn Al-Qayyim anasema katika Az-Zaad (1/315): “ Na kwa ajili hiyo Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuziacha pamoja na Sunnah ya Witr sawasawa akiwa safarini au akiwa nyumbani. Akiwa safarini, alikuwa haziachi kabisa kulinganisha na Sunnah nyinginezo zote. Na haikunukuliwa kutoka kwake kuwa yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Sunnah nyingine zaidi ya hizo mbili akiwa safarini”.

 

·        Kuzifupisha

 

Imesuniwa kuzifupisha rakaa hizi mbili za Alfajiri ili zisije kugongana na la wajibu. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Hafswah alinieleza kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaswali rakaa mbili fupi kabla ya kuqimiwa Swalaah wakati mwadhini anapokaa kwa ajili ya Alfajiri, na Alfajiri ikadhihiri”.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (583)].

 

Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali rakaa mbili fupi kati ya adhana na iqaamah katika Swalaah ya Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (584)].

 

Pia anasema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizifupisha rakaa mbili za kabla ya Swalaah ya Alfajiri mpaka nikawa najiuliza: “Je, kasoma Al-Faatihahh?” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1095) na Muslim (1189)].

 

Ama Suwrah zinazosomwa baada ya Al-Faatihah katika rakaa hizi mbili ni kuwa imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa akisoma Aayah zifuatazo katika rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri:

 

1- Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah akisema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisoma katika rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri: (( قل يا أيها الكافرون )) na (( قل هو الله أحد )). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (726)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasoma katika rakaa mbili za Alfajiri:

 

((قُولُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ 

وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ))

 

na

 

((قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا

 وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ))

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (727) na An-Nasaaiy (2/155)].

 

Husoma baada ya Al-Faatihah katika rakaa ya kwanza aya ya (136) ya Suwrat Al-Baqarah, na baada yake katika rakaa ya pili aya ya 64 ya Suwrat Aal-‘Imraan”.

 

3- Alikuwa anaweza pia kubadili Aayah ya Aal-‘Imraan katika rakaa ya pili kwa Neno Lake Ta’alaa:

 

 ((فَلَمَّا أَحَسَّ عِيسَىٰ مِنْهُمُ الْكُفْرَ قَالَ مَنْ أَنصَارِي إِلَى اللَّـهِ ۖ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ أَنصَارُ اللَّـهِ 

آمَنَّا بِاللَّـهِ وَاشْهَدْ بِأَنَّا مُسْلِمُونَ))

mpaka mwisho wa Aayah kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas.  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (727) na Abu Daawuud (1259)].

 

Ninasema: “Lililo bora ni kufanya uanuwai katika haya yote kwa ajili ya kuipata Sunnah kama ilivyo katika ‘ibaadah nyinginezo zinazofanyika kwa njia zaidi ya moja ambazo usahihi wake umethibiti”.

 

· Kulala Kwa Ubavu Wa Kulia Baada Ya Kuziswali

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “ Baada ya mwadhini kumaliza adhana ya Alfajiri, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasimama, akaswali rakaa mbili fupi kabla ya Swalaah ya Alfajiri baada ya Alfajiri kudhihiri, kisha hulala kwa ubavu wake wa kulia mpaka aje mwadhini aqimu Swalaah”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (590)].

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya kulala ubavu baada ya rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri juu ya kauli zifuatazo: [Naylul Awtwaar (3/28-32), Al-Muhallaa (3/196) na Al-Majmu’u (3/523-524)]

 

1- Ni Sunnah bila mpaka

 

Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy. Wamelisema hili pia akina Abuu Musa Al-Ash-‘Ariy, Raafi’i ibn Khudayj, Anas bin Maalik na Abuu Hurayrah. Pia Ibn Syriyn na Mafuqahaa saba.

 

2- Ni wajibu

 

Ni kauli ya Abu Muhammad bin Hazm. La kushangaza zaidi ni kuwa yeye amekufanya kulala huku ni sharti ya kuswihi Swalaah ya Alfajiri!! Sheikh wa Uislamu amesema: “Hili ndilo alilopwekeka nalo mbali na umma wote”.

