008-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Swalaah Ya Janaazah

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

008-Swalaah Ya Janaazah

 

Alhidaaya.com

 

 

· Hukmu Yake:

 

Kumswalia maiti ni Fardhi ya Kutoshelezana (wakiifanya baadhi ya Waislamu, itawapomokea wengine), Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameliamuru hilo. Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiletewa mtu aliyefariki mwenye deni naye anauliza: ((Je, ameacha ziada kwa deni lake?)) Akiambiwa kwamba ameacha cha kulipia humswalia, na kama hakuacha, huwaambia Waislamu: ((Mswalieni mwenzenu)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1251) na An-Nasaaiy (1960)].

 

Imepokelewa toka kwa Zayd bin Khalid Al-Juhaniy: "Kwamba mtu mmoja katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifariki Siku ya Khaybar, wakaitaja habari ya kifo kwa Rasuli, naye akasema: ((Mswalieni mwenzenu)). Nyuso za watu zikabadilika kwa kauli hiyo. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika mwenzenu amedokoa katika mali ya Allaah)). Tukapekua mzigo wake, tukakuta sindano katika sindano za Mayahudi za kushonea ngozi haifiki dirhamu mbili. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Maalik katika Al-Muwattwaa (2/14), Abu Daawuud (2710), An-Nasaaiy (4/64), Ibn Maajah (2848) na Ahmad (4/114, 5/192). Angalia Al-Irwaa (726)].

 

· Fadhla Yake:

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuhudhuria Swalaah mpaka janazah ikaswaliwa, basi huyo ana qiyraatw. Na mwenye kuihudhuria mpaka akazikwa, basi ana qiyraatw mbili)). Akaulizwa: "Ni nini qiyraatw mbili?" Akasema: (( Ni mfano wa milima miwili mikubwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (945)].

 

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin ‘Abbaas: “Kwamba mwanawe alifariki huko Qudayd – au ‘Asafaan – akasema: Ee Kurayb! Angalia watu waliomkusanyikia. Nikatoka, na nikawakuta watu wamekusanyika kwa ajili yake nikamweleza. Akasema: Unasema wao ni arobaini? Nikasema: Na’am. Akasema: Basi mtoeni, kwani mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakuna mtu yeyote Muislamu anayekufa, wakasimama watu arobaini wasiomshirikisha Allaah na chochote kumswalia, isipokuwa Allaah Huwakubalia shufaa yao kwake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (948)].

 

Na imepokelewa toka kwa ‘Aaishah toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakuna maiti yeyote anayeswaliwa na Umma wa Waislamu wanaofikia mia moja wote wanamtakia shufaa, isipokuwa hukubaliwa shufaa yao kwake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (947)].

 

· Wapi Asimame Imamu Kulielekea Jeneza

 

Kauli ya kwanza: 

 

Asimame imamu mkabala wa kichwa cha mwanamume, na mkabala wa kiuno cha mwanamke. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Is-Haaq. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/225)].

 

Baadhi ya Mahanafi wameikhitari kauli hii. [Al-Hidaaya (1/462), na Sharhul Ma’aaniy (1/284)].

 

Ash-shawkaaniy kasema ni haki.

 

Wametoa dalili kwa Hadiyth ya Anas bin Maalik: "Ya kwamba Abu Ghaalib Al-Khayyaat alisema: Nilimshuhudia Anas bin Maalik akiliswalia jeneza la mtu. Akasimama mkabala wa kichwa chake (katika riwaya nyingine: [Kichwa cha As Surayr]. Lilipoondoshwa, lililetwa jeneza la mwanamke wa Kikureshi – au wa Kianswaar - akaambiwa: Ee Abu Hamzah! Hili ni jeneza la fulanah binti fulanah, basi mswalie. Akamswalia na akasimama mkabala wa kiuno chake. [Na katika riwaya nyingine: Kwenye bamba lake, na amefunikwa jeneza la kijani]. Alikuwa pamoja nasi Al-'Alaa bin Ziyaad Al-'adawiy. Alipoona kutofautiana sehemu aliposimama Anas kwa mwanamke na mwanamume alisema: Ee Abu Hamzah! Je, ndivyo hivi alikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasimama hapo uliposimama, na kwa mwanamke uliposimama? Akasema: Na’am. Al-'Alaa akatugeukia akasema: Hifadhini”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3194) na At-Tirmidhiy (1034). Waliosema ni Hasan ni Ibn Maajah (1494), Ahmad (3/118, 204), Al-Bayhaqiy (4/33) na At-Twayaalsiy (2149). Angalia Ahkaamul Janaaiz cha Al-Albaaniy (uk. 138)].

 

Pia kuna Hadiyth ya Samrah bin Jun-dub aliyesema: "Niliswali nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamswalia Ummu Ka'ab ambaye alikufa akiwa na nifasi, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama kiunoni mwake kumswalia". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1332) na Muslim (964) na tamko ni lake].

