043-Az-Zukhruf: Utangulizi Wa Suwrah

 

043-Az-Zukhruf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 89

 

Jina La Suwrah: Az-Zukhruf

 

Suwrah imeitwa Az-Zukhruf (Mapambo ya Dhahabu), na inayodalilisha ni kutajwa neno hilo katika Aayah namba (35).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Tahadhari juu ya mtu kufitinishwa na mapambo ya uhai na dunia, ili yasiwe njia ya kuiendea shirki. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kusimamisha hoja za wazi za Tawhiyd ya Allaah (سبحانه وتعالى) ardhini na mbinguni na kubatilisha na kuradd (i) madai ya washirikina ya kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kumsingizia  kuwa Malaika ni mabinti Wake (iii) Visingizio vyao vya kuwafuata baba zao kwa upofu na kutoa mfano wa Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kwani baba yake alikuwa mshirikina lakini yeye alithibitisha Tawhiyd ya Allaah. (iv) Wanaodai kuwa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) ni mwana wa Allaah na kwamba yeye ni mojawapo wa alama za Qiyaamah.     

 

3-Kumliwaza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa maudhi aliyoyapata kutoka kwa washirikina na kubainisha kwamba mali zinazomfanya mtu kuwa mkubwa miongoni mwa watu hazimstahiki kuteremshiwa Qur-aan Tukufu.

 

4-Matahadharisho kuwa asiyeitafakari Qur-aan kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Atamwandalia shaytwaan awe rafiki mwandani kisha Siku ya Qiyaamah itakuwa ni majuto. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Amemwamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na Waumini kushikamana na Qur-aan kwani Qur-aan ni Tukufu mno na imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu ambayo ni lugha ya ufasaha kabisa.

 

5-Kuwabashiria Waumini neema za Jannah na kubainisha hali za makafiri na adhabu zao motoni.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzwa Qur-aan na kuwa imekuja kwa lugha ya Kiarabu ili watu wapate kuzingatia. (Ni maalumu kuwa lugha ya Kiarabu ni lugha pekee ya ufasaha, iliyo bayana kabisa hakuna mfano wake.) Na imethibitishwa kuwa Qur-aan iko katika daraja ya juu kabisa katika Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa). Rejea Al-Buruwj (85:22).       

 

2-Ameliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa yaliyomsibu kutoka kwa watu wake.

 

3-Imebainisha mambo yanayoonyesha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na  Neema Zake kwa Waja Wake. Miongoni mwazo ni vipando, na imetajwa duaa ya kipando iliyothibiti pia katika Sunnah. Rejea Aayah namba (13-14).

 

4-Imetaja baadhi ya uzushi wa washirikina na kauli zao ovu za kumpachika Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa Ana mabinti. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaradd kwa hoja nzito kuwa wao wenyewe hawakuwa wanapendelea watoto wa kike! Na kwa dhulma hii kubwa, watafika Kwake Siku ya Qiyaamah kuhesabiwa na kuadhibiwa! 

 

5-Imetajwa ada ya washirikina kukhiari kufuata nyendo za baba zao. Na hii ni ada ya watu wa nyumati za nyuma kusema hayo hayo.

 

6-Imetajwa sehemu ya da’wah ya Nabiy Ibraahiym  (عليه السلام) kwa watu wake na likathibiti neno la Tawhiyd (laa ilaaha illa Allaah) na kuendelea baada yake.

 

7-Imetajwa kuwa mapato ya dunia, anasa zake na mapambo kama fedha na Zukhruf (mapambo ya dhahabu), ni starehe ya muda mdogo tu, bali Aakhirah ndio bora kwa Waumini. 

 

8-Imetahadharishwa kuwa mwenye kujiweka mbali na Ukumbusho wa Allaah, shaytwaan humuandama mtu awe rafiki yake mwandani, kisha Siku ya Qiyaamah mtu huyo atajuta na kutamani shaytwaan awe mbali naye, umbali wa Mashariki na Magharibi. Kisha wote wataingia katika adhabu.

 

9-Imetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na dhulma ya Firawni kumwita mchawi, na kutakabari mno na kujifanya yeye ni bora kuliko Nabiy Muwsaa (عليه السّلام).

 

10-Ametajwa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام) na kwamba atakuwa ni miongoni mwa alama kubwa za Qiyaamah (atakaporudi duniani).

  

11-Watu wa Jannah wamebashiriwa mazuri, na zikatajwa baadhi ya raha na neema za Jannah. Kisha wakatajwa wahalifu kuwa watakuwa motoni na watamuomba Mlinzi wa moto awaombee kwa Allaah Awafishe kuliko kuadhibika lakini watabakishwa kudumu motoni!

 

12-Imebainishwa kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Muabudiwa wa haki mbinguni na ardhini. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akajitukuza Mwenyewe Mwenye Ufalme wa mbingu na ardhi, na kwamba viumbe wote watarudishwa Kwake.

 

13-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa washirikina kuwa  wanaowaomba badala ya Allaah, hawana uwezo wa kumiliki uombezi. Na kisha ikathibitisha kuwa washirikina waliamini Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola). Kisha akaliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na akaamrishwa awapuuze kwani karibuni watakuja kujua.

 

   

 

 

Share