006-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Kumkafini Maiti
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
Mlango Wa Janaazah
006-Kumkafini Maiti
· Hukmu Yake
'Ulamaa wote wanakubaliana kwamba kumkafini maiti kwa kinachomsitiri ni fardhi ya kutoshelezana. Kuna Hadiyth zenye kutaarifu hilo:
1- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba mtu mmoja aliyehirimia, ngamia wake alimwangusha akavunjika shingo na kufa, na sisi tuko pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli akasema: ((Mwosheni kwa maji na mkunazi, mkafinini ndani ya nguo mbili, msimtie manukato na wala msikifunike kichwa chake, kwani Allaah Atamfufua Siku ya Qiyaamah akiitikia talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1267) na Muslim (1206)]
2- Khabbaab bin Al-Arath anasema katika Hadiyth yake: “Tulihama pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Allaah, na malipo yetu yakawa juu ya Allaah. Kati yetu kuna aliyekufa hakula chochote katika malipo yake akiwemo Mus’ab bin ‘Umayr –na kuna mwingine tunda lake limeiva analichuma– aliuawa siku ya Uhud. Hatukupata cha kumkafinia isipokuwa burdah. Tukimsitiria kichwa, miguu yake inabakia wazi, na tukimsitiria miguu, kichwa kinabaki wazi. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuamuru tukisitiri kichwa chake na tuweke juu ya miguu yake majani ya mnanaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1276) na Muslim (940)].
3- Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdullah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikhutubu siku moja. Akamtaja mtu mmoja katika Maswahaba wake aliyekufa na kukafiniwa kwa sanda isiyomwenea, kisha akazikwa usiku. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakemea kuzikwa mtu usiku mpaka aswaliwe, isipokuwa kama itabidi watu wafanye hivyo. Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akimkafini mmoja wenu nduguye, basi amkafini vizuri)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (943), Abu Daawuud (3148) na An Nasaaiy (4/33). Muradi wa kumkafini vizuri ni sanda iwe safi, nzito na yenye kusitiri mwili wote. Haikusudiwi kufuja, kuvuka kiwango kinachotakiwa na kuwa na thamani ya juu sana. Yameelezwa na An-Nawawiy].
· Nani Anayegharamia Sanda?
Maulamaa wengi wanasema kwamba fedha za kugharamia sanda, kumwosha maiti na kuzika, hutolewa toka kwenye mali ya maiti mwenyewe.. Baadhi yao wamelitolea ushahidi hilo kwa Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf: “Kwamba siku moja aliletewa chakula chake akasema: Mus-‘ab bin ‘Umayr aliuliwa – naye alikuwa ni mbora kuliko mimi – hakikupatikana anachokimiliki cha kumkafinia isipokuwa burdah”. [Al-Ummu (1/236), Al-Majmu’u (5/188), Al-Muhalla (5/121) na Al-Ghuslu wal Kafan (uk 150)].
Wengi wamesema kwamba itaanzwa sanda, kisha deni halafu wasia, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuhusiana na mtu aliyeangushwa na ngamia wake akafa: ((Na mkafinini ndani ya nguo mbili)), na wala hakusaili kama ana deni au la. Hivyo Hadiyth inataarifu kwamba kinachotangulizwa ni sanda kabla ya deni, na wenye kumdai na warithi wake hawana haki ya kuzuia hilo. Na kama hana kitu, basi watatoa wale wenye kumkimu kimaisha, na kama hawako, basi itachukuliwa toka kwenye Baytul Maal. Kama hakuna, basi Waislamu watatoa na imamu atawachangisha wenye uwezo na wale anaoweza kuwasemesha.
Lakini wengine wamesema kwamba deni ndilo linalotangulizwa, kwa kuwa Allaah Hakujaalia mirathi wala wasia isipokuwa katika kile anachokibakisha mtu baada ya kutolewa deni lake. Na kama hana mali, itawalazimu Waislamu wamkafini. Ama kutolea dalili kwa huyo aliyeuawa na ngamia, hili linajibiwa kwa kusema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mdhamini wa kulipa madeni ya Waislamu kwa neno lake: (( Mimi nawastahikia zaidi Waumini kuliko nafsi zao. Basi mwenye kufa na deni na hakuacha cha kulipia, basi kulipa ni juu yetu sisi, na mwenye kuacha mali, basi ni za warithi wake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (6731) na wengineo].
Na hii ni kauli ya Abu Muhammad bin Hazm.
· Gharama Za Mke Wa Mtu
Baadhi ya Maulamaa wanasema kwamba gharama za kumkafini na za matayarisho mengineyo zitatolewa na mume wake. [Al-Majmu’u (5/188). Angalia kitabu changu cha Fiqh as Sunnah Lin Nisaai (uk. 189) chapa ya At-Tawfiyqiyyah].