 

Ya pili:

 

Asimame mkabala wa kifua cha maiti sawasawa akiwa mwanamume au mwanamke. Wameijibu Hadiyth ya Anas iliyotangulia wakisema kwamba sababu ya wao kusimama mkabala wa kiuno cha mwanamke ni sitara kwa kuwa hakukuweko majeneza. Wametolea ushahidi hilo kwa ziada aliyoisimulia Abu Daawuud katika Hadiyth ya Anas. Ziada inasema: " Abu Ghaalib akasema: Nikauliza kuhusu kitendo cha Anas cha kusimama mkabala wa kiuno cha mwanamke. Wakanieleza kwamba sababu ni kutokuweko majeneza, imamu alikuwa anasimama mkabala wa kiuno chake ili kumsitiri na wanaume". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3194)].

 

Sheikh Al-Albaaniy ameijibu kauli ya Mahanafi akisema kwamba sababu waliyoitoa inakataliwa kwa hoja zifuatazo:

 

Kwanza: Aliyeleta sababu hiyo hajulikani, na linalokuwa hivyo halina thamani.

 

Pili: Inapingana na aliyoyafanya msimulizi mwenyewe wa Hadiyth ambaye ni Anas (Radhwiya Allaahu Anhu). Yeye alisimama mkabala wa kiuno na maiti yuko ndani ya jeneza, na hili linaonyesha kwamba sababu hiyo ni batili. [Angalia Ahkaamul Janaaiz Wabidaaihaa cha Al-Albaaniy ukurasa wa 139 kwenye footnote].

 

Ibn Hazm kasema kwenye Al-Muhalla: "Maiti huswaliwa na imamu anayesimama na kuelekea Qiblah, na nyuma yake watu katika safu. Kwa mwanamume anasimama kwenye kichwa chake, na kwa mwanamke kwenye kiuno". [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (5/123)].

 

· Imesuniwa Wapange Safu Tatu Nyuma Ya Imamu Hata Kama Watu Ni Kidogo

 

Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): (( Hakuna maiti yeyote anayekufa na akaswaliwa na safu tatu za Waislamu, isipokuwa [Allah] Huwajibisha [Pepo]). [Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3150), At-Tirmidhiy (1033), na Ibn Maajah (1490)].

 

Na kila watu wanavyozidi, ndivyo inavyokuwa faida zaidi kwa maiti kwa neno lake Rasuli: ((Hakuna maiti yeyote anayeswaliwa na Umma wa Waislamu wanaofikia mia moja wote wanamtakia shufaa, isipokuwa hukubaliwa shufaa yao kwake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (947), At-Tirmidhiy (1034), na An-Nasaaiy (4/75)].

 

· Maiti Za Wanaume Na Wanawake Zikikusanyika Wakati Mmoja

 

Ikikusanyika maiti zaidi ya moja kati ya wanaume na wanawake, imamu anaweza kuiswalia kila maiti peke yake, na pia inajuzu kuwaswalia wote kwa Swalaah moja. Majeneza yatapangwa moja baada ya jingine ili maiti wote wawe mbele ya imamu. Maiti za wanaume zitawekwa mbele yake, na za wanawake zitafuatia upande wa Qiblah. 

 

Imepokelewa toka kwa Naafi'i ya kwamba Ibn 'Umar aliswalia majeneza tisa kwa pamoja. Akazipanga maiti za wanaume mbele ya imamu na za wanawake safu moja upande wa Qiblah. Majeneza ya Ummu Kulthum bint 'Aliy mke wa 'Umar bin Al-Khattwaab na mwanawe aitwaye Zayd yaliwekwa pamoja, na imamu siku hiyo alikuwa ni Sa'iyd bin Al-'Aaswiy, na watu wengine ni pamoja na Ibn 'Umar, Abu Hurayrah, Abu Sa'iyd, na Abu Qataadah. Maiti ya Zayd ikawekwa mbele ya imamu na mtu mmoja akasema: Nikalipinga hilo. Nikamwangalia Ibn 'Abbaas, Abu Hurayrah, Abu Sa'iyd na Abu Qataadah nikawauliza: "Nini hii?". Wakaniambia: "Ni Sunnah". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (4/71), Ad-daaraqutwniy (2/79), Al-Bayhaqiy (4/33) na ‘Abdul Razzaaq (6337)].

 

· Inajuzu Wanawake Kuswalia Maiti

 

Inajuzu wanawake kumswalia maiti ikiwa hawataifuata kule iliko, bali ikasadifiana kuwepo kwao pale anaposwaliwa maiti. Imepokelewa toka kwa ‘Abdullah bin Az Zubayr: "Kwamba 'Aaishah aliamuru jeneza la Sa'ad bin Abi Waqqaas lipitishwe Msikitini ili apate kumswalia. Watu wakampinga hilo, naye akasema: Watu wanasahau haraka hivyo! Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumswalia Suhayl bin Al-Baydhwaa isipokuwa Msikitini". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (973), Abu Daawuud (3173) na An-Nasaaiy (4/68)].

