Kutumia Tasbihi (Kuhesabia Shanga) Katika Kumdhukuru Allaah Inafaa?

 

Kutumia Tasbihi (Kuhesabia Shanga) Katika Kumdhukuru Allaah Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI LA KWANZA:

 

Asalam alaykum,

Naomba kuliza suali hili. kuna mtu aliniambia kuwa kusoma uradi kwa kushika mtasbihi ni ktk uzushi, na mwengine ameniambia kuwa sio kweli kwani swahaba Abuu Hurayrah alikuwa akivuta uradi kwa utumia kokwa za tende, kwa hiyo hakuna tofauti na mtasbihi. Sasa hapa nilikuwa naomba jibu la sawa kutoka kwenu wenye elimu, inafaa au haifai? Na kweli huyu sahaba alifanya hivi?

 

               

SWALI LA PILI:

 

A allakum. ningependa  kuuliza  kuhusu  utumiaji  wa  tasbih  ni  bidaah  na vipi  tutawaeleza  wazazi kuhusu   kutotumia.  mimi mzee  wangu  amenipa  yake  nitumie  jee  niifanyeje.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Jibu La Kwanza:

 

Ni wazi kwa kila Muislamu kuwa jambo lake lolote analolifanya lazima liafikiane na sheria ya Kiislamu; Qur-aan na Sunnah. Hilo ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuhimiza sana kufuata mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo bayana katika Suwrah Al-Hashri Aayah ya 7:

 

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ 

Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr: 7].

 

 

Kwetu sisi kumfuata Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inafaa tujue alilotenda au kusema. Pia kipenzi chetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia:

 

"Nawausia kumcha Allaah, na kusikiliza muambiwayo na kutii hata akiwa Kiongozi wenu ni mtumwa wa Kihabashi. Kwani hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni na kufuata mwendo wangu na mwendo wa Makhalifa wangu waongofu, yashikilieni kwa magego yenu mambo yao. Na nawatahadharisha nyinyi na uzushi katika mambo" [Abu Daawuud na at-Tirmidhiy].

 

Hebu tumsikilize tena kipenzi chetu anatueleza nini kuhusu haya mambo yanayozuliwa katika Dini:

 

"Mwenye kuzua katika hili jambo letu lisilokuwamo humo litakataliwa" [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Katika riwaya ya Muslim:

 

"Mwenye kufanya amali isiyokuwa na hukumu yetu, itakataliwa".

 

 

Suala ambalo tunafaa sisi kama Ummah bora, Waislamu kujiuliza ni kuwa: Je, Nabiy alitumia tasbihi ili kuleta uradi au alitumia kifaa gani? Je, Makhalifa waongofu walifanya hivyo? Je, Swahaba wengine nao walifuata mwendo huo?

 

Awali ya yote hebu tutazame mas-ala ya kutumia vijiwe au shanga, au kokwa za tende n.k. katika kuleta tasbihi na nyuradi.

 

Hadiyth ifuatayo ndio wanayoitumia wengi wa wanaotumia tasbiyh:

"Bora ya chenye kukumbusha ni Tasbiyh" Hii ni Hadiyth dhaifu.

 

Vilevile tunaona dalili nyingi za kuonyesha kinyume na hivyo wanavyofanya hao wenye kutumia Tasbiyh. Tutazame Hadiyth zifuatazo:

 

 

Imepokewa kwa Sa'd bin Abi Waqqaas (Radhwiya Allaahu 'anhu): Wakati mmoja Sa'ad, akiwa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walimzuru mwanamke ambaye mbele yake kulikuwa na vijiwe au kokwa za tende ambazo alikuwa akitumia kumsabihi Allaah. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Nakuambia kitu ambacho kitakuwa sahali na bora zaidi kwako kuliko unavyofanya. Akasema: Msabihi (SubhaanaLlaah) mara nyingi kama vile Alivyoviumba mbinguni, mara nyingi kama Alivyoviumba ardhini.. Mkabiri idadi kama hiyo, pia Mhimidi idadi kama hiyo na Mhalili .." [Abu Daawuud].

 

 

Sasa huyu mwanamke alikuwa atumie mbinu gani ya kuweza kuhesabu nyuradi hizo baada ya kuambiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa njia hiyo si bora kufanywa na Muislamu. Katika mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tunapata kuwa yeye alikuwa akitumia vidole vyake vya mkono wa kulia ili kuhesabu Tasbihi, Takbiri, Tahmidi na Tahlili alizokuwa akifanya. Hii imepokewa na mtu kwa Banu Sulaym:

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alizihesabu mkononi mwangu au mkononi mwake kwa kusema: Tasbiyh (SubhaanaLlaah) inajaza nusu ya mizani, Tahmiyd (AlhamduliLlaah) inajaza kamili. Takbiyr (Allaahu Akbar) inajaza baina ya mbingu na ardhi, Funga ni nusu ya subira na  twahara ni nusu ya Imani [at-Tirmidhiy].

