Uadilifu

 

Tabia Njema: Uadilifu

 

 

Alhidaaya.com

  

 

Alhamdu Lillaahi Rabil'aalamiyn) Allaahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Swallayta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym wa Baarik 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad kamaa Baarakta 'alaa Ibraahiym wa 'alaa aali Ibraahiym fil'aalamyna Innaka Hamiydun Majiyd.

 

Ndugu zangu Waislam Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema katika Qur-aan.

 

 إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ﴿٩٠﴾

Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na ihsaan na kuwapa (msaada) jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na munkari na ukandamizaji. Anakuwaidhini ili huenda mkapata kukumbuka. [An - Nahl: 90]

 

 

I. Nini Maana Ya Uadilifu?

 

Kilugha: 

a.       Hali ya kitu kuwa sawa kama inavyopasa kiwe. 

b.       Kuhukumu kwa haki bila ya upendeleo.

 

Kisharia:

a.        Kukipa kila kitu haki yake inayostahiki.

b.        Kuipa nafsi yako yale yaliyo ya haki tu.

c.     Ni hali ya kuwa katikati baina ya kuchupa mipaka katika kufanya jambo au kujizuia kufanya jambo hilo bila ya kumdhulumu mwengine.

 

 

II. Hukumu Ya Uadilifu

 

Hukumu yake ni wajibu na ni fardhi kwa kila mtu - Muislamu au asiye Muislamu.

Kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anavyosema katika Suwrah An –Nahl: 90 iliyotajwa hapo juu.

 

Uadilifu ikiwa wa kauli, vitendo, ikiwa katika mahusiano ya mtu wa karibu au wa mbali ikiwa kwa rafiki au kwa adui ikiwa kwa kiongozi au waongozwaji n.k ni WAJIBU kwa kila muislamu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٩﴾

Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na timizeni haki. Hakika Allaah Anapenda wanaotimiza haki. [Al-Hujuraat: 9]

 

 

III. Hadiyth Za Nabiy Zenye Kuhimiza Uadilifu.

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Watu saba watakuwa katika kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) siku ambayo itakuwa haina kivuli isipokuwa cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) 1. Imamu Muadilifu. 2. Kijana aliyekulia katika Ibada, 3. Mtu ambaye moyo wake umefungamana na miskiti…) [Imewafikiwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

Kutokana na Abdillaah ibn ’Amr Ibnil ‘Aas (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Hakika waadilifu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) watakuwa katika Minbar za nuru: Ambao wanafanya uadilifu katika hukumu zao na watu wao na mambo mengine) [Imepokelewa na Muslim].

 

Kutoka kwa Iyaadhw Ibn Haamir (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Watu wa Jannah ni watatu: Mwenye ufalme ambaye muadilifu aliyeridhiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na mtu ambaye ana huruma mpole kwa jamaa wa karibu na Waislamu, na anayejizuilia kuomba na aliyefika mbali katika kujizuilia) [Imepokelewa na Muslim]

 

 

IV. Fadhila Za Uadilifu

 

Malipo mema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

1.      Waadilifu watapewa viriri/minbari za nuru na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

2.      Watakuwa chini ya kivuli cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) siku ambayo hapatakuwa na kivuli chochote isipokuwa Chake Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Fadhila za Uadilifu ndani ya Jamii

1.      Kuondoka kwa aina zote za dhulma.

2.      Kuenea utulivu wa nafsi na Jamii.

3.      Kuwa na heshima upendo na kuaminiana mfano:

         a.       Baina ya mke na mume

         b.       Baina ya mtoto au mzee

         c.       Katika uchaguzi n.k

 4.  Kuondoa rushwa katika Jamii

 5.  Kuondosha choyo, uhasidi, wivu na ujambazi

 

 

V. Nyanja Za Uadilifu Ndani Ya Jamii

 

Uislamu ndio uliokuja na uadilifu na umetilia hima utekelezwe katika nyanja zote za maisha ya mwanaadamu kama vile:

 

1        Nyanja za maneno na vitendo

2        Nyanja zote za mahusiano: Jamaa au si jamaa, rafiki au adui.

3        Katika kuhukumu (Jaji, Qaadhi, Sheha, Polisi n.k)

4        Uadilifu katika vipimo.

  

1.         Uadilifu katika maneno

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema katika Qur-aan

          

وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿١٥٢﴾

Na mnaposema basi fanyeni uadilifu japokuwa ni jamaa wa karibu. Na timizeni ahadi ya Allaah. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kukumbuka. [Al- An'aam: 152]

 

2.      Uadilifu katika kuandika

وَلْيَكْتُب بَّيْنَكُمْ كَاتِبٌ بِالْعَدْلِ ۚ

Na aandike baina yenu mwandishi kwa uadilifu. [Al-Baqarah: 282]

                        

3.      Uadilifu katika Vipimo; Mizani, ujazo, mita

وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ 

Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu. [Al-An'aam :152]

 

4.      Malipo siku ya kiama yatakua ya uadilifu (Hakuna dhulma)

 

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ ﴿٤٧﴾

Na Tutaweka mizani za uadilifu Siku ya Qiyaamah; basi nafsi haitodhulumiwa kitu chochote. Na japo ikiwa uzito wa mbegu ya haradali, Tutaileta. Na inatosheleza Kwetu kuwa Wenye kuhesabu. [Al-Anbiyaa: 47]

 

 

VI. Faida Za Uadilifu

 

a.     Muadilifu atakuwa katika amani duniani na akhera (atapendwa)

 

b.     Daima atakua anajimilki na hamilikiwi na wengine

 

c.     Ataridhiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na viumbe pia

 

d.     Viumbe wataepukana na shari zake

 

e.     Ni sababu ya kupata cheo, mafanikio na maendeleo ya mtu

 

f.     Ni njia ya kufanikiwa kimaisha

 

g.    Sababu ya kupata utulivu na amani katika Jamii ya Waislamu

 

h.   