 

· Faida

 

Hadiyth hii inatueleza kwamba inajuzu kumswalia maiti ndani ya Msikiti, lakini lililo bora zaidi ni kumswalia nje ya Msikiti kwenye sehemu maalumu iliyoandaliwa kwa hilo. Hii ilikuwa ndio hadyi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alikuwa akifanya hivyo mara nyingi. [Al-Wajiyz (uk. 174)].

 

· Je, Baadhi Ya Viungo Vya Maiti Huswaliwa?

 

Kuna athar zilizosimuliwa ambazo ziko kati ya udhwa’iyf na irsaal toka kwa baadhi ya Maswahaba ya kwamba waliviswalia baadhi ya viungo vya maiti.

 

Khalid bin Mu'udaan anasema kwamba Abu 'Ubaydah aliviswalia vichwa huko Sham. [Mursal: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (4013) na Al-Bayhaqiy (4/18)].

 

Inasimuliwa toka kwa Abu Ayyuub kwamba aliuswalia mguu. [Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/40)].

 

Inasimuliwa kuwa 'Umar aliiswalia mifupa huko Sham. [Mursal: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abiy Shaybah (3/41)].

 

Kuna jumla ya kauli tatu zilizosemwa na Maulamaa katika mas-ala haya:

 

Ya kwanza: Huswaliwa, sawasawa vikiwa ni kidogo au vingi. Ni kauli ya Ash-Shaafi'iy na Ahmad. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/214)]. Ibn Hazm kasema hivyo hivyo. [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (5/214)].

 

Ya pili: Ikiwa itapatikana zaidi ya nusu ya mwili wake, basi itaoshwa na kuswaliwa. Na kama itapatikana nusu tu, basi haioshwi wala kuswaliwa. Ni kauli ya Abu Haniyfah.

Kauli ya Maalik iko karibu na hii. Anasema kwamba viungo vichache haviswaliwi. [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/214)].

 

Ya tatu: Haviswaliwi kwa hali yoyote ile. Ni kauli ya Daawuud.  [Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/214)].

 

Ninasema: " Naona nafsi yangu inanivuta kuniambia kuwa ikiwa hakuswaliwa, basi vitaoshwa, vitaswaliwa na vitazikwa. Na ikiwa maiti aliswaliwa kisha baadhi ya viungo vyake vikapatikana, basi havitaswaliwa, bali vitaoshwa na kuzikwa. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi".

 

· Kiungo Cha Aliye Hai Hakiswaliwi

 

Haikunukuliwa toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Maswahaba kwamba walikiswalia kiungo kilichokatika cha mtu hai. Kuna habari nyingi za uhakika kutoka kizazi hadi kizazi zinazoeleza kwamba adhabu zilitekelezwa wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba baada yake, na mikono ilikatwa. Haikuelezwa kwamba waliosha au kuswalia kiungo chochote katika hivyo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Kumswalia Mtoto Wa Mimba Iliyoharibika Na Mtoto Mdogo

 

Kwanza: Mtoto

 

Tunamaanisha ambaye bado kubaleghe, huyu ni sharia kumswalia. Imepokelewa toka kwa 'Aaishah akisema: " Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliletewa mtoto mdogo katika watoto wa wakazi wa Madiynah akamswalia. Nikasema: Pepo imthibitikie huyu. Ndege katika ndege wa Peponi, hakufanya baya na wala hakubaleghe. Akasema: ((Au lipo jingine ya hilo ee ‘Aaishah? Allaah 'Azza wa Jalla Ameumba Pepo, na Akaiumbia watu wake, na Akawaumba kwenye migongo ya baba zao, na Akaumba moto, na Akauumbia watu wake, na Akawaumba kwenye migongo ya baba zao)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2662), An-Nasaaiy (1/76) na tamko ni lake, na Ahmad (6/208)].

 

Pili: Mtoto wa mimba iliyoharibika

 

Hakuna makhitalifiano kati ya Maulamaa kwamba mtoto wa mimba iliyoharibika akilia wakati anazaliwa au akapiga chafya, huswaliwa. Ibn Al-Mundhir kasema: "Wamekubaliana wote kwamba mtoto akijulikana yu hai au akilia wakati anazaliwa, basi huswaliwa. [Al-Ijma’a ukurasa wa 30].

 

Lakini makhitalifiano yako kati yao ikiwa mtoto hakulia wakati anazaliwa:

Baadhi yao wamesema kwamba haswaliwi. Hilo limesimuliwa toka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah. Pia ni kauli ya Az-Zuhriy, Ath-Thawriy, Al-Awzaa'iy, Maalik, Ash-Shaafi'iy na Aswhaab ar raay. [Sharhu As-Sunnah cha Al-Baghawiy (5/373)].

