044-Ad-Dukhaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

044-Ad-Dukhaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 59

 

Jina La Suwrah: Ad-Dukhaan

 

Suwrah imeitwa Ad-Dukhaan (Moshi), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (10).  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Vitisho kwa washirikina na kuwabainishia yanayowangojea ya adhabu kali duniani na Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2- Kuthibitisha kuteremshwa Qur-aan kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) katika Usiku Uliobarikiwa (Laylatul-Qadr).

 

3-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na kwamba Yeye Ndiye Mwenye kufufua na kuwakusanya waja.

 

4-Kubainisha Neema za Waumini Jannah na adhabu za makafiri motoni.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imesifiwa Qur-aan kwamba ni Kitabu kinachobainisha wazi kimatamshi na kimaana, na kwamba Qur-aan imeteremshwa Usiku wa Baraka ambao ni Laylatul-Qadr. Na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anawaonya watu kwa kile kinachowanufaisha na kuwadhuru, nako ni kule kuwapelekea Rusuli Wake Kuteremsha Vitabu, ili hoja ya Allaah (سبحانه وتعالى) iwasimamie Waja Wake. Na kwamba Usiku huo; Laylatul-Qadr, linaamuliwa na kupambanuliwa, kutoka kwenye Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Rejea Al-Buruwj (85:22), na kuletewa waandishi kati ya Malaika, kila jambo lililokadiriwa la muda wa kuishi na riziki katika mwaka huo na mambo mengine yatakayokuwa na kukadiriwa na Allaah (سبحانه وتعالى) mpaka mwisho wa mwaka, hayabadilishwi wala hayageuzwi.

 

2-Imetajwa Dukhaan (Jina la Suwrah), ni moshi utakaotoka ambao ni miongoni mwa alama kubwa Qiyaamah, na kwamba moshi huo utawafunika watu waovu iwe ni adhabu kwao na wataomba waondolewe adhabu. Lakini hawatondoshewa! 

 

3-Imetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) na Firawni aliyetakabari akazamishwa baharini na jeshi lake.

 

4-Imetajwa ada ya washirikina kutokuamini kufufuliwa .

 

5-Imetajwa vitisho na adhabu za makafiri ukiwemo mti wa zaqquwm ambao utakuwa ndio chakula chao nao ni kama masazo ya zebaki nyeusi iliyoyeyushwa, itokote matumboni mwao.

 

6-Kisha wametajwa Waumini wakiwa Jannah (Peponi) kwenye kila aina ya raha na neema; zikiwemo mabustani na chemchemu, wanapata humo wanachokitamani na wataozeshwa hurulaini, na kwamba hawataonja tena umauti. Na hiyo ni Fadhila ya Allaah na ndio kufuzu kukubwa.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kuambiwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba amewepesisha Qur-aan, na akaliwazwa kuwa angojee, yaani angojee ushindi wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Adhabu Yake kwa washirikina, na wao washirikina wanangojea kwa hamu kumshinda Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

 

 

 

Share