 

Ninasema: “Kigezo chake ni Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( إذا صلى أحدكم الركعتين قبل صلاة الصبح، فليضطجع على جنبه الأيمن ))

((Anaposwali mmoja wenu rakaa mbili kabla ya Swalaah ya Alfajiri, basi alale kwa ubavu wake wa kulia)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (1261), At-Tirmidhiy (420), Ahmad (2/415) na wengineo. Ibn Taymiyah amesema: “Hii ni batili, si sahihi, bali sahihi ni kufanya, na si amri ya kulala. Amri ya kufanya kabaki nayo ‘Abdul Waahid bin Ziyaad peke yake]

 

Anajibiwa kwamba Hadiyth hii imetiwa walakini. Na kama tutaichukulia kuwa ni Swahiyh, basi amri ya kufanya itageuzwa kuwa ni mustahabu kwa Hadiyth ya ‘Aaishah asemaye: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali rakaa mbili. Nikiwa macho hunisemesha, na kama siko macho, hulala kwa ubavu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1092) na Muslim (1227)].

 

Inaonyesha kwamba hakuwa akilala ikiwa ‘Aaishah yu macho, hivyo imekuwa ni alama ya kuigeuza amri kuwa ni Sunnah.

 

3- Ni makruhu

 

Ni kauli ya mjumuiko wa Masalaf akiwemo Ibn Mas-’oud, Ibn Al-Musayyib na An-Nakh’iy. Al-Qaadhwiy ‘Ayyaadh ameisimulia toka kwa Jamhuri ya Maulamaa. Hoja yao ni kuwa haikujulikana toka kwa yeyote kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilifanya hilo Msikitini, kwani lau angelifanya, basi nukuu yake ingelielezewa kizazi baada ya kingine!!

 

4- Ni kinyume cha ubora

 

Hili limesimuliwa toka kwa Al-Hasan Al-Baswriy.

 

5- Imesuniwa kwa anayeswali usiku ili apumzike.

 

Ni chaguo la Ibn Al’Arabiy na Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah.

 

6- Kulala kwa ubavu si kwamba ndiko hasa kulikokusudiwa, bali ni kwa ajili ya kutenganisha kati ya Sunnah na faradhi.

 

Hili limesimuliwa toka kwa Ash-Shaafi’iy, nalo limepingwa, kwa kuwa kutenganisha kunaweza kuwa kwa kitu kingine badala ya kulala.

 

Ninasema: “Lenye nguvu ni kuwa kulala kwa ubavu baada ya rakaa mbili mbili za Sunnah ya Alfajiri, kumesuniwa kwa masharti mawili:

 

La kwanza: Kuwe ni nyumbani na si Msikitini, kwa kuwa haikunukuliwa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilifanya hilo msikitini.

 

La pili: Awe mtu anaweza kufanya hivyo na kwenda kuswali Alfajiri bila ya kupitiwa tena na usingizi Swalaah ikampita. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

·        Ulipaji Wake

 

Mwenye kupitwa na rakaa mbili za Sunnah ya Alfajiri kwa udhuru, anaruhusiwa kuzilipa wakati wowote udhuru wake unapoondoka kutokana na dalili zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “Tulilala pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hatukuweza kuamka mpaka jua likachomoza. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia: ((Kila mmoja akamate ugwe wa mnyama wake tuondoke, kwani shaytwaan ametujia katika mashukio haya)). Tukafanya, kisha akaagiza maji akatawadha, halafu akasujudu sijdah mbili. Kisha ikaqimiwa Swalaah, akaswali Swalaah ya Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (1098) na wengineo]. 

Kuna Hadiyth kama hii ya ‘Imraan bin Haswiyn ambayo tumeitaja nyuma.

 

2- Hadiyth ya Qays bin ‘Amri aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mtu mmoja akiswali rakaa mbili baada ya Swalaah ya Alfajiri. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Swalaah ya Alfajiri ni rakaa mbili)), na mtu yule akamwambia: “Mimi sikuwa nimeziswali rakaa mbili za kabla yake, nikaziswali sasa”. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akanyamaza”. [Hadiyth Hasan Litwuruqihi: Imeshatajwa katika mlango wa “Nyakati zilizoharamishwa kuswali”].

 

Yaliyotangulia hayapingani na Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Ambaye hakuziswali rakaa mbili za Alfajiri, basi aziswali baada ya kuchomoza jua)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (423), Ibn Khuzaymah (1117), Al-Haakim (1/274), Ibn Hibaan (2472) na wengineo].

 

Hadiyth hii haielezi wazi kwamba mwenye  kuziacha haziswali isipokuwa baada ya kuchomoza jua – kama walivyosema Jamhuri ya Maulamaa – kwani hakuna hapo isipokuwa amri tu kwa yule ambaye hakuziswali kabisa ya kwamba aziswali baada ya jua kuchomoza. Na hakuna shaka yoyote kwamba rakaa mbili hizi zikiachwa kuswaliwa katika wakati wake, huswaliwa katika wakati wa kulipa, na katika Hadiyth hakuna kinachozuia kuswaliwa baada ya Swalaah ya Alfajiri. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Je, Baada Ya Kuingia Alfajiri, Kuna Sunnah Zingine Zaidi Ya Rakaa Mbili Za Alfajiri?

