Husnul Khuluq (Tabia Njema)

 

 

Husnul Khuluq (Tabia Njema)

 

Imekusanywa na: Ummu Faraj

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Sifa njema zote Anastahiki Allaah Rabb wa viumbe wote na rehma na amani zimfikie Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Jamaa na Swahaba zake wote.

 

 

Hivi unajua ndugu yangu Muislam, Allaah Akulinde na Akuhifadhi, kwamba 'amali iliyo bora zaidi na inayopendwa na Allaah Mtukufu na Rasuli wake ni tabia njema?

 

Katika Hadiyth sahihi: Kutoka kwa Sa'ad bin Abiy Waqqaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika Allaah Anapenda tabia njema na Anachukia tabia mbaya"

 

 

Na tabia njema tumefahamishwa kuwa ni ukunjufu wa uso kutenda wema  na kujizuia na maovu." 

 

    

Hakika sisi Waislam wa zama hizi tumo katika tatizo kubwa la tabia, tabia za Kiislam ambazo watu wengi wa kheri wamezikosa, na zimekua kwa baadhi yao ni kama mazungumzo ya kawaida na wala hazihitaji kutekelezwa.

 

 

Tabia njema zinauweka Uislam kwenye daraja ya juu kabisa. Je, Hujui kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kwa hakika nimeletwa ili nikamilishe tabia njema" kulingana na maneno haya inaonyesha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekusanya umuhimu wote alIokuja nao kwa jambo la tabia njema na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamsifu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Qur-aan Tukufu: Amesema:

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ﴿٤﴾

Na hakika wewe uko juu ya kiwango adhimu cha tabia njema. [Qur-aaan Al-Qalaam:4]

 

 

Kwa hakika yamethibiti mambo matukufu makubwa kutokana na tabia njema, baadhi ya mambo hayo ni:

 

 

1- Wema haupatikani ila kwa tabia njema, kasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika hadithi ilyopokelewa na Nawwaas bin Sam'aan (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Wema ni tabia njema na dhambi "uovu" Ni ile iliyojificha kwenye moyo (inakutia wahka) ukachukia watu wajue. [Imepokelewa na Muslim]

 

 

2- Na tabia njema ni 'amali itakayo mpelekea mtu kuingia peponi kwa wingi kama aliyvosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) Amesema: Na aliulizwa ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema: "Kumcha Allaah na tabia njema" Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema "kinywa (mdomo) na utupu. [Imepokelewa na At-Tirmidhiy na akasema Hadiyth nzuri na sahihi]

 

 

3- Tabia njema ni katika 'amali nzito atakayoikuta Muislam katika miradi ya matendo yake siku ya Qiyaama.

 

 

Katika Hadiyth iliyopokelewa na Abu Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu), Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: "Hakuna kitu kizito katika mizani ya Muumin siku ya Qiyaama kuliko tabia njema. Hakika Allaah Humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya." [Imepokelewa na At-Tirmidhiy, na ni Hadiyth Hasan]

 

 

4- Mwenye kujipamba na kusifika na tabia njema  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemdhamini nyumba katika jannah ya juu kabisa. Kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mimi ni mdhamini wa nyumba "iliyopo" katikati ya Jannah kwa yule mwenye kuacha mijadala (ubishani) japo akiwa ana haki, Na nitakua mdhamini wa nyumba katika Jannah ya juu kwa mwenye Tabia njema."

 

 

5- Imepokelewa kutoka kwa mama wa waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) akisema, nimemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakika Muumin hupata kwa tabia yake njema daraja za aliyefunga na anayesimama usiku kufanya ibada."

 

 

6- Katika Hadiyth waliyoafikiana ma-Imaam Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa 'Abdullaah bin Amru bnil-'Aaswi (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesema, alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema "Hakika aliye bora kati yenu ni yule mwenye tabia njema"

 

 

Hakika mwenye tabia mbaya ni mwenye kuzungumza maneno mabaya na vilevile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Hakika Allaah Huwarehemu waja wake wenye huruma, basi wahurumieni walio katika ardhi na Atawahurumia aliye mbinguni"

 

 

Hivyo basi, tabia njema inafuatana na kuhurumiana na Iymaan iliyokamilika.

 

 

Mwenye kuangalia hali ya hivi sasa utakuta ni mtihani kwetu na mbele ya Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa), utaona mambo ya ajabu, utaona uongo badala ya ukweli, utaona nguvu zikitumika badala ya upole, utaona khiyana badala ya uaminifu, utaona ghadhabu badala ya subira na kuondosha ghadhabu na kusameheana baina ya watu, utaona maudhi badala ya hisani, utaona ubakhili badala ya ukarimu, utaona uchoyo katika kuchukua sehemu ya kukaa au kufanya ibada, au katika vinywaji au chakula, badala ya kuathirika na kuwatanguliza wengine kabla yake, utaona kiburi badala ya unyenyekevu, kisha mtu atajiuliza katika nafsi yake hivi hawa ni Waislam kweli? Uko wapi uchaji Allaah? Iko wapi Iymaan? Kuko wapi kuoneana hayaa? Iko wapi huruma kwa maskini, yako wapi mapenzi na huruma  kati ya Waislam???

 

 

Je, tuwafanye nini watu hawa? Tuwalipe uovu kwa uovu tukawaadhibu hapo hapo? Tukifanya hivyo hatutowazuia kitu, bali tutakuwa tumeshirikiana nao katika kueneza tabia mbaya. Lililo wajibu kwetu mimi na wewe juu ya watu hawa ni kufuata muongozo wa Allaah Mtukufu, nao ni; kuwasamehe na kufuta kabisa nyoyoni mwetu yale wanayotufanyia, na kubadilisha baya kwa kutenda jema na Allaah Mtukufu Anasema:

 

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾ 

 

Na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Al-'Imraan: 134]

 

Na Akasema tena Allaah Mtukufu kuwasifu waumini:

 

وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٢﴾

 

Na wanaepusha ovu kwa zuri, hao watapata khatima njema ya makazi ya Aakhirah. [Ar-Ra'd: 22]

 

Na Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ﴿٣٤﴾

Na wala haulingani sawa wema na uovu. Lipiza (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi; tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani.

[Fusw-swilat: 34]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: katika Hadiyth iliyopokewa na Abu Dharr Jundub bin Junaadah na Abu Abdur-Rahmaan Mu'aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhum) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kasema " Muogope Allaah popote ulipo, na lifutishe ovu (baya) kwa jema, na tangamana na watu kwa tabia zilizo njema

 

 

Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

 

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ

"Hakika mema yanaondosha maovu". [Huwd: 114]

 

 

Pamoja na hayo yote Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakulipiza kisasi kwa maudhi aliyofanyiwa yeye binafsi, ila yatakapovunjwa maamrisho ya Allaah au makatazo (maharamisho) Basi huadhibu kwa ajili ya Allaah.

 

 

Allah Atuwafiqishe Kwa Anayoyapenda Na Kuyaridhia Na Ajaalie Tuwe Wenye Kuyafanya Yalio Mema. Aamiin.
 
 
 
Wa Allahu A'lam

 

Share