Uzushi Wa Kisa Cha 'Alqamah

 

Uzushi Wa Kisa Cha 'Alqamah

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Jee kisa cha alqama na kukasirikiwa na mamake kina usahihi ?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Kisa hicho kama tulivyokinukuu hapo chini kwa kirefu, hakijathibiti na ni katika visa vya kutungwa. Kisa hicho kimeegemzwa kwa Imaam Adh-Dhahabiy kwenye kitabu chake ‘Al-Kabaair’, lakini wahakiki wanasema kisa hiko hakipo kwenye nuskha ya asili ya kitabu hicho bali kuna waliokiongeza ndani ya kitabu hicho walipochapisha mbeleni. Na Imaam Adh-Dhahabiy mwenyewe kakidhoofisha kwenye “Tartiyb Al-Mawdhwuw’aat” (namba 874).

 

 

Kadhaalika, pamoja na Imaam Ahmad kukisimulia, lakini Imaam Ahmad mwenyewe alikikataa baadae kwa kuwepo katika wapokezi wake ni Faaid bin ‘Abdir-Rahmaan ambaye hakubaliki.

 

 

Vilevile Wanachuoni wengi wamekidhoofisha kisa hicho kama tutakavyoona mwishoni.

 

 

Kisa hicho kinaelezwa kwamba kulikuwa kuna mtu aliyekuwa mwema kwa jina ‘Alqamah wakati anakata roho. Mkewe alimpelekea ujumbe Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aje kumtazama ‘Alqamah katika wakati wake wa mwisho lakini hakuweza kwa sababu ya mashughuli. Hata hivyo, aliwapeleka Swahaba wake watatu wende wamlakinie shahada kabla ya kuaga dunia. Swahaba hao walikuwa ni Bilaal bin Rabaah, Suhayb Ar-Ruumiy na ‘Ammaar bin Yaasir (Radhwiya Allaahu 'anhum).

 

 

Walipokwenda walijaribu kumlakinia lakini ikawa ni uzito kwake kutamka, nao wakarudi kumuelezea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hilo. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akahisi kuwa kuna tatizo, hivyo akauliza: "Je, wazazi wake wako hai?" Akajibiwa: "Mama yake, naye ni mzee". Akaomba aitwe. Alipokuja mama yake ‘Alqamah, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza: "Je, unasemaje kuhusu mtoto wako ‘Alqamah?" Akajibu: "’Alqamah ni mtu mzuri, anaswali Swalaah tano, anapigana Jihaad katika njia ya Allaah". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Sikuulizi kuhusu hilo bali uhusiano wako na wake". Akasema: "Mimi nimemkasirikia yeye kwa sababu yake kumfadhilisha mkewe juu yangu". Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaagiza kuletwe kuni, naye mama yake ‘Alqamah akauliza ni za nini, ee Rasuli wa Allaah. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Ikiwa hatochomwa hapa basi atachomwa Kesho Aakhirah". Mama akasema: "Usifanye hivyo bali mimi nimemsamehe na niko radhi naye. Namshuhudisha hilo Allaah, Nabiy Wake, Malaika, Waumini wote kuwa mimi niko radhi naye".

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawatuma Swahaba kwenda kumtazama ‘Alqamah, nao walirudi wakamueleza kuwa walipofika tu walimsikia ‘Alqamah akitoa shahada na hapo hapo akaaga dunia. [Mwisho wa kukinukuu]

 

 

Wanachuoni wengi wamekidhoofisha kisa hicho, kwa kutaja baadhi yao ni hawa wafuatao:

 

·       Imaam Ahmad kama alivyoeleza mwanae ‘Abdullaah bin Ahmad katika “Al-Musnad” (4/382).

 

·       Al-‘Uqayliy katika “Adhw-Dhwu’afaa Al-Kabiyr” (3/461)

 

·       Al-Bayhaqiy katika “Ash-Shu’ab” (6/198).

 

·       Al-Mundhiriy katika “At-Targhiyb wa At-Tarhiyb” (3/222).

 

·       Al-Haythamiy katika “Majma’ Az-Zawaaid” (8/148).

 

·       Ibn ‘Iraaq katika (Tanziyh Ash-Shariy’ah” (2/296-297 namba 51).

 

·       Ash-Shawkaaniy katika “Al-Fawaaid Al-Majmuw’ah” (231).

 

·       Adh-Dhahabiy katika “Tartiyb Al-Mawdhwuw’aat” (namba 874).

 

·       Ibn Al-Jawziy katika “Al-Mawdhwuw’aat” (3/87), na akasema: “Hii haikusihi kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na katika njia zake kuna Faaid ambaye Imaam Ahmad kamtaja kuwa: “Faaid ni mwenye kuachwa Hadiyth zake.” Na amesema Yahyaa: “(Yeye Faaid) Si chochote.” Na amesema Ibn Hibaan: “Haijuzu kumtolea ushahidi (kumfanya kuwa ni hoja).” Na akasema Al-‘Uqayliy: “Hamfuati yeye isipokuwa mtu mfano wake.” Na amesema Abuu Haatim Ar-Raaziy: “Alikuwa akidanganya.”

 

 

Baada ya kubainikiwa na udhaifu wa kisa hicho na kuona kauli za Wanachuoni wote hao waliokidhoofisha na waliosema ni cha kutungwa; basi ni muhimu kukiepuka kukitumia na kukitolea ushahidi hata kama kimeenea sana na kinatumiwa na Walinganiaji wengi na Mashaykh mbalimbali.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

Share