Inaondosha fitna katika jamii

 

 

VII. Hasara Za Kuacha Uadilifu Katika Jamii

 

a)   

Ni jambo rahisi sana kubomoa mfumo na uongozi

 

b)   

Ni mbolea ya kukuza udikteta na ukandamizaji katika Jamii

 

c)    Ni ufisadi mwepesi wa kufisidi dhamira na nafasi za wana Jamii

 

d)  Ni chanzo kikubwa cha machafuko ya Jamii (hasa pale dhuluma inapogeuka na kuwa ubaguzi wa wazi

 

e)   

Kutakuwepo matabaka na uadui katika Jamii

 

f)    

Chanzo cha maovu.

 

 

VIII. Aina Za Uadilifu

 

1.   Uadilifu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

Kutomshirikisha na yeyote katika ibada na sifa zake kwa: 

 

a.     Kumtii bila kumuasi kwa lolote.

b.     Kumtaja na kumdhiriki katika hali zote

c.     Kumshukuru bila kukosa

 

2.      Uadilifu wa Mtu Katika Nafsi Yake

 

a.     Ni kuilazimisha nafsi kufanya mema na kuacha mabaya kwake na kwa Jamii.

b.    Aifanye nafsi iwe na uwiano katika matendo yake. Asichupe mipaka katika kufanya jambo wala asizembee. Akifanya hayo atakuwa anaidhulumu nafsi. Na anayeidhulumu nafsi yake atakuwa anadhulumu wenzake.

 

3.   Uadilifu Wa Mtu Kwa Binaadamu Wenzake

 

a.     Kuwapendelea kheri anazozipendelea nafsi yake

b.     Kuthamini utu wao mali na heshima zao

c.     Kujiepusha na kuwaudhi na kuwafanyia maovu.

 

4.   Uadilifu Kwa Walio Sawa Na Yeye

 

a.     Kutowatendea wasiyoyataka.

b.     Kuwaepusha na maudhi

c.     Mambo yote hayo yanapelekea mapenzi baina yao.

d.    Yasipotekelezwa patatokea ufisadi ambao hautokei isipokuwa pahala pasipokuwa na uadilifu

 

5.   Uadilifu Kwa Walio Chini Yake.

      Kiongozi kwa wanaoongozwa.

 

a.     Kuwepesisha mambo

b.     Kuondosha shida

c.     Kutotumia maguvu

d.     Kutetea haki na usawa, kutodhulumu na kuwa muadilifu.

 

6.   Uadilifu Kwa Walio Juu Yake. Raia kwa viongozi       

  

a.     Kutii viongozi utiifu wa kweli

b.     Kuulinda uongozi

c.     Ufuasi wa uhakika wa kutumia akili.

 

7.   Uadilifu Kwa Viumbe Wengine Wa Mazingira

 

1.    

Kuwaonea huruma wanyama na viumbe wengine.

2.    

Kuwatumia kwa mujibu ya maamrisho ya Allaah

3.    

Kuwapa wanyama haki zao na yeye kunufaika na wanyama kwa mujibu wa sharia.

 

 

IX. Misingi Muhimu Inayojenga Na Kudumisha Uadilifu Katika Jamii

 

1.     

Uadilifu wa viongozi

 

Kiongozi ni mtu mwanzo anayepaswa kuwa muadilifu kwani yeye ni kigezo, na atakapotengenea kiongozi katika kuondoa maovu mfano. (dhulma, rushwa, zinaa, n.k) basi Jamii yote itatengenea.

 

Mfano wa viongozi waliofanikiwa katika kutekeleza uadilifu ni Sayyidna ‘Umar Ibnu-Khatwaab na ‘Umar Ibn ‘Abdul-‘Aziyz.

 

2.   Msingi wa usawa kwa wote

   Usawa ndiyo lengo linalokusudiwa na Uadilifu

 

       Suwraah/Aina za Usawa katika Uislamu:

 

-     Usawa wa mwanamke na mwanamume katika kutekeleza wajibu wa kisharia na malipo

-     Usawa baina ya binaadamu wote katika Jamii

-     Usawa baina ya watoto (kama katika kuwapa zawadi n.k).

-     Usawa wa wanaoshitakiana katika mahkama/korti.

-     Usawa katika kulindwa damu, mali na familia za kila Mmoja.

-     Usawa katika utekelezwaji wa hukumu na kuhukumiwa.

-     Usawa katika kupata malipo ya duniani na thawabu za Akhiraah kwa kila afanyae wema.

 

3. Uadilifu kwa wana Jamii wote.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Muogopeni Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu)

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۚ

Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi mmoja tu au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. [An-Nisaa: 3].

 

4.   Kupinga aina zote za dhulma.

      Dhulma ndiyo kinyume cha uadilifu malipo yake ni mabaya mno

 Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ ﴿٧١﴾

Na madhalimu hawana yeyote mwenye kunusuru. [Al-Hajj: 71]

 

Na Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

أَلَا لَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ﴿١٨﴾

Tanabahi! Laana ya Allaah iko juu ya waliodhulumu. [Huwd: 18]      

 

Na mwisho ndugu zangu Waislamu naiusia nafsi yangu pamoja na nyinyi kufanya uadilifu na kuepukana na dhulma kwani:

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Iogope du’aa ya mwenye kudhulumiwa, hakika hiyo (du’aa ya mwenye kudhulumiwa) haina baina yake na baina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kizuizi).”

 

Na pia akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) “Iogopeni dhulma, hakika dhulma ni giza siku ya Qiyaama.”

 

 

Wa BiLLaahi At-Tawfiyq

 

Share