027-An-Naml: Utangulizi Wa Suwrah

 

027-An-Naml: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 93

 

Jina La Suwrah: An-Naml

 

Suwrah imeitwa An-Naml (Sisimizi), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (18).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Shukurani na fadhila kwa Nabiy (صلى الله عليه وسلم) kwa neema ya Qur-aan, kuishukuru (neema hiyo), na subra juu ya kuifikisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kushukuru Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba mwenye kushukuru anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake kwani Allaah ni Mkwasi.

 

3-Kumwamini Allaah (سبحانه وتعالى), kumwabudu bila kumshirikisha na kuamini Wahy na Aakhirah, kuamini mambo ya ghaibu, na kuamini kwamba Allaah Ndiye Mtoaji Rizki.

 

4-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Ni Muweza wa kila kitu na jinsi gani Allaah (سبحانه وتعالى) Anaweza kumuongoza Mja Wake.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imethibitishwa kwamba Qur-aan ni Kitabu Kinachobainisha wazi, na ni mwongozo na bishara kwa Waumini, na zikatajwa sifa za Waumini hao. Kisha ikabainishwa kuhusu makafiri wasioamini, kwamba watapata adhabu ovu na watakuwa wenye kukhasirika. 

 

2-Imethibitisha kuwa Qur-aan ndio tegemeo kwa Vitabu vilivyotangulia na kwamba Qur-aan inawaongoa watu na imehabarisha visa na matukio ya watu waliopita.

 

3-Imeelezewa kwa kifupi kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام).

 

4-Kisha Suwrah ikataja kisa cha Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام) na kisa cha sisimizi aliyewatanabahisha wenzake waingie haraka masikanini mwao wasije kupondwa na jeshi la Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام).   

 

5-Imetaja kisa cha ndege hud-hud na mfalme wa Saba-a na watu wake na alivyoifanyia daawah Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى). Kisha pindi Nabiy Sulaymaan alimpompelekea barua mfalme wa Saba-a kumlingania Uislamu akaanza barua yake kwa:

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

6-Imetaja pia visa vya Nabiy Muwsa, Swaalih, na Luutw (عليهم السلام), na waliyoyapata kwa watu wao.

 

7-Imebainisha kwa dalili za wazi ya kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mmoja na Akabainisha Neema Zake kadhaa ikiwemo neema ya kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anaitikia duaa ya mwenye dhiki mno.

 

8-Imetaja baadhi ya alama za Qiyaamah.

 

9-Suwrah imekhitimishwa kwa amri kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) na kuisoma Qur-aan. 

 

 

 

 

Share