036-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sijdah Ya Kusahau
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Swalaah
036-Sijdah Ya Kusahau
- Taarifu Yake
Kusahau katika lugha ya kawaida ni kughafilika na jambo na moyo kuliacha na kwenda kwa jingine. [Lisaan Al-Arab, kidahizo “Sahaa”]
Ama sijdah ya kusahau kiistilahi, ni sijdah inayofanywa kabla ya kutoa tasliym katika Swalaah au baada yake kwa ajili ya kuunga kosa la kuacha jambo au kufanya lililokatazwa bila ya kukusudia. [Al-Iqnaa cha Ash-Sharbyniy (2/89)]
- Kuswihi Kwake
Madhehebu yote yamekubaliana kuhusu kujuzu kwa sijdah ya sahau kwa mtu ambaye limemtokea katika Swalaah yake yale yaliyojiri kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au mfano wake kwa njia ya kusahau. [Nudhumul Fawaaid Limaa Fiy Hadiythi Dhil Yadayn Minal Fawaaidi cha Al-Haafidh Al-‘Allaaiy uk. 405]
Kuna Hadiyth nyingi Swahiyh zinazozungumzia ujuzifu wa sijdah ya kusahau ambapo humo tutakuta hukumu zake. Ninakuletea hapa ili iwe sahali kuziona na kuyajua masuala husika:
1- Hadiyh ya Abu Hurayrah ya kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( Swalaah inapoadhiniwa, Shaytwaan hugeuka na kupiga mashuzi kwa sauti ili asiisikie adhana, na adhana inapomalizika huja tena. Inapoqimiwa Swalaah hugeuka, na inapomalizika huja tena akaingia kati ya mtu na nafsi yake akimwambia: Kumbuka kadha, kumbuka kadha, na mtu anakuwa hawezi kukumbuka mpaka anakuwa hajui ni rakaa ngapi kaswali. Na kama mmoja wenu hakujua kaswali ngapi, basi asujudu sijdah mbili akiwa amekaa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1231) na Muslim (389)].
2- Hadiyth ya Abu Hurayrah aliposema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali moja kati ya Swalaah mbili (ima Adhuhuri au Alasiri), akatoa tasliym baada ya rakaa mbili. Kisha akaenda kwa fadhaa kwenye Qiblah cha Msikiti akakiegemea, na watu wakatoka haraka. Na hapo Dhul Yadayn akasimama na kusema: Ee Nabiy wa Allaah! Je, umepunguza Swalaah, au umesahau? Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaangalia kulia na kushoto kisha akasema: Anasema nini Dhul Yadayn? Wakasema: Amesema kweli, hukuswali isipokuwa rakaa mbili. Hapo hapo Nabiy akaswali rakaa mbili, kisha akapiga takbiyr, akasujudu, kisha akapiga takbiyr na kunyanyuka”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1229) na Muslim (373)].
3- Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn inayofanana na Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyotangulia inayosema: “Akatoa tasliym baada ya rakaa tatu. Alipokumbushwa, aliswali rakaa moja, kisha akatoa tasliym, halafu akasujudu sijdah mbili na kutoa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (574), An-Nasaaiy (1/26) na Ibn Maajah (1018)].
4- Hadiyth ya ‘Abdullah bin Buhaynah isemayo kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama katika Swalaah ya Adhuhuri bila kukaa tashah-hudi ya kwanza. Alipokamilisha Swalaah yake, alisujudu sijdah mbili akipiga takbiyr katika kila sijdah huku ameketi kabla hajatoa tasliym, na watu wakasujudu pamoja naye kulipia tashah-hudi aliyoisahau. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1224) na Muslim (570)].
5- Hadiyth ya Ibn Mas-’oud aliyesema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali (Ibraahiym kasema: Ima alizidisha au alipunguza), alipotoa tasliym aliulizwa: Je, pametokea jambo katika Swalaah? Akasema: Kwani kuna nini? Wakasema: Umeswali rakaa kadhaa. Akaikunja miguu yake, akaelekea Qiblah, akasujudu sijdah mbili, kisha akatoa tasliym. Halafu akatuelekea kwa uso wake akasema:
Likitokea jambo katika Swalaah nitawajulisheni. Nami bila shaka ni mtu, ninasahau kama mnavyosahau, nami ninaposahau, basi nikumbusheni. Na mmoja wenu akifanya shaka kwenye Swalaah yake, basi ajaribu awezavyo kuangalia alilolifanya sawa, halafu alitimizie, kisha asujudu sijdah mbili”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1226) na Muslim (572)].
Tamshi la Al-Bukhaariy linasema: “Kisha atoe tasliym, halafu asujudu sijdah mbili”. Na katika riwaya: “Aliswali rakaa tano, akasujudu sijdah mbili”.
6- Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy asemaye kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Akifanya shaka mmoja wenu kwenye Swalaah yake, kisha asijue ni rakaa ngapi ameswali kama ni tatu au nne, basi aiweke shaka yake kando na ajengee juu ya alilo na uhakika nalo, halafu asujudu sijdah mbili kabla hajatoa tasliym. Na kama atakuwa ameswali rakaa tano, basi sijdah mbili zitaifanya Swalaah yake shufwa, na kama kaswali kutimiza nne, basi sijdah mbili zitakuwa za kumdhili Shaytwaan)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (571), Abu Daawuud (1024), An-Nasaaiy (3/27) na Ibn Maajah (1210)].