 

[Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (2/399-400)]

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na Sunnah zinginezo zaidi ya rakaa mbili za kabla ya Alfajiri kwa kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Ni karaha kuswali Sunnah nyinginezo zaidi ya rakaa mbili za Alfajiri

 

Ni kauli ya Masalaf wengi akiwemo Al-Hasan Al-Baswriy, An-Nakh’iy, Sa’iyd bin Al-Musayyib, na Abuu Haniyfah na Masahibu zake. Kauli hii imesimuliwa toka kwa ‘Abdillaah bin ‘Amri na Ibn ‘Umar lakini kuna maneno kuhusiana na Isnadi zao.

 

Imepokelewa toka kwa Yasaar mtumishi wa Ibn ‘Umar akisema: “Ibn ‘Umar aliniona nikiswali baada ya kuchomoza Alfajiri akaniambia: “Ee Yasaar! Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea nasi tunaswali Swalaah hii akatuambia:

(( ليبلغ شاهدكم غائبكم، لا تصلوا بعد الفجر إلا سجدتين))

((Aliyekuwepo wenu amfikishie asiyekuwepo wenu. Msiswali baada ya Alfajiri isipokuwa rakaa mbili)). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1264) na At-Tirmidhiy. Angalia “Swahiyhul Jaami’i (5353)].

 

Ya pili: Si vibaya kuswali Sunnah nyinginezo baada ya Alfajiri kuchomoza

 

Limesimuliwa hili na Ibn Al-Mundhir toka kwa Al-Hasan Al-Baswriy vile vile aliyesema: “Maalik alikuwa anaona kwamba atafanya hivyo yule ambaye alipitwa na Sunnah ya usiku, nalo limehadithiwa toka kwa Bilaal”.

 

Ninasema: “Kauli ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi, nayo inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyoipokea toka kwa Hafswah akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haswali isipokuwa rakaa mbili tu za Alfajiri wakati Alfajiri inapochomoza”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1173), Muslim (723) na wengineo].

 

Hadiyth hii inaitilia nguvu Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyotangulia – ingawa marejeo yake si kwa Hadiyth ya Hafswah -!! Huvuliwa katika hili kuilipa Swalaah iliyopita na Swalaah yenye sababu kama tulivyoeleza katika mlango wa nyakati zilizokatazwa kuswali. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

Zindushi mbili:

 

1- Si makruhu kuzungumza baada ya rakaa mbili za Alfajiri

 

Baadhi ya Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengineo wamekwenda kinyume na hili kwa kusema kwamba ni makruhu kuzungumza baada ya kuchomoza Alfajiri mpaka aswali mtu Alfajiri isipokuwa kama ni dhikri au lisilo na budi. Hawa hawana dalili yoyote kuhusu madai haya, bali Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia ni dalili inayowapinga pale anaposema: “Nikiwa macho hunisemesha, na kama siko macho, hulala kwa ubavu”.

 

2- Hakuna du’aa yoyote iliyothibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza rakaa mbili

 

Kuna Hadiyth mbili dhwa’iyf mno kuhusiana na hili ambazo hazifai kama ushahidi hata kwa wale wenye kutetea utumiaji wa Hadiyth Dhwa’iyf katika utendaji wa amali bora kutokana na nguvu ya udhwa’iyf wake.  [Al’Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahul Llaahu) kalitanabahisha hili katika Tamaamul Minnah (ukurasa wa 238-239)]

 

Sunnah Ya Adhuhuri

 

Sunnah hii imekuja kwa njia tatu:

 

Ya kwanza:

 

Rakaa mbili kabla ya Adhuhuri na rakaa mbili baada yake. Ni kama ilivyo katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliposema: “Nimehifadhi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) rakaa kumi: Rakaa mbili kabla ya Adhuhuri na rakaa mbili baada yake, rakaa mbili baada ya Magharibi, rakaa mbili baada ya ‘ishaa nyumbani kwake, na rakaa mbili kabla ya Alfajiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni].

 

Ya pili:

 

Rakaa nne kabla yake na mbili baada yake

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haziachi rakaa nne kabla ya Adhuhuri”. [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa karibuni].

 

Imepokelewa pia toka kwa ‘Abdullaah bin Shaqiyq akisema: “Nilimuuliza ‘Aaishah kuhusiana na Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), naye akasema: “Alikuwa anaswali rakaa nne kabla ya Adhuhuri, na mbili baada yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (730) na Ahmad (6/30)].

