Zingatio: Dunia Imejaa Ghururi

 

 

 

Naaswir Haamid

 

Hakika dunia imejaa ghururi, basi yasikudanganyeni maisha ya dunia wala asikudanganyeni yule mdanganyi mkubwa (Ibilisi) katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu. Dunia itupeni mbali kama vile Mwenyezi Mungu Alivyotutaka na itafuteni akhera yenu, kwani Mwenyezi Mungu Ameipigia mfano dunia[1].

 

"Na wapigie mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tunayoyateremsha kutoka mawinguni; kisha huchanganyika nayo mimea ya ardhi kisha ikawa majani makavu yaliyokatikakatika ambayo upepo huyarusha huku na huko. Na Mwenyezi Mungu Ana uweza juu ya kila kitu.

 

"Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vitendo vizuri vibakiavyo ndivyo bora mbele ya Mola wako kwa malipo na tumaini bora (kuliko hayo mali na watoto)". Al Kahf - 45 – 46

 

Nakuusieni waja wa Allaah kumuogopa Allaah, kwani Taqwa ni jambo bora la kunasihiana baina ya waja wa Allaah, na ndiyo amali Anayoridhika nayo Mwenyezi Mungu kutoka kwa waja wake.

 

Mumeamrishwa kumcha Mungu na kwa ajili ya wema mumeumbwa, kwa hivyo ogopeni yale Allaah Aliyokutahadharisheni nayo, kwa sababu Amekutahadharisheni na adhabu kali kabisa.

 

Muogopeni Mwenyezi Mungu kuogopa kwa kweli na tendeni matendo yenu bila ya kujionesha kwa watu wala kutaka sifa au umaarufu, kwani mwenye kufanya amali yoyote ile kwa ajili ya kujipendekeza kwa mwengine asiyekuwa Allaah, basi Mwenyezi Mungu Humsukumiza nazo amali zake kwa huyo aliyemfanyia amali hiyo.

 

Ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu Hajakuumbeni kwa upuuzi, na wala Hakuacha chochote kiende ovyo. Keshataja athari zenu na Keshajua siri zenu na kuzihesabu amali zenu na kuziandika ajali zenu. Kwa hivyo dunia isikubabaisheni kwani inawaghururisha watu wake, na ameghurika yule atakayebabaishwa nayo.

 

Na jueni ya kuwa Akhera ndiyo makazi ya milele.[2]

 [1]  Khotuba ya Sayyidna ‘Uthmaan bin ‘Affaan aliposhika madaraka.

 

[2]  Khotuba ya Sayyidna ‘Aliy bin Abi Twaalib aliposhika madaraka

 

 

 

 

 

 

 

 

x

 

Share