007-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Kubeba Jeneza Na Kulisindikiza

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

007-Kubeba Jeneza Na Kulisindikiza

 

Alhidaaya.com

 

 

Kubeba jeneza na kulisindikiza ni kati ya haki za maiti juu ya Waislamu. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Haki za Muislamu juu ya Muislamu ni tano: Kujibu maamkizi, kumzuru mgonjwa, kwenda kuzika, kuitikia wito, na kumtakia rahma aliyekwenda chafya)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1240) na Muslim (2162)].

 

Na imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtembeleeni mgonjwa, na sindikizeni jeneza, litawakumbusheni aakhirah)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (3/27), Al-Bukhaariy katika Al-Adab Al-Mufrad (518), Ibn Abiy Shaybah (4/73) na wengineo].

 

Maulamaa wamekubaliana kwamba kwenda kuzika ni Fardhi ya Kutoshelezana, wakifanya baadhi, basi wengine waliobaki huwapomokea. Na wengi wao wanasema kwamba kuisindikiza na kuzika ni Sunnah. [Ibn ‘Aabidiyn (1/624), Al-Fataawaa Al-Hin-diyyah (1/159), Al-Fat-hu (3/112) na Sharhu Muslim (1/188)].

 

Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Al-Barraa bin ‘Aazib aliyesema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamuru tusindikize jeneza”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1239) na Muslim (2066)]. Wanasema kwamba agizo hili ni la Sunnah na si la wajibu, kwa Ijma’a!!

 

Ninasema: “Ikiwa Ijma’a imethibiti, basi imethibiti, na kama haikuthibiti basi hakuna tofauti kati ya hukmu ya kubeba na kuzika, na linaloonekana ni kuwa yote mawili ni Fardhi ya Kutoshelezana. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

· Jeneza Hubebwa Mabegani Mwa Wanaume

 

Sunnah ni kubebwa jeneza juu ya mabega ya wanaume. Imepokelewa na Abu Sa’iyd Al-Khudriy kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Linapowekwa jeneza, na wanaume wakalibeba juu ya mabega yao, ikiwa ni la mtu mwema husema: Niwahisheni, na kama si la mtu mwema husema: Eh ole wake! Mnakwenda nalo wapi?! Kila kitu huisikia sauti yake isipokuwa mwanadamu, na lau angeisikia angekufa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1314), An-Nasaaiy (1/270) na Ahmad (3/41)].

 

Hadiyth hii inatutaarifu kwamba si sharia kwa wanawake kubeba jeneza ni sawa maiti akiwa mwanaume au mwanamke. Hakuna makhitalifiano kabisa katika hili. Kwa kuwa wanawake wanahemewa katika kubeba, na pia kinaweza kuonekana chochote cha miili yao wakati wa kubeba.  Zaidi ya haya, wanaweza kulia kwa kelele wakati wa kulibeba na kulitua. Isitoshe, wangeruhusiwa kulibeba, ingelipatikana njia ya kuchanganyika wao na wanaume na kuzua fitna. Hivyo imekuwa ni lazima kwa wanaume tu. [Al-Majmu’u (5/270), Al Fat-hu (3/217) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa (1/535)].

 

· Kuiharakisha Jeneza

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Iharakisheni jeneza. Ikiwa ni njema, basi ni kheri mnayoitanguliza kwake. Na kama si hivyo, basi ni shari mnayoitua toka shingoni mwenu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1315) na Muslim (944)].

 

Muradi wa kuiharakisha ni kuzidisha zaidi ya mwendo wa kawaida, lakini si kwa kasi inayoweza kuleta madhara kwa maiti, au uzito kwa mbebaji au msindikizaji.

 

Angalizo:

 

Si Sharia Kubeba Jeneza Kwa Gari Bali Inatosha Kulibeba Mabegani Kwa Haya Yafuatayo: [Angalia: Ahkaamul Janaaiz cha Al-Imaam Al-Albaaniy – Allaah Amrehemu- (uk. 99) chapa ya Al-Ma’aarif].

 

1- Hili ni katika ada za makafiri, nasi tumeamuriwa kwenda nao kinyume.

