Safari: Mume Msafiri Anamtamani Mkewe Katika Ramadhaan

SWALI:
 
Mwenyezi mungu mtukufu awazidishie kheri zake nyingi kwa kutuelimisha. Inshaallah amiin. Mimi mme wangu ni dereva wa masafa marefu. Mala nyingi siku anayorudi hua taabani kwa kuchoka hadi karibu na alfajri ndiyo angalau anataka kupewa haki yake. Sasa huku unasikia adhana ya kwanza na unahitaji kuhudhuria swala, mme anataka, mna masiku mengi hampeani. Na ramadhani mwataka mfunge. Hapo tufanye nini? Na ninaogopa nisimuache mme wangu aondoke na kiu anaweza kufanya dhambi ya uzinifu huko mbali anako kwenda. Tafadhali nisaidieni.
 

 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihiwasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muulizaji swali. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awawezeshe kuchunga mipaka yake ndani ya Ramadhaan na nje yake. Hakika mwezi wa Ramadhaan wanandoa wanafaa wajichunge sana wasije wakaingia katika kuingiliana mchana na hapo kulazimika kulipa kafara nzito.
 
 
Kile ambacho tunaweza kukushauri dada yetu, ni kuwa Muislamu wakati wa Ramadhaan anaweza kula, kunywa na kustarehe na mwenziwe kimapenzi mpaka adhana ya pili ikiwa itatolewa katika wakati wake. Baada ya hapo haifai kwenu kufanya moja kati ya mambo hayo matatu. Ikiwa mna wasiwasi huenda starehe zikawa ndefu ni afadhali siku hiyo mpumzike mpaka siku ya pili baada ya Magharibi tu.
 
 
Ieleweke kuwa wanandoa wanapoingiliana baada ya adhana ya pili ya mwezi huu wa Ramadhaan hadi Magharibi basi anafaa afanye mambo yafuatayo:
 
Baada ya Ramadhaan anatakiwa ailipe siku hiyo pamoja nayo ni kafara nzito. Katika kafara anatakiwa amuache mtumwa huru, ikiwa hawezi basi afunge miezi miwili mfululizo, na akiwa hawezi basi alishe masikini 60. Pamoja na hayo pia anatakiwa arudi kwa Allaah Aliyetukuka, aombe maghfira, ajute na aweke azma ya kutorudia tena dhambi hilo. Hivyo, tuwe na tahadhari kubwa sana kuhusu suala hilo msije mkaingia katika dhambi ambalo kafara yake ni kubwa. Inapaswa mume aelewe hilo nawe uwe utajaribu kumtimizia mumeo mahitaji yake ya kimwili lakini bila kukiuka mipaka iliyowekwa na Allaah Aliyetukuka.
 
 
Na Allaah Anajua zaidi
Share