 

Hadiyth kama hii ya Ummu Habiybah tumeitaja nyuma.

 

Ya tatu:

 

Rakaa nne kabla yake na rakaa nne baada yake

 

Ni kwa Hadiyth ya Ummu Habiybah aliyesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( من صلى أربع ركعات قبل الظهر، وأربعا بعدها حرمه الله على النار))

((Mwenye kuswali rakaa nne kabla ya Adhuhuri, na rakaa nne baada yake, Allaah Atamharamishia moto)). [Hadiyth Swahiyh bituruqihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1269), At-Tirmidhiy (428), An-Nasaaiy (3/265), Ibn Maajah (1160), Ahmad (6/326) na Al-Haakim (1/312). Ina njia kadhaa zinazoipa zote uSwahiyh].

 

·        Faida

 

Lililo bora ni kuswali nne kwa rakaa mbili mbili. Ama Hadiyth ya Abu Ayyuub (Allaah Amridhie) ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

(( أربع قبل الظهر لا يسلم فيهن، تفتح لهن أبواب السماء))

((Rakaa nne kabla ya Adhuhuri bila tasliym, hufunguliwa kwazo milango ya mbingu)) ni dhwa’iyf haifai. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1270), Ahmad (5/416), ‘Abdu bin Hamiyd (226), At-Twayaalsiy]

 

·        Kuilipa Sunnah Ya Adhuhuri

 

Kuilipa ya Qabliyyah:

 

Mwenye kupitwa na Sunnah ya kabla ya Adhuhuri kwa udhuru, basi atailipa baada yake. Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kama hakuswali rakaa nne kabla ya Adhuhuri, huziswali baada yake. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (426)].

 

Kuilipa ya Ba’adiyyah:

 

Aidha, mwenye kuondokewa na udhuru wake, atailipa Sunnah ya ba’adiyyah ya Adhuhuri hata kama baada ya Swalaah ya Alasiri. Ni kwa Hadiyth ya Ummu Salamah kwamba alimwona Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali rakaa mbili baada ya Alasiri – na hili amelikataza – naye akamuuliza kwa nini anaswali wakati huo? Rasuli akamjibu: ((Ee binti Abuu Umayyah! Unauliza kuhusu rakaa mbili baada ya Alasiri? Hakika walinijia watu kutoka Bani ‘Abdul Qays, wakanishughulisha zikanipita rakaa mbili za baada ya Adhuhuri, nazo ndizo hizo nimeziswali)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1233), Muslim (834) na Ahmad (6/310)].

 

 

Sunnah Ya Alasiri

 

Alasiri haina Sunnah raatib iliyokokotezwa, lakini hata hivyo imesuniwa mtu aswali kabla yake rakaa mbili kutokana na ujumuishi wa kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( بين كل أذانين الصلاة))

((Kati ya kila adhana na iqaamah, kuna Swalaah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (624) na Muslim (838)].

 

Na pia imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((رحم الله امرأ صلى قبل العصر أربعا))

((Allaah Amrehemu mtu aliyeswali kabla ya Alasiri rakaa nne)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1271), At-Tirmidhiy (430) na Ahmad (2/117). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh, lakini kinyume chake ndio kauli ya nguvu. Angalia Al-Miyzaan (6/332) na Al-Kaamil (6/243)].

 

Hadiyth hii kwa anayeiona ni Swahiyh, inaonyesha kuwa yajuzu kuswali rakaa nne kabla ya Alasiri.

 

·        Tanbihi

 

Imethibiti kwamba ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu Anha) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuziacha kamwe rakaa mbili sawasawa akiwa peke yake au akiwa na watu: Rakaa mbili kabla ya Alfajiri, na rakaa mbili baada ya Alasiri”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (592)].

 

Pia amesema tena: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuacha katu rakaa mbili akiwa nyumbani kwangu”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (591)].

 

Kuendelea na kudumu huko kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali baada ya Alasiri, ni katika mambo mahsusi yanayomhusu yeye peke yake. Hivi ndivyo walivyosema Maulamaa wengi. [Angalia Fat-hul Baariy (2/77)]

 

Ninasema: “Hili linaweza kutiliwa nguvu na kauli ya ‘Aaishah isemayo: “Aliloondoka nalo, ni kuwa hakuziacha kabisa rakaa mbili mpaka alipokutana na Allaah [yaani rakaa mbili baada ya Alasiri]. Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiziswali, na hakuwa akiziswali Msikitini kwa kuchelea kuutia uzito umma wake. Alikuwa akipenda kuwafanyia wepesi”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (590)].

