045-Al-Jaathiyah: Utangulizi Wa Suwrah
045-Al-Jaathiyah: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.
Idadi Za Aayah: 37
Jina La Suwrah: Al-Jaathiyah
Suwrah imeitwa Al-Jaathiyah (Kupiga magoti) na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (28).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Kubainisha hali za viumbe, kutokana na dalili za kisharia na kiulimwengu, na kuzitengua hoja za wenye kupinga ufufuo, wanaofanya kiburi kwa Allaah, na kuwatisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuthibitisha Utukufu wa Qur-aan na miujiza yake, na uthibitisho kuwa ni kutoka kwa Allaah, na kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah kwa Aayaat (Ishara, Dalili) za wazi..
3-Daawah (wito) wa Kiislamu na jinsi washirikina waliyopokea daawah hii kwa upinzani.
4-Bainisho kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwapa Wana wa Israaiyl hekima, Unabii na neema nyingi ili waweze kubeba Risala ya Tawhiyd, lakini hawakufaa kubeba Risala hiyo, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamchagua Nabiy Wake Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kubeba Risala kwa watu wote, na hili ni onyo kwa ummah wa Muhammad dhidi ya kufanya kama walivyofanya Wana wa Israaiyl.
5-Kuthibitisha ufufuo, na kuelezea baadhi ya hali zake (kufufuliwa), na kuelezea baadhi ya kauli za washirikina juu ya kufufuliwa.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzwa Qur-aan na imethibitishwa Aayaat (Ishara, Dalili,) za Allaah duniani kote.
2-Imetajwa adhabu kali iumizayo na inayodhalilisha kwa wazushi na waongo, kutokana na kung’ang’ania kwao ukafiri, na kuzifanyia istihzai Aayah za Allaah.
3-Imebainisha baadhi ya Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Waja Wake.
4-Imebainisha msimamo wa Bani Israaiyl baada ya kupewa neema za Allaah (سبحانه وتعالى) ambapo walikhalifu.
5-Imetajwa ada za washirikina kutokuamini kufufuliwa. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Amewabainishia kwamba halina shaka hilo!
6-Imetajwa kuwa kila ummah utapiga magoti kwa unyenyekevu na khofu. Na kila ummah utaitwa pamoja kitabu chao ambacho kimerikodi kila tendo. Na watu watahesabiwa na kulipwa matendo yao; mema na maovu.
7-Imerudi kutaja ada ya washirikina kutokuamini Qiyaamah, basi watasahauliwa motoni kama walivyosahau Siku hii kubwa mno ya kukutana na Allaah (سبحانه وتعالى), na watadumu humo motoni bila kuachiliwa kujitetea.
8-Suwrah imekhitimishwa kwa Kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى), Kumtukuza na kwamba Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.
Faida:
Maana ya Al-Jaathiyah ni kupiga magoti kwa unyenyekevu na khofu kwa kungojea kuhesabiwa.