 

 

Pia Yusayrah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) anasimulia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), aliwaamuru (wanawake wa Muhajirina) wawe ni wenye kushikilia sana katika kumdhukuru Allaah kwa kusema: Allaahu Akbar, SubhaanaLlaah, Laa ilaaha illa Llaah, na wasimsahau Allaah na rehma Yake. Wahesabu hizo kwa vidole vyao kwani vidole vitaulizwa na vitazungumza [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy, Ibn Maajah na al-Haakim kwa Isnadi iliyo sahihi].

 

 

Naye 'Abdullaah bin 'Amr bin al-'Aasw (Radhwiya Allaahu anhuma) anasimulia, "Nilimuona Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akihesabu kumsabihi Allaah na vidole vya mkono wake wa kuume" [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah].

 

 

Na kutoka kwa Asswalt bin Bahraam amesema, Ibn Mas'uud alimpitia mwanamke mmoja aliyekuwa na Tasbiyh akimsabihi Allaah kwa Tasbiyh hiyo akaikata na akaitupa, kisha akampitia mwanamume aliyekuwa akimsabihi Allaah kwa vijiwe akampiga kwa mguu wake kisha akasema;

 

 

"Mumetangulia, mumefanya uzushi kwa dhulma, na mumewashinda Swahaba wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa elimu"  [Sanad yake ni sahiyh mpaka kwa Asswalti, naye ni "thiqah" (mkweli mwenye kutegemewa) katika wanaowafuatia Taabi'iyn (wenye kufuatia Maswahaba).]

 

 

Hivyo, badala ya kutumia tasbihi tuwe ni wenye kutumia mkono kwani hajapatikana hata Swahaba mmoja aliyefanya hivyo. Ni salama kwetu zaidi kutumia vidole vyetu na ndio Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye tumeamriwa kumfuata.

 

Tufahamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:

 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.  [Al-Maaidah: 3] 

 

 

Imaam Maalik aliielezea Aayah hii kwa kusema: "Lolote ambalo halikuwa Dini wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haliwezi kuwa Dini sasa". Hii ina maana Dini imekamilika hatuwezi kuikamilisha zaidi ya hapo wala sisi hatuna daraja ya kuja kumkosoa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa yeye alifanya khiyana hakufikisha mengine ambayo alikuwa afaa atufikishie hivyo sisi Waislamu wa sasa tumekuja tukakamilisha hayo.

 

 

Tujiepushe na vizushi vyote nasi tutasalimika kabisa.

 

 

Jibu La Pili:

 

Ukitazama hapo juu kwa jibu la swali la kwanza utakuta kuwa utumiaji wa Tasbihi ni Bid'ah na inafaa kwetu sisi wafuasi wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tuache kuzitumia. Na badala yake tutumie vidole vyetu vya mikono ambavyo navyo tunapata baraka kwa kufanya hivyo.

 

 

Inafaa kwetu sisi tutumie hekima katika kuwaelimisha wazazi wetu kuhusu hilo na mengineyo kwani bila ya hivyo kutakuwa na fitna na mzozo mkubwa zaidi. Wapo wazee ambao wanaelewa wanapoambiwa na kurekebishwa kwa njia nzuri na wapo walio wakaidi. Ni vigumu kwa mtu ambaye huenda kwa miaka 50 anafanya jambo fulani kisha ukaja ukamuarifu na utegemee aache hayo mara moja na akufuate! Lakini pia wapo wenye uoni na kutaka haki, ambao hawatazami haki inatoka wapi au kwa nani; wao ni wenye kujisalimisha na kufuata mara moja. Allaah Aliyetukuka Anasema kuhusu kutumia hekima na busara na mawaidha mazuri:

 

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ 

Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. [An-Nahl: 125].

 

 

Ikiwa mzazi wako ni mkaidi tumia upole na njia ya taratibu wala usikate uhusiano naye kabisa. Usimsahau katika Swalaah na du'aa zako kwani kwa kufanya hivyo pia utakuwa unamsaidia kwa kiasi kikubwa. Wema ni kitu muhimu sana kuwafanyia wazazi kama alivyotuamuru Aliyetukuka:

 

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾

Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima. Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni. [ Al-Israa: 23-24].

 

 

Ama tasbihi aliyokupa unaweza kuiweka ikiwa bado ana ukaidi na kutochukua hadiya kutoka kwake inaweza kuleta zogo zaidi na kukatika kwa mahusiano, lakini usiitumie. Ikiwa ameelewa kuwa haifai basi yeye mwenyewe ataitupa na wala hatakupatia wewe.

 

 

Njia nzuri ya kutumia vidole kama tulivyopata kutoka kwa Wanachuoni walioelewa masuala hayo ya kutumia vidole, wanasema ni kutumia matumbo ya vidole karibu na kucha kuhesabia na si ile mistari mitatu ya kila kidole kama ilivyozoeleka na wengi. Lakini atakayefanya kwa njia zote hizo maadam anatumia vidole vyake, basi katimiza Sunnah na ana ujira mkubwa kwa hilo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share