Kuzidisha Matendo Ya Taqwa Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Kuzidisha Matendo Ya Taqwa Katika Mwezi Wa Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

 

Mwalimu bora kabisa wa walimwengu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

 

"Kama ukilazimika kula hakikisha theluthi moja ya tumbo lako unaijaza chakula, theluthi moja maji na acha theluthi moja kwa ajili ya hewa (yaani iache tupu)” [At-Tirmidhiy].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alihimiza kumaliza chakula, sahani isibaki na chochote cha kutupwa, na alihimiza hata kuramba vidole (kama mtu kala kwa mkono).

 

Hadiyth nyingine inasema kuwa mtu asiache hata tonge moja la chakula kwenda kutupwa, "kwani hamjui baraka iko wapi (katika chakula)" [Muslim].

 

Linganisha mafundisho haya na jinsi tunavyokula sisi, hasahasa Mwezi wa Ramadhwaan. Kila pendekezo la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lililotajwa hapo hukiukwa. Chakula ni cha kupita kiasi (isirafu) na kila mmoja hujitahidi kujaza tumbo kibao.

 

Limekuwa jambo la kuchekesha kuwa watu badala ya kupungua uzito katika Mwezi wa Ramadhwaan, wao huzidi kuongezeka. Ile nidhamu na kaba ya mchana inafidiwa kupita kiasi katika futari.

 

Hata taraawiyh inakuwa tabu kuiswali na wengine huikwepa. Kibaya zaidi chakula kilichobakishwa humwagwa ovyo.

 

Ramadhwaan ni mwezi wa kuzidisha matendo ya uchaji Allaah na hivyo, mazoea haya yaachwe kama Wafungaji wanataka kupata manufaa ya kiroho na kimwili kutokana na saumu ya Ramadhwaan.

 

 

Baadhi ya dondoo za kusaidia utekelezaji wa jambo hili ni:

 

 

1)    Kula kwa kipimo, kiwango cha wastani cha daku na futari.

 

2). Unapokuwa katika chakula cha kukirimiwa au katika mgahawa, usilazimike kumaliza chakula chote bali bakisha kihifadhiwe kwenye mfuko kwa ajili ya kula baadae.

 

Usibabaike na tabia ya kifakhari iliyo kinyume na Uislaam-usiache hata tonge lako moja la chakula liende kutupwa. Chakula tunachokula ni kitukufu, kinatolewa na Allaah na kimejaa baraka Zake - haya ndiyo maadili ya Dini yetu.

  

3).  Waalike watu masikini katika jamii yako kufuturu nawe. Namna wao wanavyoheshimu chakula linakuwa somo zuri kwako.

  

4).   Kumbuka nasaha za Nabiy - kula kwa wastani.

 

5). Wakati wa Swawm uzuie moyo wako kutamani mambo ya dunia - chakula, mavazi, burudani, majumba au watu. Mafundisho bora ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kushusha macho pale kitu cha dunia hii kinapoteka fikra na kutufanya tughafilike na Allaah.

 

6).  Soma au sikiliza Qur-aan kwa mazingatio

 

 

Jinsi Ya Kupata Zuhd

 

Zuhd haina maana kuwa wewe usimiliki kitu bali kitu hicho kisikumiliki wewe.

 

Zuhd halisi si ya mali wala si ya kuacha umiliki wa mali. Zuhd ya mali inaweza kuwa nyenzo tu kupatia zuhd halisi; nayo ni kujizuia kwa ndani kuzikumbatia mali.

 

Lakini kujiepusha kwetu kukumbatia mali katika dunia ambayo inaabudu vitu hivyo yaonekana kama ni sawa na kuoegelea baharini bila kulowana. Tunawezaje kuishi na kufanya kazi katika dunia inayoishi kwa uchumiatumbo?"

 

Tunawezaje kuwasiliana katika dunia amabayo lugha yake ni ulahidi? Twawezaje kuogelea bahari hii bila kulowana?

 

 

Dumisha Mawasiliano Yako Na Qur-aan

 

Njia ya haraka sana ya kupotea ni kupoteza muongozo wako. Usipitishe hata siku moja bila kuwasiliana na Qur-aan. Isome, itafakari, tazama mnasaba wake na maisha yako.

Kupoteza mawasiliano yako na Qur-aan ni sawa na kupoteza ramani unapokuwa safarini. Kudumisha mazungumzo na Allaah kutaulinda moyo wako usiendekeze dunia.

 

Wale wanaoacha kumkumbuka Allaah huwa na nyoyo zinazojiweka mbali na Allaah na hivyo ni rahisi kufuata miungu bandia ya dunia. Unapopita muda fulani, moyo unaojitenga na Allaah huwa mgumu na hatimaye hufa. Allaah Anatuonya jambo hili:

 

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَن تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّـهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ ﴿١٦﴾

Je, haujafika wakati kwa walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah na yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawatawilikia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki. [Al-Hadiyd: 16].

 

Share