Wengine wamesema kwamba bali hutolewa katika mali yake kama ameacha mali, na mume halazimiki, kwa kuwa mali za Waislamu ni marufuku kuzigusa ila kwa idhini toka kwenye Qur-aan au Hadiyth. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Hakika damu zenu na mali zenu ni haramu juu yenu)). [Hadiyth Swahiyh: Itakuja kwa urefu wake na takhriyj yake kwenye mlango wa Hijjah].
Kilicho wajibu juu ya mume kwa mkewe ni pesa za matumizi ya kila siku, nguo na nyumba. Na kwa lugha Aliyotusemesha nayo Allaah Mtukufu, sanda haiitwi nguo, wala kaburi nyumba. [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (5/122)].
Ninasema: “Kauli hii ndiyo yenye nguvu. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.
Faida: Inajuzu Mtu Kutayarisha Sanda Yake Kabla Ya Kufa
Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’ad: “Kwamba mwanamke mmoja alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na burdah iliyofumwa ikiwa na kitambaa chake cha pembeni na akasema: Nimeisuka kwa mkono wangu na nimekuja ili nikuvike. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaichukua hali ya kuwa anaihitajia. Halafu akatutokea akiwa amejifunga kwa chini, na mtu mmoja akaisifia akisema: Nivishe mimi, ni nzuri mno. Watu wakamwambia: Umefanya vibaya. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kaivaa kwa kuihitajia, na wewe unamwomba na huku unajua kwamba yeye hamkatalii mtu?! Akasema: Mimi wal-Laahi sikumwomba ili niivae, bali nimemwomba ili iwe ni sanda yangu”. Sahl akasema: “Na ikawa ni sanda yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1277) na Ibn Maajah (3555)].
· Sifa Ya Sanda:
(a) Sanda ya mwanaume
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikafiniwa kwa nguo tatu nyeupe za Kiyemen toka kijiji cha Sahuol zilizotengenezwa kwa pamba. Hakuna kati yake kanzu wala kilemba”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1264) na Muslim (941)].
Tunajifunza kutokana na Hadiyth hii na nyinginezo kwamba yaliyosuniwa katika sanda ni haya yafuatayo:
1- Iwe nyeupe
Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Vaeni nyeupe katika nguo zenu, kwani hizo ndizo bora ya nguo zenu, na wakafinini kwazo maiti wenu)). [Hadiyth Swahiyh Lighayrihi: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3878), At-Tirmidhiy (994), Ibn Maajah (1472) na wengineo].
2- Mwanamume akafiniwe kwa nguo tatu.
3- Sanda iwe ya pamba.
4- Isiwepo kanzu wala kilemba.
Hakuna ubaya akikafiniwa kwa kanzu ingawa kuacha ni bora zaidi. Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar kwamba alipofariki ‘Abdullah bin Ubayya, mwanawe alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Nipe kanzu yako nimkafinie, mwombee na mtakie maghfirah. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akampa kanzu yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1269) na Muslim (2774)].
Ash-Shaafi’iy kasema katika Al-Ummu (1/236): “ Kama atakafiniwa kwenye kanzu, kanzu itakuwa chini ya nguo, na nguo juu ya kanzu”.
5- Iwe nguo moja kati ya nguo hizo ya mistari au ya rangi.
Imepokelewa toka kwa Jaabir ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akifa mmoja wenu na akapata chochote, basi akafiniwe kwenye nguo ya mistari)) [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3150) na Al-Bayhaqiy (3/403). Ibn Ma’iyn kaitia doa kwa aliyojibishiwa. Iko Hadiyth mwenza kwa Ahmad (3/335), na Ibn Abiy Shaybah (3/266) kwa njia nyingine mbili na kuiweka Hadiyth katika hali ya uSwahiyh. Iko kwenye Swahiyh Al-Jaami’i (455)].
6- Sanda itiwe manukato
Imepokelewa toka kwa Jaabir akisema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Mkimfukiza maiti, basi mfukizeni mara tatu)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/331), Ibn Abiy Shaybah (3/265), Al-Haakim (1/355) na Al-Bayhaqiy (3/405)].
Hili wamelipendelea Maulamaa wengi. Wamesema: “Na kwa vile hii ni ada ya aliye hai ya kujifukiza kwa manukato baada ya kuoga na kubadili nguo, ni hivyo hivyo kwa maiti”. [Al-Mughniy (2/464). Angalia Al-Majmu’u (5/197)].
· Kama Nguo Haikutosha Kusitiri Mwili Wote
Tushaeleza katika Hadiyth ya Khabbaab ikisema : Mus’ab bin ‘Umayr aliuawa siku ya Uhud. Hatukupata cha kumkafinia isipokuwa burdah. Tukimsitiria kichwa, miguu yake inabaki wazi, na tukimsitiria miguu, kichwa kinabaki wazi. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuamuru tukisitiri kichwa chake na tuweke juu ya miguu yake majani ya mnanaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1276). Tushaieleza nyuma].