 

Sunnah Ya Magharibi

 

Kabla yake:

 

Imesuniwa - kwa anayetaka - kuswali rakaa mbili kabla ya Swalaah ya Magharibi kutokana na dalili zifuatazo:

 

1- Hadiyth ya ‘Abdullah bin Mughfal Al-Mazniy (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Swalini kabla ya Magharibi, swalini kabla ya Magharibi, kisha akasema mara ya tatu: Kwa anayetaka)) kuchelea watu kuifanya ni Sunnah raatibah. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1129) na Abu Daawuud (1281)].

 

2- Hadiyth ya Anas bin Maalik aliyesema: “Mwadhini alikuwa anapoadhini, watu katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) husimama na kuziwahi nguzo (za Msikiti) kuswali mpaka anapowatokea Rasuli wa Allaah wakiwa hivyo hivyo. Wanaswali rakaa mbili kabla ya Magharibi, na hakukuwa na chochote kati ya adhana na iqaamah”  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa ikhraaj na Al-Bukhaariy (624) na Muslim (837 na wengineo]

 

Walikuwa wakiharakia kwenye nguzo ili ziwe ni kama sutrah kwa watu wanaopita mbele yao.  

 

Na hii inaonyesha kwamba imesuniwa kuzifupisha kama katika rakaa mbili za Alfajiri. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

3- Hadiyth ya ‘Abdallah bin Mughfal kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Kati ya kila adhana na iqaamah, kuna Swalaah – mara tatu – kwa anayetaka)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (624), na Muslim (838)].

 

4- Hadiyth ya ‘Abdallah bin Az-Zubayr akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

(( ما من صلاة مفروضة إلا وبين يديها ركعتان))

((Hakuna Swalaah yoyote ya faradhi isipokuwa kabla yake kuna rakaa mbili)). [Hadiyth Swahiyh Bimaa Qablahu: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Hibaan (2455) na Ad-daaraqutwniy (1/267), na Hadiyth iliyo kabla yake inaitolea ushahidi]. 

 

Baada yake:

 

Kuswali rakaa mbili baada ya Swalaah ya Magharibi kunatiliwa nguvu kama ilivyotangulia katika Hadiyth za Ibn ‘Umar, ‘Aaishah na Ummu Habiybah. Imesuniwa kuziswali rakaa mbili baada ya Magharibi nyumbani kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa haswali rakaa mbili baada ya Magharibi, na rakaa mbili baada ya Ijumaa isipokuwa nyumbani kwake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (432), At-Twayaalsiy (1836), na At-Twahaawiy (1/336)].

 

Imepokelewa toka kwa Mahmoud bin Lubayd akisema: “Rasuli wa Allaah aliwaendea Bani ‘Abdul Ash-Hal, akawaswalisha Magharibi, na alipotoa tasliym alisema: ((Swalini rakaa hizi mbili majumbani mwenu)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (5/428) na Ibn Maajah (1165)].

 

Ama kisomo katika rakaa hizi mbili, imesuniwa kusoma

(( قل يا أيها الكافرون)) na (( قل هو الله أحد))

 baada ya Suwrat Al-Faatihah kutokana na Hadiyth ya Ibn Mas-’oud aliyesema: “Sidhibiti kwa idadi nilivyomsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisoma katika rakaa mbili baada ya Magharibi, na rakaa mbili kabla ya Alfajiri

(( قل يا أيها الكافرون)) na (( قل هو الله أحد))

[Hadiyth Hasan kwa nyinginezo mfano wake: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (431) na Ibn Maajah (1166) kwa Sanad Dhwaíyf. Ina Hadiyth mwenza iliyopokelewa na Ibn ‘Umar kwa An-Nasaaiy (992), Ibn Maajah (833) na Ahmad (4533) kwa Sanad ambayo haina tatizo]

 

Sunnah Ya ‘Íshaa

 

Kabla yake

 

Imesuniwa - kwa anayetaka - kuswali rakaa mbili kabla ya ‘Ishaa kutokana na ujumuishi wa kusuniwa kuswali kabla ya Swalaah ya faradhi kama ilivyotangulia.

 

Baada yake

 

Kuswali rakaa mbili baada ya Swalaah ya ‘Ishaa kunatiliwa nguvu katika Hadiyth za Ibn ‘Umar, ‘Aaishah na Ummu Habiybah kama ilivyotangulia.

 

 

    (b) Sunnah zisizo rawaatib

 

Hizi ni zile ambazo hazihusiani au kufungamana na Swalaah za faradhi, nazo ni:

 

Share