099-Az-Zalzalah: Utangulizi Wa Suwrah
099-Az-Zalzalah: Utangulizi Wa Suwrah
Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.
Idadi Za Aayah: 8
Jina La Suwrah: Az-Zalzalah
Suwrah imeitwa Az-Zalzalah (Zilizali: Tetemeko La Ardhi), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).
Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:
1-Ukumbusho wa hali ya Siku ya Qiyaamah, na kuhesabiwa matendo ya waja kwa umakini Siku hiyo. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]
2-Kuthibitisha kufufuliwa na yatakayotokea Siku ya Qiyaamah, na kulipwa matendo katika kheri au shari.
Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:
1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa yatakayotokea Siku ya Qiyaamah; Zilzala ambayo itatikisa mno ardhi hadi kila kilichokuweko juu yake kibomoke, kama milima, majumba, na watu kutolewa makaburini. Kisha binaadam atashangaa na kuulizwa: “Kumezuka nini?” Na Siku hiyo ardhi itatoa habari ya mambo yote iliyotendwa juu yake; mazuri na mabaya, kwani ardhi ni katika vitakavyoshuhudia matendo ya waja Siku hiyo tukufu.
2-Ikakhitimishwa Suwrah kwa kuthibitishwa kwamba kila mtu atalipwa kulingana na matendo yake aliyoyatenda duniani, matendo ya kheri au shari, hata yawe madogo kiasi cha uzito wa sisimizi au atomi, binaadam atayaona katika daftari lake la hesabu, na atalipwa malipo yake mema au maovu, na wala Allaah (سبحانه وتعالى) Hatomdhulumu mtu kwa chochote, hata kwa chembe ya hardali au atomi.