 

Wanatoa dalili kwa yaliyosimuliwa na Jaabir bin ‘Abdullah na Al-Musuur bin Makhramah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (( Mtoto harithi mpaka alie anapozaliwa)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1032), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (6358, 6359), Ibn Maajah (1508, 2750, 2751), Ad-daaramiy (4126), Ibn Abiy Shaybah (11603), ‘Abdul Razzaaq (6608), Ibn Hibaan (6032), Al-Haakim (4/348), (1/363) na Al-Bayhaqiy (4/8)].

 

Na Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtoto akilia anapozaliwa, hurithi)). [Kuna udhwa’iyf katika isnadi yake: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (2920)].

 

Lakini Maulamaa wengine wamesema kwamba huswaliwa. Linasimuliwa hilo toka kwa Ibn 'Umar na Abu Hurayrah. Pia limesemwa na Ibn Syriyna, Ibn Al-Musayyib, Ahmad na Is-Haaq. [Sharhus Sunnah cha Al-Baghawiy (5/373)]. Wametoa dalili kwa Hadiyth ya Al-Mughiyrah bin Shu-'ubah ya kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtoto wa mimba iliyoharibika huswaliwa, na mzazi wake huombewa maghfirah na rahma)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (1031), An-Nasaaiy (4/358,360), Ibn Maajah (1507), Ahmad (4/247, 249) na wengineo].

 

Is-Haaq ameijibu dalili ya kundi la kwanza akisema: "Hakika mirathi ni kwa kulia mtoto anapozaliwa. Ama Swalaah, bila shaka huswaliwa kwa kuwa ni kiumbe kilichoandikiwa hatima mbaya ya naqama au hatima njema ya furaha.” [Sharhu As-Sunnah cha Al-Baghawiy (5/373)].

 

Al-Khattwaabiy kanukuu toka kwa Ahmad bin Hanbali na Is-Haaq bin Raahaawiyyah ya kwamba wawili hao wamesema: "Huswaliwa kila kilichopuliziwa roho na kikakamilisha miezi minne na siku kumi". [Maalim As-Sunan cha Al-Khattwaabiy (1/268-269)].

 

An-Nawawiy (Rahimahul Laahu) amesema: " Lenye nguvu ni kwamba mtoto wa mimba iliyoharibika huswaliwa ikiwa ameshapuliziwa roho, na hii ni pale anapotimiza miezi minne, kisha akafa. Ama ikiwa atatoka kabla ya muda huo basi haswaliwi, kwa kuwa si maiti kama inavyodhihiri. Na asili ya hilo ni Hadiyth Marfu’u ya ‘Abdullah bin Mas-’oud isemayo: ((Hakika kuumbwa mmoja wenu, hukusanywa kwenye tumbo la mama yake siku arobaini, kisha huwa pande la damu mfano wa hivyo, kisha huwa pande la nyama mfano wa hivyo, halafu hupelekwa Malaika akampulizia roho)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (3208) na Muslim (2643)].

 

· Kuwaswalia Watu Wa Bid-'a, Wenye Madhambi Makubwa Makubwa Na Wafanyaji Maasi

 

Mjumuisho wa maneno waliyosema Maulamaa ni kuwa kila Muislamu huswaliwa hata akiwa ni mfanyaji madhambi makubwa makubwa, au fasiki, au mtu wa bid-'a - madhali hakukufuru kwa bid-'a yake -. Lakini ikiwa Maulamaa na watu wenye hadhi na ushawishi wataacha kumswalia yeyote katika hao ili iwe onyo kwa wengineo wenye kufanya hayo, basi itakuwa ni vizuri. Ni kama alivyokataa Rasuli kumswalia mtu aliyejiua na akawaambia Maswahaba wake: ((Mswalieni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (978) na wengineo].

Haya yamesemwa na Maalik, Ahmad na maimamu wengineo. [Al-Mudawwanah (1/165), Al-Mughniy (2/355), na Majmu’u Al-Fataawaa (24/289)].

 

· Kumswalia Mwenye Deni

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiletewa mtu aliyefariki na anadaiwa, na alikuwa anauliza: ((Je ameacha cha kulipia deni lake?)). Akiambiwa ameacha cha kulipia humswalia, na kama hakuacha husema: ((Mswalieni mwenzenu)). Na Allaah Alipomfungulia kombozi za nchi mbalimbali alisema: (( Mimi nawastahikia zaidi Waumini kuliko nafsi zao. Basi mwenye kufa na deni na hakuacha cha kulipia, basi kulipa ni juu yetu sisi, na mwenye kuacha mali, basi ni za warithi wake)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2298) na Muslim (1619)].

 

An-Nawawiy kasema: " Alikuwa anaacha kumswalia ili awahimize watu juu ya umuhimu wa kulipa deni kabla ya kifo, na kujihimu kutokuwa nalo ili mtu asije akakosa kuswaliwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na Allaah Alipomfungulia kombozi za nchi, alirudi kuwaswalia na kulipa deni la mtu ambaye hakuacha cha kulipia". [Muslim Sharhu An Nawawiy (11/60)].

