Zingatio: Kikata Ladha

 

Naaswir Haamid

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameiumba dunia ikiwa ni mchezo na hakuna ndani yake ila pumbao. Kuna kila aina ya starehe duniani, bila ya kusahau kwamba Pepo ndio kiboko cha starehe. Kwani huko kuna maisha ya milele, starehe zisizokuwa na mpaka, hakuna maneno ya bughudha na mengineyo. Basi kusanya vingi utakavyoweza, nenda mbali utakavyoweza, fanya ovu unaloliweza ila usisahau ile siku utakayotenganishwa na hii dunia.

 

Mkumbuke Malakul-Mawt ambaye atayakatisha maisha ghafla moja, bila ya mtu kutaraji, bila ya wakati maalum na bila ya kuletewa barua. Huyo si mwengine, ila mwenye kumpatia jina jipya mtu kuwa ni Aliyefariki, anayeligeuza jina la mke kuwa Kizuka na kumfanya kuwa Mjane. Anayempatia jina jipya mtoto kuwa ni Yatima. Anayegeuza mali iliyoachwa kuwa ni mirathi. Hiyo ni amri ya Mola wetu kuzichukua roho za wanaadamu, mmoja baada ya mmoja. Na ujira wa matendo yote yatalipwa kamili Siku ya Qiyaama.

 

{{“Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Qiyaama.”}} [3:185]

Wakati ni huu wa kujitayarisha kutenda mema, kuachana na maovu. Wakati umefika wa kujikurubisha kwa Mola bila ya kurudi nyuma. Sio wakati tena wa kuandaa ratiba za Vunja Jungu wala kupanga mikakati ya kuimaliza Ramadhaan kwa haraka ukitegemea kufanya maovu siku ya ‘Iyd.  Usiwe sawa na Firauni ambaye hadi roho yake inatolewa ndio anashuhudia kuwa Ujumbe wa Muusaa (‘Alayhis Swallaatu Wassalaam) kuwa ni haki. Wala usisubirie hadi roho inatolewa ndio uombe toba. Hapo toba katu haikubaliwi kwani sio sehemu yake.

 

{{“Hawana toba wale ambao hufanya maovu mpaka mauti yamemhudhuria mmoja wao, akasema: “Hakika mimi sasa natubu.” Wala (hawana toba) wale ambao wanakufa katika hali ya ukafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo.”}} [4:18]

 

Kifo ndugu yangu hakikimbiliki katu. Eeh hasara yetu kwa kughafilika na dunia hii. Kama umekuja duniani basi ipo siku utaondoka. Hizo zote ni haki zake mwanaadamu, Allaah lazima Amtimizie.

 

{{“Na kutoka roho kutakapomjia kwa haki (hapo ataambiwa): ‘Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia.’}} [50:19]

 

Hivyo tujihimize katika miezi hii mitukufu na kumkaribisha mgeni mwema Ramadhaan pamoja na miezi iliyobaki kwa kuchuma yale ambayo yatatuingiza Peponi na kuyaepuka yale ambayo yatatuingiza Motoni. Kwani Moto ni matokeo ya matendo maovu, wakati Pepo ni natija ya amali njema.

Share