098-Al-Bayyinah: Utangulizi Wa Suwrah

 

098-Al-Bayyinah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.

 

Idadi Za Aayah: 8

 

Jina La Suwrah: Al-Bayyinah

 

Suwrah imeitwa Al-Bayyinah (Hoja Bayana), na yanayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Faida, na pia kutajwa kwake katika Aayah namba (1). 

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha ukamilifu wa Risala ya Muhammad Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na ule uwazi wake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwakemea washirikina na watu waliopewa Kitabu juu ya kuikadhibisha kwao Qur-aan na kumpinga Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na kubainisha marejeo yao na marejeo ya Waumini.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuwalaumu watu waliopewa Kitabu ambao ni Mayahudi na Manaswara na pia kuwalamu washirikina wa aina zote katika nyumati, kwamba, hawakuwa wenye kuacha ukafiri wao mpaka iwajie hoja walioahidiwa katika Vitabu vilivyopita. Yaani wangeendelea na kuendelea katika upotevu wao, na kupita kwa zama ungewaongezea tu ukafiri wao mpaka iwafikie hoja na ushahidi wa wazi. Na ushahidi huo ni kutumiwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) akawasomea Qur-aan iliyo kwenye kurasa zilizotakasika, haziguswi isipokuwa kwa waliokuwa katika twahara. Na kwamba ndani ya Qur-aan, khabari za kweli na amri za uadilifu zenye kuongoza kwenye haki na njia iliyonyooka. Na pia hawakufarikiana wale waliopewa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Manaswara, juu ya kuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)  ni Rasuli wa kweli, kwa sifa zake walizokuwa wakiziona katika vitabu vyao, isipokuwa baada ya kuwathibitikia kuwa yeye ndiye Nabiy waliyoahidiwa katika Tawraat na Injiyl. Walikuwa wanakubali kwa umoja wao, kuwa Unabii wake ni wa kweli. Lakini alipotumwa, waliukanusha na wakatofautiana.

 

2-Imetajwa kukinzana (kutofautiana) hali zao, na kubainisha kwa ukafiri wao ulikua ni kwa sababu ya kupinga kwao na jeuri yao na husda yao kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Ilhali hawakuamrishwa katika sharia zao zilizopita isipokuwa, wamwabudu Allaah Pekee na kumtakasia ibaada kwa kuepukana na ushirikina na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah na waifanye Dini iliyonyooka. Na hiyo ndio Tawhiyd na ikhlaasw katika Dini, na ndio Dini iliyonyooka ya Kiislamu. Ikabainishwa kwamba hao washirikina, na Mayahudi na Manaswara, hatima yao ni kuingizwa moto wa Jahannam wadumu, na wao ni viumbe waovu kabisa.

 

3-Suwrah ikakhitimishwa kwa kuwabashiriwa Waumini watendao mema, kwamba wao ni viumbe bora kabisa, na Rabb wao Atawaingiza Peponi kuwa ni jazaa yao, wadumu humo milele, Allaah Awaridhie nao pia wamridhie Allaah. Na hii ndio fadhila ya mwenye kumkhofu Rabb wake.

 

Faida:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Amemumarisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amsomee ‘Ubayy Bin Ka’ab (رضي الله عنه) Suwrah hii ya Al-Bayyinah:

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم لأُبَىٍّ ‏"‏ إِنَّ اللَّهَ أَمَرَنِي أَنْ أَقْرَأَ عَلَيْكَ  ‏لَمْ يَكُنِ الَّذِينَ كَفَرُوا ‏‏ قَالَ وَسَمَّانِي قَالَ ‏"‏ نَعَمْ ‏"‏ فَبَكَى‏.‏

 

Amesimulia Anas Bin Maalik (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwambia ‘Ubayy Bin Ka’ab (رضي الله عنه): “Allaah Ameniamrisha nikusomee:

 

لَمْ يَكُنِ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ مُنفَكِّينَ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ الْبَيِّنَةُ ﴿١﴾

“Hawakuwa wale waliokufuru.” [Al-Bayyinah (98)]

 

Basi ‘Ubayy (رضي الله عنه) akauliza: Allaah Ametaja jina langu? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Akajibu: “Naam.” Ubay Bin Ka’ab akalia. [Al-Bukhaariy, Muslim, na wengineo]

 

 

Share