 

2- Ni bid-’a katika ‘ibaadah sambamba na kukinzana kwake na Sunnah ya kivitendo katika kubeba jeneza.

 

3- Kunapoteza lengo la kuibeba na kuisindikiza, nalo ni kukumbuka aakhirah.

 

4- Ni sababu ya kupungua idadi ya wasindikizaji na hususan wasindikizaji hao wakiwa kwenye magari yao.

 

5- Picha hii haiendani na yaliyo maarufu kuhusu sharia twaharifu samehevu ya kujiweka mbali na urasmi na mwonekano, na hususan kwenye mfano wa jambo hili hatari; mauti.

 

Ninasema: “Mafuqahaa wameeleza kwamba ni makruhu kubeba jeneza juu ya mgongo wa mnyama bila udhuru. Ama ikiwa ni kwa udhuru kama makaburi kuwa mbali na ikawa uzito kwa watu kulibeba, basi inajuzu. [Ibn ‘Aabidiyn (1/623) na Al-Majmu’u (5/270)].

 

Na ninasema: “ Inatakikana wakati huo wasimamishe magari na walibebe jeneza wanapofika umbali mwafaka kwa ajili ya kuipata Sunnah na kusudio lake”.

 

· Kusindikiza Jeneza Kuna Ngazi Mbili

 

1- Kulisindikiza toka linapotolewa nyumbani kwa watu wa maiti mpaka atakaposwaliwa.

 

2- Kulisindikiza toka linapotolewa kwa jamaa wa maiti mpaka atakapozikwa. Yote haya mawili Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameyafanya. [Angalia Ahkaamul Janaaiz (uk. 87-88)].

 

Na bila shaka, ngazi ya pili ni bora zaidi. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kulifuata jeneza [toka nyumbani kwake] mpaka likaswaliwa, basi ana qiyraatw, na mwenye kulifuata mpaka maiti akazikwa, basi ana qiyraatw mbili [za thawabu]. Ikasemwa: Ee Rasuli wa Allaah! Ni nini qiyraatw mbili? Akasema: ((Ni mfano wa milima miwili mikubwa)). Na katika riwaya nyingine: ((Kila qiyraatw ni mfano wa Uhud)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1325) na Muslim (945)].

 

· Ni Marufuku Wanawake Kusindikiza Jeneza

 

Fadhla hiyo iliyotajwa ya kusindikiza jeneza ni kwa wanaume tu na si kwa wanawake, kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza kufanya hivyo. Ummu ‘Atwiyyah amesema: “Tulikatazwa kusindikiza jeneza, lakini hatukukaziwa sana”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1278) na Muslin (938)].

 

Jamhuri ya Maulamaa wamelichukulia katazo hili juu ya ukaraha na si uharamu. [Al-Majmu’u (5/277), Fat-hul Baariy (2/599) na Ibn ‘Aabidiyn (1/208)] Ni kutokana na neno lake: “Hatukukaziwa sana”.

 

Lakini, Sheikh wa Uislamu katika Al-Fataawaa (24/355) amesema: “Huenda muradi wake ni kuwa katazo halijasisitizwa kwa uzito, na hii haikanushi uharamishaji. Huenda yeye amedhani kwamba si katazo la uharamishaji, lakini nguvu ya hoja inabakia ndani ya kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na si kwenye dhana ya  mtu”.

 

· Ni Upande Gani Wa Jeneza Wasindikizaji Wanakuwa?

 

Inafaa kwenda nyuma au mbele ya jeneza, kuliani au kushotoni karibu nalo. Anas (Radhwiya Allaahu Anhu) anasema: “ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr na ‘Umar, walikuwa wakitembea mbele ya jeneza na nyuma yake”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1483), At-Twahaawiy (1/278), nayo iko kwa Abu Daawuud (3179), At-Tirmidhiy (1007) na An-Nasaaiy (4/56) bila ya (nyuma yake). Angalia Al-Irwaa (739)].

