041-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Uharamu wa Kuwaasi Wazazi na Kukata Kizazi
Riyaadhw Asw-Swaalihiyn
باب تحريم العقوق وقطيعة الرحم
041-Mlango Wa Uharamu wa Kuwaasi Wazazi na Kukata Kizazi
قَالَ الله تَعَالَى:
فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ﴿٢٢﴾ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ﴿٢٣﴾
Basi huenda nyinyi mkigeuka ndio mfanye ufisadi katika ardhi na kukata jamaa zenu wa uhusiano wa damu? Hao ndio ambao Allaah Amewalaani; Akawafanya viziwi na Akawapofua macho yao. [Muhammad: 22-23]
وَالَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۙ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٢٥﴾
Na wale wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kufungamana kwake na wanakata yale Aliyoyaamrisha Allaah kuwa yaungwe na wanafanya ufisadi katika ardhi, hao watapata laana na watapata makazi mabaya (motoni). [Ar-Ra'd: 25]
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾ وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾
Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima. Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni. [Al-Israa: 23-24]
Hadiyth – 1
وعن أَبي بكرة نُفَيع بن الحارث رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( ألا أُنَبِّئُكُمْ بأكْبَرِ الكَبَائِرِ ؟ )) – ثلاثاً – قُلْنَا : بَلَى ، يَا رَسُول الله ، قَالَ : (( الإشْرَاكُ بالله ، وَعُقُوقُ الوَالِدَيْنِ )) ، وكان مُتَّكِئاً فَجَلَسَ ، فَقَالَ : (( ألاَ وَقَوْلُ الزُّورِ وَشَهَادَةُ الزُّورِ )) فَمَا زَالَ يُكَرِّرُهَا حَتَّى قُلْنَا : لَيْتَهُ سَكَتَ . مُتَّفَقٌ عَلَيهِ.
Imepokewa kwa Bakrah Nufay' bin Al-Haarith Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Je, hamtaki niwaambieni dhambi kubwa katika madhambi makubwa?"- mara tatu. Tukasema: "Ndio (tuambie), Ee Rasuli wa Allaah." Akawaambia: "Ni kumshirikisha Allaah na kuwaasi wazazi." Na alikuwa ameegemea, akakaa na kusema: "Eleweni pia kusema urongo na kutoa ushahidi wa urongo." Aliendelea kukariri hilo mpaka tukasema: "Laiti angenyamaza." [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hadiyth – 2
وعن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما ، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( الكَبَائِرُ : الإشْرَاكُ بالله ، وَعُقُوقُ الوَالِدَيْنِ ، وَقَتْلُ النَّفْس ، وَاليَمِينُ الغَمُوسُ )) رواه البخاري .
Imepokewa kutoka kwa 'Abdillaahi bin 'Amru bin Al-'Aasw (Radhwiyah Allaahu 'anhummaa) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Madhambi makubwa ni kumshirikisha Allaah, kuwaasi wazazi, kuua nafsi na kiapo (yamini) cha urongo wa kusudi." [Al-Bukhaariy]
Hadiyth – 3
وعن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما أن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ: (( مِنَ الكَبَائِر شَتْمُ الرَّجُل وَالِدَيهِ ! ))، قالوا : يَا رَسُول الله ، وَهَلْ يَشْتُمُ الرَّجُلُ وَالِدَيْهِ ؟! قَالَ : (( نَعَمْ ، يَسُبُّ أَبَا الرَّجُلِ ، فَيَسُبُّ أبَاه ، وَيَسُبُّ أُمَّهُ ، فَيَسُبُّ أُمَّهُ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .
وفي رواية : (( إنَّ مِنْ أكْبَرِ الكَبَائِرِ أنْ يَلْعَنَ الرَّجُلُ وَالِدَيْهِ ! )) ، قِيلَ : يَا رَسُول الله ، كَيْفَ يَلْعَنُ الرَّجُلُ وَالِدَيهِ ؟! قَالَ: (( يَسُبُّ أَبَا الرَّجُلِ ، فَيَسُبُّ أباهُ ، وَيَسُبُّ أُمَّهُ ، فَيَسُبُّ أُمَّهُ )) .
Kutoka kwa 'Abdillaahi bin 'Amru bin Al-'Aasw (Radhwiyah Allaahu 'anhummaa) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Miongoni mwa madhambi makubwa ni mtu kuwatusi wazazi wake ." Wakauliza (yaani Maswahaba): "Ee Rasuli wa Allaah! Na je, mtu, anaweza kuwatusi wazazi wake?" Akasema: "Ndio, atamtusi baba ya mtu, naye amtusi babake, na atamtusi mama ya mtu, naye amtusi mamake." [Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad]
Katika riwaayah nyingine: "Hakika miongoni mwa madhambi makubwa ni mtu kuwalaani wazazi ake." Pakasemwa: "Ee Rasuli wa Allaah! Vipi mtu atawalaani wazazi wake?" Akasema: "Atamtusi baba ya mtu, naye amtusi babake, na atamtusi mama ya mtu, naye amtusi mamake."
Hadiyth – 4
وعن أَبي محمد جبيرِ بن مطعم رضي الله عنه: أن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( لاَ يَدْخُلُ الجَنَّةَ قَاطِعٌ )) قَالَ سفيان في روايته : يَعْنِي : قَاطِع رَحِم . مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .
Imepokewa kutoka kwa Abu Muhammad Jubayr bin Mutw'im (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hataingia Peponi mwenye kukata." Amesema Sufyaan katika riwaayah yake: "Yaani mwenye kukata kizazi." [Al- Bukhaariy na Muslim]
Hadiyth – 5
وعن أَبي عيسى المغيرة بن شعبة رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( إنَّ اللهَ تَعَالَى حَرَّمَ عَلَيْكُمْ : عُقُوقَ الأمَّهَاتِ ، وَمَنْعاً وهاتِ ، وَوَأْد البَنَاتِ ، وكَرِهَ لَكُمْ : قِيلَ وَقالَ ، وَكَثْرَةَ السُّؤَالِ ، وَإضَاعَةَ المَالِ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .
Imepokewa kutoka kwa Abu 'Iysa Mughyrah bin Shu'bah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameharamisha kuwaasi mama zenu; na kuzuia na lete (kuzuia kilicho wajibu kutoa na kutaka kisicho chake); na kuzika wasichana wakiwa hai; na Amechukia kwenu kusema ovyo; kuomba sana; na kufuja mali." [Al-Bukhaariy na Muslim]