Uzushi Wa Unoadaiwa Ni Fadhila Za Siku Kumi Za Dhul-Hijjah

 

Uzushi Wa Unoadaiwa Ni Fadhila Za Siku Kumi Za Dhul-Hijjah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swali:

Nimepokea e-mail iliyotumwa yenye kutaja fadhila za siku kumi kila siku kuwa ni jambo fulani limetokea na kadha kama inavyoeleza hapa chini. Je hii ipo dalili au ni katika uzushi?
 

 

Siku Kumi Bora

Allaah subhanahu wataala ameapa kwa masiku bora katika quraan takatifu sura 89 aya 1-2 isemayo : Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametusimulia vilivyotendeka na umuhimu wa siku hizi kumi bora za mfungo tatu (DhulHijja); Rasula-Allah atueleza sisi ummati wake  kuwa, mwenye kufunga siku hizo hupata fadhla kubwa mno,kwani kila   siku ina fadhila na kheri zake:

 

 

Siku Ya Kwanza Ya Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa - "Ni siku  ambayo Allah alimsamehe Nabiy Adam ('Alayhis-Salaam)  kwa makosa yake".Mwenye kufunga siku hiyo, Allah humsamehe madhambi  yake.  
 

 

Siku Ya Pili Ya Mfungo Tatu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:-"Ni siku  ambayo  Allaah alikubali maombi ya Nabiy Yunus ('Alayhis-Salaam)  ya kumtoa  katika matumbo ya samaki".Mwenye kufunga siku hiyo,  ni kama  aliyefanya ibada ya mwaka mzima pasi na kufanya makosa.

 

 

Siku Ya TaTa Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:- "Ni siku ambayo  Allaah aliitikia Dua ya Nabii Zakariya ('Alayhis-salaam)  yakumpata  mtoto". Mwenye kufunga siku hiyo, Allah huitikia dua  yake.

 

 

Siku Ya Nne Ya Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:-"Ni siku ambayo  alizaliwa Nabiy 'Issa ('Alayhis-Salaam) .Mwenye kufunga siku hiyo, Allah humuondolea matatizo na umasikini.

 

 

Siku Ya Tano Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:- "Ni siku   alizaliwa  Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam)  "Mwenye kufunga siku hiyo, Allaah humtakasa na unafiki na humuondolea adhabu za kabori.

 

 

Siku Ya Sita Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:- Ni siku ambayo  Allah alimfungulia Nabiy wake Muhammad(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kheri". Mwenye kufunga siko hiyo, Allah humuangalia kwa  jicho la huruma wala hapati adhabu siku ya kiyama.

 

 

Siku Ya Saba Ya Mfungo Tatu  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:- "Ni siku ambayo  Milango ya Jahannam (Moto) hufungwa na hayafunguliwi hadi masiku kumi  yatimie". Mwenye kufunga Allah humfungia Milango  thelathini ya mambo mazito na humfungulia Milango thelathini ya  mambo mepesi.

 

 

Siku Ya Nane Ya Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:- "Ni siku  iitwayo  Tar-wiya". Mwenye kufunga hupewa malipo ambayo hakuna ayajuwaye  isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

 

Siku Ya Tisa Ya Mfungo Tatu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:- "Ni siku  iitwayo  Arafat". Mwenye kufunga siku hiyo, hufutiwa makosa ya mwaka uliopita, na utakao kuja.

 

 

Siku Ya Kumi Ya Mfungo Tatu:- Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asema kuwa:-"Ni siku ya  kuchinja Mnyama (itakuwa Iddi Kubwa), tone la kwanza la damu  litakapo tona Allah humsamehe dhambi zake na za jamaa  zake. Na mwenye kumpa chakula Masikini au akatowa sadaka siku hiyo, Allah atamfufua siku ya Kiyama kwa amali na mizani ya  uzito, thawabu zake zitashinda uzito wa Mlima Uhud".

 

Please Do Not Forget To Enlighten Other Muslims By Forwarding This Mail
 
 
Jibu:
 
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kwanza kabisa haifai kufupisha kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Manabii wote kwa kuandikwa hivyo kifupi (S.A.W) au (A.S) na pia haifai kufupisha kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) au kuwaombea radhi Swahaba na kadhaalika. Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo bayana. (Tumeondosha na kurekebisha vifupisho hivyo).

 

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

 

 

Tunasikitika kwamba siku hizi fitna za kusambaza uzushi zimezidi kutokana na wepesi wa mawasiliano kupitia mitandao ya jamii.  Jambo linaloshangaza ni kwamba Hadiyth zilizo Sahihi zimejaa tele lakini hizo hazisambazwi kama zinavyosambazwa za uzushi. Ni dhahiri kwamba wanaofanya hivyo ima hawajui tofauti ya mafunzo sahihi na yale potofu ima kwa uchache wa elimu, au kwa pupa tu za kutafuta thawabu kwa njia za mkato ndiko kunakowasababisha wao kueneza haya mambo yasiyo na dalili wala asili. Lakini wanaghafilika ndugu hao kutambua madhara yanayopatikana kutokana na hayo wanayoyaeneza kila mara.

 

 

Moja ya dhara kubwa  ni kupoteza mafundisho sahihi ya Dini yetu, na kueneza ya uongo na hivyo kutawala upotofu katika jamii ya Kiislam, Kwani kama wanavyosema wema waliotangulia, kuwa, bid’ah inavyoenea, ndio Sunnah hupotea.