 

Lakini bora ni kutembea nyuma yake kwa mujibu wa Hadiyth zenye kuamuru kusindikiza jeneza. Linatiliwa nguvu na kauli ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu Anhu) isemayo: “ Kutembea nyuma yake ni bora kuliko kutembea mbele yake, ni kama fadhla ya Swalaah ya mtu kwa Jamaa na kuswali peke yake”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah, (4/101), Ahmad (1/97) na Al-Bayhaqiy (4/25). Al-Haafidh kasema ni Hasan, na ina hukmu ya Umarfu’u]. 

 

Na hii ni kauli ya ya Al-Awzaa’iy, Abu Haniyfah na Is-Haaq kinyume na Jamhuri. [Al-Ummu (1/240), Bidaayatul Mujtahid (1/344), na Fat-hul Baariy (3/219)].

 

Inajuzu kwa wasindikizaji kupanda lakini wawe nyuma ya jeneza kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kupanda atembee nyuma ya jeneza, na mwenye kutembea popote atakapo pa jeneza)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3180), At-Tirmidhiy (1031), An-Nasaaiy (1/275) na Ahmad (4/247)].

 

Ingawa kupanda kunajuzu, lakini kutembea ni bora zaidi kwa kuwa hilo limezoeleka kufanywa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Thawbaan (Radhwiya Allaahu Anhu) anasimulia: “Kwamba Rasuli wa Allaah aliletewa mnyama – akiwa na jeneza – akakataa kumpanda. Alipomaliza, aliletewa mnyama akampanda, akaulizwa akasema: (( Hakika Malaika walikuwa wanatembea, na haikunifalia kupanda na wao wanatembea. Walipoondoka, nilipanda)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3177), Al-Haakim (1/355) na Al-Bayhaqiy (4/23). Angalia Ahkaamul Janaaiz (uk. 97)].

 

· Adabu Za Kusindikiza Jeneza

 

1- Kutolisindikiza kwa chetezo au moto

 

Mafuqahaa wamekubaliana kwamba jeneza halisindikizwi kwa moto wa mwenge (chetezo) wala mshumaa au mfano wa hivyo ila kama vitahitajika kwa ajili ya mwanga. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: ((Jeneza halisindikizwi kwa sauti wala moto)). [Al-Albaaniy kaipa nguvu kwa Hadiyth wenza: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3171) na Ahmad (2/427). Angalia Ahkaamul Janaaiz (uk. 91)].

 

Sanad yake ina walakin isipokuwa inapata nguvu kwa aliyoyasema ‘Amri bin Al-‘Aaswiy katika wasia wake: “Nikifa, asinisindikize mwanamke mwombolezaji wala moto”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (121) na Ahmad (4/199)].

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba alisema mauti yalipomwadilia: “Msinijengee hema, wala msinisindikize kwa mwenge (na katika riwaya nyingine: Kwa moto)”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/292)].

 

Na imepokelewa toka kwa Abu Muusa kwamba aliusiua wakati mauti yalipomwadilia akisema: “ Mkiondoka na jeneza langu, basi nikazieni mwendo, na wala msinisindikize kwa kijinga cha moto”. [Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1487), Ahmad (4/397) na Al-Bayhaqiy (3/395)].

 

2- Kulisindikiza kimya kimya

 

Haijuzu kulisindikiza jeneza kwa sauti, si kwa dhikri wala kwa jingine lolote. Imepokelewa toka kwa Qays bin ‘Ubbaad akisema: “Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wanachukia sauti kunyanyuliwa kwenye majeneza”. [Wapokezi wake wanaaminika: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (4/74) na Ibn Mubaarak katika Az-Zuhd (83)].

 

Kunyanyua sauti ni kujishabihishana Manaswara. Wao hunyanyua sauti kw kusoma sehemu ya Biblia yao na nyiradi zao kwa kuvuta sauti, kwa mahadhi na kwa mdundo wa kugusa huzuni.

 

An-Nawawiy kasema kwenye Al-dhkaar (uk. 203): “Jua kwamba sahihi ni lililokhitariwa, na ukimya waliokuwa wakiufanya Masalaf (Radhwiya Allaahu Anhum) wakati walipokuwa wakilipeleka jeneza. Sauti hainyanyuliwi kwa kisomo, wala dhikri wala kwa jingine lolote lile. Na hikma ya hilo iko wazi, nayo ni kuwa ukimya hutuliza mawazo ya mtu, na huijumuisha akili yake kufikiria kuhusu mauti. Na hili ndilo linalotakikana katika hali hii, na hii ndio haki. Basi usidanganyike na wengi wenye kwenda kinyume na hili”.