 

Juu ya msingi wa haya, haitakikani kwa Muislamu yeyote aache kumswalia mdaiwa eti kwa kuwa ana deni. Shukrani ni za Allaah Bwana wa ‘alamina.

 

· Kumswalia Aliyejiua

 

Maulamaa wana kauli tatu kuhusiana na hili:

 

Ya kwanza:

 

Haswaliwi. Hii ni kauli ya 'Umar bin ‘Abdul 'Aziyz na Al-Awzaa'iy. [Muslim Sharhu An Nawawiy (7/47)].

 

Hoja yao ni ni Hadiyth ya Jaabir bin Samurah aliyesema: "Rasuli aliletewa mtu mmoja aliyejiua kwa ncha ya mshale, hakumswalia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (978)].

 

Ya pili:

 

Huswaliwa. Ni kauli ya Jamhuri ya Maulamaa, Al-Hasan, An-Nakh'iy, Qataadah, Maalik, Abu Haniyfah na Ash-Shaafi'iy. Wameijibu Hadiyth iliyotangulia ya Jaabir kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumswalia yeye binafsi ili iwe onyo kwa watu wasije kufanya kitendo kama hicho, lakini Maswahaba walimswalia. Na ndivyo kama Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoacha kumswalia mwenye deni mwanzoni ili kuwaonya wasitasahali kukopa na kuzembea kulipa deni, lakini aliwaamuru Maswahaba wamswalie kwa kuwaambia: ((Mswalieni mwenzenu)).

 

Al-Qaadhwiy amesema: "Kauli ya Maulamaa wote ni kumswalia kila Muislamu aliyekufa kwa kutekelezewa adhabu ya kisharia, aliyepigwa mawe kwa kuzini, aliyejiua na mtoto wa zinaa". [Angalia Sharhu Muslim (7/47) cha An-Nawawiy].

 

Ya tatu:

 

Waheshimiwa wenye hadhi na wenye madaraka waache kumswalia. Hili limesimuliwa toka kwa Maalik na wengineo, nalo ndilo lenye nguvu. [Sharhu Muslim (7/47) cha An-Nawawiy].

Ibn Taymiyah amepondokea kwenye kauli hii aliposema: "Inafaa kwa watu wa kawaida kumswalia. Ama Maulamaa wa dini wenye sauti na ushawishi, kama wakiacha kumswalia ili iwe onyo kwa wengineo na kukiiga kitendo cha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi hii ni haki. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi". [Maajmu’u Al-Fataawaa (24/289)].

 

· Je, Shahidi Wa Vita Huswaliwa?

 

Maulamaa wamekhitalifiana juu ya hili katika kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Haswaliwi. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi'iy, Is-Haaq na moja ya riwaya toka kwa Ahmad. [Naylul Awtwaar (4/54) na Al-Afnaan An-Nadiyyah (2/295)].

 

Wametoa dalili kwa jumla ya Hadiyth ambazo baadhi yake ni:

 

1- Hadiyth Marfu’u ya Jaabir kuhusu maiti wa Uhud ambapo alisema: "Akaamuru wazikwe na damu zao,  hawakuoshwa, na wala hawakuswaliwa". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1343)].

 

2- Hadiyth ya Anas ya kwamba Mashahidi wa Uhud hawakuoshwa, wakazikwa na damu zao, na wala hawakuswaliwa [isipokuwa Hamzah]. [Al-Albaaniy kasema ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3137), na ziada ni yake, Al-Haakim (1/520) na Al-Bayhaqiy (4/10-11). Angalia Ahkaamul Janaaiz cha Al-Albaaniy (73)].

 

3- Hadiyth ya Abu Barzah kuhusiana na kuuawa Julaybiyb ambapo anasema: " Akamweka kwenye mikono yake miwili, hana kitanda isipokuwa mikono ya Rasuli. Akachimbiwa shimo, akawekwa kwenye kaburi lake na hakutaja osho". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2472), At-Twayalsiy (924), Ahmad (4/421, 422, 425) na Al-Bayhaqiy (4/21)].

 

Ya pili:

 

Ni lazima Shahidi aswaliwe. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Ath-Thawriy, Ibn Al-Musayyib na Al-Hasan. Imeungwa mkono na Al-'Utrah. [Naylul Awtwaar (4/54) na Al-Afnaan An-Nadiyyah (2/295)].

 

Wametoa dalili kwa jumla ya Hadiyth ambazo miongoni mwazo ni:

 

1- Hadiyth ya Shaddaad bin Al-Haad ya kwamba mtu mmoja bedui alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamini na kumfuata. Hadiyth inasema: " Walikaa kidogo, kisha wakanyanyuka kwenda kupambana na adui. Bedui akaletwa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amebebwa baada ya kupigwa mshale, na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ni huyu ndiye?)). Wakasema: Ndiye. Akasema: ((Amemsadiki Allaah, na Yeye Akamsadikisha)). Kisha Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamkafini kwa juba lake, halafu akamweka mbele na kumswalia. Halafu ikawa kati ya aliyomwombea Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni: Ee Allaah! Huyu ni mja Wako, ametoka akihajiri katika Njia Yako akauawa kishahidi, na mimi ni shahidi juu ya hilo". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (4/60), ‘Abdul Razzaaq kwenye Al-Muswannaf (9597), Al-Haakim kwenye Al-Mustadrak (3/595/596) na Al-Bayhaqiy (4/15-16)].

