034-Saba-a: Utangulizi Wa Suwrah
034-Saba-a: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 54
Jina La Suwrah: Saba-a
Imeitwa Saba-a (Mji wa Yemen), na inayodalilisha ni kutajwa kisa cha watu wake katika Aayah namba (15).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha hali za watu wanapopata neema (wakaikufuru), na Desturi za Allaah katika kuibadilisha hali hiyo (ya neema). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kubatilisha ushirikina na kuwapinga washirikina.
3-Kubainisha Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa dalili na ukweli wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى) Aliyetakasika na kila mapungufu, Mmiliki wa vilivyomo mbinguni na ardhini, na kubainisha upana (kuenea) wa Ilimu Yake.
2-Imebainisha kwamba washirikina wanapinga Siku ya Qiyaamah na kufufuliwa, na baadhi ya maneno yao ya yaliyokuwa ni baatwil.
3-Imetajwa sehemu fulani ya kisa cha Nabiy Daawuwd (عليه السّلام) na mwanawe Sulaymaan (عليه السّلام) na neema na fadhila zake za kutiishiwa majini.
4-Imetajwa kisa cha kabila la Saba-a waliokufuru Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) na hatima yao.
5-Imebainishwa Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba Yeye Ndiye Mwenye kuruzuku waja.
6-Imebainishwa kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametumwa kwa watu wote ulimwenguni na sio Waarabu pekee.
7-Imetajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah, na mijadala itayokuwepo kati ya wafuasi na wanaofuatwa.
8-Radd kwa matajiri ambao walidai kuwa mali zao na watoto wao vitawanufaisha Siku ya Qiyaamah.
9-Imetajwa baadhi ya ada za washirikina kutokuamini Qur-aan na kutokumuamini Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).
10-Daawah kwa makafiri ya kuwataka waifikirie sana Daawah ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).
11-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwatisha makafiri ya kwamba watakuwa na mwisho mbaya, kama wataendelea na misimamo yao ya ukafiri na ukaidi.
Faida:
Suwrah Saba-a (34), ni miongoni mwa Suwrah tano zinazoanzia kwa AlhamduliLlaah. Nyenginezo ni Al-Faatihah (1), Al-An’aam (6), Al-Kahf (18), na Faatwir (35).