035-Faatwir: Utangulizi Wa Suwrah
035-Faatwir: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 45
Jina La Suwrah: Faatwir
Suwrah imeitwa Faatwir (Mwanzilishi), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1) kumkusudia Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni Mwanzilishi au Muumbaji. Rejea chini kwenye Faida.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha uhitaji wa waja kwa Allaah Mwanzilishi wa mbingu na ardhi (uhitaji) usio na mpaka, na Ukamilifu wa Ukwasi Wake kwao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah kwa njia ya kuwakumbusha waja Neema Zake zilizoenea ulimwenguni.
3-Kubainisha Uwezo wa Allaah Uliokamilika, pamoja na Uwezo wa kufufua.
4-Kuthibitisha Ukweli wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى) Mwanzilishi wa mbingu na ardhi na kuwafanya Malaika kuwa ni Wajumbe wenye mbawa, na kwamba Uwezo Wake Allaah (سبحانه وتعالى) upo kwenye kila kitu.
2-Imetajwa baadhi ya mambo yanayodalilisha Uwezo wa Allaah kwa Viumbe, na Neema Zake kwa waja wake.
3-Imetajwa kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumpa thabati kwa kumbainishia hali ya Manabii waliotangulia.
4-Imetoa tahadhari ya dunia na kutodanganyika na shaytwani.
5-Imetajwa kuwa neno zuri ambalo ni aina yoyote ya kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) hutukuzwa na kupandishwa juu kwa Allaah.
6-Imebainisha malipo ya Waumini na malipo ya makafiri.
7-Imetajwa Neema ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuupelekea upepo, na kuteremsha mvua, na kuhuisha ardhi iliyokufa, na hivyo ndivyo mfano wa kufufuliwa.
8-Imebainishwa Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya Uumbaji Wake viumbe na Neema Zake mbalimbali, na kwamba washirikina hawana uwezo wa kumiliki chochote kile hata kiwe kidogo vipi.
9-Imetajwa uhitaji wa viumbe kumuhitajia Allaah (سبحانه وتعالى) Naye ni Mkwasi Asiyehitaji lolote lile.
10-Imebainishwa kuwa hakuna mwanaadam atakaebeba madhambi ya mwenzie hata kama ni jamaa wa karibu.
11-Imepigwa mifano mbalimbali ya kulinganisha Muumini na kafiri, au aliyekuwa na ilimu na mjinga.
12-Imebainishwa kuwa wenye kumkhofu zaidi Allaah (سبحانه وتعالى) ni wenye ilimu na ikatajwa fadhila za kusoma Qur-aan na kusimamisha Swalaah na kutoa mali kwa njia ya Allaah.
13-Imetajwa hali za Waumini watakapokuwa Jannah (Peponi) na hali za makafiri watakapokuwa motoni.
14-Imetajwa ujinga wa washirikina kuabudia kwao masanamu ambayo hayamiliki kwao madhara wala manufaa.
15-Imetajwa zingatio kubwa la Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) Kuzuia mbingu na ardhi zisitoweke.
16-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa Utukufu wa Allaah na Uwezo Wake kwamba hakuna linalomshinda na pia ikatajwa Rehma Yake ya kutokuwaadhibu pale pale viumbe wanapokosea lakini Anawaakhirishia mpaka muda maalumu.
Faida:
1-Faatwir (Mwanzilishi): Imetajwa Sifa ya Allaah kuwa Ni Mwanzilishi wa mbingu na ardhi, katika Suwrah nyenginezo. Rejea Al-An’aam (6:14), (6:79), Suwrah Yuwsuf (12:101), Ibraahiym (14:10), Al-Anbiyaa (21:56), Az-Zumar (39:46), Ash-shuwraa (42:11). Na imekuja katika Sifa ya Muumbaji katika Suwrah Huwd (11:51) Al-Israa (17:51), Twaahaa (20:72), Yaasiyn (36:22), Az-Zukhruf (43:27).
2-Suwrah Faatwir (35) ni miongoni mwa Suwrah tano zinazoanzia kwa AlhamduliLlaah. Nyenginezo ni Al-Faatihah (1), Al-An’aam (6), Al-Kahf (18), na Saba-a (34).