Sha'baan: Kufunga (Swawm), Kukutanika Usiku Wa Niswf Sha’baan, Kufanya Kisomo Inajuzu?

 

Kufunga (Swawm) Na Kukutanika Usiku Wa Niswf Sha’baan Na Kufanya Kisomo Inajuzu?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:   

 

Assalaamu 'alaykum

 

Naomba tafadhali tujulisheni kama inafaa kufunga siku hiyo ya nusu Shaabani peke yake na kufanya ibada hasa kwa sababu huku  tuliko jamaa wanaalikana kusoma kisomo hasa siku hiyo kwa kusoma Yasin  kisha wanaomba duaa mfano mtu aongezewa umri wake au pato lake. Mimi nimewajibu kuwa ni uzushi lakini wao wanakataa na wameshaalikana kufanya hicho kusoma. 

 

 

Tujulisheni kama ni jambo la sahihi au ni uzushi tupate kuwapa dalili labda watasikia.

 

 

Wa billahi tawfiyq.

 

 

JIBU:  

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

 

Hakuna dalili yoyote tuliyopata kwamba siku hiyo inapaswa kufunga pekee, au usiku huo unafaa kuupwekesha kwa ajili ya ‘ibaadah fulani; si Qiyaamul-layl (kisimamo cha usiku kuswali) wala kukusanyika watu kusoma du'aa fulani.

 

 

Swawm Siku Ya Niswfus-Sha'baan (Katikati Ya Sha’baan)

 

Hakuna ubaya kufunga siku nyingi mtu awezavyo katika mwezi wa Sha’baan kwani kufanya hivyo ni Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyopata mafunzo katika Hadiyth nyingi mbali mbali, tunanukuu mbili zifuatazo:

 

عن عائشة رضي الله عنها قالت: "كان رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم  يصوم حتى نقول لا يفطر، ويفطر حتى نقول لا يصوم، وما رأيت رسول الله استكمل صيام شهر إلا رمضان وما رأيته أكثر صياماً منه في شعبان" رواه البخاري ومسلم

 

Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ambaye amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha swiyaam hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Rasuli wa Allaah akifunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhwaan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyofunga katika Sha’baan.))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Kukithirisha kwake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘ibaadah katika mwezi huu wa Sha'baan, ni kutokana na maelezo yake mwenyewe alipoulizwa na Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu 'anhu) sababu ya kufunga sana katika mwezi huu alijibu:

 

[Sha'baan] Ni mwezi ambao watu hawautilii sana maanani, ulio kati (ya miezi miwili mitakatifu) Rajab na Ramadhwaan, na ni mwezi ambao matendo yanapandishwa kwa Rabb wa ulimwengu. Nami napenda matendo yangu yapandishwe na hali nikiwa katika Swawm [An Nasaaiy, at-Targhiyb wat-Tarhiyb, uk. 425.]

 

 

Kuhusu ‘ibaadah maalumu au du'aa mahsusi ya usiku huo:

Uzushi huo umesambaa na kujulikana kuwa usiku huo ni usiku ambao mambo yafuatayo yanakadiriwa kwa mwanaadamu ya mwaka mzima, yaani tokea Niswfus-Sha’baan ya mwaka huu hadi Niswfus-Sha'aban nyingine. Nayo ni; rizki yake, majaaliwa yake (ya kheri na shari) na uhai wake (yaani kama atakuwa miongoni mwa watakaaga dunia).

 

 

Haya yametokana na mapokezi yasiyo sahihi 'mawdhwuw', yaani yalizozushwa na yanayojulikana kuwa ni batili au dhaifu sana zilizotaja mas-ala kama hayo. Mfano ni usiku ambao maisha ya mtu yanaandikwa, hivyo wale watakaoaga dunia mwaka huo watakuwa wanaadikwa majina yao usiku huo. Uzushi huo ukasambaa katika baadhi ya nchi kwa wingi ukawa maarufu kwa sababu ya kupokelewa na wengi kwa ujinga.   

