Zingatio: Wa Kulaumiwa Ni Nani?

 

Zingatio: Wa Kulaumiwa Ni Nani?

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tumeziacha nyuma ya migongo yetu na kuyafanya matashi yetu kuwa ndio muongozo wa maisha yetu.

 

Uzinifu tumeufanya kuwa ni ada yetu na pombe ndio muongozo wa maisha ya leo. Imefika hadi ya kuona haramu kuwa halali na halali kuwa ni haramu. Tumejikubalisha kuwa akiba haina faida bila ya riba. Mauziano yasiyokuwa na uongo, utapeli sasa yamepitwa na wakati.

 

Imekuwa ni desturi kuona kila kona za majengo na sehemu za mikusanyiko ya watu pamoja na barabarani kuwepo picha za utupu zenye kuamsha hisia za uzinifu. Sio matangazo ya biashara halali wala haramu zenye uadilifu wa kutilia mkazo ubinaadamu na haki za imani zisiopendelea picha hizo.

 

Matangazo ya pombe yameshika kasi huku simu, sigara, vyakula na kadhalika vikiwa havipo nyuma kurusha mabomu ya uzinifu. 

 

Matokeo yake hayo, ni kubakia jamii kwenye matatizo na udhaifu wa mwaadamu wa uchu wa kutosheleza hisia zake kwa kujamiiana tu. Utakuta kwa mfano tangazo la simu lenye msichana aliyevaa jeans yenye kubana akiwa na mvulana aliyesokota nywele zake kwa mtindo wa rasta. Huku ujumbe wa tangazo hilo likisomeka:

 

“Leo nitakosa masomo, nahitaji kupunga upepo”.

 

Nini tunawafunza vijana wetu kwa matangazo kama hayo? Na yareti tangazo hilo lingelikuwa ni moja, lakini kona za barabara nzima zimetapakaa matangazo mfano wa hayo. Lahaula! Kama vijana hawakutoroka shule, tutegemee kutumbukia kwenye uzinifu wa kuiga hizo picha.

 

Alhamdulillaah, tumepewa macho lakini hakika atakayeyakemea mambo hayo kwa sauti kali ndio ataambiwa kuwa ni kipofu, mpinga maendeleo, mjinga, hafai katika jamii, mshamba na kadhalika. Wale Waislamu wenye imani zisizoeleweka, ndio wataanza kumuita kwa istihzai na kejeli; Ustadh, Shaykh na kadhalika.

 

Tuikumbuke kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliposema kuwa tuna viungo lakini hatuvitumii: 

 

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ لَهُمْ قُلُوبٌ لَّا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَّا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَّا يَسْمَعُونَ بِهَا ۚ أُولَـٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٧٩﴾

Kwa yakini Tumeumba Jahannam kwa ajili ya wengi katika majini na wana Aadam. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama, bali wao ni wapotovu zaidi. Hao ndio walioghafilika. [Al-A'raaf: 179]

 

Yote yametokana na wigo wa kuwaiga wasio kuwa Waislamu na kuanza kidogo kidogo kufuata tabia na vitendo vyao. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Mtafuata nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia. Wakasema (Swahaba):  Ee Nabiy! Je, unamaanisha Mayahudi na Manaswara?  Akasema: “Hivyo nani basi mwengine?” [Al-Bukhariy na Muslim]

 

Na sasa yamedhihirika kwa upeo wa macho yetu ukweli wa Hadiyth hiyo. Kwani sisi Waislamu ni wakosa kutokana na unafiki wetu wa kuacha kanuni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kukubali hayo matendo na picha hizo kuanzia majumbani mwetu hadi kwenye ardhi zetu. Zile harakati za kuanzisha taifa la Kiislamu ni budi kuzifuta kabisa kwa sasa au kwa uchache kuzisimamisha kwanza hadi tuanze kusimamisha hizo serikali kwenye nafsi zetu kwanza na familia zetu, kwani hatujawa tayari hata kuanzisha hilo taifa la Kiislamu ndani ya nafsi yetu au familia zetu. Hatuwezi hata kuvaa mavazi au kujiweka katika mtazamo wa Kiislam katika miili yetu kwa kuona aibu au kuogopa kupachikwa sifa na majina kadhaa, vipi tutaweza kusimamisha taifa hilo na hali wenyewe hatujawa tayari? Hata idhaa zenye muelekeo wa Kiislamu zimekuwa zikichanganya ala za muziki na kudhani kuwa ni halali. Je, ni bora kubaki kwenye shaka au kule ambapo hakuna shaka?

 

 

Share