Vipi Amuongoze Nduguye Aliye Na 'Aqiydah Potofu na Mambo ya Bid'ah?

SWALI:

Allaah awalipe heri kwa kazi hii.

Swali: Mimi ni mtanzania lakini kwa sasa niko India kimasomo, chuo ninachosoma,wako waislamu wachache mno wahindi na kwa ukweli hawajui chochote katika dini. Pia nipo na mwafrika mwenzangu mmoja toka west Africa, pia ni mwislamu, lakini ni mchache mno katika dini kielimu,sina elimu kubwa ya dini lakini nilijitahidi kusoma kidogo dini na kuhudhuria madarsa mbalimbali, Tanzania,tatizo linakuja ndugu yangu kakulia kwenye nchi yenye waislam wengi lakini anazikumbatia bidaa na Akida yake kwa kweli ina mashaka sana, mf, anaamini wapo mitume waliopita waliokuwa wakristo, uislamu ni dini mpya na imekuja mwishoni na mengine mengi, na kila ninapojitahidi kumweka sawa, ni mbishi na hataki kubadilika, mara nyingi tumekua tukigombana kwa kutaka tu kumweka sawa.Nifanyeje?

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muuliza swali. Mwanzo tunataka kukufahamisha kuwa hizo bid‘ah huku Afrika Mashariki zilitoka katika nchi za Waislamu. Kwa mfano Mawlid yalianza mwanzo katika nchi ya Misri karne tano baada ya kuaga dunia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hata Lamu, kisiwa ambacho kinajulikana kuwa ni kitovu cha Mawlid ya ngoma katika Afrika Mashariki yaliletwa kama miaka 120 tu iliyopita. Mashaykh wakubwa, na hasa Shaykh Fayswal al-Laamiy aliyapinga kabisa na hata kuna baadhi ya Misikiti mpaka sasa katika kisiwa hicho hakusomwi Mawlid. Mawlid yaliletwa na Shariyf katika ukoo wa Jamalil Layl, kwa jina Habib Swaalih kutoka Ngazija (Comoro). Kwa sasa bid‘ah zinaendelea kufanywa maradufu katika nchi za Waislamu kama Misri, Sudan, Pakistan, Bangladesh, India, Yemen na nchi nyinginezo. Hakika hilo si la kustaajabisha kabisa.

Pia utapata serikali za nchi nyingi za Waislamu zikiupinga Uislamu na Waislamu wenye msimamo mzuri dhahiri shahiri. Mfano wa nchi kama hizi ni Misr, Algeria, Morocco, Libya, Tunisia na nyinginezo. Nyingine zimekuwa za kisekula kabisa hadi kuwa wanapiga marufuku uvaaji wa hijabu kwa wanawake barabarani, katika taasisi na vyuo vya serikali kama Tunisia, Uturuki na kadhalika.

Hata hivyo katika kufanya Da ‘wah na kumlingania huyo nduguyo wa Afrika Magharibi usife moyo bali endelea kwa busara na mawaidha mazuri kama alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora” (16: 125).

Ukiona ameanza kubishana ni bora zaidi kuacha kuzozana na ungoje wakati mwengine muafaka. Sababu ni kuwa unapozozana watu hawatajua tofauti baina yenu na kufanya hivyo ni sifa ya kuwa na Imani. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na waja wa Ar-Rahmaan Mwingi wa Rehema ni wale wanaotembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!” (25: 63).

Tuna imani kuwa kwa juhudi zako na tawfiki ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) atabadilika siku moja, InshaAllaah.

Unachotakiwa kufanya ni wewe kumuelewesha nduguyo kuhusu maana ya Dini ambayo sio sawa na neno la Kiingereza Religion. Dini ina maana pana kuliko Religion na inajumlisha maisha yote ya mwanadamu. Yaonyesha kuwa nduguyo katekwa na kasumba ya wasio Waislamu kuwa Uislamu ni Dini aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ni ya Waarabu peke yake. Katika hili inatakiwa umueleweshe kuwa Uislamu umeanza kuanzia kuumbwa kwa mwanaadamu wa mwanzo, Nabii Aadam (‘alayhis Salaam). Hii ni kuwa mwanzo Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametuma Mitume (‘alayhimus Salaam) kwa kila Ummah:

Na kwa hakika kwa kila ummah tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Allaah, na muepukeni Shetani” (16: 36).

Kisha mfahamishe kuwa Dini inayokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ni Uislamu tu:

Bila ya shaka Dini mbele ya Allaah ni Uislamu. Na waliopewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao” (3: 19).

Ni wazi kuwa hilo linajulikana na waliopewa Vitabu pia lakini wakavipotosha na kupotosha hayo. Tujue kuwa yeyote anayetafuta na kufuata Dini isiyokuwa ya Uislamu haitakubaliwa kwake:

Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri” (3: 85). 

Mfahamishe kuwa Manabii na Mitume wote (‘alayhimus Salaam) walikuwa Waislamu. Dalili ya kauli hiyo ni Aayah zifuatazo:

Sema: Tumemuamini Allaah, na tuliyoteremshiwa sisi, na aliyoteremshiwa Ibraahiym, na Ismaa‘iyl, na Is-haaq na Ya‘qub na wajukuu zao, na aliyopewa Muusa na ‘Iysaa na Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi. Hatubagui baina yao hata mmoja, na sisi ni wenye kusilimu kwake (yaani Waislamu)” (3: 84);

pia, “Je! Mlikuwapo yalipomfikia Ya‘qub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibraahiym na Ismaa‘iyl na Is-haaq, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake (nasi ni Waislamu)” (2: 133).

Ama kuhusu Nabii ‘Iysaa (‘alayhis Salaam) Qur-aan inatueleza kuwa alikuwa yeye pamoja na wafuasi wake ni Waislamu:

Hakika Allaah ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyonyooka. ‘Iysaa alipohisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Allaah? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Allaah. Tumemuamini Allaah, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu” (3: 51 – 52).

Pia, “Na nilipowafunulia Wanafunzi kwamba waniamini Mimi na Mtume Wangu, wakasema: Tumeamini na shuhudia kuwa sisi ni Waislamu. Wanafunzi waliposema: Ewe ‘Iysaa bin Maryam! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Allaah ikiwa nyinyi ni Waumini. Wakasema: Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia” (5: 111 – 113).

Pia mueleze kuwa Ukristo haukuwepo wakati wa Nabii ‘Iysaa (‘alayhis Salaam) kwani yeye alikuwa Muislamu. Hata Biblia inatuarifu kuwa Ukristo haukuwepo wakati wa Nabii ‘Iysaa (‘alayhis Salaam) bali ulikuja baadaye. Mpatie changa moto katika hilo akuonyeshe katika kitabu hicho sehemu ambayo Nabii ‘Iysaa (‘alayhis Salaam) anasema kuwa amekuja na Ukristo na akatutaka sisi tumfuate. Hakika ni kuwa Biblia inatueleza: “Nao wote wawili (yaani Saulo na Barnaba) walikaa na ile jumuiya ya kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antioka, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo” (Matendo 11: 26).

Wakati huu Nabii ‘Iysaa (‘alayhis Salaam) alikuwa hayupo tena duniani na Ukristo huo ulianzishwa nje ya Jerusalem, mji ambao alikuwa akihubiri.

Kwa sababu ya ubishi wa nduguyo, jaribu njia nyingine kama kumpatia vitabu vizuri kuhusu Uislamu vya Kiingereza kama anajua au VCD au CD au kaseti. InshaAllaah tunaamini kuwa siku moja atabadilika.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share