- Sababu Za Sijdah Ya Kusahau
Sijdah ya sahau imewekwa katika Swalaah kutokana na sababu tatu:
1- Kupunguza kitu
Pakitokea upungufu katika Swalaah kwa kughafilika au kusahau, chenye kuachwa kitakuwa ima nguzo, au wajibu au Sunnah.
(a) Ikiwa ataiacha nguzo katika rakaa kwa kusahau kisha akaikumbuka kabla ya kuanza kisomo kwenye rakaa inayofuatia, basi itamlazimu arudi kwenye nguzo hiyo, aifanye pamoja na vitendo vinavyofuatia baada yake, kisha itamlazimu asujudu sijdah ya kusahau mwishoni mwa Swalaah yake kama tutakavyokuja kulielezea hilo zaidi katika mahala pake. Na kama hakuikumbuka nguzo hiyo ila baada ya kuanza kisomo katika rakaa inayofuatia, basi rakaa yenye upungufu itabatilika. Itamlazimu aifute, akamilishe Swalaah yake, na kisha asujudu sijdah ya kusahau. [Haya ndiyo waliyoyaeleza Mahanbali, na Madhehebu ya Maalik na Ash-Shaafi’iy yako karibu nao. Angalia Ad-Dusuwqiy (1/293), Al-Majmu’u (4/116), Kash-Shaaful Qinaa (1/402), na Al-Mughniy (2/6)]
Ikiwa atasahau rakaa moja au zaidi, basi atazikamilisha, kisha atasujudu sijdah ya kusahau. Asili ya hili, ni Hadiyth ya Abu Hurayrah – kuhusu kisa cha Dhul Yadayn – na ‘Imraan bin Haswiyn.
(b) Ikiwa atawacha wajibu katika nyajibu za Swalaah kama tashah-hudi ya kati kwa mfano, ataifanya ikiwa ataweza kuiwahi kabla hajaondoka mahala pake na hatolazimiwa na lolote. Na ikiwa ataikumbuka baada ya kuondoka mahala pake na kabla ya kufika kwenye nguzo inayofuatia, basi atarudi ili aifanye, kisha ataikamilisha Swalaah yake na hatosujudu sijdah ya kusahau. Ikiwa ataikumbuka baada ya kuondoka mahala pake na baada ya kufika kwenye nguzo inayofuatia, itakuwa imempomoka na hatorudi ili aifanye, bali atakamilisha Swalaah na atasujudu sijdah ya kusahau.
Asili ya hili ni Hadiyth ya ‘Abdullah bin Buhaynah tuliyoitaja nyuma.
Imepokelewa toka kwa Ziyaad bin ‘Allaaqah akisema: “Al-Mughiyrah bin Shu’ubah alituswalisha. Aliposwali rakaa mbili, alisimama moja kwa moja bila kukaa na walio nyuma yake wakampigia tasbiyh lakini yeye aliwaashiria wasimame. Alipomaliza Swalaah, alitoa tasliym, kisha akasujudu sijdah mbili na kusema: Hivi ndivyo alivyofanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Na katika riwaya nyingine amesema: “Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ikiwa mmoja wenu atapitiliza na akawa tayari ashasimama, basi aikamilishe Swalaah na asujudu sijdah mbili za sahau. Lakini kama hakuwa bado hajasimama vyema, basi akae na hana sijdah ya sahau)). [Hadiyth Swahiyh kwa Sanad zake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1036), At-Tirmidhiy (365), Ahmad (4/247) na At-Twahaawiy katika Al-Ma’aniy (1/439). Angalia Al-Irwaa (388)].
(c) Ikiwa amewacha lililosuniwa, kuna kauli mbili. Ya kwanza inasema kwamba hatosujudu kwa kuwa yaliyosuniwa hayana ubaya yakiachwa, na ya pili inasema kwamba imesuniwa asujudu lakini si lazima ili asije kuongeza tanzu juu ya shina kutokana na Hadiyth Dhwa’iyf isemayo: ((Kila sahau ina sijdah mbili)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1038), Ibn Maajah (1219), Ahmad (5/285), ‘Abdul Razzaaq (3533), At-Twayaalsiy (997), Al-Bayhaqiy (2/337) na At-Twabaraaniy (2/92). Kuna mvutano katika Sanad yake, kuna udhwa’iyf na mkatiko]
2- Kuzidisha
Ikiwa mwenye kuswali amesahau akazidisha rakaa moja au zaidi katika Swalaah yake, kama atakumbuka kabla hajaimaliza Swalaah, itambidi akae –kwa hali yoyote awayo- asome tashah-hudi, atoe tasliym, kisha asujudu sijdah ya kusahau na kutoa tasliym. Na kama hakukumbuka ila baada ya kutoa tasliym, basi atasujudu sijdah ya kusahau na kutoa tasliym.
Hii ni kutokana na Hadiyth ya Ibn Mas-’oud inayosema kwamba Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali adhuhuri rakaa tano. Akaambiwa: “Je, Swalaah imeongezwa?” Akauliza: “Kivipi? Akaambiwa: “Umeswali tano”, hapo hapo akasujudu sijdah mbili baada ya kutoa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja nyuma kidogo].
