026-Ash-Shu’araa: Utangulizi Wa Suwrah
026-Ash-Shu’araa: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 227
Jina La Suwrah: Ash-Shu’araa
Suwrah imeitwa Ash-Shu’araa (Washairi), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (224).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha dalili za uwepo wa Allaah (سبحانه وتعالى) katika kuwaunga mkono Rusuli, na kuwaangamiza wanaokadhibisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuipa heshima na kuitukuza Qur-aan, na kuonyesha kushindwa kwa washirikina juu ya kuipinga kwao.
3-Kuelezewa visa vya baadhi ya Rusuli pamoja na waliyofanyiwa na watu wao na maangamizi ya Allaah kwa watu hao.
4-Kumliwaza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa maudhi aliyokutana nayo kutoka kwa watu wake.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imebainishwa Utukufu wa Qur-aan, na kutaja misimamo ya washirikina kuhusu Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na kumliwaza (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na maudhi waliyomfanyia watu wake.
2-Imeelezea kwa kiasi, kisa cha Nabiy Muwsaa na ndugu yake Haaruwn (عليهما السلام), na Firawni na kisa cha wachawi walioamini. Kisha ikaelezewa hatima ya Firawni ya kugharakishwa baharini na jeshi lake kwa namna ya muujiza mkubwa! Na kuokolewa Nabiy Muwsaa (عليه السلام) na kaumu yake.
3-Imeelezwa dawaah ya Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) kumlingania baba yake.
4-Imetajwa kisa cha Nabiy Nuwh (عليه السلام) na daawah ya kuwalingania watu wake, na kilichotokea kwa kuangamizwa wale waliompinga na kuokolewa Waumini.
5-Vimetajwa visa vinginevyo vya baadhi ya Rusuli akiwemo: Huwd, Swaalih, Luutw, na Shu’ayb (عليهم السلام) na yale yaliyowapata kutoka kwa watu wao.
6-Imetajwa heshima ya Qur-aan, na ushuhuda wa Ahlul-Kitaab juu ya Qur-aan, na kwamba imetakasika na kuepukana kuwa kama mashairi na maneno ya mashaytwaan.
9-Imetajwa kuamrishwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kutakiwa kuwaonya jamaa zake wa karibu, na kwamba adhabu ni mafikio ya madhalimu.