Hadiyth hii inatufunza kwamba kama hakikupatikana kabisa cha kumsitiri, basi atasitiriwa mwili wote kwa majani ya mnanaa. Kama hayakupatikana, atasitiriwa kwa majani yaliyopo. [Fat-hul Baariy (3/142)].
· Aliyehirimia Hukafiniwa Kwa Nguo Zake Za Ihraam, Na Kichwa Hakifunikwi
Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyotangulia nyuma. Anasema: “Wakati mtu mmoja akiwa amesimama pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Arafah, ghafla alianguka toka juu ya ngamia wake akavunjika shingo na kufa. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mwosheni kwa maji na mkunazi, na mkafinini ndani ya nguo mbili, - au alisema: Ndani ya nguo zake mbili - na wala msikifunike kichwa chake, kwani Allaah Atamfufua Siku ya Qiyaamah akiitikia talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1849). Ishaelezwa nyuma].
· Shahidi (Wa Jihaad) Hukafiniwa Kwa Nguo Yake Aliyouawa Nayo Au Nguo Nyingine
Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Tha’alabah bin Swafiyr kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema siku ya Uhud: ((Wafunikeni kwenye nguo zao)). [Hasan kwa Sanad zake tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” kwa tamshi hili na Ahmad (5/431) kwa Sanad Layyin. Baadhi ya Maulamaa wamesema ni Dhwa’iyf kwa kuwa inakwendana kinyume na riwaya zake nyinginezo (5/431), na An-Nasaaiy (4/78-6/28) kwa tamshi la: “Wafunikeni na majeraha yao na damu zao”. Ninasema: “Hakuna kuendana kinyume, kwa kuwa matokeo ya matamshi mawili ni mamoja kama inavyoonekana. Isitoshe, Hadiyth hii ina mwenza ya Jaabir kwa Abu Daawuud (3133), na nyingine toka kwa Ibn ‘Abbaas (3134), Ibn Maajah (1515) na wengineo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”].
Maulamaa wamekubaliana kwamba inapendeza kuwakafini Mashahidi kwa nguo zao zile zile walizouawa nazo. Na wengi wao wamesema: “Watavuliwa nguo zao endapo kama si desturi ya watu kuzivaa kama ngozi, manyoa na chuma”. [Al-Mughniy (2/531)].
Kati ya yanayotaarifu kwamba inapendeza kuwakafini Mashahidi kwa nguo walizofia nazo lakini si wajibu wa lazima, ni Hadiyth ya Az-Zubayr asemaye kwamba Swafiyyah alipeleka nguo mbili kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) za kumkafinia Hamzah (Radhwiya Allaahu Anhu). Moja akamkafinia Hamza, na nyingine akamkafinia M-answaar ambaye hakuwa na sanda. [Hadiyth Swahiyh kwa Sanad zake tofauti: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/165), Al-Bayhaqiy (3/401) na wengineo].
Hadiyth inataarifu kwamba msimamizi ana khiyari. Pia Hadiyth iliyotangulia ya kukafiniwa Musw’ab bin ‘Umayr aliyeuawa katika vita vya Uhud.
(b) Sanda Ya Mwanamke
Sanda ya mwanamke ni sawa na sanda ya mwanamume isipokuwa linalopendelewa zaidi iwe ni nguo tano kwa mujibu wa kauli ya Maulamaa wengi. Hadiyth yenye Isnadi Dhwa’iyf imesimuliwa kuhusiana na hili isemayo kwamba Laylaa binti Qaaif Ath-Thaqafiyyah amesema: “Nilikuwa miongoni mwa waliomwosha Ummu Kulthum binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki. Cha kwanza alichotupa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni nguo ya chini (izari), kisha kanzu, halafu mtandio, halafu shuka kisha akaingizwa kwenye nguo ya mwisho. Akasema: “ Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekaa kwenye mlango akiwa na sanda yake na kuwapa nguo moja baada ya nyingine”. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3157) kwa Sanad Dhwa’iyf].
Ibn Al-Mundhir kasema: “Wengi katika Maulamaa tunaowajua vyema wanasema kwamba mwanamke hukafiniwa kwa nguo tano, na hilo linapendeza kwa kuwa mwanamke katika uhai wake hujisitiri zaidi ya anavyojisitiri mwanaume kutokana na uchi wake kuuzidi uchi wa mwanaume. Na hali ni hivyo hivyo baada ya kufa”. [Al-Mughniy (2/470). Angalia Al-Majmu’u (5/205)].
· Kukafiniwa Mwanamke Kwa Hariri
Inajuzu, kwa vile anaruhusiwa kuivaa wakati wa maisha yake. Lakini ni makruhu kumkafinia kwa kuwa ni israfu inayofanana na ufujaji mali kinyume na anapoivaa wakati yu hai, kwani hujipambia nayo kwa ajili ya mumewe. [Al-Majmu’u (5/197) cha An-Nawawiy].