3- Kufanya shaka
Ikiwa mwenye kuswali atafanya shaka kama ameswali rakaa tatu au nne kwa mfano, hapo atajitahidi kuyakumbuka aliyoyafanya katika Swalaah yake. Ikiwa atalitilia nguvu jambo moja kati ya mawili, basi atalishika hilo na atasujudu baada ya tasliym kama ilivyo kwenye Hadiyth iliyotangulia ya Ibn Mas-’oud.
Na kama hakulitilia nguvu lolote kati ya mawili, basi atalishika lenye yakini ambalo ni kuswali zilizo chache, na atasujudu kabla ya tasliym. Hii ni kutokana na Hadiyth iliyotangulia ya Abu Sa’iyd pamoja na Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf anayesema: “Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Anaposahau mmoja wenu katika Swalaah yake, asijue kama kaswali rakaa moja au mbili, basi ashike kwamba kaswali moja. Na kama hajui kama kaswali rakaa mbili au tatu, basi ashike kwamba kaswali mbili. Na kama hajui kaswali rakaa tatu au nne, basi ashike kwamba kaswali tatu, na kisha asujudu sijdah mbili kabla ya tasliym)). [Kuna ulaini: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhy (398), Ibn Maajah (1209), Al-Haakim (1/325) na Al-Bayhaqiy (2/332). Kuna 'an'anah (fulani toka kwa fulani) ya Ibn Is-Haaq, naye ameingizwa kwenye isnadi bila kuwepo].
- Angalizo: Shaka haizingatiwi katika ‘ibaadah kwenye hali tatu
[Kitabu cha sijdah ya kusahau cha Sheikh Mahmoud Ghariyb ukurasa wa 17]
1- Ikiwa ni fikra tu zisizo kweli, kama wasiwasi.
2- Ikiwa mtu ana ugonjwa wa wasiwasi kwa namna ambayo haswali Swalaah yoyote ila hufanya shaka.
3- Ikiwa shaka itakuja baada ya kumaliza ‘ibaadah, hatoitia maanani madhali hajayakinisha bali atalifuata alilo na yakini nalo.
- Hukmu Ya Sijdah Ya Kusahau
Maulamaa wana kauli mbili kuhusiana na hukmu ya sijdah ya kusahau wakati inapopatikana sababu yake: [Fat-hul Qadiyr (1/502), Al-Qawaaniyn (67), Al-Majmu’u (4/152), Al-Mughniy (2/36), Kash-Shaaful Qinaa (1/408), Al-Muhallaa (4/159) na Majmu’u Al-Fataawaa (23/27)]
Kwanza: Ni wajibu
Ni madhehebu ya Hanafi na kauli ya Maalik. Mahanbal na Adh-Dwahiriyyah wamelipitisha hivyo, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. Hoja yao ni:
1- Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameliamuru jambo hili katika Hadiyth zilizotangulia, na katika baadhi ya Hadiyth ni kwa kufanya shaka tu.
2- Kudumu na kutoacha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kusujudu sijdah mbili za kusahau inapotokea sababu yake.
Ya pili: Ni Sunnah:
Hili ni mashuhuri likipokelewa toka kwa Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Mahanbali. Hoja yao ni:
1- Yaliyoelezwa katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd asemaye: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Akifanya shaka mmoja wenu kwenye Swalaah yake, basi aache shaka na ajengee juu ya yakini. Akiyakinisha ukamilifu, asujudu sijdah mbili. Ikiwa Swalaah yake ni kamili, basi rakaa ya ziada pamoja na sijdah mbili zitakuwa ni Sunnah. Ama ikiwa pungufu, basi rakaa itakuwa ni kamilisho la Swalaah yake na sijdah mbili zitakuwa ni za kumdhili shaytwaan)). [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1024) na Ibn Maajah (1210). Asili yake ni kutoka kwa Muslim lakini bila ya kutaja neno "sijdah mbili ni Sunnah"].
Wanasema kwamba Hadiyth hapa inaonyesha kwamba sijdah mbili ni Sunnah na wala si wajibu.
Lenye nguvu ni kuwa sijdah hizi ni wajibu. Sheikh wa Uislamu amewajibu wenye kusema ni Sunnah kwa hoja mbili:
1- Tamshi hili “rakaa ya ziada pamoja na sijdah mbili zitakuwa ni Sunnah” haliko katika Hadiyth Swahiyh, na tamshi swahiyh ni: “basi aiweke shaka yake kando na ajengee juu ya alilo na uhakika nalo, halafu asujudu sijdah mbili kabla hajatoa tasliym. Na kama atakuwa ameswali rakaa tano, basi sijdah mbili zitaifanya Swalaah yake shufwa, na kama kaswali kutimiza nne, basi sijdah mbili zitakuwa za kumdhili shaytwaan”, nalo lashurutisha wajibu wa mawili; rakaa na sijdah mbili.
2- Tukijaalia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, basi maana yake ni kuwa yeye ameamuriwa hilo pamoja na kuweko shaka. Na ikiwa tutakadiria kwamba Swalaah yake ni kamili bila ya kupungua chochote, basi hiyo inakuwa ni ziada katika kitendo chake, naye atalipwa thawabu kama katika Sunnah.
- Mahala Pa Sijdah (Kabla Ya Tasliym Au Baada Yake)?
Maulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na hili katika kauli tisa kwa mujibu wa Hadiyth Thabiti zinazohusiana na mlango huu:
[Ibn ‘Aabidiyn (1/495), Al-Mabsuwtw (1/219), Al-Qawaaniyna (67), Ad-Dusuwqiy (1/274), Rawdhwat At-Twaalibiyna (1/315), Al-Majmu’u (4/154), Al-Mughniy (2/22), Al-Kaafiy (1/209), Al-Awsatw (3/307) Bidaayatul Mujtahid (1/279) na Naylul Aw-Twaar (3/132-135)]
Ya kwanza:
Sijdah yote ni kabla ya tasliym. Ni kauli ya Abu Hurayrah, Mak-houl, Az-Zuhriy, Ibn Al-Musayyib, Rabiy’ah, Al-Awzaa’iy na Al-Layth. Ni madhehebu mapya ya Ash-Shaafi’iy.
Ya pili:
Sijdah yote ni baada ya tasliym. Ni kauli ya Sa’ad bin Waqqaas, Ibn Mas-’oud, Anas, Ibn Az-Zubayr, na Ibn ‘Abbaas. Pia imesimuliwa toka kwa ‘Aliy, ‘Ammaar, Al-Hasan, An-Nakh’iy na Ath-Thawriy. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maswahibu wake.
Ya tatu:
Kama amezidisha kitu atasujudu baada ya tasliym, na kama kapunguza atasujudu kabla ya tasliym. Ni kauli ya Maalik, Al-Mazniy, Abu Thawr na Ash-Shaafi’iy.
Ya nne:
Kila Hadiyth itatumika kwa mujibu wa inavyoeleza, na kama haikueleza kitu, basi atasujudu kabla ya kutoa tasliym. Ni kauli ya Ahmad na Ibn Abu Khaythamah, na ni chaguo la Ibn Al-Mundhir.
Ya tano:
Kila Hadiyth itatumika kwa mujibu wa inavyoeleza, na kama haikueleza kitu, basi atasujudu baada ya kutoa tasliym kama alizidisha, na kabla yake kama alipunguza. Ni kauli ya Is-Haaq bin Raahawiyyah.
Ya sita:
Ni kama iliyotangulia, lakini mwenyewe atachagua kusujudu kabla au baada ya tasliym kama Hadiyth haikuelezea kitu. Ni chaguo la Ash-Shawkaaniy.
Ya saba:
Mwenye kujengea juu ya uchache, atasujudu kabla ya tasliym na mwenye kupima usahihi atasujudu baada ya tasliym. Ni kauli ya Ibn Hibaan.
Ya nane:
Ana khiyari ya kusujudu kabla ya tasliym au baada yake. Hilo limesimuliwa toka kwa ‘Aliy, na ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na At-Twabariy.
Ya tisa:
Atasujudu baada ya tasliym isipokuwa mahala pawili ambapo mwenyewe atachagua. Pa kwanza ikiwa atasimama bila kukaa tasha-hudi ya kwanza, na pa pili ni kama hakujua kama ameswali rakaa tatu au nne. Hapa atashika kwamba ameswali zilizo chache na mwenyewe atachagua kusujudu kabla au baada ya tasliym. Ni kauli ya Ibn Hazm na Ahlu Adh-Dhwaahir.
- La Sahihi Ambalo Hadiyth Zilizotangulia Zinakutania
Kupambanua kati ya kuzidisha na kupunguza, na kati ya shaka pamoja na kuhakiki, na shaka pamoja na kujengea juu ya yakini. Hili ni chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah.
[Majmu’u Al-Fataawaa (23/24-25)]
Amesema: “Na hili ni moja ya riwaya toka kwa Ahmad, na madhehebu ya Maalik yako karibu nalo, na si mfano wake. Na hili, pamoja na matumizi yaliyomo ya Hadiyth zote, lakini kuna tofauti ya kimantiki, nayo ni kwamba:
1- Ikiwa ni kupunguza - kama kuacha tasha-hudi ya kwanza - Swalaah itahitajia kuungwa, na cha kuungia kinakuwa kabla ya kutoa tasliym ili Swalaah ikamilike, kwani tasliym ni kuimaliza na kuifunga Swalaah.
2- Ikiwa ni kuzidisha – kama rakaa – basi haikusanywi ziada mbili kwenye Swalaah moja, na sijdah ya sahau itakuwa ni baada ya tasliym, kwa kuwa hilo linamdhili shaytwaan sawa na Swalaah ya kando ambayo ameiungia kwayo upungufu wa Swalaah yake, kwani Nabiy amezifanya sijdah mbili kama rakaa.
3- Vile vile, akifanya shaka na akahakiki, basi ataikamilisha Swalaah yake na atasujudu baada ya tasliym ili kumdhili shaytwaan.
4- Aidha, akitoa tasliym huku akiwa amebakisha sehemu ya Swalaah yake kisha akakamilisha, basi anakuwa ameshaitimiza na tasliym itakuwa ni ziada. Hapa sijdah ya sahau itakuwa baada ya tasliym kwa kuwa ni ya kumdhili shaytwaan.
5- Ikiwa atafanya shaka na hakuweza kujua lipi la uhakika, hapa itakuwa ima ameswali rakaa nne au tano. Kama ameswali tano, sijdah mbili zitaifanya Swalaah yake kuwa shufwa ili awe kama ameswali rakaa sita na si tano, na hii inakuwa kabla ya tasliym.
