Imaam Ibn Baaz: Al-Muharram: Lini Huanza Swawm Za Al-Muharram Na Je Siku Ngapi Za Swiyaam?
Lini Huanza Swawm Za Mwezi Wa Al-Muharram Na Je Siku Ngapi Za Swiyaam?
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu-Allaah)
SWALI:
Ni lini huanza Swawm ya mwezi wa Al-Muharram au Swawm ya 'Aashuraa. Je, huanza mwanzo wa Al-Muharram au katikati yake au mwisho wake. Na siku zake za kufunga ni ngapi? Kwani nimesikia kuwa Swawm ya 'Aashuraa huanza tarehe moja Al-Muharram na kuisha tarehe kumi Al-Muharram. Allaah Akuwafikieni.
JIBU:
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Swawm bora kabisa baada ya Ramadhwaan ni Swawm ya mwezi Mtukufu wa Allaah (mwezi wa) Al-Muharram" [Muslim] Nayo ni 'Aashuraa na maana ni kuwa hufunga yote mwanzo hadi mwisho hii ndio maana ya Hadiyth, lakini inaainisha siku ya tisa na siku ya kumi, au kumi na kumi na moja kwa ambaye hatofunga zote kwasababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga ‘Aashuraa katika zama ujaahiliyyah na ma-Quraysh walikuwa wakifunga vile vile.
Kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipofika Madiynah aliwakuta Mayahudi wakifunga akawauliza kuhusu hilo wakajibu: “Ni siku ambayo Allaah Alimuokoa (Nabii) Muwsaa pamoja na kaumu yake, na kumwangamiza Fir-‘awn na kaumu yake. Hivyo Nabiy Muwsaa akafunga akimshukuru Allaah na sisi tunafunga. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Sisi ndio wenye haki zaidi kwa Nabiy Muwsaa na wa mwanzo kufunga kuliko nyinyi." Akafunga na kuamrisha Maswahaba wafunge.
Hivyo Sunnah ni kufunga siku hii ya 'Aashuraa na Sunnah kufunga siku moja kabla au siku moja baada yake kwa kilichopokelewa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: "Fungeni siku kabla yake au siku baada yake." Na katika Hadiyth nyingine: "Nikiishi hadi mwakani nitafunga siku ya tisa yaani pamoja na ya kumi." Hii ndio bora zaidi kufunga siku ya kumi kwa kuwa ni siku adhimu ambapo Nabiy Muwsaa na Waislamu walipata kheri kubwa na Nabiy wetu alifunga.
Na sisi tunafunga siku ya tisa kwa maelekezo na kumfuata Nabiy wetu na tunafunga siku moja kabla yake au moja baada yake ili kwenda kinyume na Mayahudi, na bora zaidi ni tisa pamoja na kumi kwa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Nikiishi hadi mwakani nitafunga siku ya tisa." Naa akifunga kumi na kumi na moja au akifunga siku tatu; zote ni bora. Nazo ni kinyume na Mayahudi na akifunga mwezi mzima ni bora kwake.
[Mawqi’a Ar-Rasmiy li-Samahaat Ash-Shaykh Imaam Ibn Baaz]