Hajaridhika Na Mume Aliyeozeshwa Kwa Nguvu

 

 

SWALI:

Ndugu zangu na nawatakia kila la kheri alhidaaya wote na Mwenyezi Mungu awajaliye kila la kheri na mzidi kutusaidia....inshaalah ameen swala langu ni: mimi ni bint wa kisilam ambae sijaolewa, kwa bahati nzuri nimekuja kuposwa ila huyo mwanamme sijaridhika nae kwa uzuri wake, na wazazi wameamua kuniozesha kwa nguvu bila ya ridhaa yangu na sijui nifanye nini kwahiyo naomba mnisaidie na ikiwezekana mnijibu haraka iwezekanavyo maasalam...

 


 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu kwa swali lako. Kuhusu suala lako kuna tofauti baina ya wanazuoni kuhusu kumlazimisha binti bikira aliye baleghe. Ipo kauli ya kukubalika hilo lakini iliyo sahihi ni kuwa haifai, nayo ni kauli ya Abu Haniyfah, riwaya moja ya Ahmad, Awzaa‘iy, ath-Thawriy, Abu ‘Ubayd, Abu Thawr, Ibn al-Mundhir na ikachaguliwa na Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyah. Dalili zilizopo katika hilo ni kama zifuatazo:

 

  1. Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa msichana mmoja bikira alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuarifu kuwa babake amemuozesha naye anachukia hilo. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamchaguzisha (yaani baina kukubali na kukataa) {Abu Daawuud, Ibn Maajah, ad-Daraqutwniy na al-Bayhaqiy}.

 

Na mfano wake ni ile Hadiyth ya Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhuma), ambayo ndani yake ipo ibara: “…akawatenganisha” (an-Nasaa’iy).

 

  1. Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Bikira haozeshwi mpaka atakiwe idhini”. Akaulizwa: “Ewe Mtume wa Allaah! Idhini yake ni vipi?” Akajibu: “Kunyamaza kwake” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

 

Shaykh wa Uislam Ibn Taymiyah amesema: “Kuozeshwa kwake pamoja na kuchukia kwake Nikaah inakwenda kinyume na msingi na akili. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hajampatia walii nafasi ya kumlazimisha kuuza au kuajiri ila kwa idhini yake wala kwa chakula, kinywaji na kivazi ambacho hataki. Vipi walii atamlazimisha kuishi na anayemchukia. Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Amejaalia baina ya wanandoa mapenzi na rehema ikiwa haipatikani ila kwa kumkasirisha na kumkimbiza, ni mapenzi na rehema gani katika hilo?”

 

  1. Hakika ni kuwa sheria ya Kiislamu imeweka kanuni kuwa lau mwanamke atamchukia mumewe anaweza kujivua na ndoa hiyo, vipi itafaa mwanzoni kumuozesha yeye kwa nguvu? Hakika hilo ni jambo haliingii hata katika mizani ya akili.

Hivyo, Uislamu umewakataza kabisa wazazi kumlazimisha binti yao kuolewa na mume asiyemtaka kwa sababu yoyote ile aliyonayo.

Ushauri wetu wa mwanzo ambao tunaweza kukupatia ni kuswali rakaa mbili kumtaka ushauri Allaah Aliyetukuka. Tawadha vizuri na uswali Sunnah hiyo ya Istikhaarah na uombe du’aa yake mwisho wa Swalah na Allaah Aliyetukuka Atakuongoza kwa lililo la kheri. Huenda ukamchukia kumbe ana kheri nawe na mara nyingine huenda ukampenda mtu kumbe ni shari kwako. Allaah Aliyetukuka Anatuambia: “Huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui” (2: 216).

Nasaha ambayo tunaweza kukupatia ingawa kwanza ni kutaka kufahamu, je, kati ya wazazi wako wawili – mama na baba ni yupi aliyeshikilia hilo la lazima wewe kuolewa? Kulingana na kauli yako inaonyesha kuwa wote wawili wameshirikiana katika hilo. Ikiwa si hivyo unaweza kuanzia hapo. Mfano ni kuwa ikiwa baba ndiye aliyeshikilia unaweza kuzungumza na mamako jambo hilo kwa hekima na makini kwa kumkinaisha kwa hoja bila kumkosea heshima.

Ikiwa njia ya kuzungumza na wazazi wote imeshindikana na wameshikilia msimamo wao ule ule inabidi utafute jamaa wa karibu kama mashangazi, wajomba, maami na wengineo. Ni vyema upate wale ambao wanafahamu masuala haraka, hao ndio wanaweza kuwa mabalozi wako kwenda kuzunguza na wazazi wako. Inatakiwa uwaeleze hizi hoja za kidini ambazo tumeziandika na pia za kiakili kwa lengo kubwa la kupatikana masikilizano halitakuwepo na hivyo hamna faida ya ndoa hiyo.

Ikiwa njia hiyo imeshindikana itabidi kama unawajua wazazi wa huyo kijana hasa mamake uende kwake na uzungumze naye yaliyo moyoni mwake na kuwa wewe hutaki ndoa hiyo na sababu zako. Ikiwa mamake hakukusikiliza itabidi umtafute huyo kijana aliyekuja kukuposa ukiwa na maharimu yako na umweleze hisia zako na kuwa wewe hutaki kuolewa naye kwa sababu hizo ulizozitaja.

Ikiwa hayo yote yameshindikana utakuwa kweli hutaki nikaha hiyo itabidi uende kwa Qaadhi na umweleze shida zako.

Twatumai kuwa hutafika kote huko bali utapata faraja na wepesi wa hilo kwa watu wako wenyewe.

Tunakuombea kwa Allaah Akiyetukuka Akusaidie na Akuepushe kwa lile usilolitaka, Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share