Ibn Taymiyah kasema: “Kauli hii tunayoishabikia, ndiyo inayotumia Hadiyth zote bila kuacha Hadiyth hata moja pamoja na kutumia Qiyaas Swahiyh kwa lile ambalo halijagusiwa na Hadiyth, na kuliambatisha lisilotajwa na Hadiyth kwa lile linalofanana nalo lililotajwa”.
- Ikiwa Mtu Kasahau Kusujudu, Kisha Ukapita Muda Au Wudhuu Wake Ukatenguka, Je Atajengea Juu Ya Swalaah Yake Na Kusujudu Sijdah Ya Kusahau, Au Ataianza Tena Swalaah Upya?
(a) Ikiwa utapita muda mrefu lakini wudhuu bado anao, Maulamaa wana kauli mbili:
Ya kwanza:
Ataianza tena Swalaah upya. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Mabsuwtw (1/224), Al-Mudawwanah (1/135), Al-Majmu’u (4/156) na Al-Mughniy (2/13)]
Wanasema kwamba Swalaah ni moja na haijuzu kuijenga vipande vipande mbali na muda kurefuka.
Ya pili:
Atajengea juu ya Swalaah yake na atasujudu ikiwa wudhuu haujatenguka. Ni kauli ya Maalik, na kauli ya zamani ya Ash-Shaafi’iy. Pia Yahya bin Sa’iyd Al-Answaariy, Al-Layth, Al-Awzaa’iy, Ibn Hazm na Ibn Taymiyah, isipokuwa yeye ameihusisha na sijdah ya baada ya tasliym. [Al-Mudawwanah (1/135), Al-Muhalla (4/166) na Majmu’u Al-Fataawaa (23/32-35)]
Wanasema kwamba urefu wa muda hauna kidhibiti maalumu, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa tasliym kwa kusahau, akazungumza, akakagua hali, akatoka Msikitini, akaingia nyumbani kwake, kisha akalijua hilo, akatoka na kutimiza kilichopungua katika Swalaah yake, kisha akasujudu sijdah mbili kutokana na sahau aliyoifanya.
Na kwa vile yeye ameamuriwa kuitimiza Swalaah na kusujudu sijdah ya kusahau, imekuwa ni wajibu kutokana na ujumuishi wa kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenye kusahau Swalaah, au akalala ikampita, basi kafara yake ni kuiswali anapoikumbuka)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (684), An-Nasaaiy (614) na kwa Al-Bukhaariy mfano wake (597)].
Ninasema: ”Hii ni kauli madhubuti kabisa, lakini mwenye kutaka kuwa salama zaidi, ni vyema aswali upya, nayo ni haki yake. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.
(b) Kama wudhuu umemtenguka baada ya kutoa tasliym katika Swalaah aliyoiswali pungufu, basi Swalaah yake ni batili kwa mujibu wa itifaki ya Jamhuri. Ikiwa amesahau kusujudu – baada ya tasliym - kwa kuongeza kitu katika Swalaah yake, inaruhusiwa asujudu hata kama wudhuu umemtenguka, kwa kuwa sijdah mbili ni za kumdhili shaytwaan kama alivyosema Ibn Taymiyah. [Majmu’u Al-Fataawaa (23/36)]
Ninasema: “Yaani atatawadha na kusujudu. Hili ni madhubuti na lenye mwelekeo zaidi”.
- Kusahau Zaidi Ya Mara Moja Kwenye Swalaah Moja
[Raddul Muhtaar (1/497), Mawaahibul Jaliyl (2/15), Sharhul Minhaaj (1/204) na Al-Mughniy (2/39)]
Kama mwenye kuswali atasahau zaidi ya mara moja, basi hatosujudu isipokuwa sijdah mbili tu za sahau. Hii ni kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa, kwa kuwa haikunukuliwa toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala kwa Swahaba yeyote ya kwamba walifanya sijdah ziada kutokana na sahau ya zaidi ya mara moja pamoja na kwamba hilo linaweza kumpata yeyote mwenye kuswali.
Na kwa kuwa lau si maingiliano, basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelisujudu baada ya kusahau. Na alipokawiza hadi mwisho wa Swalaah, tumejua kwamba alifanya hivyo kwa ajili ya kuzijumuisha sahau zote zilizotendeka ndani ya Swalaah.
Ninasema: “Ama Hadiyth Marfu’u ya Thawbaan: ((Kwa kila sahau sijdah mbili baada ya kutoa tasliym)), ni Dhwa’iyf, haifai”.
- Sijdah Ya Sahau Katika Swalaah Ya Sunnah
[Sharhu Muslim (5/60), Fat-hul Baariy (3/125-126) na Al-Awsatw (3/325)]
Jamhuri ya Maulamaa wanasema kwamba mtu atasujudu sijdah ya sahau katika Swalaah ya Sunnah kama anavyofanya katika Swalaah ya Faradhi kutokana na kutobaguliwa kati ya Swalaah ya Faradhi au ya Sunnah katika Hadiyth husika mbali na kutokuwepo dalili ya ufarikishaji.
Imepokelewa toka kwa Abul ‘Aaliyah akisema: “Nilimwona Ibn ‘Abbaas akisujudu sijdah mbili baada ya Witri yake”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Al-Bukhaariy kasema ni Mu’allaq (3/125-Fat-h) na Ibn Abu Shaybah kasema ni Mawswuul kwa Sanad Swahiyh (2/81)].
Imepokelewa toka kwa ‘Atwaa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Ukipitikiwa kwenye Swalaah ya Sunnah, basi sujudu sijdah mbili”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abil Mundhir katika Al-Awsatw (3/325)].