 

Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate faida:

 

Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

 

Tumepekuwa vitabu mbalimbali vya Hadiyth vikubwa na mashuhuri na hakuna hata sehemu moja tuliyokuta kuna Hadiyth inayotaja Fadhila za masiku kumi ya Dhul-Hijjah kwa mtindo huo na kwa maelezo hayo! Vilevile ‘Ulamaa waliowahi kukumbana na maelezo hayo, wamesema kuwa ni ‘Mawdhuw’ – yaani ya kutungwa na si ya kweli.

 

 

Kuna hatari vilevile ya watu kutumbukia katika maonyo na makemeo aliyoyatoa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Ukiwa umeeneza mambo hayo na hali unajua kuwa si sahihi, basi tambua kuwa ushaingia katika walioelezwa ndani ya Hadiyth hiyo.

 

 

Na ikiwa una mazoea ya kueneza au kutuma kila unachopata ukidhani utapata thawabu kwa kufanya hivyo na hali huna uhakika nacho, au huna elimu ya jambo hilo kama ni sahihi au la, basi utakuwa pia una majukumu kwa kuwa Uislam umesisitiza sana elimu na umuhimu wa kuitafuta; hivyo kwanini ubakie katika ujinga na kutokufahamu unayotuma? Pia ikiwa hujui, ushaelezwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), uulize wenye elimu na upambuzi, je, ulijaribu kufanya hayo kabla hujasambaza mambo hayo ya kutunga yenye kupotezea Waislam muda, juhudi, na hata ‘amali zao kwa kufanya yasiyo sahihi na yasiyo katika mafundisho ya Dini?

 

 

Na madhara mengine ni kwamba dhambi za mwenye kueneza uzushi huzidi kila uzushi unapozidi kusambaa na mwenye kuanza kueneza uzushi hubeba dhambi za kila mtu anayepokea na kujifunza uzushi huo:

 

 عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم أنه قال : ( من دعا إلى هدى كان له من الأجر من أجور من تبعه لا ينقص من أجورهم شيئاً ومن دعا إلى ضلالة كان عليه من الإثم مثل آثام من تبعه لا ينقص ذلك من آثامهم شيئاً)   رواه مسلم  

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Atakayelingania kwenye uongofu atapata thawabu (ujira) wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika thawabu zao. Na atakayeelekeza katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) [Muslim]

 

Tumefanya utafiti mkubwa kutafuta kauli kama hizo kuhakikisha kama ipo kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayotaja fadhila za siku hizo kama zilivyotajwa humu lakini hatukupata.  Mojawapo ya matokeo ya utafiti ni kupata fatwa kutoka kwa ‘Ulamaa kutoka Markaz ya Fataawa walioulizwa kuhusu ujumbe huo nao pia wamehakikisha kuwa ni uzushi usio na dalili yoyote [Markaz al-Fataawa 24 Dhul-Hijjah 1424/16-02-2004].

 

Tunawanasihi ndugu zetu Waislamu wasome mada muhimu katika kiungo kifuatacho ili watambue hatari ya kueneza uzushi:

 

 
Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

 

Vilevile mtu anatakiwa asome mada hii hapa chini yenye kuhusu uzushi wenye kufanana na huo:

 

 

Uzushi Unaodaiwa Kuhusu Mambo Yaliyotokea Siku Ya Ashuraa Tarehe 10

 

Pia tunawaomba ndugu zetu kwamba wanapopata jambo lenye shaka kwanza wawe wanahakikisha kabla ya kutuma kwa wenzao kwani tutambue kuwa Muislamu inapomfikia kauli inayodaiwa kuwa ni ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi imeshakuwa ni waajib kwake kuhakikisha.  Na ikiwa hakupata dalili yake ni bora kuacha kutuma kuliko kuleta madhara ya uzushi na kuzidisha ufisadi katika dini na jamii kwa ujumla kwa kupoteza mafunzo sahihi na kueneza mafunzo ya uzushi.

 

 

Kidokezo Cha Kuweza Kutambua Hadiyth Zisizo Sahihi Au Ujumbe Wa Uongo:

 

Ndugu Muislam, ukitaka kugundua haraka ujumbe ulioupata kwenye mitandao ya jamii, kwanza kitakachokujulisha kuwa ujumbe huo una utata na sio sahihi, ni kuwa, mara nyingi maelezo yaliyomo ndani ya ujumbe huo zikiwemo zinazosemwa ni Hadiyth, utakuta hazitajwi zilipotolewa, kama ni Hadiyth utaona haisemwi nani kasimulia, nani kapokea, kitabu gani, hakuna hata Imaam wa Hadiyth (Muhaddith) aliyetajwa kwenye Hadiyth hiyo n.k. Hayo yote yanatosha kumtia mashaka mtu kuhusiana na alichokipokea. Hivyo, endapo utapokea ujumbe au Hadiyth ambayo imekuja tu na kudaiwa kasema Mtume bila kutajwa zaidi ya hivyo… basi mrudishie aliyekutumia na muombe akueleze Hadiyth hiyo iko kwenye kitabu kipi, na nani kaisimulia na kama ni sahihi au dhaifu. Usiwe na pupa ya kueneza au kusambaza kwa wengine hadi kwanza upate uhakika 100%. Vilevile unaweza kutuandikia maswali@alhidaaya.com kuulizia masuala kama hayo na tukiweza In Shaa Allaah tutakusaidia haraka katika masuala hayo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share