 

2- Hadiyth ya 'Uqbah bin 'Aamir ya kwamba Rasuli aliwaswalia maiti wa Uhud baada ya miaka minane. Swalaah yake kwa maiti ni kama mwenye kuwaaga walio hai na waliokufa. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (4042) na Muslim (2296)].

 

Wana jumla ya Hadiyth nyinginezo ambazo Sanad zake hazikosi kosoleo.

 

Ya tatu:

 

Hii ina nguvu na nafsi inapondokea kwayo. Inasema kwamba inajuzu kumswalia au kutomswalia. Ikiwa ataswaliwa aliyeuawa vitani basi ni vizuri, na kama hakuswaliwa pia ni vizuri. Hii ni rai ya Ibn Hazm [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (5/115)],  na riwaya moja toka kwa Ahmad.  Ibn Al-Qayyim kasema iko barabara. [Angalia Al-Afnaan An-Nadiyyah (2/294)].

Kauli hii inafanya kazi kwa Hadiyth na nususi zote zilizothibiti.

 

Faida: Ama Shahidi ambaye si wa vitani, huyu huoshwa, na huswaliwa kama maiti wengineo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

· Kumswalia Maiti Wa Mbali Asiyekuwepo

 

Maulamaa wana kauli tatu kuhusiana na hili:

 

Ya kwanza: Inajuzu kumswalia maiti wa mbali. Ni kauli ya Ash-Shaafi'iy, na Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili. [Zaadul Ma’ad cha Ibn Al-Qayyim (1/197)].

 

Mhimili wa hoja yao katika hili ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatangazia watu maombolezo ya kifo cha Negus katika siku aliyofariki, akatoka nao hadi kwenye muswalla, akapiga takbiyrah nne". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (951) toka Hadiyth Marfu’u ya Abu Hurayrah].

 

Ya pili: Haijuzu kumswalia maiti wa mbali, na kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumswalia Negus kimahususi, hakuwezi kufanywa kwa wote. Ni kauli ya Maalik na Abu Haniyfah. [Al-Muhalla cha Ibn Hazm (5/139)].

 

Ya tatu: Ina uchanganuo kidogo. Ni kwamba inajuzu kumswalia maiti wa mbali aliyekufa katika nchi ambayo hakuswaliwa na yeyote, na kama ameswaliwa huko alikofia, basi hatoswaliwa Swalaah ya maiti wa mbali kwa kuwa faradhi inakuwa ishaondoka kwa kuswaliwa na Waislamu. Huu ni msimamo wa Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah [Zaadul Ma’ad cha Ibn Al-Qayyim (1/197)].

 

Ni chaguo pia la Sheikh 'Uthaymiyn. Hoja yao ni kwamba Rasuli hakumswalia mwingine yeyote Swalaah ya maiti wa mbali isipokuwa Negus peke yake, kwa kuwa alikufa kwenye umma wa kipagani usio na Swalaah. Na kama alikuwepo kati yao aliyeamini, basi hakuna chochote kijulikanacho kuhusu Swalaah hiyo. [Ash-Sharhul Mumti’i cha Ibn ‘Uthaymiyn (5/439)].

 

· Haijuzu Kumswalia Kafiri

 

Haijuzu kumswalia kafiri kutokana na Neno Lake Ta’alaa:

(( وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ))

((Na wala usimswalie yeyote abadani miongoni mwao akifa; na wala usisimame kaburini kwake. Hakika wao wamemkufuru Allaah na Rasuli Wake, na wakafa hali wao ni mafasiki)). [At-Tawbah (9:84)]

 

Na Neno Lake Ta’alaa:

(( مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ •  وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ))

((Haimpasi Nabiy na wale walioamini kuwaombea maghfirah washirikina japokuwa ni jamaa zao wa karibu baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa moto uwakao vikali mno • Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya ahadi aliyoahidiana naye. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym ni mwenye huruma mno na mvumilivu)). [At-Tawbah (9:113 na 114)]

 

· Kuwaswalia Watoto Wa Mapagani

 

Haijuzu kuwaswalia watoto wa kipagani, kwa kuwa wanafuata hukmu ya wazazi wao ila kwa mtoto tunayemhukumu kuwa ni Muislamu. Ni kama kusilimu mmoja wa wazazi wake, au mtoto huyo kufa au kutekwa akiwa peke yake bila wazazi. Kama atakuwa hivyo, basi ataswaliwa. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/507, 508)].