- Miongoni Mwa Hukmu Za Sahau Katika Swalaah Ya Jamaa
Katika Swalaah, imamu au maamuma anaweza kupitikiwa na sahau.
(1) Imamu akipitikiwa
(a) Maamuma anaruhusiwa kumzindusha imamu wake kama atasahau. Kwa wanaume inakuwa ni kwa kusema “Subhaanal Laah” na kwa wanawake ni kupiga kikofi. Hii ni kauli ya Jamhuri ya Maulaama kinyume na Maalik. [Fat-hul Qadiyr (1/356), Mawaahibul Jaliyl (2/29), Nihaayatul Muhtaaj (2/44) na Al-Mughniy (2/19)]
Ni kutokana na Hadiyth ya Sahl bin Sa’iyd ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Mwenye kupatwa na jambo katika Swalaah yake, basi aseme “Subhaanal Laah”)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1218) na An-Nasaaiy (784)].
Na katika tamshi jingine: ((Likikupateni jambo, basi wanaume waseme “Subhaanal Laah”)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (7190), An-Nasaaiy (793) na Abu Daawuud (940)].
Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Tasbiyh ni kwa wanaume, na kupiga kikofi ni kwa wanawake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1203) na Muslim (422)].
Ama kwa upande wa Maalik, yeye anasema kwamba wanaume na wanawake watasema “Subhaanal Laah” na ni karaha kwa wanawake kupiga kikofi katika Swalaah!! Na Hadiyth ni hoja dhidi yake. Kupiga kikofi ni kupiga kwa tumbo la kiganja chake mgongo wa kiganja kingine kwa ajili ya kumtanabahisha imamu.
(b) Imamu kuitikia uzindushi wa maamuma na maamuma kumfuata.
[Ibn ‘Aabidiyn (1/507), Nihaayatul Muhtaaj (2/75), Al-Khurashiy (1/322) na Al-Mughniy (2/20)]
Jamhuri ya Maulamaa; Hanafi, Ash-Shaafi’iy na Hanbali wanasema kwamba ikiwa imamu atazidisha katika Swalaah, naye akawa na yakini au ikamghilibikia dhana kwamba yeye yuko sawa na huku maamuma wanaona kwamba amekwenda kwenye rakaa ya tano kwa mfano, basi hatowaitikia.
Maalik anasema kwamba ikiwa maamuma ni wengi kwa maana kwamba ni vigumu wao wote kukosea, basi imamu itambidi aachane na yakini yake na awafuate kwenye lile walilomwashiria. Na hii yote ikiwa imamu imemghilibikia dhana au akawa na yakini kwamba yeye yuko sawa. Lakini ikiwa atakuwa na shaka, basi hapo itamlazimu kiwajibu kuwasikiliza maamuma kutokana na Hadiyth ya Dhul Yadayn iliyotangulia. Haya ndiyo waliyosema Jamhuri kuhusiana na shaka kinyume na Mashaafi’i ambao wanaona kwamba imamu ataijengea yakini yake mwenyewe na hatowasikiliza maamuma!!
Ninasema: “Kauli ya Jamhuri ina uzito zaidi, kwa kuwa ushuhuda wa maamuma wanaoaminika, ni uthibitisho tosha. Ikiwa itamghilibikia kwamba maamuma wako sawa, basi atawafuata. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.
(c) Imamu akisahau na akasujudu, basi ni lazima maamuma wamfuate.
Hii ni sawasawa ikiwa maamuma atasahau pamoja naye au imamu akasahau peke yake. Ibn Al-Mundhir amesema kwenye Al-Awsatw (3/322): “Maulamaa wote tunaowajua vyema wamekubaliana ya kwamba maamuma anawajibika kusujudu pamoja na imamu pindi imamu anaposahau akasujudu. Hoja yao ni Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
((Hakika si jinginelo, imamu amewekwa ili afuatwe)). [Hadiyth Swahiyh: Imetajwa nyuma].
Hii ni kwa vile maamuma anamfuata imamu, na hukmu yake ni hukmu yake anaposahau na anapokuwa hakusahau pia.
(d) Imamu akisahau asisujudu, je maamuma watasujudu?
[Al-Awsatw (3/322), Ibn ‘Aabidiyn (1/499), Al-Khurashiy (1/331), Al-Majmu’u (4/143) na Al-Mughniy (1/41)]
Maulamaa wamekhitalifiana katika suala hili. ‘Atwaa, Al-Hasan, An-Nakh’iy, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na Masahibu zake wanaona kwamba ikiwa hakusujudu, basi nao wasisujudu, kwani wakisujudu watakwenda kinyume naye.
Ama Ibn Syriyna, Qataadah, Al-Awzaa’iy, Maalik, Al-Layth, Ash-Shaafi’iy, Abu Thawr na riwaya toka kwa Ahmad, wao wanaona kwamba maamuma watasujudu hata kama imamu wao hakusujudu. Hii ni kwa kuwa jambo hili ni wajibu kwao na kwake na haliwaondokei kwa imamu kuliwacha, bali kila mmoja ni lazima autekeleze wajibu wake na faradhi yake.
(e) Je, maamuma aliyepitwa na baadhi ya rakaa atasujudu imamu wake akisujudu?
