Zingatio: Krismasi 2: Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) Hakuzaliwa Desemba

 

Zingatio: Krismasi 2:  Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) Hakuzaliwa Desemba

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Kama ilivyo kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakuna ushahidi wa kwamba Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) amezaliwa tarehe 25 Disemba. Sasa suala linakuja ni nani aliyeamua kwamba tarehe 25 Disemba iwe ni ya kusherehekea kuzaliwa Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam)?

 

Hiyo tarehe wenyewe iliyowekwa haina ukweli wowote, na Waislamu hawatakiwi kusema wala kushuhudia uongo. Kwa masuala ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wameshatolea hukumu, Uislamu hauhitajii mawazo ya mwengine yeyote awe ni Swahaba, Mwanachuoni, mcha Mungu wala ya mtu yeyote. Tofauti na Ukiristo ambao kutokana na khofu za walimu wao kwamba huenda Wakristo wakachanganya imani za kipagani, waliamua kuichukua tarehe hiyo ya kipagani (25 Disemba) kuwa ni siku ya kuzaliwa ‘Iysaa ('Alayhis-salaam).

 

Biblia yenyewe inasema kwamba tarehe 25 Disemba sio tarehe ya kuzaliwa Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam). Sehemu ambayo inaaminika na Wakristo kwamba alizaliwa Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) ni Palestina – kwenye sehemu za mbuga za wanyama wakiwepo wachungaji (Luka 2: 8-12). Kama walikuwepo wachungaji siku aliyozaliwa, basi bila ya shaka haitakuwa ni kipindi cha Disemba, kwani hicho ni kipindi cha baridi huko Palestina. Wachungaji hao wanakuwepo mbugani baina ya mwezi Machi hadi Oktoba. Hivyo, huenda Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) amezaliwa baina ya Septemba na Oktoba.

 

Pia Yohana Mbatizaji anaweza kufafanua zaidi kwamba Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) hakuzaliwa tarehe 25 Disemba. Kutokana na mafunzo ya Ukristo, Elisabeti alikuwa ni mama wa Yohana na binamu wa bibi Maryam ('Alayhas-salaam). Yohana kwa mujibu wa mafundisho ya Ukiristo, alianza upadri mnamo mwaka 15 wa Tiberius Caesar. Umri wa chini wa kuanza kazi ya upadri ulikuwa ni miaka 30. Kwa vile Augustus alifariki tarehe 19 Ogasti mwaka wa 14 AD, huo ulikuwa ni mwaka wa Tiberius kufanywa kuwa ni padri. Iwapo Yohana amezaliwa tarehe 19-20 Aprili BC, tarehe yake ya kuanza kazi ya upadri itakuwa ni tarehe 19-20 AD au ni mwaka wa 15 wa Tiberius. Hili pia linathibitisha huo mwaka wa pili BC, na kwa vile Yohana ni mkubwa wa Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) kwa miezi mitano, inathibitisha kwamba Nabiy ‘Iysaa amezaliwa kipindi cha masika (kwa Ulaya hichi ni kipindi baina ya Septemba-Novemba).

 

Ushahidi mwengine ni kutoka kwa Elisabeti mwenyewe. Kwa mujibu wa mafundisho ya Ukiristo, bibi Maryam alijificha kwa kipindi cha miezi mitano na baadaye Malaika Jibriyl ('Alayhis-salaam) alimueleza bibi Maryam kuhusu hali ya Elisabeti na kwamba bibi Maryam atazaa mtoto wa kiume atakayekuja kuitwa ‘Iysaa. Bibi Maryam alienda kumtembelea Elisabeti, ambaye alikuwa ndani ya wiki ya mwanzo ya mwezi wa sita ama wiki ya nne ya Disemba, mwaka wa tatu BC. Iwapo Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis Salaam) amezaliwa siku 280 baadaye, basi siku yake ya kuzaliwa itakuwa ni tarehe 29 Septemba, mwaka wa 2 BC. Wanazuoni wa Kikristo wanafasiri miezi sita kuwa ni sawa na ile miezi ya Kihibru au baina ya miezi ya Ogasti-Septemba. Kwa vile mimba ya bibi Maryam ('Alayhis-salaam) ilianza kipindi kifupi kabla ya miezi hiyo sita mnamo Julai, Nabii ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) atazaliwa mnamo kipindi cha Machi-Juni.

 

Ni jambo la kutilia maanani kwamba tarehe halisi ya kuzaliwa Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia haijulikani. Hivyo, wanaosherehekea uzawa wa Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis Salaam) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wote hawana ithbati yoyote. Lililo bora ni kujiweka mbali na uzushi wowote. Ni afadhali kuacha kusherehekea ukakosa thawabu (kama zipo) kuliko kupata dhambi (ambazo atapata) kwa kushuhudia uongo huo.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema juu ya kushuhudia (kushiriki) mambo ya uongo:

 

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا ﴿٧٢﴾

Na wale ambao hawashuhudii uongo, na wanapopita kwenye upuuzi hupita kwa heshima. [Al-Furqaan: 72]

 

Wamewazushia uongo Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) na Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya siku zao za kuzaliwa. Siku ya Qiyaamah watakwenda kujibu tuhuma hizo. Sio Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-salaam) wala Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyewahi kuamrisha kuadhimishwa siku yake ya kuzaliwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anajua zaidi.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atughufirie madhambi yetu na Atuongoze njia iliyonyooka.

 

 

 

Share