 

· Hukmu Ya Mtu Aliyekutwa Amekufa Bila Kutambulika Kama Ni Muislamu Au Kafiri

 

Maulama wanasema kwamba zitaangaliwa alama za Uislamu kama kutahiriwa, nguo zake, mpako wa hina na kadhalika. Kama zitapatikana, ataoshwa na kuswaliwa. Na kama hakuna na maiti yuko katika nchi ya Kiislamu, basi ataoshwa na kuswaliwa. Na kama yuko katika nchi ya kikafiri, hatooshwa wala kuswaliwa. Haya kayaeleza Ahmad. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/478). Angalia Al-Mabsuutw cha As-Sarkhasiy (1/54) na Al-Majmu’u cha An-Nawawiy (5/213)].

 

· Zikichanganyika Maiti Za Waislamu Na Makafiri

 

Maulamaa wamekhitalifiana juu ya hili katika kauli mbili:

 

Ya kwanza: Zikichanganyika bila kuweza kutofautisha kati ya Waislamu na makafiri, wataswaliwa wote kama Waislamu. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’i na Ahmad. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/477)].

 

Ya pili: Ikiwa maiti nyingi ni za Waislamu, wataoshwa na kuswaliwa wote kwa kuzingatia wingi isipokuwa kwa maiti itakayojulikana ni ya kafiri. Na kama nyingi ni za makafiri, haziswaliwi isipokuwa maiti zitakazojulikana kama ni za Waislamu kwa alama. Kama idadi italingana, hawataswaliwa kwa kuwa kuwaswalia makafiri ni marufuku, na pia inajuzu kuacha kuwaswalia baadhi ya Waislamu. Hii ni kauli ya Abu Haniyfah. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (3/477) na Al-Mabsuutw cha As-Sarkhasiy (1/54-55)].

 

· Ni Wapi Maiti Huswaliwa?

 

Kuswalia maiti kwenye muswallah

 

Imesuniwa kuswalia maiti katika muswallah, kwa kuwa Swalaah nyingi za maiti alizoziswali Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zilikuwa katika muswallah, nayo ni sehemu maalumu kwa ajili hiyo kama ilivyosimuliwa:

 

- Imepokewa toka kwa Ibn Habiyb kwamba muswallah wa maiti Madiynah, ulikuwa umeshikana na Msikiti wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa upande wa mashariki. [Fat-hul Baariy (3/237)].

 

- Abu Hurayrah kuhusu Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumswalia Negus amesema: “Rasuli aliwapanga safu katika muswallah, akampigia takbiyrah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1328) na Muslim (952)].

 

- ‘Abdullah bin ‘Umar kasema: “Mayahudi walimleta mwanamume kati yao na mwanamke waliozini kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli akaamuru wapigwe mawe karibu na muswallah wa maiti mbele ya Msikiti”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1329)].

 

Ibn Hajar kasema: “Hadiyth iliyotajwa ya Ibn ‘Umar inaonyesha kwamba Swalaah za maiti zilikuwa na sehemu yake maalum iliyoandaliwa” [Fat-hul Baariy (3/237)].

 

· Kuswalia Maiti Ndani Ya Msikiti

 

Maulamaa wana kauli tatu kuhusu hili:

 

Ya kwanza: Ni makruhu. Ni mwelekeo wa Hanafi na Maalik. [Fat-hul Baariy (3/224)].

 

Hoja yao ni dalili tulizozitoa za kumswalia maiti kwenye muswallah. Pia wanatolea dalili Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kumswalia maiti Msikitini, basi hana kitu)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3191), Ibn Maajah (1517), Ahmad (2/444, 455, na 505). Angalia As-Silsilat As-Swahiyhah (2352)].

 

Ya pili: Inajuzu. Ni kauli a Mahanbali. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (16/36)].

 

Wametoa dalili kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumswalia Suhayl bin Baydhwaa isipokuwa Msikitini”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (973)].

 

Ya tatu: Ni Sunnah kama uko usalama wa Msikiti kutochafuliwa. Ni kauli ya Mashaafi’iy. [Al-Mawsuw’at Al-Fiqhiyyah (16/36)].

 

Wametoa dalili kwa Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia, na wanasema pia kumswalia Msikitini ni utukufu zaidi.

 

· Kumswalia Maiti Kwenye Kaburi

 

Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu hili kwa aliyepitwa na Swalaah katika kauli tatu: [Al-Ummu (1/414), Al-Majmu’u (5/210), Al-Mudawwanah (1/170), Al-Mughniy (3/500) Naylul Maarib (1/66), Sunan At-Tirmidhiy nambari 1037, Al-Muhalla (5/139) na Al-Badaai-’i (1/314)].

 

Ya kwanza: Huswaliwa. Ni kauli ya Maulamaa wengi katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waliofuatia baada yao. Pia ni kauli ya Ibn Mubaarak, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, Ibn Hazm na wengineo. Wametoa dalili kwa:

 

1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali kwenye kaburi baada ya maiti kuzikwa, akapiga takbiyrah nne”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy kwa urefu (1247) na Muslim (954), na tamko ni lake].