Mtu akipata sehemu ya Swalaah ya imamu, na imamu ni lazima asujudu sijdah ya kusahau, hapa Maulamaa wana kauli nne:
[Maulamaa wamekhitalifiana juu ya kiasi cha mtu kumpata imamu kinachomlazimu kumfuata katika sijdah ya sahau. Jamhuri wamesema: “Akiipata nguzo moja kabla hajasujudu sijdah ya sahau, itamlazimu asujudu naye sawasawa ikiwa sahau ilikuwa kabla hajamfuata au baada ya kumfuata”. Maalik anasema: “Kama hakuipata rakaa moja, hatosujudu”. Ninasema: “Hii ndiyo yenye nguvu zaidi. Lakini ikiwa atasahau pamoja na imamu, basi atawajibika kusujudu kwa kusahau mwenyewe na si kwa sahau ya imamu wake. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.]
Ya kwanza:
Atasujudu pamoja na imamu kisha atakamilisha rakaa zilizobakia. Ni kauli ya Ash-Sha’abiy, ‘Atwaa, An-Nakh’iy, Al-Hasan, Ahmad, Abu Thawr, Abu Haniyfah na Masahibu zake. [Al-Awsatw (3/323), Masaail Ahmad cha Abu Daawuud (55) na Al-Aswl (1/234)]
Ya pili:
Ataimaliza Swalaah, kisha atasujudu kwa sahau ya imamu wake. Ni kauli ya Ibn Syriyn na Is-Haaq bin Raahawiyyah. [Al-Awsatw (3/323)]
Ya tatu:
Atasujudu pamoja na imamu, halafu atakamilisha, kisha atasujudu baada ya kumaliza Swalaah yake. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy. [Al-Ummu cha Ash-Shaafi’iy (1/132)]
Ya nne:
Akisujudu imamu kabla ya kutoa tasliym, atasujudu naye lakini akisujudu baada ya tasliym, atasimama aikamilishe Swalaah yake kisha asujudu. Ni kauli ya Maalik, Al-Awzaa’iy na Al-Layth bin Sa’ad. [Al-Awsatw (3/323) na Al-Mudawwanah (1/139)]
Ninasema: “Huenda kauli hii ya mwisho ndiyo iliyo karibu zaidi na neno lake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika si jinginelo, imamu amewekwa ili afuatwe. Basi akisujudu nanyi sujuduni)). Na nyuma tushasema kwamba kusujudu kabla ya tasliym kunakuwa ni kuunga upungufu, hivyo imepasa kumfuata.
Ama zinazosujudiwa baada ya tasliym, hiyo ni kumdhili shaytwaan. Atasimama akamilishe rakaa zake zilizobakia, kisha atasujudu kwa ajili ya sahau ya imamu wake kutokana na neno lake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mlioipata basi swalini, na iliyokupiteni basi itimizeni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (635) na Muslim (602)].
Na kwa hivi, anakuwa amemfuata imamu kwa upande wa kuwa imamu alisujudu mwishoni mwa Swalaah yake, naye pia kadhalika.
2- Maamuma akisahau nyuma ya imamu
[Al-Awsatw (3/320) na Al-Muhalla (4/167)]
Maamuma akipitikiwa akasahau kitu nyuma ya imamu basi hatosujudu, bali imamu atambebea sahau yake. Hii ndio kauli ya Maulamaa wengi wakiwemo maimamu wanne na wengineo. Kuna Hadiyth Marfu’u iliyokuja kuhusiana na suala hili iliyopokelewa na ‘Umar toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
((Aliyeko nyuma ya imamu hana sahau. Na ikiwa imamu atasahau, basi ni juu yake sahau na aliyeko nyuma yake. Na ikiwa atasahau nyuma ya imamu, basi hana sahau bali imamu atamtosheleza)). [Hadiyth hii ni Dhwa’iyf na haifai na imefanyiwa “ikhraaj” na Ad Daara Qutwniy (1/377) na Al-Bayhaqiy (2/352)], .lakini wengi wanaitumia.
Ibn Syriyna, Daawoud na Ibn Hazm wako kinyume na hili. Wanasema kwamba maamuma atasujudu akiwa kama yuko peke yake au imamu kwa kuwa agizo la Nabiy la kusujudu sijdah mbili kwa kila mwenye kupitikiwa katika Swalaah yake, halimhusu imamu tu wala maamuma mwenye kuswali peke yake.
Ninasema: “Kauli ya Jamhuri ndiyo yenye uzito zaidi na si Hadiyth Marfu’u. Na hii ni kwa yale aliyoyaelezea Al’Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahul Laahu) aliposema: [Irwaaul Ghaliyl (2/132)]
“Sisi tunajua kwa yakini kwamba Maswahaba waliokuwa wakimfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Swalaah, walikuwa wakisahau sahau za kuwawajibisha kusujudu lau kama wangelikuwa wanaswali mtu peke yake. Na jambo hili hakuna anayeweza kulipinga. Na ikiwa ni hivyo, basi haikunukuliwa kwamba kuna yeyote kati yao aliyesujudu baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa tasliym. Na lau kama hilo lingelikuwa linajuzu, basi wangelifanya, na kama wangelifanya basi wangelinukuu. Na kwa kuwa hakuna nukuu yoyote, tunajua kwamba hilo halijuzu na suala liko wazi kabisa. Haya yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Mu’aawiyah bin Al-Hakam ambaye alizungumza ndani ya Swalaah nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa hajui uharamu wa hilo, lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumwamuru asujudu sijdah ya kusahau”.
