Mume Wangu Aliyesilimu Hataki Nivae Hijaab

 

Mume Wangu Aliyesilimu Hataki Nivae Hijaab

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam Aleykum

 

Jamani ndugu zangu waislam nina swali, mimi nimeolewa na mume wangu alikuwa ni mkristo lakini kabadili dini kabla ya kunioa, sasa mie naona kama hapendi mie nivae hijab. (kabla ya kunioa nilikuwa sivai)sasa naomba mnipe ushaurii. nimuulize na akisema ndio hapendi niseme nini? ama nichukue uamuzi gani? nilisha mweleza nini umuhimu wa kuvaa hijab.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika ni kuwa lipo tatizo kubwa linalopatikana kwa wanaosilimu wanaume na wanawake kisha wakaoa au kuolewa kabla ya kufundishwa Dini ya Uislamu. Hawa mara nyingi hasa wanaume huwa wanasilimu kwa ajili ya kuoa kwani Muislamu mwanamke hafai kabisa kuolewa na kafiri yeyote yule. Zipo kesi nyingi za wanaume kurudi katika Dini zao za asili pindi wanapopata walitakalo.

 

 

Hili ni kosa ambalo linafanywa na wazazi na mabinti wenyewe. Uislamu umeweka sifa kwa binti kutazama kwa anayemuoa kabla ya kuolewa kwenyewe. Sifa hizi ni Dini na maadili mema kwa mwanamume. Kule kusilimishwa mwanamme na pengine wakati huo huo kuozeshwa huwa kweli tumepata kumjua? Baada ya hapo hutokea matatizo kwani ima mwanamme huwa hataki kushika Dini au kuritadi.

 

 

Tatizo ulilokuwa nalo dada yetu hapo awali ni kuwa hukuwa umeshika Dini, hivyo kutokuwa na mwelekeo sahihi wa Dini ya kuchagua mume. Maisha ya unyumba mwanzoni ni muhimu sana kwani huenda ukamuathiri kwa uzuri au ubaya. Mume alikuona ukiwa katika hali ya kutovaa hijabu jambo ambalo linamshangaza anapokuona mara kwa ghafla umeanza kujifunika. Lau kama angekuwa amepata mafunzo ya Uislamu, hilo angekuwa ni mwenye kulifahamu kwa urahisi. Hakika wewe ndiye unayeweza kutueleza kuhusu jinsi alivyoshika Dini. Je, anafanya ‘Ibaadah? Je, Uislamu wake uko imara au vipi?

 

 

Kabla hatujaingia katika kiini cha swali lako na kukupatia nasaha tungependa kukueleza uwajibu wa hijabu kama alivyoeleza Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema: 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ 

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. [Al-Ahzaab: 59].

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewausia na kuwahimiza wanawake wawe ni wenye kuvaa hijabu kwa kuisitiri miili yao yote. Na ameonya vikali kuwa mwanamke aliyevaa nguo lakini yupo uchi hatasikia hata harufu ya Pepo.

 

 

Ni muhimu sisi kufahamu kuwa ni lazima kwetu sisi kufuata maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kutofuata maagizo yao na kuwaasi ni kujiingiza katika janga na balaa hapa duniani na kesho Akhera. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:  

 

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾

Na yeyote atakayemuasi Allaah na Rasuli Wake na akataadi mipaka Yake Atamuingiza motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kudhalilisha. [An-Nisaa: 14].

 

 

Na mwenye kuwatii zawadi yake ni kubwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:  

 

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٣﴾

Na yeyote atakayemtii Allaah na Rasuli Wake Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, watadumu humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa. [An-Nisaa: 13]. 

 

 

Tuelewe kuwa hatuna hiyari katika maagizo tunayoamriwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:  

 

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36)]

 

 

Utiifu usio na masharti ni kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) peke Yake na ndiyo kwa ajili hiyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Usimtii mtu asiyemtii Allaah" (Ahmad).

 

Amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Asitiiwe yeyote katika kumuasi Allaah" [Ahmad].

 

Na tena: "Utii ni wajibu tu katika yaliyo mazuri na halali" [Al-Bukhaariy].

 

 

Hivyo katika Aayah na Hadiyth zilizopo juu utiifu wa moja kwa moja ni kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Pindi anapokuamuru yeyote awaye kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi hufai kumtii kabisa.

 

 

Nasiha ambazo tunaweza kukupa ni kuwa unafaa usimame kwa msimamo wa sawa na haki wala usimtii mumeo wala mwingine yeyote katika kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa). Awali ya yote mueleze mumeo kwa njia nzuri na ya hekima kuwa hijabu ni vazi la Kiislamu wala sio vazi la utamaduni wa Kiarabu kwa wanawake wote wanaojiita ni Waislamu. Kutovaa kwako hapo awali ilikuwa ni kosa kwa upande wako na hivyo huwezi kabisa kuishi na kosa hilo daima. Kwa ajili hiyo, mwanamke mwenye chembe ya Imani hafai kutoka nje ya nyumba yake bila kulivaa. Ikiwa atafahamu na kukukubalia itakuwa kheri kwenu na lau hatakubali basi itabidi uendelee na kuvaa hijabu wala usifuate atakavyo mumeo. Amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) inatakiwa uziweke juu na mbele ya zile za mumeo.

 

 

Usijali kuambiwa kuwa hufai au umepitiwa na wakati kwani zaidi ya hayo na maneno ya matusi wameambiwa waliokuwa bora yetu maradufu. Kanuni yetu kuu ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala tusijali maneno ya watu. Kama ni hivyo basi inafaa kwetu sisi kuwa makafiri kwani wao wanatuona sisi tuko nyuma na bado tuko katika ujinga, lakini tukifanya hivyo kwa kufuata walio wengi basi tutakuwa tumeangamia. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:  

 

وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴿١٠٦﴾

Na wengi kati yao hawamwamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki [Yuwsuf: 106].

 

 

Uelewe kuwa lawama itaendelea kuwepo hata ukiwa mzuri namna gani. Kwa hiyo, Muumini haogopi kulaumiwa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Ametutanabahisha pale Aliposema: 

..وَلَا يَخَافُونَ لَوْمَةَ لَائِمٍ ۚ

Wala hawakhofu lawama za mwenye kulaumu. [Al-Maaidah: 54].

 

 

Kuwa na msimamo huo ni uthibitisho kuwa wewe uko imara na Imani yako imeiva.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Akusahilishie mambo yako na Amnyooshe mumeo katika muelekeo ulio mzuri.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share