Wanawake Wanaweza Kufanya I'tikaaf Nyumbani?
Wanawake Wanaweza Kufanya I'tikaaf Nyumbani?
SWALI:
Je, Mwanamke anaweza kufanya I'tikaaf nyumbani? Na vipi ikimbidi kupika?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
I'tikaaf inapasa kufanyika msikitini pekee kwa sababu ya maana ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلاَ تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ
Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini Al-Baqarah 2:187
Hukumu hii inawahusu wote wanaume na wanawake.
Ibn Qudaamah kasema katika Al-Mughni:
"Mwanamke ana haki kufanya I'tikaaf katika msikiti wowote na sio sharti uwe msikiti ambao unaswaliwa Swalah za Jama'ah kwa sababu kwa mwanamke sio fardhi kwake kuswali Jama'ah". Hii ni rai ya Imaam Al-Shaafi'iy.
Hana haki kufanya I'tikaaf nyumbani kwake kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
أَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ
hali mnakaa Itikafu msikitini
na kwa sababu wake wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walimuomba ruhusa wafanye I'tikaaf msikitini na aliwaruhusu.
An-Nawawy amesema katika Al-Majmu'u (6/480) "Haimpasi mwanamume au mwanamke kufanya I'tikaaf mahali popote isipokuwa msikitini".
Na hii ni rai ya Sheikh Ibn 'Uthaymiyn katika Al-Sharh Al-Mumti'I 6/513
Na Allaah Anajua zaidi.