035-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sijdah Ya Kutoa Shukran
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
035-Sijdah Ya Kutoa Shukran
- Taarifu Yake:
Sijdah ya kutoa shukran ni sijdah anayoifanya mtu wakati inapomjia neema, au inapomwondokea balaa. [Sharhul Minhaaj wa Haashiyatul Qalyuubiy (1/208)]
- Kuswihi Kwake
Imethibiti katika Hadiyth ndefu ya Ka’ab bin Maalik ya kwamba alisujudu ilipomjia habari ya furaha ya kuwa Allaah Kaikubali toba yake. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4418) na Muslim (2769)].
Aidha, kuna Hadiyth nyingi (ambazo kuna maneno kuhusu Sanad zake) zilizopokelewa toka kwa zaidi ya Maswahaba kumi na mbili ambazo zote zinathibitisha kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisujudu kwa ajili ya kumshukuru Allaah. Kati ya hizo ni Hadiyth ya Abu Bakrah (Radhwiya Allaahu Anhu) isemayo kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alikuwa anaporomoka kwenda kusujudu kwa ajili ya kumshukuru Allaah linapomjia jambo la furaha au jambo alilobashiriwa kheri. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (2774), At-Tirmidhy (1578), Ibn Maajah (1394) na wengineo kwa Sanad laini. Nimezitaja Hadiyth wenza za kutosha katika kitabu cha Taadhiymu Qadris Swalaat. Unaweza kuzipitia ukitaka].
Haya ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Maulamaa; Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, Abu Thawr, Ibn Al-Mundhir, na Maswahibu wa Abu Haniyfah. [Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/324), Al-Mughniy (1/627) na Al-Fataawaa An-Nahdiyyah (1/135)]
- Inavyofanyika
Inafanyika kama inavyofanyika sijdah ya Swalaah kama tulivyoeleza kwenye sijdah ya kisomo. Sijdah hii haina ulazima mtu kuwa twahara au kuelekea Qiblah, kwa kuwa si Swalaah ingawa hayo yanapendeza. Aidha, haina ukaraha kuifanya katika nyakati ambazo ni marufuku kuswali kama tulivyoeleza kwenye mlango wa sijdah ya kisomo.
- Je, Inajuzu Ndani Ya Swalaah?
Haijuzu mtu akiwa ndani ya Swalaah, kwa kuwa sababu yake iko nje ya Swalaah. Ikiwa atasujudu ndani ya Swalaah, basi Swalaah yake itabatilika isipokuwa kama hajui au amesahau. Itachukuliwa ni kama mtu aliyezidisha sijdah kwa kusahau.
Yameelezwa haya na Ash-Shaafi’iy na Hanbali. Mahanbali wanasema kwamba haina ubaya ndani ya Swalaah!! [Al-Majmu’u (40/68) na Al-Furu’u (1/505)] Na hii ni kauli dhwa’iyf, na Allah Ndiye Mjuzi Zaidi.