 

2- Hadiyth ya Abu Hurayrah: “Kwamba mtu mweusi – mwanaume au mwanamke – alikuwa akisafisha Msikiti na akafariki. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakujua habari ya kifo chake, na siku moja akamkumbuka na kusema: (( Kitu gani kimemsibu mtu yule?)). Wakasema: Amekufa ee Rasuli wa Allaah. Akasema: ((Kwa nini msinijulishe?)). Wakasema: Alikuwa hivi na hivi – kisa chake – wakamdunisha. Akasema: (( Nionyesheni wapi kaburi lake)), akaenda kwenye kaburi hilo na kumswalia”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1337)].

 

Wenye kauli hii, wako baadhi yao waliojuzisha kuswali kwenye kaburi mpaka siku tatu na zikipita basi, wengine wamejuzisha mpaka mwezi, wengine wanasema mpaka mwili uharibike, na wengine milele.

 

Ya pili: Haijuzu kabisa kumswalia kwenye kaburi.

 

Ya tatu: Haijuzu kumswalia kwenye kaburi isipokuwa kama alizikwa kabla ya kuswaliwa. Kauli hizi mbili (ya pili na ya tatu) zimesimuliwa toka kwa An-Nakh'iy, Abu Haniyfah na Maalik. Na hoja yao ni:

 

1- Hadiyth zenye kukataza kuswali kwenye makaburi na kuswali kulielekea kaburi.

 

2- Nyongeza iliyopo kwenye Hadiyth ya Abu Hurayrah inayozungumzia Rasuli kumswalia mwanaume au mwanamke mweusi. Inasema: ((Hakika makaburi haya yamejaa giza kwa watu wake, na hakika Allaah Huyatia nuru kwa mimi kuwaswalia)). [Imefanyiwa "ikhraaj" kwa nyongeza hii na Muslim (956) kwa njia ya Abu Ar-Rabiy'i na Abu Kaamil Thanaa Hammaad toka kwa Thaabit toka kwa Abu Raafi'i toka kwa Abu Hurayrah].

 

Wamesema: "Kumswalia maiti kwenye makaburi ni katika mambo mahsusi yanayomhusu Rasuli peke yake".

 

· Kauli Yenye Nguvu:

 

Dalili za kumswalia maiti kwenye kaburi zimethibiti uthibiti usiokabilika ila mtu kusalimu amri tu. Ama kwa maiti ambaye hakuswaliwa, bila shaka jambo liko wazi bayana, na uhalali wa kumswalia utaendelea kuwepo madhali watu wanajua kwamba hakuna aliyemswalia. Ama kwa ambaye ameswaliwa, Hadiyth iliyotangulia kuhusu mwanaume au mwanamke mweusi inaweka wazi. Na ni maarufu kwamba katika enzi yake Rasuli, maiti alikuwa hazikwi bila ya kuswaliwa. [Ar-Rawdhwah An-Nadiyyah (1/171)].

 

Ama Hadiyth zenye kukataza kuswali kwenye makaburi na kuswali kuyaelekea, bila shaka katazo hili ni mahususi kwa Swalaah nyinginezo zisizo za maiti. Kwani aliyekataza hilo ndiye huyo huyo aliyeswalia maiti kwenye kaburi. Hii ni kauli yake na hiki ni kitendo chake, na viwili hivi havipingani. [Al-Muhalla (5/139) na Zaadul Ma’ad (1/195)].

 

Ama madai ya umahususi, haya hayana mashiko. Yanakhitilafiana na asili, na hayawezi kuthibiti ila kwa dalili. Ama ziada walioitumia kama hoja, la sawa ni kuwa imeingizwa katika Isnadi hii, nayo ni katika Mursali za Thaabit. Limebainishwa hili na Maswahiba wengi wa Hammaad bin Zayd. Na kwa ajili hiyo, Al-Bukhaariy hakuikhariji nyongeza hiyo. [Fat-hul Baariy (baada ya Hadiyth 458), na Sunan Al-Bayhaqiy (4/47)].

 

Na hata tukijaalia kwamba imethibiti, basi kuwa tu kwamba Allaah Anayatia nuru makaburi kutokana na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwaswalia waliomo humo, hakukanushi uhalali wa mtu mwingine kumswalia mtu kwenye kaburi na hasahasa baada ya neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Swalini kama mnavyoniona nikiswali)). [Naylul Awtwaar (4/64) chapa ya Al-Hadiyth].

 

Isitoshe, baadhi ya Maswahaba waliswali kwenye kaburi nyuma ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na yeye hakuwakataza. Hivyo basi, la sahihi ni kuwa inajuzu kuswali kwenye kaburi kwa ambaye hakumswalia maiti na hususan akiwa ni katika wahishimiwa wenye sifa ya wema. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Share