- Namna Ya Kusujudu
Sijdah ya sahau ni sijdah mbili kama sijdah zile zile za kwenye rakaa. Atapiga takbiyr katika kila kinyanyuko na kiinamo, kisha atatoa tasliym, sawasawa sijdah ikiwa kabla ya tasliym au baada yake.
Ama takbiyr, ni katika Hadiyth ya Ibn Bujaynah isemayo: “Alipoitimiza Swalaah yake, alisujudu sijdah mbili; akapiga takbiyr katika kila sijdah akiwa ameketi kabla ya kutoa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja mwanzoni mwa mlango huu]. Na hii ni kabla ya tasliym.
Ama baada ya tasliym, hilo limethibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah isemayo: “…Akaswali rakaa mbili akatoa tasliym, kisha akapiga takbiyr akasujudu, halafu akapiga takbiyr akanyanyuka, kisha akapiga takbiyr akasujudu, halafu akapiga takbiyr akanyanyuka”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja mwanzoni mwa mlango huu].
- Je, Sijdah Ya Sahau Ina Takbiyr Ya Kuhirimia?
Kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri na Hadiyth zinavyoonyesha ni kuwa atatosheka kwa takbiyr ya kusujudu. [Fat-hul Baariy (3/99)]
Maalik amesema: “Ni lazima takbiyr ya kuhirimia kabla ya kusujudu kutokana na ziada iliyopo kwenye Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusiana na kisa cha Dhul Yadayn isemayo: “Ni kwamba alipiga takbiyr akasujudu. Hisham akasema – yaani Ibn Hassan – alipiga takbiyr, kisha akapiga takbiyr, na akasujudu”. Hii ni ziada isiyo ya kawaida na haithibiti.
Ibn ‘Abdul Barri anasema: [Al-Istidhkaar (4/345)]
“Sisi na Jamhuri ya Maulamaa tunasema kwamba kutoa tasliym kwa kusahau hakumtoi mtu katika Swalaah yake wala hakuiharibu. Akiwa kwenye Swalaah yake ataikamilishia, hakuna maana kuhirimia, kwa kuwa haanzi upya Swalaah bali anaitimiza na kuikamilisha. Anayeamuriwa takbiyr ya kuhirimia ni yule anayeanza kuswali”.
Ama kutoa tasliym baada ya sijdah mbili, hilo limethibiti kwenye habari ya Dhul Yadayn, na Hadiyth ya Ibn Mas-’oud toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba aliswali rakaa tano, na Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn isemayo: “Akaswali rakaa kisha akatoa tasliym, halafu akasujudu sijdah mbili, kisha akatoa tasliym”. [Hadiyth Swahiyh: Tumeitaja mwanzoni mwa mlango huu].
- Je, Atasoma Tashah-hudi Baada Ya Sijdah Mbili Za Sahau?
Maulamaa wana kauli nne kuhusiana na suala hili. [Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (3/314-317). Kuna kauli inayothibitisha, inayozuia, inayokhiyarisha na inayofarikisha kati ya sijdah ya baada ya tasliym ambayo husomewa tashah-hudi na kati ya sijdah ya kabla yake ambayo haisomewi tashah-hudi]
Kauli sahihi zaidi ni ile isemayo kwamba mtu hasomi tashah-hudi baada ya sijdah mbili za sahau kwa vile hilo halikuthibiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Aliyesema kuwa inasomwa ametegemea yaliyohadithiwa kwenye Hadiyth ya ‘Imraan bin Haswiyn isemayo kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaswalisha akasahau, kisha akasujudu sijdah mbili, halafu akasoma tashah-hudi, kisha akatoa tasliym. [Hadiyth Shaadh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (1039), At-Tirmidhy (395), Ibn Al-Jaaroud (247) na wengineo. Al-Bayhaqiy, Ibn ‘Abdul Barri, Ibn Taymiyah na wengineo wamesema ni Dhwa’iyf. Pia Al’Allaamah Al-Albaaniy kama ilivyo kwenye Al-Irwaa (403)]
Ni Hadiyth Shaadh isiyofaa, na kwa ajili hiyo Sheikh wa Uislamu (23/48) amesema: “Imethibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisujudu baada ya tasliym zaidi ya mara moja kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Ibn Mas-’oud wakati aliposwali rakaa tano, na pia katika Hadiyth ya Abu Hurayrah kuhusu Dhul Yadayn na ‘Imraan bin Haswiyn. Lakini hakuna kauli yake hata moja yenye kuamuru kusoma tashah-hudi baada ya sijdah wala kwenye Hadiyth zozote Swahiyh, bali tashah-hudi ni kitendo kirefu kinachoweza kuwa sawa na sijdah mbili au zaidi, na kitendo kama hiki kinastahiki kuhifadhiwa na kusajiliwa kwenye kumbukumbu na kupewa shime na uzito wa kuhadithiwa na kunukuliwa. Na lau kama angelikuwa amesoma tashah-hudi, basi angelieleza hilo yule aliyeeleza kwamba alisujudu, na sababu ya kulitaja hilo ingelikuwa na nguvu zaidi kuliko kuitaja tasliym na takbiyr wakati wa kuinama na kunyanyuka. Na hizi ni kauli nyepesi, wakati tashah-hudi ni kitendo kirefu, basi vipi wanukuu hili na waliache lile?!