 

Ninasema: “Ama waliyoyazoea watu ya kuleta dhikr mbele ya jeneza katika zama zetu za leo, au mmoja wao kusema: “Wahhiduuh” (Mpwekesheni!) na wasindikizaji kumwitikia, au kusema: “Mshuhudilieni!!”, hayo ni bid-’a kama walivyoeleza Mafuqahaa. [Ibn ‘Aabidiyn (1/608), Ash-Sharhu As-Swaghiyr (1/229), na Mughnil Muhtaaj (1/247)].

 

Al-Albaaniy kasema: [Ahkaamul Janaaiz (uk. 92) chapa ya Al-Ma’aarif (1412H = 1992)]  “Baya zaidi ya hilo, ni kusindikiza jeneza kwa kupiga ala za muziki mbele yake kwa mahadhi ya mguso wa huzuni kama inavyofanywa katika baadhi ya nchi za Kiislamu kwa kuwaiga makafiri. Allaahul-Musta’anu”.

 

3- Wasindikizaji wasiketi kabla ya jeneza kuwekwa chini

 

Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mkiliona jeneza basi simameni, na mwenye kulisindikiza asikae mpaka liwekwe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1310) na Muslim (959)].

 

Muradi ni mpaka walitue toka mabegani kuliweka chini, na wengine wanasema mpaka maiti atiwe kwenye mwanandani.

 

Maswahaba wengi pamoja na Taabi’iyna wamesema ni vizuri zaidi watu wasimame mpaka jeneza iwekwe chini kama alivyonukuu Ibn Al-Mundhir. Ni kauli ya Al-Awzaa’iy, Ahmad, Is-Haaq na Muhammad bin Al-Hasan. Imekhitariwa na Ash-Shaafi’iy. [Fat-hul Baariy (3/213), Al-Majmu’u (5/280) na Al I-’itibaar cha Al-Haazimiy (uk. 138)].

 

4- Je, mtu asimame jeneza likipita?

 

[Fat-hul Baariy (3/216), Al-Majmu’u (5/280), Al I-‘itibaar (uk. 138), Al-Fataawaa Al-Hin-diyyah (1/160) na Al-Muhalla (5/…)].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Aamir bin Rabiy-’ah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mkiliona jeneza basi simameni mpaka liwapite [au liwekwe chini] )). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1307) na Muslim (958)].

 

Na Jaabir bin ‘Abdullah amesema: “ Lilitupitia jeneza, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akalisimamia, nasi pia tukalisimamia. Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ni jeneza la Myahudi. Akasema: ((Mkiliona jeneza, basi simameni)).  [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1311) na Muslim (960)].

 

Na katika tamshi toka kwa Sahl bin Haniyf na Qays bin Sa’ad: ((Je, si nafsi?)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1312) na Muslim (961)].

 

Lakini, Maulamaa wengi wakiwemo Maimamu wanne na wengineo, wanasema kwamba kulisimamia jeneza kumenasikhiwa na Hadiyth ya ‘Aliy bin Abiy Twaalib aliyesema: “Rasuli wa Allaah alilisimamia jeneza nasi tukasimama, kisha akakaa nasi tukakaa”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (962), Ibn Maajah (1544) na Ahmad (1/13)].

 

Na katika tamshi jingine: “Kisha alikaa baada ya hapo, na akatuamuru tukae”. [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (1/82) na At-Twahaawiy (1/282). Angalia Ahkaamul Janaaiz (uk. 101)].

 

Ibn Hazm, Ibn Habiyb na Ibn Al-Maajithuna katika wafuasi wa Maalik na baadhi ya wafuasi wa Ash-Shaafi’iy ikiwa pia ni chaguo la An-Nawawiy, wanasema kwamba kukaa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kuamuru kusimama, ni kubainisha kujuzu, na kwamba amri ilikuwa ni ya Sunnah, na naskh haifanyi kazi hapa isipokuwa ikishindikana kukusanya, na hapa inawezekana.

 

 

Share