 

 

Al-'Allaamah Ash-Shawakaani (Rahimahu-Allaah) amesema katika Al-Fawaaid Al-Majmuw'ah:

 

 

"Hadiyth inayosema: "Ee 'Aliy! Yeyote  atakayeswali Rakaa mia usiku wa Niswfus-Sha'baan akisoma katika kila Rakaa ufunguo wa Kitabu (Suwrah Al-Faatihah) na Qul Huwa-Allaahu Ahad mara kumi, Allaah Atamkidhia haja zake zote”. Hii ni Hadiyth mawdhuw' (sio sahihi bali ni uzushi - yaani imezuliwa uongo kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Maneno yake yanataja kwa uwazi thawabu atakazozipata mwenye kutenda hivyo, na hakuna mtu mwenye akili ya kuzaliwa nayo kuwa hatoitilia shaka kuwa ni ya kuzuliwa. Pia watu katika isnaad yake ni majhuwl (wasiojulikana). Imesimuliwa pia kutoka isnaad nyingine ambayo pia ni mawdhwu' (ya kutungwa) pamoja na wasimulizi wake ambao ni majhuwl (wasiojulikana)"

 

 

Kwa mukhtasari, akasema: "Hadiyth kuhusu Swalaah usiku wa Sha'baan ni ya uongo, na Hadiyth ya 'Aliy iliyosimuliwa na Ibn Hibbaan ..”Inapofika katikati ya Sha'baan, kesha usiku huo kwa kuswali na funga mchana wake"  ni dhaifu"  

 

 

Aina zote hizo za uzushi zimejumuisha ‘ibaadah mbali mbali zinazotekelezwa kama kukusanyika watu baada ya Swalaah ya Magharibi na kusoma Suwrah Yaasiyn mara tatu kwa niyyah tatu tofauti. Ya kwanza kwa niyyah ya kuomba kuongezewa umri; kwa maana, ikiwa mtu ameandikiwa kuwa ni miongoni mwa watakaoaga dunia baina ya Niswfus-Sha'baan ya mwaka huu hadi Niswfus-Sha'baan ya mwaka ujao, basi mtu anaomba afutwe jina lake na aongezewe umri. Niyyah ya pili ni kuomba kuondoshewa balaa na shari zote. Na niyyah ya tatu ni kuomba kujaaliwa rizki njema. Kisha inafuatiwa na du'aa makhsusi.

 

 

Hakika huo ni uzushi unaopasa kuepukana nao na kujibakiza mtu katika ibada zake zilizothibiti katika Sunnah.

 

 

Ikiwa mtu ni kawaida yake kuswali Qiyaamul-Layl na akapenda kuamka pia usiku huo kuswali hakuna ubaya ikiwa hatozidisha lolote katika ‘ibaadah zake kuufanya usiku huo kuwa ni makhsusi kwa ‘ibaadah fulani zaidi ya masiku mengine.

 

 

Lakini kuipwekesha siku ya Niswfu-Sha'baan kwa Swawm pekee si Sunnah. 

 

Siku hiyo mtu anaweza kufunga ikiwa ni katika hali zifuatazo:

 

1.      Ikiwa ni kawaida yake mtu kufunga siku za masiku meupe ‘ayyaamul-biydhw’ (tarehe 13, 14 na 15) kila mwezi aendelee kufunga hizo siku japo itamkuta katika Niswfu Sha’baan.

 

2.      Pia ikiwa ni kawaida yake kufunga Jumatatu na Alkhamiys kisha ikaangukia kuwa ni siku ya tarehe 15 Sha'baan anaweza kufunga bila ya kukusudia kupata thawabu maalumu kwa ajili ya Niswfus-Sha'baan.

 

3.      Hali kadhaalika ikiwa mtu ameanza kufunga tokea mwanzo wa Sha’baan ikiwa ni siku zote hadi kufikia Niswfus-Sha'baan au kufunga tu Jumatatu na Alkhamiys na akapenda kufunga ayyaamul-biydhw, hakuna ubaya kwani kufunga siku nyingi mwezi huu ni kutokana na mafunzo sahihi kama tulivyoona kwenye Hadiyth juu.

 

 

Soma makala ifuatayo upate ufahamu zaidi wa mas-alah haya:

 

Sha'abaan - Fadhila Zake Na Uzushi Wa Nisfu Sha'abaan    

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share