036-Yaasiyn: Utangulizi Wa Suwrah
036-Yaasiyn: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 83
Jina La Suwrah: Yaasiyn
Suwrah imeitwa Yaasiyn, na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (1) na herufi hizo ni ambazo zinajulikana kuwa ni Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah zinazotokea katika mwanzo wa baadhi ya Suwrah.
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kuthibitisha Risala na ufufuo, na dalili za vyote hivyo. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuithibitisha misingi mikubwa ya Dini, nayo ni Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) Rabb wa walimwengu, Risala ya Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), kuthibitisha kufa, kufufuliwa na kukusanywa, na malipo ya Jannah na moto.
3-Kubainisha Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) na Hikma Zake, Uwezo Usimamizi Wake kuendesha ulimwengu huu, ikitaja dalili nyingi tofauti katika kuhuisha ardhi baada ya kufa kwake, mfuatano wa mchana na usiku, mwendo wa sayari, mzunguko wa dunia, jua na mwezi, na mambo ambayo yamo Mikononi mwa Muumba Pekee (سبحانه وتعالى).
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzwa Qur-aan kuwa ni yenye hikma. Kisha imethibitishwa ukweli wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na kuthibitishwa kuwa Qur-aan ni Uteremsho Wake (Wahy).
2-Imetajwa hali za makafiri kutokukubali haki na kwamba wanaoikubali haki ni wenye kumkhofu Rabb wao kwa ghaibu.
3-Imetajwa kwamba kila jambo limeandikwa katika Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa na kwamba athari za mema na maovu yanaendelea kurekodiwa humo.
4-Imetajwa kisa watu wa kijiji, na yaliyotokea kati yao na Rusuli ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwatuma kwao.
5-Imebainishwa baadhi ya mambo yanayoonyesha Uwezo wa Allaah katika kuendesha ulimwengu na Neema Zake kwa Waja Wake.
6-Imetoa khabari za madai ya baatwil ya washirikina.
7-Imetajwa hali za watu watakapofufuliwa makaburini.
8-Imetajwa hali za Waumini watakapokuwa Jannah (Peponi) na watapata maamkizi ya Salaam kutoka kwa Rabb wao Mwenye Kurehemu. Kinyume chake ni wahalifu watakaoingizwa katika moto wa Jahannam ambao walimwabudu shaytwaan akawapoteza.
9-Imetajwa kuwa viungo vya mwanaadamu vitashuhudia matendo yao Siku ya Qiyaamah.
10-Imetajwa kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokana na kukanushwa na washirikina.
11-Imetajwa ukanushaji wa mmoja wa washirikina, aliyepiga mfano wa mifupa kuoza na kusagika, ya kwamba haiwezekani kufufuliwa, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akamradd kwa kuthibitisha wazi, Qudra Yake Adhimu na Uwezo Wake wa kuumba na kufufua.
12-Suwrah imekhitimishwa kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Kujithibitishia Mwenyewe Tawhiyd Yake ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola), na Kujitukuza Mwenyewe Allaah (عزّ وجلّ) na Kujitakasa (سبحانه وتعالى) kutokana na kila kosa na Akabainisha kwamba mambo yote yamo Mkononi Mwake na kwamba kwa Utukufu na Uwezo Wake, Anafanya Atakalo!